Uliza chochote kuhusu Karagwe na Wanyambo wanaopatikana mkoa wa Kagera

Chachu Ombara

JF-Expert Member
Dec 11, 2012
5,897
10,358
Wilaya ya Karagwe ni kati ya wilaya zilizobahatika kuwa na hali nzuri ya hewa na mandhari nzuri.Wilaya hii inakaliwa na kabila la wanyambo (sio wahaya).

Ardhi ya Karagwe ina rutuba nzuri ya kustawisha migomba,kahawa,karanga,maharage,mahindi na mazao mengine mengi.

leo asubuhi karagwe1.jpg

Ukiamka asubuhi hali ya hewa asubuhi inakuwa ya ukungu na baridi sana kiasi kwamba unaweza usione mita chache kutoka ulipo.

leo asubuhi karagwe2.jpg

Udongo wenye rutuba na mvua za mara kwa mara ufanya mazao kustawi vizuri na mandhari yake kuwa ya
kijani.

Nashauri kwa wale wanaopenda kilimo basi wajitahidi sana kupata ardhi katika wilaya hii.


-----
Tunapozungumzia historia ya watu wa mahali fulani hatuna budi kuzungumzia Jiografia ya sehemu husika, hali ya hewa na mazingira , wakazi wake ,uoto wa asili ,utamaduni wao ,utawala ,mawasialiano na uchumi . Lengo la kutafuta na kuifahamu vyema historia ya watu wa Karagwe ni la msingi sana.

Lengo kuu ni kuandaa mazingira ya watu mbalimbali ili waweze kuielewa vyema historia ya Karagwe, kukusanya na kuzihifadhi zana na kumbukumbu za kimila na jadi ambazo katika siku za karibuni zinaelekea kuanza kupotea. Makala hii itachambua kwa kina historia ya kabila la Wanyambo ambao kwa asili wanatoka Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera.

CHIMBUKO LA KARAGWE NA WATU WAKE (WANYAMBO).

Jina “ Karagwe “ kutokana na simulizi za wazee wetu mbali mbali na watafiti wa historia ya Karagwe kama ( Katoke 1975; 162) inaelezwa kwamba jina hili linatokana na kilima (angalia kielelezo hapa chini) kinachopatikana Kusini Magharibi ya Makao makuu ya wilaya ya Karagwe ,kwenye kijiji cha Kandegesho ,kata ya Nyakakika ambacho mtawala ( Omukama ) wa kwanza alifanya kafara ya kwanza.

Taarifa zilizopo mtawala huyo alijulikana kwa jina la Nono ya Malija kutoka ukoo wa Basiita. Na kwamba kumbukumbu hii ya “Karagwe ka Nono “inatokana na ukweli kuwa Nono alikuwa mtawala wa mwisho wa wenyeji asilia wa Karagwe kabla ya kuondolewa madarakani na Omukama Ruhinda mtoto wa Wamara. Inasemekana kwamba Nono son of Marija alikabidhi madaraka yake bila ya misukosuko wala mapigano ya aina yoyote kwa ajili ya kuokoa watu wake waliokuwa wanakabiliwa na wimbi la njaa. Kwa kifupi hii ndio kumbukumbu yake na chimbuko la historia ya jina Karagwe.

Hiki ndicho kilima kiitwacho na kijulikanacho kama “ Karagwe “
Kielelezo ”B”

Mlima Karagwe unapakana na ziwa linaloitwa na wenyeji kuwa “ ziwa Kitete “ lenye wanyama aina ya kiboko wengi ambalo pia linapakana na hifadhi ya wanyama pori ya Kimisi. Kielelezo “C”

Cory (1949; 18) anaendelea kueleza kuwa “Ruhinda alipofika Karagwe kutoka kusini alimkuta mtawala mwenyeji aliyekuwa akiitwa Nono son of Malija wa ukoo wa Basiita. Nono hakushindwa katika vita bali alidanganywa na ujanja wa Ruhinda “.

Tafiti hii inashabihiana na simulizi za wazee wengi wa Karagwe na nchi jirani kuwa Wasiita kutokana na njaa kali iliyokuwepo wakati huo waliuza ngoma ya utawala kwa wahinda /Ruhinda na kupewa ulezi kwa ajili ya chakula na kuanzia wakati huo wakawa chini ya utawala wa Abahinda /Ruhinda .

Ruhinda alijenga Boma lake eneo la Bwehange nchi iliyo kusini ya ziwa lililoitwa Speke “The little Windemere” na baadae kuhamia Bweranyange, mahali palipo karibu na uwanda wa juu penye mteremko wa vilima vinavyozunguka ziwa. Hapa ndipo watawala wote waliopotawalishwa hadi walipofika wadachi.

Birigitta Farelius 2008 katika utafiti wake anasema “ Popote unapokuta ng’ombe machungani katika Afrika ya Mashariki macho huvutiwa sana na ndege weupe (white cow herons ) wajulikanao kama Nyange Nyange , nao watu wa Karagwe huwaita Enyange ,wakifuatana na ng’ombe na kazi yao kubwa husaidia kudonoa kupe na wadudu wanashambulia mifugo.

Ndege hawa hupendwa na wenyeji kutokana na tabia yao ya kutoa huduma kwa mifugo yao tofauti na ndege wengine waharibifu wanaoshambulia mazao, hawa hawana madhara ya aina yoyote. Makao makuu ya Omukama Rumanyika wa Karagwe yalikuwa katikati ya makundi ya wafugaji na kulikuwepo na ndege hawa wengi na hivyo kupewa jina la Bweranyange kutokana na ndege hawa kupenda kutanda eneo hili muda wote “.

Na hili linathibitishwa na simulizi za wenyeji wa eneo hili ambao wengi walikuwa wafugaji, na sisi pia tunalazimka kukubaliana na matokeo ya utafiti huu unaonyesha chimbuko la jina la Bweranyange wakiwa na maana sehemu safi na nyeupe (makao makuu ya mtawala wao) kutonana na umaarufu wa ndege hawa.

Ni kutokana na ukweli huu wenyeji walitunga wimbo maarufu wa kumsifia mtawala wao ,na kwa mtawala halisi na makini kama alivyokuwa Omukama Rumanyika alitakiwa kuwa na roho nyeupe ya upendo kwa watu wake na wimbo huu ulikuwa unaimbwa popote pale alipotembelea na kulala . Wimbo huu uliwaasa na kuwaonya wananchi kuwa wasikivu, wastaarabu, wenye kufuata kanuni, sheria na kutokuwa wasumbufu kwa mgeni wao aliyewatembelea.

