Umdhaniaye Siye, Kumbe Ndiye

Mwl.RCT

JF-Expert Member
Jul 23, 2013
13,573
18,600
HIVI karibuni, mmoja wa marafiki zangu alinishauri nianze kupenda kusoma riwaya maana zina mafunzo mengi sana. Huwa nasoma zaidi vitabu vya kitaaluma na kitafiti na mara chache sana huchukua riwaya. Mwaka huu wa 2015, nimezisoma nyingi mpaka sasa kuliko vitabu vingine. Katika vitabu Kumi na Tatu ambavyo nimesoma toka mwaka uanze, vinane ni riwaya.


Mwanzoni mwa mwezi huu nilisoma riwaya ya Act of Treason: Can he take out the enemy within? Iliyoandikwa na mwandishi maarufu Vince Flynn na kupigwa chapa na kampuni ya Simon and Schuster.
Mitch Rapp mpelelezi mahiri anapewa kazi ya kupeleleza tukio la kigaidi lililofanyika ndani ya Marekani na kumlenga Mgombea Urais wa nchi hiyo Josh Alexander. Shambulizi hilo lilimwua mke wa mgombea huyo. Juujuu, shambulizi lilionekana ni kazi ya kundi la kigaidi la Al-Qaeda.


Zilikuwa zimebaki wiki mbili tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Marekani shambulizi hili lilipotokea. Mgombea Alexander alishinda kwa kura za huruma. Uchunguzi ulipoendelea, ulikuta ushahidi ambao ulishtusha. Ilibidi kukamilisha uchunguzi kabla ya Rais mpya kuapishwa.


Mgombea mwenza wa Alexander, akiitwa Mark Ross, alikuwa Seneta na mtu mwenye nguvu sana. Alikuwa akipenda madaraka na uteuzi wake wa kuwa mgombea mwenza ulitokana na ushawishi mkubwa kwa mgombea kutoka kwa watu wenye nguvu waliobobea katika siasa za Washington.


Ross alikuwa na mtandao mpana wa watu wakiwemo wenye rekodi za makosa ya kijinai. Mmoja wao Bwana Green alikuwa na makosa ya kutorosha fedha nje ya Marekani na alikamatwa na FBI na kukimbia hivyo kuhukumiwa akiwa nje. Bwana Green alitoa msaada mkubwa kwenye kampeni kupitia Ross ili apewe msamaha wa Rais.
Kawaida nchini Marekani, Rais anayemaliza muda wake hutoa msamaha kwa watu waliohukumiwa na mara kadhaa anayeingia hupendekeza majina yake kwa anayemaliza ili wapewe msamaha. Bwana Green ambaye sasa alikuwa anaishi nchini Uswiss alitegemea msamaha huu.


Siku ya shambulio kwa Alexander, Mkuu wake wa Kampeni za Urais aliyefahamika kwa jina la Keith Garret alimbadili mlinzi wa Makamu wa Rais na kumfanya kuwa mlinzi wa mke wa mgombea Urais. Pili alibadili mfuatano wa magari na kumtoa mke wa mgombea wa Urais katika gari la Rais na kumweka katika gari yake peke yake nyuma ya mgombea mwenza.


Dakika tano baada ya msafara ule kuondoka bomu likalipuka. Mlinzi Mkuu wa mgombea Urais, mwanamama aliyekuwa anakua kwa kasi sana katika CIA akawekwa kwenye wakati mgumu sana na kuwa mwisho wa kazi yake. Kila uchunguzi ukionyesha kuwa Al Qaeda wamefanya kazi hiyo na mlinzi yule jasusi wa CIA asiyejua hili wala lile kuhusu hujuma, anayeitwa Rivera alizembea kazi.


CIA walipata picha za ngono zinazomwonyesha mke wa mgombea Urais Jillian Alexander akifanya mapenzi na mmoja wa walinzi wa msafara wa kampeni. Wapinzani wao walizipata mapema lakini waliona sio vema kuzitumia katika kampeni. Hata hivyo picha hizo zilitumiwa na mpelelezi Mitch Rapp na kugundua haswa kiini cha shambulizi lile.


Uchunguzi wake ulimfikisha nchini Cyprus na kumkamata mtu aliyelipua bomu lile na baada ya mapigano Mitch alimzidi nguvu na kumtia nguvuni mhalifu huyo aliyeitwa Gazich. Uchunguzi wa nyaraka za kibenki ulimpeleka Mitch mpaka Uswisi na kuhusisha moja kwa moja Green aliyekuwa anaombewa msamaha na makamu wa Rais mteule.


Hatimaye CIA wakagundua kuwa shambulio lile lilifanywa na Makamu wa Rais mteule kwa msaada mkubwa wa Green aliyemkodi mlipuaji wa bomu. Katika kuhangaika ukweli usijulikane, Ross alianza kutumia vyombo vya habari kupaka matope CIA.


Alitumia hususan gazeti la The New York Times, mhariri wake na mwandishi wake kumpa taarifa za ndani kuwa CIA wamemkamata mtu asiyehusika katika shambulio lile. CIA hawakutetereka maana walikwisha kusanya ushahidi wote ikiwemo safari ya ghafla ya msaidizi wa Ross jijini Geneva katika kujaribu kuficha ukweli wa mambo.
Siku ya mwisho ya utawala wa Rais anayeondoka madarakani, Ross aliomba miadi ya kumwona Rais ili aweze kutoa msamaha kwa bwana Green. Mkurugenzi Mkuu wa CIA alichukua fursa hiyo kuweka sumu kwenye chai ya makamu wa Rais mteule na akafa pale pale Ikulu kwa kilichoitwa ugonjwa wa moyo.


Mkurugenzi Mkuu wa CIA alinukuliwa akisema kumwua makamu wa Rais mteule ilikuwa ni kazi bora zaidi ya kizalendo aliyowahi kufanya katika maisha yake yote ndani ya taasisi hiyo.
Wakati wananchi wote wa Marekani waliaminishwa kuwa Al Qaeda ndio walishiriki shambulio lile, uchunguzi wa CIA uligundua ilikuwa kazi ya mtu wa ndani sana, namba mbili katika Serikali mpya iliyokuwa inaingia madarakani.
Hakuna mtu mwenye akili ya wastani angeweza hata kuhisi kwamba mgombea umakamu wa Rais angepanga kumwua mke wa mgombea Urais wake.


Act of Treason ni kitabu cha aina yake. Licha ya ukubwa wa wastani, nilitumia siku mbili kukimaliza. Sikukiweka chini mpaka nilipokimaliza. Mafundisho yake ni dhahiri.

Mwandishi Zitto Kabwe
Gazeti la Raia Mwema
Code:
 http://raiamwema.co.tz/umdhaniaye-siye-kumbe-ndiye
 
Back
Top Bottom