Umewahi kumpiga au kupigwa na mpinzani wako kibiashara? Mbinu gani zilitumika?

Izzi

JF-Expert Member
Nov 30, 2016
553
1,107
Kuanzia Azam Dhidi ya Azania, Mwana FA & AY Dhidi ya MIC Tanzania (Tigo), FIESTA Dhidi ya Wasafi Festival, Simba Dhidi ya Yanga, Adidas Dhidi ya Nike, Facebook Dhidi ya Snapchat, Pepsi Dhidi ya Cocacola, Uber Dhidi ya Lyft mpaka wewe dhidi ya mpinzani wako... biashara ni vita. Kinachopiganiwa ni waleti zetu au wakati mwingine ni ubabe tu ili kupata 'attention' na kutawala soko. Wakati mwingine, ni ile raha tu ya kumpiga na kumkalisha mpinzani. Lakini matokeo ya hivi vita huwa yanabadilisha mazingira ya kibiashara na maisha kwa ujumla.

"Vita vya biashara" ni uzi wa kupeana simulizi fupi fupi na zinazoeleweka (Ambazo zinatuelimisha, zinatuhamasisha & kutuburudisha) juu ya nini kinawasukuma wajasiriamali, wabunifu, makampuni, viongozi na wawekezaji wake kuelekea kwenye kilele cha mafanikio - au shimoni. Tuongelee namna mbinu, figisu figisu, janja janja, rafu au hata kamati za ufundi zinavyotumika katika ulimwengu wa biashara.

Je, umewahi kumwangusha mpinzani wako kibiashara? Au umewahi kuangushwa na mpinzani wako kibiashara? Labda pengine hukumwangusha au kuangushwa - lakini 'ulipigwa' kipigo cha mbwa koko. Well, labda wewe sio mfanyabiashara lakini unafahamu vita fulani ya kibiashara iliyowahi kutokea au inayotokea hivi sasa; vyovyote iwavyo tafadhali tusimulie kwasababu lengo ni kupata taarifa na maarifa.

Karibu.
*********
UBER Vs LYFT
Ridesharing imeitikisa tasnia ya usafirishaji, na wala haioneshi dalili ya kupunguza kasi. Ndani ya miaka michache tu Uber na Lyft zimekuwa kubwa dhidi ya kampuni za kukodisha magari (rental cars) na taxi . Sasa kwa kuwa huduma za rideshare zimetawala barabara, kuna ushindani mkubwa baina ya vigogo hawa wawili wa rideshare.

uber-vs-lyft-banner.jpg


Mwaka 2014, kulikuwa na Uber, ambayo kwa wakati huo ilitawala soko la ride-sharing kwa 93%, na kulikuwa na vi-startups vidogo vidogo vya ride-share ambavyo vilikuwa vinapambana kudonoa japo sehemu ndogo ya soko. Ile tu kwamba Uber imekuwa ya kwanza kuingia sokoni katika tasnia ya ride-share, ilimaanisha walikuwa na uwezo wa kuvimeza vi-startup vyote vya ride-share. Moja ya startup ndogo zilizokuwa zinapambana kula keki ambayo Uber alikuwa anaifaidi peke yake... ni Lyft.

Mwaka ambapo Lyft inaanza ilikuwa na market share ya 7% tu, lakini leo hii Lyft ni mpinzani mkubwa Uber. Lyft ilikuwa ndio kampuni ya kwanza ya ride-share kwenda public (IPO) ikimwacha Uber ametoa macho kwa mshangao.

HISTORIA.

Uber ilianza kama 'on-demand vehicle service' mjini San Francisco na, ndani ya miaka mitano, ikakua na kuwa 'top ride-hailing app' katika nchi 60 duniani. Punde tu baada ya uzinduzi wa Uber, Lyft ilianzishwa hapo hapo mjini San Francisco kama 'ridesharing service' nyingine.

Uzinduzi wa Lyft ulikuja wakati muafaka kabisa, kwasababu, wakati Lyft inazinduliwa (Mwaka 2017) Uber iliwekwa kikaangoni - kwa tuhuma chafu chafu. Kashfa lukuki zikawa zinaibuka katika kile kilichoitwa 'Uber scandals', kama vile malalamiko ya unyanyasaji wa kingono, kujiuzulu kwa viongozi wa juu wa kampuni, na madai ya Uber kuficha taarifa za udukuzi (cyber-attack ) waliyofanyiwa.