Mtayomba mwalirwa enyange ……….
Mtayomba …………………………….
Ne enyange ti nyange …………………
N’omwana ‘womuntu ……………..
Mtayomba …………………………..
Leba no omwana wo omuntu ……….
Mtayomba ………………………….

Hapa ndipo ilipokuwa makao makuu ya watawalala wa Karagwe, Bweranyange ambayo yamebaki magofu.

Kielelezo “D” Mabaki ya majengo ya Bweranyange

“The little windermere lake “ Kama lilivyobatizwa na John Hanings Speke linavyonekakana toka makao makuu ya Bweranyange

Kielelezo “E”

Taarifa za Utafiti huu unashabihiana kwa karibu sana na ule wa Bwana HALLEY katika kitabu chake cha “An African Survey “ ukurasa 23/24 “ akielezea kwamba kaskazini magharibi ya ziwa Victoria ‘’ Watu wa makabila ya Waganda ,Wanyankole , Watoro ,Wanyoro na makabila manane ya wilaya ya Bukoba katika Tanganyika na Ruanda (Nchi ya udhamini ya ubeligiji) ni mchanganyiko wa makabila ya wenyeji wakulima wabantu na makabila ya wafugaji wa kihima toka kaskazini ambao yasadikiwa kwamba yalizishambulia nchi hizo zama za miaka mia tatu iliyopita na kuwashinda wenyeji wake . Katika falme hizi wafugaji wa ng’ombe waitwao wahima mpaka sasa ni jamaa wa watawala”.

Wakaazi wote wa Karagwe walimtegemea Omukama kwa ushauri na ulinzi. Alitoa maelekezo katika masuala yote muhimu kuhusu maeneo ya Karagwe. Pamoja na kuwepo kwa makabila lukuki Wilayani Karagwe; hatimaye iliwezekana kuanzishwa kwa Umoja wa Karagwe ambao uliwezesha makabila yote kukaa pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya kijamii.

Kuanzishwa umoja wa Karagwe na utawala (Kingship) uliwezekana kwa wakati huo kutokana na mambo makuu yafuatayo;
Kuongezeka ka idadi ya watu kutokana na mapinduzi ya kilimo
Uongozi bora uliooneshwa na mtawala “Omukakama” na
Ongezeko la wahamiaji kutoka Bunyoro ambapo walikuwa wanalazimika kukimbia mapigano na uvamizi wa watu toka maeneo ya kaskazini.

Kuwepo kwa mchanganyiko wa makabila mbali mbali katika Karagwe unaanzia karne ya 18 ambapo Stanley (1876) anaripoti kuwa “in Karagwe there were Wanyambo, Wanyarwanda, Wasuwi, Wanyamwezi, Arabs, and Swahili, as observed at the court of King Rumanyika .

Taarifa hii inatuonyesha kuwa Karagwe na Kyerwa toka zamani hadi leo imekuwa ni kisiwa cha utulivu na amani. Ni kutokana na kuwepo kwa utulivu na amani hii, kumekuwepo na mwingiliano wa makabila mbali mbali. Aidha; kutokana na sababu mbali mbali zilizowakabili majirani kama ukame, njaa ,matatizo ya kiuchumi na kisiasa , na wakati mwingine mapigano ya koo na kabila yamesababisha watu wengi kutoka makabila tajwa kuhamia Karagwe . Hivyo, Karagwe na Kyerwa kwa sasa pamoja wenyeji wake (Wanyambo) wanaishi na watu wa makabila mbali mbali kutoka ndani ya nchi na wengine kutoka nchi jirani za Rwanda, Burundi na Uganda.

Leo hii ukitembelea kijiji cha Kafuro katika kata ya Nyabiyonza utaona mwembe mkubwa ulipandwa na kuachwa na wafanyabiashara wa kiaarabu waliofika Karagwe katika karne ya 18 kwa ajili ya biashara ya kubadilisha pembe za ndovu na bidhaa nyingine.

Huu mti wa mwembe uliopandwa na Waaarabu katika karne ya 18 katika kijiji cha Kafuro

Kielelezo “F”
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa wakati Omukama Rumanyika Orushongo anaingia madarakani, Karagwe ilikuwa tayari imekua kiuchumi kiasi ambacho wafanyabishara toka maeneo ya mbali walikuwa wameanza kuingia Karagwe wakifanya biashara ya meno ya tembo, mazao ya chuma (Iron products) kama vile visu, majembe na vitu vingine wakibadilishana na bidhaa waliyoleta toka maeneo waliyotoka.

Mwishoni mwa karne ya 18 na mwanzoni mwa karne ya 19, habari za kushamili
kwa Karagwe kutokana na biashara zilikuwa zimesambaa sehemu mbalimbali za nchi ya Tanganyika pamoja na nchi za jirani za Rwanda, Kongo, Uganda, Burundi na hata nchi za Falme za Kiarabu. Wakati huo Karagwe ilikuwa imekwishatembelewa na wajasiliamali toka Unyamwezini na Usumbwa ambao walileta chumvi toka Uvinza na chuma toka Katanga (nchini Kongo) .

Hili linathibitishwa na msemo wa kinyambo wa muda mrefu unaosema “Omwonyo ngunula, chonka Omushumbwa nanunka”kwa kiswahili maana yake ni kwamba chunvi yao ni tamu pamoja na kwamba wachuuzi wenyewe wanatoa harufu mbaya ya jasho tokana na safari yao ndefu.


Inaaminika pia kwamba Wanyamwezi walifika Karagwe wakiwa watu wa kwanza kufanya biashara na kwamba walileta chumvi, visu, pilipili,na matunda kama vile maembe, machungwa na mtama kabla ya Waarabu kuingia ambao walijenga Kituo chao maeneo ya Kafuro na Kitengule.

Shughuli za Kisiasa, biashara na watu wa mbali (Tabora na Pwani) ilianzisha na kujenga mahusiano mazuri na watawala (Abakama) wa Karagwe, kiasi kwamba Omukama Rumanyika I wakati huo alilazimika kumteua msadidizi wake « Kiyango kya Mpiga Ifumula Bikungu « kuwa Balozi wake katika tawala za jirani zake ambaye wakati huo alikuwa akisafiri kati ya Bweranyange, Buganda, Bunyoro, na Tabora.Kazi kubwa ya mteule Kiyango kya Mpiga Ifumula Bikungu ambaye unaweza kumuita kama balozi ilikuwa ni kufanya mawasiliano na kuimarisha kati ya Mtemi Rumanyika na watawala wa sehemu hizo.

