"Umoja wa ndani, na Umoja wa Nje" Nguvu, uweza na Utajiri

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,339
51,883
"UMOJA WA NDANI, NA UMOJA WA NJE" NI NGUVU, UWEZA NA UTAJIRI.

Kwa Mkono wa, Robert Heriel


Jumbe hii isomwe na wapenda hekima, wenye kutafuta ufahamu, iwe taa kwao wapendao heri, lakini iwe giza kwao wenye hila na njama, hao wenye kudhulumu.

Leo Taikon nimekuja na somo muhimu na lalazima kwao wapendao mambo hayo matatu; NGUVU, UWEZA NA UTAJIRI.
Lengo la Makala hii: Kuifunza jamii ulazima wa umoja( wa ndani na wa nje) Katika kupata nguvu, uweza na Utajiri katika familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Ifikapo mwisho wa makala hii, kila msomaji natarajia ajue na kubadilika kwa kuhakikisha anautafuta umoja kwa manufaa ya familia, jamii na taifa.

Kwenye umoja kila jambo ni bora na muhimu, kila kitu kinaheshimiwa na kupewaa kipaombele. Kwenye umoja kila mmoja ananafasi ya kufanikisha malengo yaliyopangwa. Umoja ni akili, Umoja ni upendo, umoja ni utajiri, umoja ni nguvu, umoja ndio msingi wa uwepo wa dunia na Ulimwengu kwa ujumla. Umoja ni Mfumo.

Umoja ni kupatana,kuafikiana,kuelewana na mwingine,pia ni hali ya kulingana katika roho,katika nia,katika mawazo,katika maneno na matendo. Pasipo na umoja hakuna kinachoweza kufanyika kikafanikiwa, umoja ni maendeleo.

AINA ZA UMOJA
1. UMOJA WA NDANI
2. UMOJA WA NJE

1. UMOJA WA NDANI
Umoja wa ndani ni hali ya mtu kupatana, kuafikiana na kuelewana na nafsi, akili, Nia, mtazamo na Matendo yake wa ndani. Mtu mwenye umoja wa ndani huwa na nguvu kwa wengine, huwa na mamlaka kwa wengine, watu wa namna hii kuupata utajiri ni asubuhi kabisa. Mtu mwenye umoja wa ndani huwa na msimamo kwani kila kitu ndani ya mwili wake kinamuunga mkono. Hii ni kusema, akili, roho, na nafsi zikinia mamoja lazima mtu huyo awe na nguvu, uweza na lazima awe tajiri. Mbinu moja kuu ambayo adui huitumia na ambayo mimi naitumia na kushauri watu waitumie kwenye mapambano ya kivita, iwe ya kiuchumi, kisiasa au kijamii ni kuuvuruga umoja wa ndani wa adui yako. Ukiweza kuathiri akili ya mtu isipatane na imani yake, au imani yake isipatane na akili yake, au mtazamo na falsafa ya mtu isifanane na matendo yake basi hapo utakuwa umemuangusha adui yako.

Kwenye vita, hasa vya watu wenye akili na muono wa mbali hupiga umoja wa ndani zaidi kuliko umoja wa nje. Watu hawashindi vita kwa kuwaua adui zao. Labda tuseme, Tanzania ilivyoipiga Uganda ya Idi Amin Dada, haikushinda vita bali ilishinda lile pambano hii ni kutokana na sababu kuwa, tulishinda vita baada ya kuua majeshi ya adui mpaka yakasalimu amri, ambapo ni umoja wa nje.

Wazungu walipopigana na sisi ili watutawale walishinda vita, hii ni kutokana na sababu kuwa, wao walijikita zaidi na kutushinda zaidi kwenye UMOJA WA NDANI, kwa kuathiri Imani, Mila na desturi zetu(Utamaduni) zetu na kisha wakaleta imani, mila na desturi zao na kuzifanya imani,mila na desturi zetu kuonekana mavi kama sio uchafu mwingine. Nadiriki kusema, kitendo cha Wazungu na Waarabu kutupiga pigo la Millenium na wala sio pigo la msimu kulifanya rasmi watangazwe washindi wa Vita ile.
Waafrika tumezaliwa tukiwa hatuna umoja wa ndani, kwani tayari tumeshaathiriwa kwenye ngome ya ndani kabisa ulipo umoja wa ndani. Ikiwa tumeathiriwa kwenye Imani, kisha wakatuathiri kiakili kwa kutuletea elimu yao, ni wazi mpaka sasa hatuna ujanja. Tumeshindwa.