Sasa wakati Uber ikiwa busy kusafisha taswira yake iliyochafuka, Lyft wao walikuwa wako kazini kuijenga brand yao kwa nguvu zote ili iweze kupenya miongoni mwa jamii. Hii ilifungua fursa kwa madereva na abiria ambao hawakutaka kujihusisha na kampuni inayokumbatia mambo machafu yaliyokosa maadili (Uber). Kwa jinsi hii, Lyft waliweza kupata app users wengi, wengi zaidi, kwasababu tu walikuwa ni mbadala wa Uber.

Lyft ads.jpg


Ingawa kashfa za Uber zilirahisisha ukuaji wa Lyft, Uber ilikuwa tayari imejiimarisha vizuri kabla jipu la kashfa halijaibuka. Uber ilikuwa imeshafanikiwa kuji-brand kwa namna ambayo likawa ni neno linalotumika kumaanisha 'ride-hailing'. Yaani mfano wake ni namna M-Pesa ilivyojikita kiasi ambacho mtu anaweza akasema "Hivi, kuna M-Pesa karibu hapa?" hata kama anatumia Airtel Money. Ilikuwa kawaida kabisa kusikia watu wanasema “I Uber-ed here” au “should we Uber?”. Kwa kuwa Brand ya Uber imekuwa ni neno lililozoeleka zaidi, Uber ikaendelea kutamba katika vichwa vya wateja (na kwenye simu zao).

VITA INAANZA KIBABE.

Kitendo cha Lyft kuwachapa Uber kuelekea kwenye soko la hisa (IPO) ilikuwa ni ushindi mkubwa kwa Lyft ukizingatia Uber walifanya kila figisu figisu ili waizamishe Lyft. Hii ilikuwa ni baada ya Co-Founders wa Lyft kukataa kuiuza startup yao kwa Uber mwaka 2014; Uber kwa ghadhabu wakaanza kutumia makombora ya mbinu chafu kuifumua Lyft.

Kwanza walianza kwa kuajiri watu ambao walipewa 'kazi maalumu'. Watu hao walipewa simu (Na bundle za kutosha), na maelekezo yalikuwa rahisi tu kuelewa; Unaingia kwenye app ya Lyft, unaita gari - linapokaribia kufika, una-cancel.

Unarudia tena na tena. Kisha hama mtaa, ingia kwenye app ya Lyft, agiza gari - ikikaribia kufika, cancel. Rudia kama mara 30 hivi. Hama mtaa, saivi nenda Masaki, kisha ingia kwenye app ya Lyft, ita gari - ikikaribia kufika, cancel. Hama, nenda Buguruni, ukifika - ingia kwenye app ya Lyft, ita gari, ikikaribia kufika ....eeeh si ndio, cancel!!! (Nani angekataa hii kazi ukizingatia malipo ni manono!)

Ghafla Lyft wakakuta idadi ya madereva na wateja inaporomoka kwa kasi. Hawakujua sabababu mpaka walipoanza uchunguzi. Walikuja kugundua kuwa madereva walianza kuchukizwa na kitendo cha wateja wa Lyft ku-cancel order pindi tu gari linapokaribia kuwafikia. Kwahiyo, madereva wakawa wanahamia Uber. Hali hiyo ikapelekea magari yanayotumia app ya Lyft kubaki machache barabarani. Kwa uchache wa magari ya Lyft, wateja wakawa wanalazimika kutumia Uber (Nani abaki na app ambayo magari ni machache?)!!!

Uber hawakuishia hapo; wakaachia makombora mengine ambayo yalilenga kuiua njaa Lyft. Uber ilihakikisha inaminya na kuziba mianya yote ya 'Venture capital funding' ili Lyft wasipate pesa za kuendesha kampuni na hivyo wafunge biashara. CEO wa wakati huo wa Uber, Travis Kalanick alikiri kwamba alifanikisha moja kwa moja kuzuia juhudi za Lyft kupata mtaji, kwa kuwachepusha wawekezaji ambao wangeweza kuwekeza kwenye kampuni ya Lyft.