Balozi huyu alionekana kupata sifa nyingi za utendaji kazi, sifa ambayo ilitolewa wazi wazi na wageni kama Captain John Hanings Speke na Grant (katika kitabu chaek kiitwacho The jouney of discovery of River Nile ) walipozuru Karagwe. Ilikuwa ni kupitia kwake wageni hawa waliweza kupokelewa na watawala ikiwa ni pamoja na Omukama Rumanyika bila matatizo yeyote.

Haya yanathibitishwa na mzee wetu marehemu Profesor Katoke (1975;55) ambaye aliandika “ Ikumbukwe kuwa Speke na Grant walipata upinzani mkubwa katika sehemu zingine za Kigoma na Tabora ambapo waliingia bila kuwasiliana na Kiyango, waliweza kuzuiliwa kwa muda na wakati mwingine kutozwa ushuru mkubwa na watawala wa maeneo hayo wakiwa safarini kuelekea Karagwe “. Hii inathibitisha umuhimu wa Balozi huyo Kiyango cha Mpiga Rufumura Bikungu.

3.JE , WANYAMBO NI WATU WA AINA GANI?

Neno “Wanyambo “hakuna mtu mwenye uhakika na mwenye kutoa maelezo mazuri ya kuridhisha kuwa linatokana na nini au lina maana gani. Katoke (1975;7 ) anaeleza katika utafiti wake kuwa zipo simulizi mbali mbali mbali kuwa wanyambo wanatokana na kizazi cha “Kanyambo” ,mtoto wa “ Ruhanga “ambaye alitumwa kuanzisha nchi ya Karagwe toka Bunyoro .

Hivyo ,watoto na vizazi vyake ndani ya Karagwe kuitwa wanyambo , na kwamba kabila hili limegawanyika katika makundi ya wakulima na wafugaji. Pia , wapo watu wanatoa simulizi huko Bunyoro (nchini Uganda ) kuwa mababu zao walizaliwa kutoka Karagwe . Aidha, ipo aina ya ndizi asilia inaitwa “enyambo” na ng’ombe asilia mwenye pembe fupi aitwaye “ente ye enyambo”

Lakini, watafiti wengine kama Birgitta (2008) na wengineo wanaeleza kuwa neno “Wanyambo “linatokana na jamii ya “Abaragwe” waliohamia Ankore toka Karagwe miaka mingi iliyopita. Inaaminika kuwa watu hawa ambao walikuwa wabantu waliongea lugha ya “Oluragwe” na kwamba lugha hii imepotea kutokana na mwingiliano na mchanganyiko wa lugha toka katika makabila mbali mbali yaliyoingia Karagwe na kutengeneza kinyambo cha sasa kinachozungumzwa na wanyambo wa Karagwe .

Ni kutokana na kukinzana kwa maelezo ya tafiti hizi tunapenda kuamini kuwa hakuna mtu mwenye maelezo mazuri ndani ya karagwe au nje Karagwe mwenye kuelezea bila ya mashaka yoyote kuhusu neno “Wanyambo” linatokana na nini au chimbuko lake halisi ni nini.

Hata hivyo hatuna budi kukubaliana na Birgita Farelius (2008; 35-38 ) katika utafiti wake ambaye anasema yafuatayo nami bila kupotosha nanukuu “ To the South of Ankole, the people of Karagwe in the former Tanganyika were placed under the heading of the “Haya” in for example Audrey Richard’s Volume on East African Chiefs (1959;174-194) .The Bahaya proper were basically fishing people whom the first Europeans had found along the Lake Victoria .

However, it was recognized that the Inhabitants of Karagwe ,the Banyambo were not to be “ considered as pure Bahaya because of their strong Rundi element ,also in their language “ (Cory 1949;13). In principle Karagwe can be termed as free state from Bukoba and is separated from the Bukoba area “in terms of geology ,climate ,vegetation ,population density and economy” (Schmidt 1978;12) quoting the 1988 population census that , the figure for Karagwe was 292.589 people ,while Bukoba Urban and Rural including Muleba had 665.412 inhabitants.

Moreover, In the Kingdom of Buhaya power evolved around the ownership of cultivated land; while in Karagwe power evolved around cattle ownership (Katoke 1975;36 , Anacleth and Ndagala 1981; 154) . In the Nyarubanja land tenure system in the Buhaya, the kings could confiscate banana plantations and then confer them in his favourities or relatives .And the original occupants, who could have been clan heads, were allowed to stay on as tenants, the landlords enjoying the tribute from their labour. Again, this system did not exist in Karagwe (see for example Cory and Hartnoll 1945;123-124 and Ishumi 1971;724).

Naye Bishop J. Kibira (1974; 11) as quoted by Birgita (2008 ) says, for the purpose of colonial administrative expediency, Karagwe was categorized as part of Buhaya “tribe “under Bukoba district, although their socio –economic structures, their culture and their language differ. In fact Buhaya and Karagwe have been characterized as “almost two different countries in one region”.

The Luhaya spoken by the Bahaya and the Runyambo of the Banyambo in Karagwe are treated as dialects of one language belonging to Rutara group of Great lakes Bantu Speakers. But, Bashungwa (1988) , a Mnyambo linguistic in his research does not support this conclusion, but suggests that there is a closer affinity between Runyambo and Runyankole than Runyambo and Ruhaya .

Moreover, Karagwe and Buhaya traditionally had different political systems; the kingdom of Karagwe ,which the colonialists found in place ,had more in common with Nkole than with the Buhaya Kingdoms.

Kwa tafsri yangu napenda kuamini kwamba wakoloni kwa sababu za kiutawala waliunganisha (Wanyambo) toka Karagwe na (Wahaya) toka Bukoba na wote kuitwa “Wahaya” ili kurahisisha utawala wao walipoingia nchini Tanzania. Lakini ,ni ukweli usipingikika kwamba Wanyambo wanaopatikana katika wilaya ya Karagwe na wahaya toka Bukoba wanatofautiana sana kutokana na asili yao , shughuli za kiuchumi ,kijamii , Mila na desturi , mazingira , na lugha zao kama tafiti hapo juu zinavyoeleza . Aidha, Kinyambo kutokana na tafiti hapo juu kinashabihiana zaidi na Kinyankole kuliko kihaya.

Hata hivyo ,jamii ya watu wanaoishi katika wilaya ya Karagwe kwa sasa ina mchanganyiko wa makabila mbali mbali kama vile wanyambo ,wahaya ,wasubi ,wanyarwandwa ,wanyankole ,warundi ,wazinza ,wahangaza n.k .Kwa mbali na historia wanyambo ni watu wakarimu sana na wanaopenda kuishi na watu toka makabila tofauti bila ubaguzi.