Huwezi kuwa na umoja wa nje kama hauna umoja wa ndani, kuwa na umoja wa nje bila umoja wa ndani ni kukaribisha Usaliti.

Mtu asiye na Umoja wa ndani hufanya mambo asiyokubaliana nayo, au hufikiri mambo asiyoyafanya, au huamini mambo asiyo yatenda. Yaani hana umoja wa kinafsia. Watu wa hivi hawawezi ona umuhimu wa maisha, pia huwa hawana misimamo, ni bendera fuata upepo, ni watu wenye majuto. Yaani akili yake anaona kunywa pombe ni kosa, lakini moyo wake unapenda kunywa pombe, hivyo hujikuta kwenye mgogoro wa kinafsi hasa akili na moyo vinapopigana ndani yake.

Watu wasio na umoja wa ndani mara kwa mara huwa na ile falsafaa isemayo, 'hakuna mkamilifu' wakati watu wenye umoja wa ndani huamini kuwa wao ni kamilifu kwani umoja ndio ukamilifu wenyewe. Mtu mwenye umoja wa ndani, huwa ni wakamilifu, kila wakifanyacho ni kikamilifu kwani hukifanya kwa moyo wote, akili yote, na nguvu zote. Hawaombagi msamaha kwani wanajijua kuwa walifanya wakiwa wanajielewa na wakiwa na malengo yao.

Wazungu walivyotutawala kamwe hawatakuja kuomba msamaha kwani walikuwa wanamaanisha, wanajiona walikuwa wana haki ya kufanya hayo. Kwenye imani za kiroho, miungu ikiamua jambo haipindishi hata mlie kwa machozi ya damu, Mathalani Mungu akisema iwe hivi itakuwa bila kujali nani atapenda au nani hatapenda, nani ataumia au nani atafurahia. Shetani, tangu ameasi hana mpango na hatakuja kuwa na mpango wa kuomba msamaha. Hii ni kutokana anaumoja wa ndani kabisa.

Kikawaida mwanaume anapaswa awe na Umoja wa ndani, ili aweze kujiamini, kuwa na msimamo, mkamilifu,kwamba atakachosema na kukifanya kinatokana na makubaliano, mapatano, maelewano ya akili, roho na moyo wake. Kamwe hapaswi kujisaliti au kujipinga.
Mwanaume asiye na umoja wa ndani anapoteza sifa kuu ya uanaume ambayo ni msimamo, ukamilifu na kujiamini. Mtu mwenye umoja wa ndani kamwe hawezi kuomba msamaha kwani anaamini hakosei, kuomba msamaha ni kujisaliti, lakini wengi huomba msamaha kwa sababu hawana umoja wa ndani, yaani ndani yao hakuna ushirikiano wa kuelewana, kupatana kwa akili, moyo na roho.
Yaani wakati anaamua jambo, basi akili ndio iliamua bila kuushirikisha moyo na Roho, au wakati moyo unaamua, akili na roho havikushirikishwa, au wakati Roho inaamua, akili na moyo havikushiriki. Na hapa mtu ndio hujuta na kulia lia. Lakini kama kulikuwepo maelewano ya akili, roho na moyo basi hakuna haja ya kujuta na mtu kamwe hawezi kujuta.

Ili mtu afanikiwe katika jambo lolote lile basi lazima awe na umoja wa ndani kabisa. Ili mtu awe tajiri au na pesa lazima awe na umoja wa ndani kabisa baina ya akili yake, moyo na roho yake.
Kama mtu akikuuliza kwa nini familia yenu ni masikini au taifa lako lako ni masikini, basi usijiume ume kumjibu, mwambie 'Hakuna umoja wa ndani baina ya watanzania'

Watu wasio na umoja wa ndani huzaa umoja wa nje wa kinafiki, ubinafsi wa nje, ufisadi, wizi, Rushwa na mauaji.

