SoC01 Umuhimu na uhitaji wa Katiba Mpya iliyo Bora

Stories of Change - 2021 Competition

kunubwa

New Member
Sep 13, 2021
2
3
Utangulizi.
Katiba ni sheria na kanuni zinazotungwa ili kuongoza nchi, shirika au taasisi fulani. Katiba ya nchi inatambulika kuwa sheria kuu na sheria mama na ndio msingi wa nchi. Katiba ni msingi wa mihimili mikuu mitatu ambayo ni dola, bunge na mahakama. Katiba inafafanua na kutoa mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili hiyo. Jamhuri ya muungano wa Tanzania inatumia katiba ya mwaka 1977. Katiba hii inajumla ya sura kumi.

Sura ya kwanza inaelezea misingi mikuu ya sera ya taifa, haki za msingi na wajibu wa wananchi; Sura ya pili mpaka sita inatoa masharti ya uanzishaji wa serikali ambayo inajumuisha dola, bunge na mahakama na pia inafafanua mgawanyo wa madaraka na kazi miongoni mwao; Sura ya saba inaeleza masharti kuhusu fedha za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Sura ya nane inaunda mamlaka na serikali za mitaa, majiji, manispaa na wilaya; Sura ya tisa inatoa masharti ya kuwepo na udhibiti wa majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sura ya kumi inatoa masharti yanayotumika ndani ya katiba. Haya ndio yaliyomo ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kiini.
Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imetoa mchango mkubwa sana katika kuongoza nchi na imeongoza kwa takribani miaka arobaini na moja(41) sasa. Pamoja na mchango wake mkubwa katika kuiongoza nchi, pamoja na marekebisho yake yote kumi na nne(14) lakini kumekuwa na malalamiko na changamoto mbalimbali kupitia katiba hiyo na changamatozo hizo zimepelekea wananchi kudai katiba mpya ambayo itakua katiba bora.

CHANGAMOTO ZINAZOPELEKEA WATU KUDAI KATIBA MPYA:-

1. Wananchi kutoshirikishwa kikamilifu katika utungaji wa katiba hiyo. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 haikutoa fursa nzuri kabisa ya wananchi wote kushiriki katika kutunga katiba hiyo. Hivyo, kupelekea wananchi kukosa kutoa maoni yao juu ya katiba nzuri. Kwa maana hiyo wananchi wanataka katiba mpya ambayo itaruhusu wananchi wote waweze kushiriki kikamilifu katika utungaji wa katiba.

2. Rais wa Jamhuri kupewa madaraka ambayo yamepitiliza na hayana kikomo. Wananchi wanataka katiba mpya ambayo itaweka ukomo wa nguvu na mamlaka ya rais. Kwasababu katiba ya 1977 imempa rais nguvu na madaraka yasiyo na kikomo hivyo kuleta shida na ugumu wakumkosoa na kumshtaki ata pale anapofanya kosa au anapokwenda kinyume na sheria. Kama inavyoonekana kwenye ibara ya 33(1-2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Inaonesha madaraka na nguvu alizonazo rais ambazo hazina kikomo.

3. Kuwepo kwa migogoro ya kimuungano. Hii ni changamoto nyingine ambayo imepelekea wananchi kuwa na uhitaji wa katiba mpya. Kumekua na migogoro ya kimuungano kati ya Tanzania na Zanzibar. Hii ni kwa sababu ya kutokua na usawa kuanzia kwenye wawakilishi wa serikali mbili yaani baraza la mawaziri na bunge. Hivyo, wananchi wanataka katiba ambayo itaweka usawa wa wawakilishi na kutatua migogoro hii ya kimuungano.

4. Katiba ya mwaka 1977 imekosa masuala muhimu ambayo sasahivi nchi inayo. Kuna maswala muhimu ambayo yamejitokeza sasahivi kama sheria lakini kwenye katiba ya 1977 hayapo maana ni muda mrefu umepita tangu katiba ya 1977 imeongoza mpaka leo. Hivyo inakosa vitu vingine ambavyo sasahivi vipo nchini kama sheria. Kwamfano swala la kulipia maji na tozo kwa kila mtanzania. Hivyo basi hii inapelekea watu kutaka katiba mpya amabayo itazungumzia na maswala ya sasahivi.

5. Katiba ya mwaka 1977 haijatoa muafaka wa maswala mbalimbali ya kitaifa na kwamba maoni ya watu yamewekwa kando. Masuala hayo ni kama tume huru ya uchaguzi, masuala ya muungano kwamba hakuna usawa, mamlaka yanayotajwa kuwa makubwa ya rais, madaraka ya umma na haki za binaadamu pamoja na utawala bora. Hivyo basi hizi ni baadhi ya changamoto hizo na malalamiko hayo ya katiba zilizopita ikiwemo ya mwaka 1977.