UTAWALA NA WATAWALA WA Karagwe

Kama ilivyokwishaelezwa hapo juu mtawala wa kwanza wa Karagwe alijulikana kwa jina la Nono ya Malija , Ruhinda alipofika Karagwe kutoka kusini alimkuta mtawala huyu mwenyeji ambaye alilazimika kuachia madaraka yake na kumpisha Omukama Ruhinda ili kuokoa watu wake waliokuwa wanakabiliwa na njaa wakati huo.

Ruhinda baadae alijenga Boma lake eneo la Bwehange eneo lililopo kusini mwa ziwa Kajunju ambalo baade lililobatizwa na Bwana Speke “The little Windemere” akiwa na maana ya kuwa lilifanana sana na ziwa Windemere linalopatrikna nchini Uingereza ,na baadae Omukama Ruhinda aliweza kuhamia Bweranyange, mahali palipo karibu na uwanda wa juu penye mtelemko wa vilima vinavyozunguka ziwa hili .

Hapa ndipo watawala wote waliofuatia waliopotawalishwa hadi walipofika wadachi. Inaelezwa kuwa hakuna msukosuko mkubwa uliotokea wakati wa utawala wa Omukama Ruhinda, na inasemakana alitawala watu wake kwa haki na utulivu kwa miaka mingi.

Omukama Ruhinda alirithiwa na mwane Ntare mwaka 1800, wakati huo kulitokea mashambulio ya Wanyoro katika Karagwe na kwa vile Omukama Ntare alikuwa bado mdogo alikimbia na mama yake, akabaki wakili wake ambaye pia aliuawa na Wanyoro. Baadae wanyoro walishambuliwa na ugonjwa mbaya ambao unasemekana kuwa ulitokana na uchawi wa Ntale aliopewa na Mfalme wa Uha (Buha –Kigoma) na wakati anarudi na mama hakukuta mnyoro hata mmoja kwani wale ambao hawakufa walikimbia kwa woga.

Mfalme Ntare alifuatiwa na Ruhinda VI ambaye maisha yake yalikuwa marefu sana hata mwisho watu kuamini kwamba hatakufa. Omukama Ruhinda VI aliamua kujiua mwenyewe ili kumpisha mwanae Ndagara ili atawale , Ndagara alikuwa shujaa wa vita alipigana vita na Kiziba ,Kyamtwala na Ihangiro .Hakuna ushahidi wa kutosha lakini mara zote simulizi za wazee wanyambo husema Ushindi katika vita hii ulikuwa wa kwao!!.

Ndagara alikufa mwaka 1855 na mwanae Rumanyika alitawazwa kuwa mfalme wa Karagwe kabla ya kukutana na Bwana Speke mwaka 1861.

Watawala wengine waliotawala Karagwe walikuwa kama ifuatavyo;

Ruhinda I
Ntare
Ruhinda II
1550 Ntare II
1575 Ruhinda III
1595 Ntare III
1620 Ruhinda IV
1645 Ntare IV
1675 Ruhinda V
1700 Rusatira
1725 Mehiga
1750 Kalemera
1775 Ntare V (Kiitabanyoro)
1795 Ruhinda Orushongo
1820 Ndagala I
1853 Rumanyika I
1883 Kayenje Kalemela
1886 Ndagala II
1893 Ntare VI
1916 D.Rumanyika II
1939 B.I.Ruhinda VII –The last Muhinda ruler of Karagwe
1963 End of political power of traditional rulers in Tanzania.

Chifu David Rumanyika II

Omukama Bernado Itogo Ruhinda VII aliyetawala kuanzia mwaka 1939

5. TARATIBU ZA KUMWEKA MTEMI (OMUKAMA ) MADARAKANI.

Kabla sherehe ya kutawazwa Omukama kuanza ilikuwa ni jukumu la mmoja wa watu wa ukoo wa ”Abasindi” kuandaa ,kusafisha na kuhakikisha zana zote zilizotakiwa kutumika katika sherehe za kutawaza mtawala zinawekwa tayari. Wakati ukifika Omukama mtarajiwa alikaa katika viganja vya mmoja katika watu wanaotoka katika ukoo wa ”Abakaraza” .

Huyu mara zote alikaa karibu na kiti cha Omukama ambacho kilikuwa kimetengenezwa kwa shaba ( kigoda hiki kilichukuliwa na wajerumani hadi leo hii hakijawahi kurudishwa). Sherehe hizi za kumtawaza mfalume ziliendeshwa na mjumbe toka ukoo wa Abasindi. Alichukua fito ndogo (Emiziyo) na kumkabidhi Omukama mtarajiwa ambaye aliombwa kupiga ngoma.

Kitendo cha kupiga ngoma ikatoa sauti kiliashiria kuwa sasa ni mtawala rasmi mwenye uwezo wa kuongoza na kutoa maamuzi ya nchi iliyo mikononi mwake , anakuwa na uwezo wa kuita watu kwake kwa kutumia ngoma na kuwaamrisha kufanya lile atakalowambia .

Aidha ,mtawala alikabidhiwa upinde na mishare , mkuki na ngao ikiwa ishara kwamba analo jukumu la kulinda na kutetea kiti chake na watu wake. Baada ya kupiga ngoma na kukabidhiwa zana za ulinzi ,alikaa katika kigoda cha utawala kilichokuwa kimetengezwa kwa shaba tupu (Copper Royal stool).

Wakati haya yakitendeka mtu toka ukoo wa ”Omukaraza ” atakuwa amesimama kushuhudia Mtawala mpya akitawazwa na kula kiapo cha ofisi mpya. Huyu angeweza kufananishwa kama mama au baba wa ubatizo katika ubatizo wa kikristo (i.e Christian baptism).

Baada ya kutawazwa Omukama alipelekwa mtoni sehemu iliyojulikana kama ”Mwogamarinzi” ili kumalizia sehemu ya mwisho ya sherehe za kumweka madarakani mtawala .Sehemu hii ipo katika pango kando kando ya ziwa lijulikanalo kama Lweru rwa Bijunju. Alichukua mkuki wake na kuvaa sandals (Enkeito) na ngozi ya mnyama. Alipofika katika eneo hili alizamishwa kwenye maji kwa ajili ya utakaso na kusafishwa , wakati wote eneo hili takatifu lilitunzwa na mtu mmoja tu toka ukoo wa ”Abasabya” ambao walikuwa wakiishi eneo hilo wakilitunza .

