SoC01 Umuhimu wa kujali afya na mtu kuwa na afya

Stories of Change - 2021 Competition

Kayombo Tips

JF-Expert Member
Jun 19, 2020
572
490
Mwishoni mwa mwaka 2019 ndiyo kipindi ambacho habari za kuwepo kwa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya korona yaani UVIKO-19, kwa kiingereza COVID-19 zilianza kuripotiwa na kuenea duniani. Nilipokuwa nasikia taarifa hizo nilikuwa nachukulia kawaida tu. Kwamba ugonjwa huo utaishia Nchini China peke yake, na kwamba hauwezi kuvuka mipaka nje ya China na kuenea dunia nzima, kusababisha na kuendelea kusababisha vifo kwa mamilioni ya watu duniani, kuharibu uchumi, ajira za watu kupotea nk.

Pengine kwa watu wengi waliozaliwa miaka ya 1950 na kuendelea ndiyo janga kubwa la kwanza kukumbana nalo. Na litaendelea kuwekwa kwenye vitabu vya historia juu ya mlipuko wa ugonjwa huu, ambao umeigharimu karibia kila Nchi moja kwa moja. Dunia nzima inaendelea kupambana ili kuondoa ugonjwa huu, usiendelee kuleta madhara makubwa yanayoendelea kuletwa na ugonjwa huu.

Inawezekana ni watu wengi au wachache wamejifunza na kupata somo juu ya kipindi kigumu ambacho dunia ipo inapitia. Dunia bado haijui ni lini ugonjwa huu utatokomezwa kabisa, na dunia kurudi katika hali yake ya utulivu iliyokuwa nayo miaka ya 2018 kurudi nyuma, ambapo binadamu tulikuwa tuna furaha, tupo huru kukusanyika, kusafiri mahali popote bila masharti magumu kama ya sasa hivi.

Watu wachache tumejifunza juu ya umuhimu wa kujali afya na mtu kuwa na afya nzuri. Watu wengi licha ya mlipuko wa ugonjwa huu, bado hawajajifunza umuhimu wa kujali afya pindi mtu anapokuwa mzima wa afya, yaani akiwa hana ugonjwa unaomsumbua. Watu bado wanaendelea kufanya vitu kwa mazoea, hawajali kabisa afya zao.

Kwa miaka mingi watu wamekuwa wanaelimishwa juu ya umuhimu wa kujali afya zao. Lakini licha ya elimu kutolewa wengi wamekuwa hawafuati na kufanyia kazi mafundisho wanayopewa. Wanafanya vitu vinavyo hatarisha afya zao, licha ya kuambiwa vitu wanavyotumia kuwa na madhara makubwa kwa afya zao.

Haiingii akilini mtu aliyesoma kuwa uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya na anaona kwa macho watu wengi waliokuwa wanavuta sigara wamepata au wanataabika kwa magonjwa yaliyosababishwa na uvutaji sigara, ila bado anaendelea kuvuta sigara. Mtu amejifunza kuwa ni muhimu sana kufanya mazoezi kwa ajili ya afya ya mwili wake ila hafanyi mazoezi. Mtu ameambiwa kuwa awe anachagua vyakula ili awe na afya nzuri ila anakula hovyo. Mtu anaambiwa uzito wake umezidi, hivyo achukue hatua za kupunguza uzito wake ila anaishia kutochukua hatua na kuendelea kuishi kwa mazoea.

Kwa mfano inasemekana kuwa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya korona unaleta madhara zaidi, kwa watu wenye matatizo mengine ya kiafya kuliko kwa mtu mwenye afya nzuri. Watu wenye uzito uliopitiliza, watu wenye magonjwa ya moyo, kisukari, na watu wenye kinga dhaifu ndiyo wanakuwa wahanga zaidi. Lakini licha ya uhalisia huo watu wengi wanaendelea kufanya vitu kwa mazoea.

Mimi nilitegemea baada ya mlipuko wa ugonjwa huu, basi watu wengi watakuwa na mwamko wa kujali afya zao, kwa kuanza kufanya mazoezi, kwa kuanza kula zaidi vyakula vya asili, kwa kuanza kula viungo mbalimbali vinavyoongeza kinga ya mwili, ila hali ni tofauti. Inashangaza kutokuona watu wanafanya mazoezi ambayo ndiyo yanaenda kuimarisha mifumo ya upumuaji na kuyeyusha mafuta yaliyo sehemu mbalimbali za mwili. Watu bado wanakula vyakula ambavyo haviongezi kinga ya mwili. Inawezekana ni kwa sababu bado jamii haijajua umuhimu wa kujali afya na mtu kuwa na afya. Kwa mtu anayesumbuliwa na ugonjwa unao onekana kuwa hauna tib abasi anaelewa nini nazungumza hapa. Mtu aliyepoteza ndugu kutokana na ugonjwa huu anaelewa nini nazungumza hapa, na mtu anayeumwa sasa hivi anaelewa nini nazungumza hapa.

Kama kuna jambo muhimu watu wamejifunza katika zama hizi basi ni juu ya umuhimu wa kujali afya zao na kuishi katika afya, yaani kuishi katika mwili usio na maumivu yoyote yale. Hivyo ndugu zangu ni muhimu kujali afya zetu na kuishi maisha ya afya pindi tunapokuwa wazima wa afya. Wakati mtu unapokuwa mzima wa afya ndiyo wakati unaofaa kufanya vitu vitakavyofanya uendelee kuwa mwenye afya siku zote. Tunaweza kuwa wenye afya kama tutaamua kuishi maisha yanayopelekea mtu kuwa na afya.

N.B Mtu unayemwona leo mwembamba ndiye mnene wa kesho kama hatajenga tabia za kuhakikisha anakuwa mwembamba siku zote, na mtu mwenye afya leo ndiye mgonjwa wa kesho kama hatachukua hatua za kuendelea kujali afya yake. Na ni kweli kuwa mtu mwembamba ana nafasi ya kuishi miaka mingi kuliko mnene, labda huyo mnene awe ana unene wa asili.
 
Back
Top Bottom