Ukweni pamoto jamani, pole mchumba angu

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,337
51,858
UKWENI PAMOTO JAMANI; POLE MCHUMBA WANGU.

Na, Robert Heriel
Chereko chereko ziliendelea pale nyumbani. Vigele gele na vifijo vilirindima. Mtaa mzima ulijua kuwa Siku ile Mchumba wa Taikon anakuja kwa mara ya kwanza kutambulishwa. Kila mmoja alikuwa na shauku ya kumuona mchumba wa Taikon.

Alikuwa mweupe; hawakujua. Alikuwa mweusi, hawakujua. Alikuwa mfupi au mrefu hawakujua. Alikuwa mnene au mwembamba, nasema hawakujua. Na hii ndio iliwafanya waje siku hiyo kumuona mchumba wa Taikon anafananaje.
Pengine wengine walikuja kumuona ili wanidhihaki, au wanicheke kabisa. Hakika ni kuwa wapo waliokuja kunipongeza, bila kujali Mchumba wangu angeonekana vipi.

Sio kama hawakuwahi kumuona, baadhi yao walimuona huko kwenye mitandao ya kijamii, wapo waliomuona Instagram, wengine Facebook, na mitandao mingine. Sasa iweje wasimjue Mchumba wa Taikon ikiwa walishamuona huko kwenye mitandao? Subiri nimeze mate, maana habari hii ni nzito.

Huko Mitandaoni walishangazwa na Mchumba wa Taikon, Ati alikuwa kama kinyonga, nakumbuka Bibi yangu wa Makanya alinipigia simu akaniambia; Watu wa siku hizi wanabadilika kama kinyonga. Sikumuelewa mpaka aliponambia habari za watu wanaobadilika badilika huko kwenye mitandao ya kijamii. Kiaje sasa? Wanabadilikaje? Niliuliza.

Kumbe picha za Mchumba wangu za mitandaoni zilikuwa mithili ya Kinyonga. Ati leo alikuwa mweupe, kesho alikuwa mweusi, kesho kutwa anamasikio ya sungura, mtondogoo analipsi nyekundu. Looh! Mambo ya Photoshop kijijini wayajulie wapi watu pori.

Sasa siku ile hicho ndicho kilichowaleta, kumuona kwa macho yao huyo Binti Kinyonga, naam ndiye Mchumba wangu.
Basi tulipanda Basi liitwalo Ngorika ambalo kwa Nyuma liliandikwa maandishi meusi yaliyosomeka " SAUTI YA MANKA" Ni basi hili lililokuwa tishio kwa kutupeleka msobe msobe kama vikaragosi tunaokimbia mikosi. Nilimtazama mchumba wangu tulipofika Mji wa Hedaru, uso wake ulikuwa na hofu kama pofu awindwaye. Niliitambua hofu yake. Nayo ni kitimu timu cha Ukweni.

Ukweni ni pamoto penye joto. Panaunguza bila kupuliza. Ukweni panatoa jasho bila kupewa posho. Huko ndio Ukweni ambapo mchumba wangu anajipeleka kama Kondoo wa kafara.

Sasa tuliukaribia mji wa Makanya, mawazo mabaya yalipitia pale nilipomuona mchumba wangu akitazama nje kupitia dirisha la gari. Pengine ningekuwa na Gari langu binafsi angefurahi, angeringa kupanda gari la Mchumba wake. Wazo hilo nilililaani sana, kwa nini lije muda ule, kwa nini lakini? Liliniumiza moyo wangu. Lakini sikuwa na chakufanya zaidi ya kunyamaza.

Simu yangu iliita, alikuwa ni Mama yangu mzazi aliyekuwa akiniuliza tumefika wapi. Hapo tulikuwa tumeshapita kijiji cha Nkwini, na sasa tuliuona mji wa Makanya kwa mbali kama kilometa tano tuu. Hii ilimaanisha dakika tano zijazo tungekuwa tumefika Makanya.