Ili jamii iendelee lazima iwe na umoja wa ndani miongoni wa watu wenyewe

2. UMOJA WA NJE.
Huku ni kuelewana, kufanana, kupatana baina ya mtu na mtu, yaani wewe na mimi, au mimi na Yule.
Umoja huu umegawanyika kama Ifuatavyo;
2.1, Umoja wa Mume na Mke (Ndoa) /Familia
2.2. Umoja wa kijamii
2.3. Umoja wa kisiasa
2.4 Umoja wa Kiuchumi.

Kama nilivyosema, umoja wa nje hutokana na umoja wa ndani, huweza ukaweka mahusiano ya kindoa na mtu asiye na umoja wa ndani, yaani mtu ambaye akili, moyo na roho yake vinafanya kazi separate bila umoja(makubaliano). Huwezi oa mwanamke au kuolewa na mwanaume asiye na umoja wa ndani, kwani kwa vyovyote lazima hamtakuwa wamoja bali mtakuwa wapinzani ndani ya ndoa yenu.
Ndio maana zamani popote duniani ili uoe ilikupasa umchukue mtu anayetoka kabila moja nawe, dini moja nawe, na utamaduni mmoja nawe. Hii ni kuzifanya akili, mioyo na roho zenu kupatana, kuelewana, kukubaliana kwa pamoja. Lakini kuoa mtu ambaye ni tofauti na wewe kimtazamo, kiakili, kidini, na kihisia na kusema ni mkeo au mumeo hiyo ni dalili ya ukichaa na wendawazimu. Hakuna umoja hapo bali kuangamizana.

Ili nchi au jamii iendelee lazima kuwe na umoja, watu wawe na umoja kiakili, kimwili, kiroho, na kimoyo. Hakuna maendeleo kwenye jamii au taifa lililogawanyika kimtazamo, kifalsafa, kiimani, kiakili, na kihisia.

Mara kwa mara ninasema kuwa, kama ningekuwa Rais wa taifa hili, jambo la kwanza ningefuta Dini zote za kigeni na kuunda dini ya taifa hili, ningefumua mfumo wote wa elimu kisha mambo mengine yangefuata.

Hayati, mwl, Julius Kambarage Nyerere alijitahidi jambo moja tuu pindi akiwa kwenye utawala wake, nalo ni kufuta mfumo wa vyama vingi na kuibakiza TANU pekee yake. Hii tosha ilinifanya nimuone alikuwa Great Thinker, sasa alichobakiza alipaswa aondoe utitiri wa dini zote za kikoloni ambazo kimsingi mungu anayeabudiwa huko ni mungu wa kikoloni, futa Ukristo na Uislam, kisha angeunda dini ya taifa hili. Nafikiri kipindi kile ndio ilikuwa wakati muhimu kwani ingewezekana kama ilivyowezekana kufuta vyama vingine vya kisiasa. Kisha angefumua mfumo wote wa elimu na kuunda mfumo mpya.

Hakika hapo watu wangekuwa na umoja na taifa lingekuwa na umoja kama alivyokusudia kwenye kauli mbiu isemayo "Uhuru na Umoja"
Hatuwezi kuwa na umoja kwenye taifa lililokuwa na tofauti nyingi za kimtazamo, kiimani, kifalsafa, kiakii n.k. Labda umoja wa kudanganyana.

Mataifa yote makubwa duniani kabla ya kuwa makuba, yenye nguvu. uwezo na utajiri, yalihakikisha dini inakuwa moja, na elimu inazingatiwa, kwa sababu dini, na elimu ndio huongoza mioyo ya watu na maisha ya watu.
Uingereza ilikuwepo dini ya Anglican
Ujeruman ilikuwepo dini ya Lutheran
Ufaransa na Italia ilikuwepo dini ya Roman Catholic
Hizo zilikuwa ni dini za taifa.
Mataifa hayo yalikuwa makubwa mno,baadaye Taifa la china lilipopata uhuru wake, lilifutilia mbali dini zote za kimagharibi.

Umoja wa ndani huzaa umoja wa nje.