Nini kifanyike?
•Serikali pamoja na taasisi ya kutengeneza katiba itengeneze katiba ambayo itagusia na kukazia sehemu zifuatazo:

1. Ulinzi bora wa haki za binaadamu. Katiba mpya hiyo iweze kugusia haki za binaadamu. Maana haki za binaadamu ndio msingi wa maisha ya mwanadamu. Hii ni kwasababu katiba ya 1977 haijaeka mkazo sana kwenye maswala ya unyanyasaji wa haki za binaadamu na ata ufatiliaji wa wahalifu umekua mdogo sana.

Sikuhizi kumekua na unyanyasaji wa haki za binaadamu. Watoto kuuliwa ovyo, wanawake kunyanyaswa. Wanawake wengi wanakosa haki ya faragha. Miili yao inaoneshwa mitandaoni na hakuna adhabu kali zinatolewa kwa wahalifu. Watoto kuuliwa wakiwa wadogo pia ni tatizo na hii inazuia haki ya msingi ya kuishi kama ilivooneshwa kwenye ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Zifuatazo ni picha zinazoonesha unyanyasaji wa haki za binaadamu;

A2A7B823-8088-4E93-AF73-96303BD1738B.jpeg


(Picha kutoka kwenye page ya millardayo instagram

2. Masuala ya muungano. Kutokana na migogoro iliyopo kwenye muungano wa Tanzania na Zanzibar na kutokua na usawa wa serikali mbili, katiba mpya pia inatakiwa iongelee masuala ya muungano. Hii ni kwasabau kumekua hakuna usawa kabisa haswa kwenye serikali mbili ambapo wawakilishi wa Tanzania ni wengi kuliko wawakilishi wa Zanzibar. Hakuna haja kujadili muundo wa kuwa na serikali tatu.

Serikali mbili zinatosha ila tu kuwe na usawa wa wawakilishi kwa Zanzibar na Tanzania. Pia, kitu cha msingi kingine ni kutafuta njia sahihi ya kutatua migogoro iliyopo. Maana ukilinganisha serikali mbili yaani bunge na baraza la mawaziri, wawakilishi wa Tanzania ni wengi kuliko Zanzibar. Hususani baraza la mawaziri wawakilishi wengi ni kutoka Tanzania huku Zanzibar muwakilishi ni Rais wa Zanzibar. Kama ilivyooneshwa kwenye ibara ya 54(1) ya katiba ya 1977. Hivyohivyo bunge la muungano lina viongozi wachache sana kutoka Zanzibar ambao ni wawakilishi watano kutoka nyumba ya wawakilishi Zanzibar kama ilivooneshwa kwenye ibara ya 66(1) ya katiba ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Hivyo, katiba mpya ilete muungano sawiya haswa kwenye wawakilishi bungeni na baraza la mawaziri. Hii itasaidia kutatua matatizo mengi ya kimuungano hususani kutengeneza sheria nzuri na kufanya maamuzi yatakayokubalika kwa uzuri katika pande zote. Mfano bora ni kwa nchi za ulaya ambapo mgawanyo wa chemba zake au serikali mbili zake umetawaliwa na idadi sawa ya viongozi.

3. Uboreshwaji wa tume huru ya uchaguzi. Tume huru ya uchaguzi ni tume ambayo inaongoza uchaguzi wa viongozi. Ibara ya 74(1) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ndiyo inayounda tume ya sasa. Imeeleza kwamba “kutakua na tume ya uchaguzi na wajumbe wake watateuliwa na Rai ambao ni Mwenyekiti, makamu na wajumbe wengine. Lakini pia Mkurugenzi wa uchaguzi anateuliwa na ikuru. Hii ndiyo sababu wapinzani wanalalamika wakitaka kuwe na mabadiliko na hasa kuhusu tume hiyo inayozungumzwa tangu mwaka 1992 hadi leo ni namna ya kupata wajumbe wa tume hiyo.

Wapinzani wanataka kuwe na utaratibu mwingine wa kuwapata wajumbe wa tume ya uchaguzi tofauti na huu wa sasa ambao wote huteuliwa na iIulu.