Kituo cha Makanya niliona kundi kubwa la kina mama lililokuja kutulaki. Alikuwepo Mama yangu, Mama Mkubwa, Mashangazi, na Mzee mmoja mwenye mvi ambaye sikumfahamu kwa mara moja. Moyo wangu ulishindwa kufurahi au kuchukia. Nisingejiongopea kuwa nilikuwa sina hofu. Moyo ulipiga kwa pupa. Hapo Ngorika Sauti ya Manka lilisimama tayari Konda alikuwa amefungua mlango akitangaza abiria wa Makanya tushuke upesi. Kauli zake zilikuwa za kawaida lakini ziliniboa; niliona kama anatufukuza.

Tukiwa tunashuka niliwaona ndugu zangu wakichungulia ndani ya gari wakitutafuta. Waliniona nikiwa nimeshafika mlangoni nikishuka. Kwa pamoja walinifuata na kupiga vigele vigele alulululululu! Kisha mchumba wangu naye akashuka kwani alikuwa nyuma yangu. Wakampokea mkoba wake, kisha wakapiga tena vigelegele Alululululu!

Nani ambaye hakushangaa, nani ambaye alikuwa ndani ya gari ambaye hakuchungulia nje, Hakuna. Abiria wote walitoa vichwa vyao nje kushangaa tukio hilo. Nani kafanya nini mpaka ashangiliwe hivyo? Macho yao ndio yalitazama na kuuliza swali hilo. Lakini hakuna aliyewajibu zaidi ya matendo yetu pale chini ya gari. Watu wa pale Stendi walibaki wametutolea macho lakini hatukuwajali. Hatimaye Tuliliacha gari likituacha likiendelea na safari nasi tukielekea nyumbani.

Njiani kina Mama wakiongozwa na Mama yangu waliimba nyimbo za Kipare, ungedhani kesho ni harusi. Waliimba wakicheza huku sisi tukiwa tumewekwa katikati. Nilimuona Mchumba wangu akiwa anatabasamu kwa aibu, macho yake aliyatiisha nayo yakatii, yalikuwa yamepoa kama uji dundi. Sijui alifurahi au laa. Ninachoweza kuelezea, alikuwa na wasiwasi sana.

Dakika kumi zilitupeleka mpaka kukaribia nyumbani. Mtaani watu walitutazama Kwa mshangao. Wengine niliowaacha muda mrefu pale kijijini walinitazama kama watu wanaonifananisha. Walionijua walinipungia mikono huku wakipiga milunzi na mbinja.

Kundi jingine lilitulaki tulipokaribia nyumbani. Walikuwa ni kinamama waliobeba vilemba wakivipunga juu wakiimba kwa kipare. Wengine niliwatambua wengine sikuwatambua. Walituvamia na kututupia kwa furaha vile vilemba kisha wakatufunika na kanga nyingi, harufu ya kanga zile walizotufunika nazikumbuka mpaka hivi leo.

Zilikuwa mpya kabisa walizonipulizia marashi yenye harufu nzuri sana. Mule ndani, ndio ndani ya kanga tulipofunikwa hapo tukapata nafasi ya kutazamana na Mchumba wangu. Alitabasamu ni kama hofu ilipungua. Akanambia:
"Nina hofu sana Mume wangu. Ila nitavumilia" " Usijali, jikaze utazoea, hii ni hatua muhimu sana kwetu" Nilimpa moyo, sauti zetu zilinong'ona pasipo kusikika.

Shangwe ziliendelea mpaka tulipofika nyumbani na kuingia ndani. Ile kanga ilitolewa. Sasa macho yetu yalishuhudia sebule ikiwa imefurika watu waliokuwa wamekaa kwenye masofa, wengine wakiwa wamekaa kwenye viti ambavyo nilitambua vilikuwa vimekodishwa. Nilimuona Bibi yangu akiwa kazeeka jamani. Uso wake ulikuwa umekunjika sana, lakini aliponiona mikunjo ilikunjuka kwa furaha ya kuniona. Alitabasamu na kunifuata kwa kujikongoja mpaka aliponikumbatia.

