Umoja wa Ulaya wataka wapiganaji mamluki kuondoka Libya

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,007
9,873

Umoja wa Ulaya umetoa wito wa kuondoka kwa wanajeshi wa kigeni na wapiganaji mamluki nchini Libya ukisema hilo ni sharti muhimu kuelekea kurejea kwa uthabiti wa taifa hilo liloharibiwa kwa vita.


Libyen Tripolis EU Charles Michel bei Najla Al-Manqoush
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel (Kushoto) akiwa kwenye mkutano na waandishi habari pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Libya Najla Al-Manqoush mjini Tripoli.

Akizungumza na waandishi habari kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, rais wa Baraza Kuu la Umoja Umoja Charles aliye ziarani nchini humo, amesema ni lazima wapiganaji kutoka nje waondoke na kutoa nafasi kwa Libya kujiimarisha upya.

Michel pia ametoa wito kwa pande hasimu za siasa nchini Libya kutumia nafasi iliyopatikana ya kuundwa kwa serikali ya mpito kujenga taifa thabiti na lililostawi akiitaja hatua ya kupatikana serikali hiyo kuwa jambo la kihistoria.
Libyen Tripoli | Portrait | GNA Kämpfer
Ripoti ya hivi karibuni kabisa iliyotolewa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa imezituhumu serikali za kigeni kwa kuigeuza Libya kuwa uwanja wa mapambano kwa pande hasimu na kupuuza vikwazo vya Umoja huo pamoja na marufuku ya kuingiza silaha iliyodumu kwa karibu muongo mmoja.

Wataaalamu hao wamezitaja Uturuki na Qatar kuwa waungaji mkono wakubwa wa vikosi vya wapiganaji wa serikali inayotambuliwa kimataifa iliyokuwa na makao yake mjini Tripoli huku Umoja wa Falme za Kiarabu, Urusi na Misri zinamuunga mkono Khalifa Haftar, jenerali wa jeshi anayedhibiti eneo la mashariki na kusini mwa Libya.

Taifa hilo la kaskazini mwa Afrika limetumbukia kwenye mzozo tangu kuondolewa madarakani na kisha kuuwawa kwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Ghaddafi mnamo mwaka 2011.
Matumaini mapya kwa Libya
Kuna matumaini kuwa kupatikana kwa serikali ya mpito kutasaidia kuzileta pamoja pande hasimu nchini humo hususani makundi ya mashariki na magharibi yanayoungwa mkono na madola ya kigeni.
Libyen Parlament
Waziri Mkuu wa serikali ya mpito nchini Libya Abdul Hamid Dbeibeh
Umoja wa Mataifa unakadiria bado kuna wapiganaji wa kigeni 20,000 nchini Libya na muda wa mwisho uliowekwa mwezi Januari mwaka huu wa kuwataka kuondoka umepita bila dalili ya watu hao kukusanya virago.

Miito ya kuwataka kuondoka imeongezeka wiki za hivi karibuni na kutiwa nguvu na waziri wa mambo ya kigeni wa Libya Najla al-Mangoush aliyewata kwa mara nyingine waondoke nchini humo.

Michel ambaye amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali mpya ya Libya, ametumia ziara yake nchini humo kuahidi uungaji mkono wa kanda ya ulaya katika kufikia maridhiano na kumaliza uhasama kwenye taifa hilo lenye utajiri wa mafuta.

"Tutafanya kazi na serikali mpya na kuingua mkono" amesema Michel baada ya kukutana na waziri mkuu wa serikali ya mpito Abdul Hamid Dbeibah ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo chini ya mchakato wa kisiasa uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Mwanasiasa ambaye aliidhinishwa na bunge la Libya mwezi uliopita ataongoza serikali hiyo kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Disemba mwaka huu.
"Kufufua uchumi, uchaguzi na kupambana na uhamiaji haramu ni maeneo ambayo Umoja wa Ulaya unaweza kusaidia" amesema Michel baada ya mazungumzo hayo.
Uhamiaji ni suala la kipaumbele kati ya Libya na Umoja wa Ulaya
Libyen, Tripoli: Übernahme des Flughafens
Katika ziara hiyo Michel amesema uhamiaji ni ajenda muhimu na ya kipaumbele kwenye mahusiano kati ya Libya na Umoja wa Ulaya.
Taifa hilo ni lango kuu linalotumiwa na wahamiaji wanaojaribu kuingia Ulaya kupitia bahari ya Mediterrania na walanguzi wa biashara hiyo walishamiri wakati wa machafuko kuelekea kuangushwa kwa utawala wa Ghaddafi.

Michel pia amesema balozi wa Umoja wa Ulaya kwa Libya atarejea kwenye mji mkuu Tripoli katika kipindi cha wiki chache zinazokuja.
Kadhalika Umoja wa Ulaya umeahidi kutoa msaada wa dozi 50,000 za virusi vya corona kwa Libya, shehena inayoongeza idadi ya chanjo kwa taifa hilo baada ya kupokea dozi 100,000 za chanjo iliyotengenezwa na Urusi ya Sputnik V iliyowasili siku ya Jumapili.

Ziara ya Michel itafuatiwa na ziara ya viongozi wengine wa Ulaya wanaotarajiwa kuizuru Libya katika muda wa wiki chache zinazokuja.
Mwezi uliopita mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa, Ujerumani na Italia waliizuru Libya kama sehemu ya hatua za kuonesha mshikamano na serikali mpya iliyoundwa nchini humo.

Ufaransa ilikwenda mbali zaidi na kufungua tena ubalozi wake nchini Libya mwezi uliopita na wiki inayokuja waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis anatarajiwa kuutembelea mji mkuu Tripoli ambapo amepangiwa kufungua ubalozi wa nchi yake katika ziara itayofangamana na ziara ya waziri mkuu wa Italia Mario Draghi.
 
Wapuuzi Hawa si wamesababisha wenyewe huu upuuzi, waache kutuona mazwazwa.
 
Waliopeleka wapiganaji mamluki huko Libya ni mshirika wao Uturuki na hasimu wao Urusi.

Isitoshe wao pia (EU) hasa Uingereza (mwanachama mwenzao wa zamani) na Ufaransa wana hatia kwa kinachoendelea huko Libya kwa sasa.

Hivyo hawapaswi kuitelekeza Libya walioshiriki kuiharibu.
 
Back
Top Bottom