Wakati akioga /anasafishwa mtu mmoja toka ukoo wa ”Abasabya” aliuwawa na damu yake kuwekwa kwenye mto wa maji haya yanayotumika kumuosha Omukama .

Damu hii iliyomwagika katika mto huu wakati mtawala huyu anatakaswa ilikuwa na maana zifuatazo;-
Kumsafisha Omukana awe safi (mtakatifu)
Kudhihirisha kuwa Omukama kuwa sasa ana uwezo wa kutoa hukumu ya kifo kama ataona kuna sababu za msingi za kufanya hivyo.

Baada ya hapa sherehe ziliendelea siku nzima na jioni Omukama na watu wote waliongozana wakirudi Ikulu ambapo alikuja kufanya mambo ya mwisho kwa siku hiyo . Alipofika ikulu yake alisimama mbele ya nyumba aliyojulikana kama ”Kajumilo” , kama utaratibu ulivyokuwa alitumia nafasi hii kama sehemu ya ibada ya kuombea nchi yake amani , kuwakemea na kuwalaani watawala wa nchi jirani wenye mahusiano mabaya na nchi yake . Pia , aliwaombea majirani zake wenye mahusiano mema na nchi yake ya Karagwe kuendeleza mahusiano mema na utawala wake .

Katika hatua nyingine ya mwisho katika kukamilisha utaratibu , Omukama alipewa mbegu na watu wa ukoo wa ”Abaitila” ambazo alizitupa kuonyesha kila kona ya Karagwe wakati huo akitoa maneno ya baraka .Aliombea nchi yake neema ya kupata mvua za kutosha , rutuba ya ardhi na ya utu, amani na mshikamano. Katika maombi haya alisaidiwa na mtu maalum ambaye alimpatia dawa iliyosadikiwa kuwa na nguvu maalum inayomsaidia Omukama katika maombi yake. Baada ya kukamilisha ratiba hii Omukama aliondoka na kurudi katika Ikulu yake kwa mapumziko .


MAHAKAMA ZA JADI – KARAGWE .

Mahakama ni chombo muhimu kwa serikali yoyote hapa duniani . Kazi kubwa ya mahakama ni kuhakikisha kwamba sheria za utawala /nchi zinafuatwa na kutekelezwa ipasavyo. Kila Mahakama ina wajibu wa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata haki yake ilivyo kisheria. Vivyo hivyo nao wananchi hawana budi kutekeleza wajibu wao kisheria ,maana hakuna haki bila ya wajibu.

Utawala wa watu wa Karagwe ulikuwa na mahakama ya jadi na utaratibu wake wa kuhakikisha kila mtu anapatiwa haki yake .Aidha ,kabla ya ujio wa wakoloni malalamiko na madai mbali mbali yalisikilizwa na kutolewa uamuzi kupitia mahakama za jadi. Utaratibu huu ulikuwepo hata wakati wa mtawala wa kwanza wa Karagwe aiyeitwa Nono ya Malija .

Kuondolewa kwa utawala wa asili wa wabantu na kuingia kwa utawala wa Bahima kulileta utaratibu mpya wa kutatua migogoro na mashauri katika jamii . Baadhi ya migogoro iliyokuwa inatatuliwa ndani ya koo na mfumo wa vijiji ilibadilishwa na kuelekezwa kwa mtawala mpya, kwani utawala mpya ulikuwa umehaidi kutenda haki na kutoa ulinzi kwa kila mwananchi.

MAHAKAMA ZA JADI ZILIVYOFANYA KAZI .

Ni kwamba mashauri madogo madogo yalikuwa yanatatuliwa na wanaukoo au wanakijiji husika. Kwa mfano mashauri mgogooro wa mali kati ya wanafamilia yalitatuliwa na baba , na kama mgogoro unahusu ukoo ingewezekana kusikilizwa na kutatuliwa na na mkuu wa ukoo.

Iwapo shauri ,kwa upande mwingine ,linahusisha watu wa koo mbili tofauti ,lakini toka kijiji kimoja ,shauri hili lilikuwa lilisikilizwa na kutolewa uamuzi na viongozi wa kijiji (Abakungu) ambao walikuwa wakichaguliwa kwa kuzingatia uwezo na busara zao.

Shauri lililowahusisha Wahima na Wanyambo asilia lilisikilizwa na mwakilishi wa Omukama aliyejulikana kama “Omukungu” kiongozi wa kijiji au Omulagilwa (msaidizi wa Omukungu). Vyombo vyote hivi vilikuwa na uwezo wa kusikiliza na kutatua mashauri ya madai tu.

Mashauri ya jinai yalikuwa yanasikilizwa na Omukama mwenyewe au mtoto wake aliyemchagua mwenyewe kufanya kazi hiyo kwa niaba yake.

Adhabu zilitolewa kulingana na mazingira ya hali ya kila kosa na ukubwa wa kosa lenyewe .Iwapo kosa linahusu mauaji mali ya marehemu walipewa ndugu zake, mkosaji alitobolewa /kutolewa macho au mshtakiwa kutupwa kwenye korongo refu kwenye mwamba lililokuwa jirani na makao makuu Bweranyange lililojulikana kama “Rwebagira “. Rwebagira ilimaanisha sehemu inayochinja yenyewe, au mahali pa kutekelezea huku ya kifo kwa mkosaji aliyekuwa amehukumiwa adhabu ya kifo.

Sehemu hizi za kutekelezea hukumu ya kifo “Rwebagira” zikuwa zimetengwa kwa jinsi , ilikuwepo sehemu ya kunyongea wanaume na ile ya kunyongea wanawake waliopatikana na makosa ya jinai na wasichana waliopata mimba nje ya ndoa.

Kesi za kujeruhi kwa kutumia mkuki, upinde na mishale, mali za mshtakiwa zilitaifishwa na nusu kuchukuliwa na OMUKAMA. Mwanaume alikuwa anaruhusiwa tu kuua mwanaume yoyote akimfumania akifanya zinaa na mke wake maana zinaa ilisemekana na kuaminiwa kuwa ingeleta mikosi kwa mhusika mwenyewe na nchi kwa ujumla. Watuhumiwa waliopatikana na makosa ya wizi walipewa adhabu ya kukatwa mikono yao ili wasirudie na iwe fundisho kwa wengine ambao walikuwa na mawazo ya aina hiyo.