Ili familia zetu ziwe ziendelee lazima kuwepo na umoja baina ya;
Baba na Mama
Wazazi na watoto
Watoto kwa watoto

Kama Baba na mama hawana umoja basi moja kwa moja hakutakuwa na umoja baina ya watoto kwa watoto. Hii baadaye haina tija kwenye maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla

Zamani ulikuwa ukisikia kuwa kuna laana sijui ya Mama au Baba, hakuna kitu kama hicho, hakuna cha laana wala ndugu yake laana.
Wazazi wa zamani wengi hawakuwa na umoja baina yao, kisha hawakuwa na umoja na watoto wao, umoja kwao waliita heshima ambapo haikuwa heshima isipokuwa VITISHO vitupu. Umoja hauletwi kwa kutishiana, umoja unaletwa kwa makubaliano, mapatano, maelewano na kupendana. Pasipo kuwa na mambo hayo hakuna umoja. Umoja haulazimishwi bali unaletwa kwa kupewa elimu ya upendo.

Zamani wazazi walikuwa wakitishia watoto wao kuwa wasipowaheshimu watalaaniwa na kuharibikiwa maisha, basi watoto walikuwa wakiwapenda wazazi wao kwa woga wala haukuwa upendo wa kweli, na kama atatokea mtoto mmoja ambaye atakiuka amri za wazazi wake iwe ni mama au Baba basi wazazi wanamlaani na mtoto ati anadhurika. Hakukuwa na laana isipokuwa walikuwa wakiwaloga watoto wao, ni uchawi uliokuwa unatumika, hakuna la ziada. Ilikuwa ni rahisi kumloga(wanajifanya wanampa laana kumbe wanamloga mtoto wao) mtoto wa zama zile kutokana na kuwa zama zile Baba na mama walitoka kwenye kabila moja kumaanisha ni damu moja. Lakini kwa sasa sio rahisi kutokana na kuwa Baba ni Msukuma, Mama ni Mmakonde,mtoto anatoka chotara, anaanzajwe kulogwa kama wanavyoiita laana.

Usishangae siku hizi unaweza hata mpiga mzazi wako na usipate madhara, utapataje madhara ikiwa damu yako ni mchanganyiko wa makabila, mchanganyiko wa imani, uliona wapi mtu anadhurika kwa jina la Yesu au la Muhamad, hakuna kitu kama hicho, ila mpige mama au Baba yako alafu wote ni wakabila moja yaani Baba Mnyakyusa na Mama Mnyakyusa hapo wakiamua kwenda kwa miungu yao(kukuloga alafu watasema wamekulaani kumbe kwa siri wamekuendea kwa sangoma) uone kama hauokoti makopo. Lakini kama watakuombea kwa jina la Yesu au Muhamad baki ukicheka tuu, hakuna kitakachofanyika hapo.

Nilikuwa naelezea umoja, kwenye ngazi ya familia,
Damu ni falme, huwezi iloga tuu unavyotaka ati kisa wewe ni Baba au Mama, lazima uongee na wakulungwa waliotangulia, uwasilishe madai yako kwao kisha wakikubali ndio madhara yapatikane, sasa embu assume mtoto wako ni mchanganyiko wa makabila manne, unafikiri kumlaani(Kumloga) itakuhangaisha kwa kiasi gani kupeleka madai yako kwa falme hizo nne za damu yake. Jibu ni kwamba ni gharama, hivyo ndio maana siku hizi wazazi laana zao(kuloga) hazishiki. Wataishia kusema mungu atakulaani lakini hawataji mungu yupi. Wasijue kuwa kila damu inafalme zake kiroho.

Huo ni umoja wa nje katika familia.

Nimeelezea jambo hili kwa sababu, zipo jamii ambazo hazina umoja, ndugu yao mmoja akifanikiwa badala ya kushukuru na kumpa sapoti azidi kuendelea mbele kwa mbele, wao huhangaika kumshusha na kumloga, alafu mwisho husema kuwa ni laana kwa sababu watakazozitoa wao labda ni kutowasaidia vile walivyokuwa wanataka, au sababu yoyote ile.

Ni jukumu letu wanaume, kuhakikisha tuna umoja wa ndani ya nafsi zetu, kisha tunapoenda kuoa tuhakikishe kuwa wake zetu tumewa-shape na wao wana umoja wa ndani kama sisi. Na hapo tutajenga familia yenye umoja, watoto wenye umoja, jamii yenye umoja, na taifa lenye umoja.

Kwa leo niishie hapa.

Taikon nimemaliza mwenye swali leo ruhusa kuuliza.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa, Dodoma
 
Back
Top Bottom