Pia kuwe na ruhusa ya wapinzani kupinga matokeo. Hii mada imekua ikizungumzwa na wapinzani wa siasa. Wapinzani wanataka matokeo ya uchaguzi wa uraisi yapingwe mahakamani. Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na katiba ya Tanzania, matokeo ya urais yakishatangazwa na tume hayaruhusiwi kuhojiwa au kupingwa mahakamani kwa namna yoyote ile. Hii imepelekea vyama pinzani kusisitiza kuwa hakuna sababu ya kukataza matokeo hayo kupingwa mahakamani kwani yote hiyo ni michakato ya kidemokrasia.

4. Uwepo wa mgombea binafsi. Uhitaji wa katiba mpya uende sambamba na ruhusa ya ugombeaji binafsi. Mtu apewe haki ya kugombea yeye kama yeye. Hii itasaidia hata kudhibiti rushwa maana rushwa kwenye uchaguzi imekithiri. Hivyo, uwepo wa mgombea binafsi ni njia muhimu ya kudhibiti rushwa kwa maana kwamba itakua ngumu sana kwa mgombea binafsi kutoa rushwa kwa wananchi wote, lakini jambo hili ni jepesi kwa vyama vya siasa kwasababu wajumbe au wanachama wanaweza kupewa rushwa ili tu wamchague mgombea fulani ili aweze kupata nafasi aitakayo. Kwa mgombea binafsi ni ngumu maana hata uwe na fedha kiasi gani ukiwa unataka kupata nafasi ya uongozi, wewe binafsi huwezi kutoa rushwa kwa wananchi

5. Kupunguza na kuweka ukomo wa mamlaka yanayotajwa kuwa makubwa ya Rais. Raisi wa Tanzania amepewa mamlaka na madaraka ambayo ni makubwa na hayana kikomo. Hii inakua ni ngumu hata hata kumkosoa rais pale anapokua kakosea lakini pia hata kumshtaki inakua ni ngumu. Rais pia ni binaadamu, kuna muda anakosea na hivyo anahitaji kurekebishwa na kukosolewa. Mamlaka aliyopewa rais hasa ibara ya 33(1-2) ya katiba ya Jamhuri ni mamlaka ambayo yanaleta ugumu wa kumshtaki na kumkosoa rais. Hivyo basi, katiba mpya ipunguze angalau mamlaka hayo na kumuekea mipaka baadhi

6. Kuwepo kwa madaraka ya umma. Madaraka ya umma ni hali ambayo raia wa nchi ya Tanzania wanapewa ruhusa ya kuwa na uwezo wa kujihusisha katika masuala mbalimbali ya nchi. Ikiwemo kuweza kushiriki kwa kina kwenye kufanya maamuzi. Kama inavyofahamika kwamba nchi ni watu hivyo bila watu hakuna nchi. Nchi hujengwa na watu hivyo watu wapewe nafasi ya kushiriki vizuri katika masuala mbalimbali ya nchi haswa kwenye kufanya maamuzi, masuala ya uchaguzi na kutoa maoni. Kwa kufanya hivi hii ndio italeta maana halisi ya nchi yenye demokrasia.

Ukiangalia kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sura ya kwanza imeongelea utangulizi. Imeongelea haswa watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mchango wa kuijenga nchi yao kwa uhuru na amani. Hii inamaanisha kwamba watu ndio wanaojenga nchi hivyo wapewe nafasi ya kushiriki kwa kina kwenye shughuli za nchi bila unyanyasaji wala ubaguzi wa aina yoyote.

7. Uwepo wa mahakama maalumu ya kushughulikia makosa zoelefu. Katiba mpya iweze pia kuunda mahakama maalumu kwaajili ya kupambana na vitendo gaidi kama vile ufisadi, rushwa na biashara za madawa ya kulevya pamoja na uhujumu uchumi maana ni vitendo vibaya na vinakandamiza maendeleo ya nchi. Nchi imegubikwa na suala kubwa la vitendo vya rushwa, ufisadi na uhujumu uchumina ndio inapelekea vijana kuangamia. Nguvu kazi ya taifa inaangamia maana vijana ndio nguvu kazi ya taifa. Mahakama hiyo iwe na uwezo wa kutoa adhabu kali sana kwa watu watakaobainika kuwa na makosa hayo.

Hivyo basi, kwa kupata katiba mpya kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katiba ambayo itaongelea na kutibu majeraha yaliyoelezwa hapo awali kama changamoto basi tutakua tumepata katiba bora.

UMUHIMU WA KUWA NA KATIBA BORA:-

• Katiba bora ndio msingi imara wa maendeleo endelevu. Hii inamaanisha kwamba nchi yetu ikiwa na katiba bora na inayofuatwa vizuri, basi maendeleo ya nchi yetu yatakua kwa kasi sana. Unyanyasaji utatokomezwa, rushwa pamoja na uhujumu uchumi utaisha. Sekta mbalimbali zitaendelea na kukua na hii itapelekea hata nchi kukua kiuchumi zaidi na zaidi.