Amri ya kuua mtu ilitolewa na Omukama pekee. Aidha , ukoo wa Abayango ni ukoo pekee ambao viongozi wake wangeweza kubatilisha amri iliyotolewa na Omukama . Birgitta Farelius (2008; 178) anathibitisha hili katika utafiti wake anaposema ” There was only one clan in Karagwe ,whose officials had the power to reverse an order given by the King .If the king gives an order to kill some one nobody else but an official of the Bayango clan could ask the king to forgive the victim.” Na hii ilitokana na imani kwamba ngoma ya utawala mzimu wake ulikuwa “Muyango” , hivyo aliwathamini Wayango kuwa sehemu ya utawala wake .

Aidha , Watuhumiwa wote wakati wakisubiri hukumu zao walipelekwa na kuhifadhiwa katika kisiwa kilichojulikana kama “Kazingaine “ kinachopatikana katika Ziwa Kajunju karibu na yaliyokuwa makao makuu ya Chifu (Omukama) Bweranyange .
Mtuhumiwa alipohukumiwa adhabu ya Kifo alipelekwa na kurushwa akiwa amefungwa kamba kwenye mwamba mkali ujulikanao “Rwebagira “ ili afe .

Chini ni picha ya mwamba huu kama unavyoonekana hadi sasa.

Huu ndio mwamba “Rwebagira “mahali palipotumika kunyongea wahalifu wa makosa ya jinai kama panavyoonekana tokea upande wa pili.

UTARATIBU WA MAZISHI YA OMUKAMA ALIPOFARIKI.
Chifu (Omukama) wa wanyambo alipofariki ( hawakutumia neno kuwa kafariki bali walisema ”Omukama yataha”kwa maana ya kwamba amerudi alikotoka) mwili wake ulishonwa kwenye ngozi ya mnyama (Pundamilia) na kuwekwa kwenye mtumbwi ambao ulijazwa maziwa na kupelekwa katika Ziwa Kajunju ambapo alikaa kwenye maji kwa muda wa siku 3 hadi 4 ,wadudu watatu walitolewa katika mwili wake na kukabidhiwa kwa mrithi wake(inasadikiwa kwamba wadudu hawa mmoja aligeuka simba aliyetoa ulinzi kwa Omukama, wa pili chui na tatu fimbo ya utawala) na baadae mwili ulipekwa makaburini sehemu iliyojulikana kama Kahwela .

Hapa mwili uliweka na kujengwa nyumba juu yake ,wasichana 5 na ng’ombe 10 walitolewa kafala ambapo walifungiwa katika nyumba hiyo na kufa kwa njaa . Tendo la mazishi ya Omukama lilijulikana kama ”O’kubyarila”. Shughuli ilifanyika kwa siri sana na ukoo mmoja tu ndio ulihusika na shughuli zote za kuzika mwili mtawala (Omukama ) . Inaaminika ukoo huu ni ule wa ”Abahunga” ,ambao baada ya shughuli hii ya mazishi hawakuruhusiwa kuongea chochote juu ya shughuli hii na kila mmoja alirudi kwake bila kupita tena makao makuu ya mtawala ili wasije kutoa siri.


KUKUA KWA TEKNOLOJIA YA KUFUA CHUMA KATIKA WILAYA YA KARAGWE.
Wanyambo walikuwa wakijua kufua vyuma (to melt and forge iron ) toka zamani kabla ya utawala wa Wahinda /Wahima katika Karagwe . Waliweza kufua na kuchonga vyuma kutokana na mawe maalum yaliyokuwa yakijulikana kwa lugha ya wenyeji kama “Obutale “(The white stones) . Kazi hii ilikuwa inafanywa na watu wa ukoo wa Abasindi. Na hawa zamani waliishi katika vijiji cha Kibondo, Nyabiyonza karibu na Bweranyange. Makundi mengine ya wafua vyuma yalipatikana katika maeneo ya Nyakabanga, ambayo pia sio mbali sana na Bweranyange .Na pia katika maeneo ya Igurwa, na Kayanga sehemu za Nsheshe.

Mawe makubwa “Obutale” yaligawanywa na kupondwa katika vipande vidogo vidogo na kuchemshwa kwa moto mkali hadi kuyeyuka. Chuma iliweza kutengenezwa tokana na uji uji ulioyeyushwa na mabaki yaliachwa kupoa yenyewe katika umbo la kifaa kinachotakiwa. Katika kazi hii waliweza kutengeneza bidhaa kama vile majembe, visu, vijiko, mikuki n.k
Historia inaonyesha kwamba kukua kwa tekinolojia katika Karagwe ilianza miaka mingi iliyopita. Cory (1949;128) akiwanukuu wageni mashuhuri waliwahi kuzuru Karagwe katika karne ya 18 kama T.A. Grant , H.M.Stanley na R.de Z .Hall ;” A Tribal Museum at Bweranyange “ Tanganyika Notes &Records , anasema “ katika nyumba ambayo haitilafiani na nyumba ya kawaida kwa ndani vimewekwa vitu vya kushangaza na kupendeza ambavyo vyaheshimiwa sana na watu wa Karagwe .Navyo ni pamoja na ;-

Ngoma tano zisizo na ngozi ,zilizotengenezwa kwa shaba ; kila moja na mkono wa bangili za chuma zilizofungwa na mikanda na misumari kwenye ngoma .Ngoma mbili zina kimo cha futi mbili na inchi sita kila moja .

Hii ni moja ya mabaki ya ngoma zilizopatikana katika ikulu ya Bweranyange iliyotengenezwa kwa shaba.

Mikuki saba ,ambayo miwili na ina mipini ya chuma na makali ya shaba ,minne mingine ina mipini ya miti na makali ya chuma ; miwili kati ya hiyo ina makali pande nne na moja ina umbo la jembe ,na wa saba ni chuma tupu; mpini wake umetengenezwa kama mlija .

c) Sampuli nane za chuma zipatazo urefu wa inchi sita mifano ya ng’ombe mmoja zilizogeuzwa chini na watatu wenye nundu.
d) Magudulia mawili na midumu mingi iliyovunjika iliyotengenezwa Udachi.
Wanyambo wanaamini kuwa Ndagara alileta baadhi ya zana hizi toka Bunyoro na nyingine nyingi alizitengeneza mwenyewe katika shimo alilokuwa akilitumia kwa shughuli ya kufua vyuma. Inasemekana kwamba Omukama Ndagara alifanya kazi yake kwa siri na majira ya usiku. Na aliweza kutengeza baadhi ya vifaa vilivyokuwa vinaonekana Bweranyange kama ilivyoelezwa hapo juu. Ni bahati mbaya sana kwamba alikuwa na usiri sana kiasi kwamba hakuweza kurithisha utalaamu huu kwa watu wengine na inasemekana kuwa hata wale waliokuwa wakimsaidia kazi hii ndani ya shimo aliwapofua macho na wengine kuwauwa ili wasitoe siri ya utalaamu huu.


