Ulizaliwa kwa tishio, utakufa kwa tishio (Muungano).

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
Waumini wa dini ya kiislamu wakiwa ndani ya msikiti wa Mbuyuni wakionesha mabango ya kukataa Muungano wakati Sheikh Farid (hayupo pichani) akizungumza










Amir Farid Hadi Ahmed akiwaongoza mamia ya wazanzibari katika maandamano yaliofanyika jumapili iliyopita kuanzia viwanja vya Lumumba na kuishia katika viwanja
hivyo Zanzibar na kuendelea na mhadhara ambao ulipangwa kufanyika Mjini hapa












NDUGU zetu Wakiristo wanapofanya ibada za kuzika wafu, huwa wana msemo mmoja usemao, “ulitoka kwa udongo, utarudi tena kuwa udongo, udongo kwa udongo, na Mungu atakufufua siku ya mwisho”.
Maneno haya husemwa wakati padri au mchungaji anamwaga udongo au mchanga mara tatu ndani ya kaburi. Ni maneno mazito yanaoashiria asili ya mwanadamu kuwa ni kwenye udongo na kwa hiyo, tunapokufa tunarudi tena kwenye udongo.
Udongo au ardhi ni baba na mama yetu (mother earth) na ndiyo maana kuna tamaduni chache ambazo mtu akifa hutundikwa mtini, bali tamaduni nyingi huzika wafu ardhini. Hata wale wanaochoma miili, huishia kuzika majivu ili yarudi kuwa udongo.
Maneno haya nayafananisha sana na hali inayoukabili Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano tulioupenda sana na kuuenzi kwa vizazi viwili. Kimekuja kizazi cha tatu, yaonekana hautakiwi.
Ni taharuki kila mahali. Waliouanzisha hawapo; walioshuhudia wamechoka kuutetea; waliourithi hawajui thamani yake. Walioapa kuulinda wanakimbilia mabomu na bunduki kuulinda wakati waliouanzisha waliuanzisha kiungwana bila kukabana koo. Kimsingi Muungano hauna mwenyewe, inabidi urudi ulikotoka.
Jambo moja la kufurahisha tulijadili; kwamba Muungano ulianza kutokana na tishio la usalama wa mataifa yetu na sasa unataka kuvunjwa kwa tishio la usalama wa taifa letu.
Wakati ule, dunia ilikuwa katika mvutano wa Vita Baridi. Warusi na ukomunisti wakiwa kushoto na Wamarekani na ubepari wao wakiwa kulia. Si hoja ni nani hasa alikuwa kushoto au kulia, bali ikiwa mmoja kati ya hao alikwenda kulia, ni lazima wa pili alihamia kushoto haraka sana.
Dunia ikagawanyika vipande viwili, Mashariki na Magharibi, na mgawanyiko huu ukaenea dunia nzima. Ukienda hata katika nchi mmoja iwe Afrika, Asia au Amerika ya Kusini, ulikuta minyukano kati ya Magharibi na Mashariki au Marekani na Urusi.
Majina yakatungwa, wengine wakiita Vita Baridi, na wengine wajamaa na mabepari. Baadaye kidogo wakatokea wajanja fulani wakaanzisha umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote ili kuepuka mnyukano wa Mashariki na Magharibi, lakini hilo si somo langu leo hii katika makala hii.
Kipindi cha Vita Baridi, visiwa vya Zanzibar chini ya Sultani aliyechoka, vilikuwa kivutio cha mataifa ya Magharibi. Urusi na Ukomusti walitaka visiwa hivyo, na Mmarekani na ubepari wake alivitaka visiwa hivyo.
Katikati wakawapo wazee wetu Abeid Karume na Julius Nyerere, wajiuliza wapinde kulia au kushoto. Katika nchi zote mbili kulikuwa na vijana wasomi moto moto waliosomea katika kambi zote mbili. Wazee wetu ama kwa kutaka au kutokutaka kwao, wakaamua kuungana ili kuepusha au kuchelewesha tishio la nchi za Magharibi. Ulikuwa ni mchezo wa tukifa tufe wote, tukipona tupone wote.
Wakaungana. Wanahistoria wanadai muswada uliandaliwa haraka, ukapelekwa bungeni kwa hati ya dharula, na hata siku ya Jumapili, bunge lilifanya kazi kupitisha muswada huo uwe sheria.
Wana historia wanadai, lile shirika maarufu la kijasusi la CIA la Marekani lilikuwa nyuma ya msukumo huo wa dharula. Ama alishinda Mmarekani au alishinda Mrusi, si juu yetu kujua kwa sasa. Tunachopaswa tukubaliane bila kupotezeana muda ni kwamba, Muungano wetu, wa Tanganyika na Zanzibar ulizaliwa katika mazingira ya dharula kutokana na tishio la usalama wa eneo letu lisimezwe na haya manyang’au ya ama Magharibi au Mashariki.
Kama tuliyashinda au yalighairi, hilo ni suala jingine, ila ukweli unabaki, tishio la usalama lilizaa Muungano huu unaotugharimu kwa sasa.
