Ulinzi mkali wa viongozi unahujumu mahusiano na raia

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Sep 20, 2021
3,216
3,587
Nyanja: Utawala Bora/Mahusiano

(siyo tukio halisi)

Mazoea ya kuwa na ulinzi mkali wa Askari wenye sare na bunduki kwenye ziara za viongozi na operesheni za kitaifa kama mitihani ya taifa na uchaguzi mkuu yamezua jambo nchi moja ya Afrika Mashariki iliyogundua mafuta na iliyo katikati ya wanachama wa Afrika Mashariki kijiografia (jina linahifadhiwa).

Kitongoji kimoja kilichoko mpakani kabisa na nchi jirani lakini kikiwa kilomita 200 toka kwenye barabara kuu; ambacho kilisajiliwa rasmi serikalini siku za karibuni bila kuwa na miundombinu ya barabara, afya, mawasiliano nk, kilifanya mahafali ya kwanza ya darasa la saba kwenye shule waliyojenga Wanakitongoji kwa nguvu zao wenyewe na kusajiliwa sambamba na usajili wa Kitongoji. Baada ya sherehe ya mahafali ya kuwaaga wahitimu hao siku ya Jumapili, ukafuata mtihani wa taifa wa darasa la saba siku ya Jumanne. Siku ya Ijumaa kabla ya mahafali shule ilitangaza mapumziko ya siku 2 Jumanne na Jumatano kwa madarasa ya kwanza hadi sita kupisha mitihani hiyo ya taifa ya darasa la saba.

Jumatatu watahiniwa wakawahi kama kawaida shuleni wakahakikiwa na kuingia madarasani kusubiria wasimamizi, muda ulipowadia wasimamizi wakafika na mitihani kwa usafiri wa bodaboda na baada ya muda mfupi maofisa wa Polisi walio kwenye sare na bunduki nao wakawasili kwa usafiri wa bodaboda na wote kupokelewa na Mkuu wa shule na kusaini daftari la wageni. Maofisa hawa wa Polisi walipoingia tu kwenye vyumba vya mitihani ili kukagua makabrasha ya mitihani na kujiridhisha na usalama wake kwamba hayakuhujumiwa, wanafunzi walitaharuki na kupiga kelele za hofu kuu na wote kutokomea nje kupitia madirishani na mlangoni na kuwaacha wasimamizi, Polisi na Mkuu wa shule wakiduwaa, Mkuu wa shule akagonga kengele kwa nia ya kuwaita na kuwakusanya lakini hakuna aliyejitokeza hata mmoja. Baada ya majadiliano ya pamoja, wakakubaliana kwamba waende kwa Mwenyekiti wa Kamati ya shule ili awasiliane na Mwenyekiti wa Kitongoji apige mbiu ya kuwaita Wanakitongoji watoke mashambani na machungaji waje kwenye ofisi ya Kitongoji kwa ajili ya kuwaambia kesho wawalete watoto wao hao watoro wakafanye mitihani hiyo.

Wanakitongoji walipofika tu na kukuta Maofisa wa Polisi wako pale, 99% ya wazazi hawa wakatimua mbio kwa kelele kuwa wamevamiwa na majambazi kuja kuwateka, huku wengi wao wakifunga miji yao na kutoroka nje ya Kitongoji kutafuta hifadhi. Wazazi 1% waelewa hawakutoroka na wakasema watoto hao hawakurudi nyumbani. Wakaambiwa kwamba watakaporudi nyumbani wawazuie ili kesho wawalete wakiwa chini ya ulinzi wao lakini pia waisaidie serikali ya Kitongoji kuwashawishi wazazi wenzao waliotoroka kuwa wale ni Maofisa wa Polisi waliokuja kulinda mitihani siyo majambazi. Kesho ilipowadia wazazi wale 1% wakafika shuleni bila watoto wao na ikabidi mitihani irudishwe Halmashauri kwa ajili ya hatua zaidi. Serikali ikatangaza msako mkali wa watoto hao lakini bila mafanikio. Ndipo baada ya mwezi kupita taarifa za kipelelezi zikapatikana kwamba wengi wao walivuka mpaka wa nchi yao na kwenda mafichoni nchi jirani huku wengine wakidhaniwa kuanza maisha mapya ya ndoa za wenyewe kwa wenyewe huko mafichoni. Mkuu wa Wilaya akaunda tume ya uchunguzi na kufuatilia nchi jirani na kufanikiwa kuwakamata wachache wao waliohamia kwenye kisiwa cha wavuvi.

Baada ya mahojiano nao, wakawaambia Wajumbe wa tume ya uchunguzi kwamba waliamua kutoroka baada ya vyumba vya mitihani kuvamiwa na wanamgambo wa Boko Haram wenye bunduki kuja kuwateka (wakimaanisha wale Maofisa wa Polisi wawili walioletwa kulinda mitihani). Serikali ikawarudisha kuwaunganisha na jamii zao huku wengi wakiwa wametokomea kusikojulikana. Aidha, tume ilibaini kwamba uoga huo wa watoto na wazazi wao ulitokana na ukweli kwamba tangu kuanzishwa kwa Kitongoji kile wananchi hawakuwahi kushuhudia Polisi kwa macho yao hivyo hawajui Polisi wanafananaje, kwamba hii ilitokana na ukweli kwamba hapakuwahi kuwa na operesheni za kiserikali katika Kitongoji kile ukiwemo uchaguzi mkuu nk ambavyo vinahusisha ulinzi wa Polisi, kwamba shughuli za Polisi zinafanywa na walinzi wa jadi na mashauri ya kimahakama yanasikilizwa na kuamuliwa na Baraza la Kitongoji kwa sheria za mila na desturi; ambalo limeundwa na viongozi wa kujitolea bila malipo.

Tukio hili lilifanya Halmashauri ya Wilaya kuandaa mwandiko wa mradi wa dharura (Emergency Project Proposal) kuomba fedha Benki ya Dunia na kuanzisha miradi ya kimkakati kama kuchonga barabara ya moram kuunganisha Kitongoji na barabara kuu, kujenga kituo cha afya, kujenga kituo cha Polisi, kuchimba bwawa kubwa la uvuvi na kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya mbogamboga, matunda na mpunga, kujenga soko mpakani kuvutia biashara toka nchi jirani pia, kupeleka huduma za maafisa ugani, maafisa uvuvi, maafisa mifugo mara moja kwa juma, kuanzisha mnada mkubwa wa mifugo unaofanyika mara mbili kwa juma, kupeleka nishati ya umeme, kujenga mnara wa mawasiliano ya simu za viganjani na mnara wa redio, kupeleka huduma za Mahakama inayotembea (Mobile Court) mara moja kwa mwezi, kuthibitisha viongozi wa Kitongoji na hatimaye kupandisha Kitongoji hadhi kuwa Halmashauri ya Kijiji. Matumizi makubwa ya vyombo vya dola kwenye shughuli zinazokutanisha viongozi wa serikali na wananchi yanawatenga wananchi na viongozi wao waliowachagua na kuwaamini wenyewe bila kushinikizwa na mtu. Kiongozi safi aliyepatikana bila hila na anayekubalika na wananchi hana sababu ya kubomoa daraja linalomuunganisha na wananchi wake kwa kutumia ulinzi mkali wa vyombo vya dola kwenye ziara zake.

majwalaoriko@yahoo.co.uk
 
Back
Top Bottom