KUFIFIA KWA UMAARUFU WA UTAWALA WA KARAGWE (The Decline of Karagwe Kingdom).
Inaonyesha kwamba utawala wa Karagwe ulianza kuyumba mara baada ya kifo cha Rumanyika I. Cory (1949; 32- 34) anasema tangu wakati huo historia ya Karagwe imekuwa hafifu na uhafifu huo umekuwa ukiendelea mwaka hadi mwaka. Anaeleza sababu kubwa zilizochangia kuwa kwanza wafalme wote wa wakati huo walikufa wakiwa bado vijana ,na mawakili waliochaguliwa manaibu wa warithi wao wadogo walikuwa wabaya sana hata yakawepo mabadiliko mengi; pili maradhi mengi yalitokea kwa nguvu sana yaliyoua watu na ng’ombe kwa wingi sana . Mwishoni mwa mwaka 1889 ugonjwa wa sotoka (Rinderpest) uliwaingilia sana ng’ombe katika wilaya ya Karagwe hata mwisho badala ya kuendelea kuwa nchi tajiri sana ya mifugo ikawa maskini.

Jinamizi hili liliwafanya wahima waliokuwa na mifugo ambao walikuwa hawajapata hasara kuikimbia Karagwe wakiwa na mifugo yao kuelekea Kiziba, Kianja na wengine walihamia Rwanda, Burundi na Ankole.

Pia, kufifia kwa umaarufu wa Karagwe ulichangiwa na utawala wa vibaraka waliowekwa na wakoloni mfano Kyobya toka Bukoba na Kaketo toka Bunyoro nchini Uganda. Kyoba aliitawala Karagwe kwa mabavu na majivuno akiwaona Wanyambo kama watu wa chini na wakati mwingine kuwachapa viboko na kuwanyang’anya mifugo yao.

Lakini,hata hivyo wahenga husema “Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpatie” kila mtu anayo mema na mabaya yake , Kyobya atakumbukwa katika Karagwe kwa kuingiza zao la Kahawa na ndizi za kupika kwani kabla yake Wanyambo walikuwa wanalima migomba kwa ajili ya kutengezea pombe , hivyo kuingia kwa zao la ndizi kwa ajili ya chakula iliwafanya kujifunza hata upishi wake kwani walizoea ugali wa ulezi tu na nafaka .

10. HITIMISHO.
Pamoja na changamoto nyingi ambazo zinaikabili zetu (Karagwe na Kyerwa) na watu wake za kama zile za kijamii, kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni bado ni moja ya wilaya zenye fursa na maliasili nyingi ambazo hazijatumika vizuri.

Katika wilaya zetu za Kyerwa na Karagwe tunayo Mapori manne ya Akiba za wanyamapori. Mapori hayo ni pamoja Rumanyika Orugundu, Kimisi, Ibanda na Burigi. Mbuga hizi zina wanyama wengi kama vile pofu, nyemera, mamba ,viboko, twiga ,simba, kuro, nyati, tembo na ndege wa aina wa aina mbali Mapori haya ya Akiba mbali na kuwa kivutio kwa watalii na wananchi wanaopenda kuangalia wanyamapori, mito na mabonde; vile vile hutumika kwa shughuli za uwindaji wa kitalii. Taarifa kutoka kwa wawindaji bingwa pamoja na Menejimenti ya Pori la Akiba Ibanda inaonesha kuwa kuna densite kubwa ya chui kwenye Pori la Ibanda ikilinganishwa na mapori mengine ya akiba hapa nchini.

Pori la Akiba Rumanyika ndilo lenye idadi kubwa ya miti ya aina ya Misambya (Markhamia rutia) ambayo inatoa mbao zenye thamani kubwa ukilinganisha na mbao zinazotokana na aina nyingine za miti. Pia , tofauti na mapori mengine ya akiba nchini ,pori hili linasifika kwa kuwa na nyati wafupi (Dwarf Buffalo) .

Aidha, kando kando mwa Pori la Akiba ibanda; yapo maporomoko ya Mto Kagera ambayo kwa sasa serikali za Tanzania na Uganda zimeanza mchakato wa ujenzi ili kufufua mitambo ya umeme iliyoharibiwa wakati wa vita vya Kagera mwaka 1978.

Kivutio kingine katika katika wilaya zetu ni Msitu wa Hifadhi ya Maji Moto (Mutagata Hot Spring catchment forest ) unaopatikana katika kijiji cha Rwabigaga eneo la Mutagata, kata ya Kamuli ,tarafa ya Kituntu/mabira .Kutoka makao makuu ya wilaya ni umbali wa kilomita 70. Msitu huu ni mdogo wa kijani kibichi muda wote uliotanda miti ya Misambya (Markhamia Lutea) na miti mingine ambayo majina yake hayafahamiki vyema. Katika msitu huu vipo vyanzo vinne vya maji moto, vyanzo hivi ni; (1) Kasiyoza ambacho ni chanzo kikubwa cha maji moto katika eneo hili ambalo maji yake ni nyuzi joto 60-90 ; (2) Chabakazi ambalo ni eneo dogo linalotoa maji ya moto yenye nyuzi joto 40-60 ; (3) Katagata kake ( hili ni eneo jingine ambalo maji yake ya moto yana nyuzi joto 30-50 na (4) Chandagala chenye maji ya baridi. Historia inaonyesha kwamba chemi chemi hii ilitumiwa na machifu kuogea. Chifu Rumanyika alitembelea eneo hili na kuliwekea Baraka ,akaitukuza chemi chemi chemi hii na kulitangaza eneo hili kuwa sehemu takatifu na kuanzia wakati huo ,maji hayo hutumika kwa ajili ya tiba ya magonjwa ya ngozi kama vile upele na mapunye ,kifua ,uvimbe wa miguu ,magoti n.k.

Wilaya ya Karagwe na ile ya Kyerwa bado ina ardhi yenye rutuba inayostawisha mazao mengi ya ya kilimo na ufugaji ambayo bado haijatumika ipasavyo. Wakulima wengi katika wilaya hii wanalima kilimo na kufuga kienyeji bila ya kutumia utalaam kuzalisha kwa wingi. Mazao kidogo yanayozalishwa ndio yanasafirishwa kwenda mikoa mingine yanayoifanya Karagwe kusifika. Mazao ya mifugo (Ngozi, maziwa na pembe za ng’ombe) nayo bado hayajatumika vyema, hatuna viwanda vya kusindika mazao haya.