Gharama za kuutengeneza Muungano huu ni kubwa sana. Kadhalika, gharama za kuulinda mpaka hapa tulipo ni kubwa sana. Sina hakika ni nani zaidi ametugharimu kati ya Mapinduzi matukufu na Muungano huu. Idadi ya waliokufa katika mapinduzi matukufu yaweza kujulikana, lakini waliokufa katika kuunda Muungano na baadaye kuulinda huu Muungano, tunaweza tusiijue.
Majasusi wana siri kubwa na ndiyo maana si wote wafanyao vizuri. Mpaka leo kuna familia za Wazanzibar wanauliza ndugu zao walikwenda wapi na hawatakaa wapate jibu. Iliwezekana wakati ule, mtu kupotea na kimya kikapita na lisitokee jambo.
Lakini sasa hiyo haiwezekani, na mtawala yeyote anayekusudia kuulinda Muungano kwa mtindo huo amekosea sana. Anaweza kuishia kujuta kuwa mtawala na ukoo wake waweza kujuta vizazi vingi vijavyo.
Sasa limezuka zogo kuhusu Muungano. Kalianzisha mtawala wetu kwa kupiga marufuku watu wasijadili kuwapo au kutokuwapo kwa Muungano. Akawataka wajadili rangi zake, miguu yake na mikono yake. Matokeo yake ni maasi na kufuru. Nyumba za ibada zimenajisiwa kwa kisingizio cha kukataa Muungano.
Aliyesababisha unajisi huo kaibuka na mawili: Moja kajifanya hajazuia mtu kuzungumzia kuwapo na kutokuwapo kwa Muungano. Pili, kafanya kufuru ya kuagiza polisi wajaze risasi na mabomu na kuzuia watu kukutanika. Muungano gani huu unazuia watu kukutanika?
Nilidhani watu wanakutanika na kuunganika ndipo Muungano unakuwapo! Ama kweli, madaraka yanalevya zaidi ya bangi. Tunajenga Muungano kwa kuzuia watu kuungana halafu tunajigamba kwamba watu hawakutokea kuandamana? Ni mwenyezi peke yake anayejua kuchanganyikiwa kwetu!
Tuseme ukweli. Kwa mtutu wa bunduki hatuwezi kuulinda Muungano. Kama bunduki, wanatakiwa wananchi wenyewe washike, ili waulinde Muungano wao.
Lakini serikali kushika bunduki dhidi ya wananchi walio kiini cha Muungano, ni kupoteza wakati na rasilimali zetu bure. Labda tujiulize nini kiliungana?
Kuna majibu mengi hapa. Wapo wanaodai waliungana wazee wetu Karume na Nyerere. Wapo wanaodai ni udongo ulioungana. Wapo wanaodai zilizoungana na serikali, yaani dola. Ndiyo, kuna wakati dola si watu na tumeona kwa macho yetu katika historia. Rais hawezi kuiba kisha akadai serikali imeiba. Rais si serikali kama ambavyo serikali inaweza kuwa si watu wenyewe.
Uwe muungano wa marais, udongo, au dola zetu, mwisho wa siku ni ridhaa ya watu inayoweza kuponyesha Muungano huu.
Kuna uzembe wa hatari ulitokea huko nyuma kidogo. Watu walirithi majengo ya Ikulu, wakalalia kitanda alicholalia Kambarage, kisha wakadhani na wao wamekuwa Kambarage.
Wakalala usingizi wa pono, wakaamini Muungano utajitetea. Wana Uamsho wamewaamsha kwenye usingizi, sasa wanakimbia na magobore kuwajeruhi ili kuulinda Muungano usio mioyoni.
Napenda niwape ushauri nasaha, tena wa bure. Watawala walianza na Azimio la Arusha, wakaliua. Akafuata mwasisi wake, naye akatutoka. Chama chake alichokianzisha kiko mnadani kimekosa mnunuzi hata madalali wanakikimbia.
Sasa wanataka kuunyonga Muungano kwa kuulazimisha watu waupende. Kubalini wananchi waamue wenyewe. Wakiamua kuuvunja, hiyo ndiyo njia pekee ya kuuenzi. Wakiamua kuubakiza, wataulinda wenyewe na kuukarabati.
Wakiulinda kwa bunduki, utadumu kwa bunduki na hiyo ni gharama kubwa. Tuliungana kuepusha bunduki za Wamarekani na Warusi, pengine sasa ni wakati wa kutengana ili tuepuke bunduki za wenyewe kwa wenyewe.
Nachelea kusema, hakuna msiba mbaya kama wa Mtanzania kumgeuzia mtutu wa bunduki Mtanzania mwenzake eti anaulinda Muungano. Mtutu anapaswa kuelekezewa adui wa nje anayevamia ardhi yetu. Muungano wa sisi kupigana mabomu, kunajisi mahekalu, kulishana vilivyo najisi, na kuitana majina mabaya hautakiwi na yeyote.
Wosia wangu kwa wana Uamsho, wamwache Kambarage apumzike kwa amani ya Mola wake kama wanavyomwacha Karume akapumzika na Mola wake.
Mtukuzeni Aboud Mwinyi Jumbe bila kuwakashifu hawa wazee maana walifanya kazi yao njema. Kosa lililofanyika ni kuwakabidhi vipofu na mabubu, wasiosikia wala kuzungumza. Nchi inayeyuka wao wanacheza rumba, Muungano unayeyuka wao wanajiandaa wacheze soka. Tuliungana kwa tishio la usalama, na sasa tuachane kwa tishio la usalama.


Chanzo Raia Mwema
 
Back
Top Bottom