Uber ni kama walikuwa wamehodhi sehemu kubwa ya vyanzo vya kawaida vya mitaji kuanzia New York mpaka San Francisco - yaani kampuni zote za Venture Capital katika miji hii zilikuwa na 'uswahiba' na Uber. Mapema mwaka 2015, Uber ilikuwa imepata mtaji wa $2.5 bilioni katika 'VC funding'.

Hali ilikuwa tofauti sana kwa Lyft, ambayo wakati huo ilikuwa 'inatembela choki' - ilikuwa imebakiza akiba kiduchu benki ambayo ingewasukuma kwa miezi michache sana. Co-founders Logan Green na John Zimmer walikuwa katika wakati mgumu sana, na suluhisho pekee ambalo wengi walipendekeza ilikuwa ni kuifunga kampuni na kutumia pesa iliyobaki benki kuwalipa wawekezaji na kuwapa wafanyakazi wake chochote cha kupunguza makali ya maisha wakati wanatafuta ajira mpya huko kwingineko.

Lakini Green na Zimmer, walikuwa wabishi, wasiokubali kushindwa kirahisi. Walipambana mpaka wakafanikiwa kupata mtaji kutoka kwa vyanzo ambavyo Uber hawakudhani kama Lyft wangeweza kupata.

Waliishawishi kampuni ya Rakuten toka Japan, ikawekeza $300 milioni ambazo zilikuwa muhimu sana kwa wakati huo, ukizingatia walikuwa wanapumulia mashine. Muda mfupi baadae, mwanzoni mwa mwaka 2016, General Motors iliwekeza $500 milioni. Basi Lyft ikajishikilia katika pesa hizo kutoka GM na Rakuten ili wasizame na tangu hapo hawajageuka nyuma.

NANI MBABE MPAKA SASA?

Leo hii, Lyft haiko nyuma sana ya Uber huko Amerika ya Kaskazini. Lyft ilikua kwa haraka wakati ambapo Uber inapitia misuko suko ya kashfa zisizoisha wakati wa uongozi wa CEO aliyepita, Travis Kalanick. Lyft, hivi sasa, imepalilia taswira yake kama kampuni rafiki zaidi kwa wafanyakazi wake hususani madereva ukilinganisha na Uber.

Ikiwa ni kampuni ya kwanza kwenda public kati ya kampuni mbili zinazoongoza katika tasnia ya Ride-share, Lyft ingeweza kutumia mwanya wa kuongezeka kwa kundi la wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika tasnia ya usafiri.

Uber_driverless.jpg


Lyft ni kampuni ndogo inayokua kwa kasi zaidi ambapo kwa hali ya kawaida wawekezaji wangeweza kuvutiwa nayo zaidi. Lakini Uber, bado ni wababe katika tasnia ya ridesharing na inaingiza pesa nyingi katika robo mwaka kwa kiwango ambacho Lyft inaingiza kwa mwaka mzima. Pia ni ukweli usiopingika kuwa Uber umegeuka kuwa msamiati pendwa zaidi unaomaanisha ride-hailing.

Ni muhimu kuelewa kuwa wakati Uber na Lyft zinatazamwa kama direct competitors, lakini kampuni hizi mbili, kiuhalisia, zipo tofauti.

Lyft ipo laser-focused kwenye usafiri wa abiria, Amerika ya Kaskazini. Hawaoneshi mpango wowote wa kutoka nje ya North America au ride-hailing. Uber, kwa upande mwingine, ni kampuni ya usafirishaji inayojihusisha na kusafirisha vitu kutoka pointi A kwenda B duniani kote. Wao hawajali nini kinasafirishwa, kivipi au wapi hivyo vitu vinasafiri, ilimradi tu Uber ndo inahusika katika huo usafirishaji.

Muhimu zaidi, Uber imeunda platform kubwa ya food delivery - UberEats, ambayo thamani yake peke yake inakadiriwa kuwa sawa na thamani ya Lyft. Uber pia imewekeza kwenye commercial freight network (UberFreight), flying taxis (UberElevate), hospital rides (UberHealth) na bike rides (Jump).