Kila mmoja wetu anajua kuwa wilaya zetu za Karagwe na Kyerwa zinategemea sana kilimo kwa ajili ya chakula na biashara ,lakini mito mingi na mabonde tuliyo nayo haijatumika vyema kuongeza uzalishaji wa chakula . Ili kuinua kipato cha wananchi wa wilaya hizi kuna haja kubwa kwa Halmashauri zetu kutenga bajeti na kuhimiza wananchi kutumia kilimo cha umwagiliaji.

Katika wilaya hii eneo la Kibanda huko Bugomora lilikuwepo shamba la NAFCO na lilikuwa na uwezo wa kuzalisha ngano bora kuliko eneo lolote hapa nchini, eneo hili halitumiki. Tunaweza kufufua shamba hili kama tutakuwa na nia.

Kuhusu namna ya kuhifadhi utamaduni na mila za watu wa Karagwe na Kyerwa hatuna budi kuanzisha makumbusho ya utamaduni wa watu wa Karagwe hapa ,kufufua maeneo ya historia kama vile Bweranyange ,Nyakahanga na Mutagata . Jengo la Nyakahanga linalotumika kwa sasa kama Kituo Kidogo cha Polisi, jengo hili lilikuwa makao makuu ya utawala wa jadi (yaani Olukiko) baada ya kuhamisha mako yake toka kule Bweranyange. Sasa basi ili kutopoteza historia nzuri ya Karagwe tunaomba jengo hili kukarabatiwa bila kubadilisha mfumo wake na kutunzwa vyema kama sehemu ya kumbukumbu ya historia ya utawala wa jadi. Pia, eneo la Bweranyange linatakiwa pia kutunza vyema kama sehemu muhimu ya historia ya watu wa Karagwe

Aidha, hatuna budi kuzienzi na kudumisha mila na desturi nzuri za wanyambo ambazo tayari zimeanza kufifia na kupoteza umaarufu wa kabila hili la wanyambo. Pia, zile mila na desturi mbaya za kibaguzi na zinazowanyanyasa akina mama na zile zenye kurudisha maendeleo nyuma tuachane nazo kabisa.

Tunaomba sherehe hizi za kuadhimisha siku ya utamaduni wa kila kabila kufanyika kila mwaka na Halmashauri zetu kutenga bajeti ya kutosha kufanisha lengo hili.

Mwisho, naomba kutoa wito kwamba Karagwe na Kyerwa yenye maendeleo inawezekana iwapo tutakuwa na mshikamano wa pamoja katika kuhifadhi maeneo ya kihistoria pamoja na kuendeleza mila nzuri za kabila hili. Kwa maana taifa lisilokuwa na utamaduni wake ni sawa na taifa lililokufa. Ni ukweli usipingika hata nchi zote zilizoendelea bado wametunza na wanaendeleza maeneo ya kumbukumbu ya kihistoria kwa ajili ya utalii na pia kwa faida ya vizazi vijavyo.
 
Asante kaka, Kwetu ni Nkwenda barabara ya kwenda Mabira kama unapajua.
Umenikumbusha mbali sana niliwahi kupita maeneo hayo katika pilika za maisha na nikapita maeneo kama ya Chanyangabwa, Kitwechenkura, Mabira, Kituntu, mpaka Nyabiyonza kote huko (maisha haya yalinifikisha mpaka Karagwe sehemu ambayo sikutegemea kama nitafika, usipochagua kazi unafika sehemu nyingi lakini leo nimerudi eneo ambalo ndio chaguo langu siku zote) yaani naijua Karagwe kuliko hata mzaliwa wa Karagwe
 
kuna sehemu inaitwa oumurushaka na nyingine kayanga vipi ile barabara wameshaweka lami?
Kuna mama mmoja wa kichaga alikuwa anatengeneza mbege nzuri sana bado yupo?
Na kuna jamaa mmoja almaaruf mnywaji anaitwa palanjo nae yupo?
 
mugajamii, Ok, wewe upo kwenye kundi la wanyamahanga maana utakuwa hujui vizuri wilaya yako.
Jina la ni Muga? Mimi pia naitwa Muganyizi.
 
Last edited by a moderator:
Jodoki Kalimilo, Maisha siku zote ndivyo yalivyo,unaenda sehemu ambazo hata hukutarajia kufika,BTW najua ulipata kuona ukarimu wa watu wa Karagwe na kwa namna moja au nyingine kuna jambo ulijifunza.
 
Last edited by a moderator:
Kuna hadi waarabu pale mjini wamezaliwa pale.

Ukifika Omurushaka ndio kuna Waarabu kibao wamezaliwa pale,ila pia wilaya hiyo kuna wanarwanda wengi sana wamechanganyika mpaka kujipachika jina la wanyambo.Pia wameolewa na kuolewa na wanyambo pamoja na waarabu.

Nakumbuka wanakati nasoma karagwe lile vuguvugu la kamata kamata wanyarwanda kuna kijiji kimoja Bushangaro walikamata wanakijiji wote na kuwarudisha Rwanda.
 
Jodoki Kalimilo, Maisha siku zote ndivyo yalivyo,unaenda sehemu ambazo hata hukutarajia kufika,BTW najua ulipata kuona ukarimu wa watu wa Karagwe na kwa namna moja au nyingine kuna jambo ulijifunza.
Nili-enjoy unajua nilikwenda miaka ya 2000 mwanzani hata mitandao ya simu ilikuwa bado zaidi ya Tigo walikuwa Bukoba mjini, kiujumla nimejifunza mengi maana perception ya watu wa mjini dhidi ya maeneo ya vijijini / wilayani huwa ipo tofauti na uhalisia maana hata mie nilikwenda nifanyaje lakini nilipofika nikakuta kazi zinakwenda na Tv kupitia cable operator napata maisha yakasonga mbele.

Nadhani sasa hivi kutakuwa bomba zaidi maana ile barabara ya kutoka BK mpaka Kyaka ina Lami pia kuna Bus la moja kwa moja kutoka Mwanza kwenda Karagwe tofauti na zamani ilikuwa ni meli. Btw ni eneo zuri kwa mtu ambae ni mpiganaji ukiacha mashauzi tuliyonayo watu wa mjini tunapoingia wilayani maana hata mjini life ipo tight tu kwa watu walio wengi

Nilipofika ndio nikagundua kuna kabila linaitwa Wanyambo maana wengi wakitoka nje ya mkoa wa Kagera wanajulikana kama Wahaya
 
Back
Top Bottom