• Katiba bora ndio waraka wa muafaka wa wananchi kisheria, kisiasa na kiutawala. Juu ya namna wananchi watakavyotaka nchi yao iongozwe. Kama inavyofahamika kwamba katiba ndio msingi wa sheria zote na ndio hutoa maelekezo ya namna au kwa jinsi gani nchi iendeshwe. Hivyo, kuwa na katiba bora nchini itasaidia kufika muafaka wa migogoro na matatizo mbalimbali ua kisheria, kisiasa na hata kiutawala.

• Katiba bora inamchango katika kuleta usalama na amani nchini. Hii ni maana kwamba nchi inapoongozwa na katiba bora yenye kufuata demokrasia bila kubagua watu basi hata amani na usalama vitakuwepo nchini. Hakuna kitu kizuri kama wananchi kuishi katika mazingira tulivu yenye amani na usalama.

Mapendekezo.
Mapendekezo yangu juu ya swala zima la katiba na utawala bora ama ni nini naona kifanyike ni kama ifuatavyo;

• Serikali iweze kuifanya katiba kuwa miongoni mwa vipaumbele muhimu. Hii ni moja ya pendekezo langu kwamba serikali tuliyonayo iweze kuhakikisha kwamba katiba ndio inakua kipaumbele cha kwanza. Maana katiba ndio msingi wa nchi hivyo inatakiwa ifuatwe kikamilifu. Hapa nyuma katiba imekua haifuatwi kama inavyitakiwa. Watu wanakiuka sheria. Ifahamike kwamba katiba ndio sheria mama. Sikuhizi hata haki za binaadamu zinakiukwa na ni kwasababu watu hawajui uzito na umuhimu wa katiba.

Pia, rais anaweza tu akaamuru kitu fulani kiwe sheria na kweli ikafatwa kama sheria bila hata kufuata utaratibu maalumu ulioekwa na katiba kuhusu utungaji wa sheria. Hivyo, serikali iweke msisitizo sana kwenye kuipa kipaumbele katiba na kuifuata katiba hiyo.

• Kuhusu kutatua migogoro ya kimuungano, tunaiomba serikali iweze kuweka usawa wa zile serikali mbili kwenye wawakilishi wake. Yaani, kama baraza la mawaziri litakua na wawakilishi hamsini basi wawakilishi ishini na tano watoke Zanzibar na hivyo hivyo wawakilishi ishirini na tano watoke Tanzania. Hii itasaidia ata kwenye kufanya maamuzi na kupata maoni sawa kwa kila wawakilishi wa kila pande.

• Tanzania ni nchi inayojulikana kama nchi ya demokrasia. Lakini nchi hii haimpi uhuru wa kujieleza na kutoa hoja na maoni mwananchi wake. Hii inamaana kwamba, watu hawana uhuru wa kujieleza na kutoa maoni yao. Hivyo kupelekea sifa ya demokrasia na uhuru kupotea. Hivyo basi napendekeza serikali iweke utaratibu maalumu aidha katika kila wilaya kuwe na utaratibu wa kukusanya maoni ya wananchi na utaratibu wa kuyasikiliza maoni hayo. Maana hii nchi ni ya watu.

• Serikali iweze kutoa mfumo ambao utasaidia wananchi kuijua katiba na kuielewa vilivyo. Kwasababu sio kila mwananchi anaweza kuisoma katiba. Hivyo basi wananchi waweze kupewa elimu juu ya kuijua na kuifuata katiba. Hii itasaidia hata kupunguza idadi ya wahalifu nchini.

Hitimisho.
Viongozi na watunga sheria za nchi wanatakiwa kuwa makini sana haswa pale wanapotunga sheria hizo. Watunge sheria ambazo ni bora. Wananchi wanataka sheria bora na sio bora sheria. Hii ni kwasababu kwa kua na sheria bora nchini kutasaidia kuleta mafanikio katika nyanja mbalimbali za maisha. Ikiwemo, kuwepo kwa usalama na ulinzi nchini; ongezeko la uchumi maana sheria bora zitasaidia kuzuia na kupambana na rushwa, uhujumu uchumi. Sheria bora zinaleta umoja na mshikamano kwa kuondoa matabaka katika jamii.

Asanteni.
 
Kazi nzuri mkuu. Umeichambua katiba vzr hongera yako mkuu
 
Back
Top Bottom