Pia wako mbele ya Lyft katika uundaji wa magari yanayojiendesha (autonomous vehicle technology). Hii, naitazama kama barabara kuu ya kuelekea kwenye faida kwa kampuni zote mbili. Ni muhimu kutaja pia kuwa Uber ipo katika nchi zisizopungua 60 duniani, kwa mujibu wa taarifa walizoziweka wazi. Lyft ipo katika nchi mbili tu.

Licha ya Lyft kupata umaarufu fasta ndani ya miaka kadhaa iliyopita, Uber inabaki kuwa baba lao, iliyoenea zaidi na innovative zaidi. Hii ndo sababu valuation ya Uber ni mara sita ya mpinzani wake.

Hata hivyo, kama kuna kitu kampuni hizi mbili hazichekani, ni kwamba zote zinachoma (zinapoteza) mamilioni ya pesa - they are bleeding money.

Lyft ilipoteza kiasi cha $1 billion mwaka 2018 kwa mujibu wa Forbes, na Uber ikapoteza kiwango kama hicho kwa robo ya pili ya mwaka pekee. Platform zote zinalazimika kuchoma pes ili kuwapa motisha madereva na kutoa punguzo la nauli kwa wateja kwa lengo la kupata wateja zaidi. Madereva ni 70% ya gharama za uendeshaji wa kampuni hizi.

Ili waepuke uvujaji huu wa pesa wana njia moja tu; kuondoa magari yanayoendeshwa na watu na kuleta magari yanayojiendesha. Hili ni, of course, suala la kama wakitaka, na sio lini, kwasababu Uber tayari inaongoza katika hili.

Je, kampuni hizi zitajiingiza katika passenger drones pia? Kwenye Hyperloop je?... hayo sijui, lakini najua jambo moja ambalo ni uhakika; vita ya Uber na Lyft ndo kwanza inaanza. Na wahanga wa vita hii ni sisi wasafiri; itabadilisha kabisa namna tunavyosafiri.

Umejifunza chochote? Weka comment yako hapa chini na usisahau kuweka simulizi yako. Mimi.. ninashukuru.

Lyft app.jpg
 
Hiyo lyft ilitakiwa ingejipanua zaidi ingebase sana kwenye nchi ambazo uber hawajashika kasi ili wawe na sehem ambayo kwao wanajidai mfano kama kampuni za kitanzania za soda kuna mikoa ambayo pepsi ana demand kubwa sna ya wateja haswa mikoa ya Pwani,Dar, Moro na Iringa na mengine michache lakini katika mikoa hyo cocacola hajashika sna ambaye yeye demand yake ya soko ipo kwenye kanda ya ziwa saana

So nae lyft angefanya hvyo angeweza kuleta ushindani mkubwa sna upande wangu mimi mpka sasa naona uber ndio mshindi kwenye hyo biashara
 
Hyo lyft ilitakiwa ingejipanua zaidi ingebase sana kwenye nchi ambazo uber hawajashika kasi ili wawe na sehem ambayo kwao wanajidai mfano kama kampuni za kitanzania za soda kuna mikoa ambayo pepsi ana demand kubwa sna ya wateja haswa mikoa ya Pwani,Dar,Moro na Iringa na mengine michache lakini katika mikoa hyo cocacola hajashika sna ambaye yeye demand yake ya soko ipo kwenye kanda ya ziwa saana
So nae lyft angefanya hvyo angeweza kuleta ushindani mkubwa sna upande wangu mimi mpka sasa naona uber ndio mshindi kwenye hyo biashara
Sahihi kabisa, uwanja bado ni mpana. Sema kila kampuni ina mikakati yake, tusubiri kuona kama Lyft ataingia kwenye soko la kimataifa.
 
Ila ukianzisha kitu kikapokelewa vema Marekani basi jua hapo kishapokelewa na dunia yote.
 
Nondo kama hizi sisi watanzania zinatuumizaga kichwa kuzisoma, mi nimeishia aya ya kwanza.Ngoja nirudi zangu kwenye thread ya Shilole na Uchebe
 
Back
Top Bottom