Nilishindwa kujizuia, nikatoa machozi ya furaha iliyopitiliza. Bibi akiwa kanikumbatia nilisikia mapigo yake ya moyo yakipiga kwa taratibu sana, hapo nikakumbuka mambo mengi aliyonifundisha enzi zile nikiwa mtoto. Mwili wake Haukuwa na joto sana, lakini nilihisi joto la upendo wake. Aliniachia na kunitazama usoni, nami nikamtazama. Wote tulikuwa tukitoa machozi. Yalikuwa machozi ya furaha.

Watu wengine walikaa kimya wakitutazama, hata Mchumba wangu alitutazama mimi na Bibi yangu. Niliwaona watu wenye hisia za karibu wakifuta machozi na kanga zao. Looh!

Basi tukaketi mimi na Mchumba wangu mahali tulipokuwa tumeandaliwa. Hapo wajomba, Baba, na kaka na wadogo zangu wakiume walikuwepo. Niliwaona watu wakimtazama Mchumba wangu kama wakaguzi na wasanifu wa majengo ya serikali.

Leo maswali yao yalijibiwa; walimuona mchumba wa Taikon wa Fasihi kwa macho yao.

Kwa habari ya mavazi aliyokuwa amevaa mchumba wangu ilikuwa ni hivi. Alikuwa amevaa gauni la kitenge lililomkaa vyema, kichwani alikuwa amesuka mtindo uliompendeza sana. Mkononi alikuwa kavaa saa ndogo iliyompendeza. Chini alivaa viatu vyeusi vya kuchomeka vyenye kisigizo cha wastani. Shingoni alivalia mkufu niliokuwa nimemnunulia. Alipendeza sana.

Mimi nilivalia suruali nyeusi, na shati la kitenge kilichofanana na Gauni alilokuwa amevaa Mchumba wangu. Nilinyoa nywele zangu vizuri, huku ndevu zangu zikiwa zimekatwa vyema. Mkononi nilivalia saa ya silver, chini nikiwa nimevaa viatu vya rangi ya ugoro. Sijui walinionaje lakini Mchumba wangu yeye aliniambia nimependeza.

Mchumba wangu ilifikia muda wake wakujitambulisha licha ya mimi kumtambulisha kwa ufupi. Mimi ndiye nilipewa nafasi ya kumkaribisha ili aongee. Kwa sauti nyororo yenye dalili zote za adabu na maadili Mchumba wangu alizungumza.

Sikumbuki kama kuna siku Mchumba wangu aliongea sauti nzuri kama ile siku. Jamani kila mtu alijikuna masikio. Walikiri kuwa Taikon nimepata mwanamke mzuri asiye na mfano.

Baada ya utambulisho, muda wa kula ulifika, hiyo ilikuwa saa kumi na moja jioni. Tulikula na kunywa. Huku Dada zangu mara kwa mara wakichagiza kwa vimaneno vya kishapenga ilimradi kuifanya siku ile iwe ya kipekee.

Usiku uliingia, muda wa kulala ukafika. Siku ile hatukulala pamoja yaani mimi na mchumba wangu. Kila mmoja alilala chumba alichopangiwa.

Asubuhi na mapema nilitoka, nilishangaa kumuona Mchumba wangu akiwa anafagia uwanja. Tayari alikuwa ameshawasha moto na chai ilikuwa jikoni inachemka. Alikuwa akisaidiana na Dada yangu. Nikasema kimoyo moyo hapa nimepata Mke. Tukasalimiana.

Mchumba wangu akaambiwa akande chapati kisha asukume. Looh! Hapo ndipo kimbembe kilipoanza. Mchumba wangu alinitumia sms nikiwa chumbani, akinitaka nitoke nje. Nikatoka, akanambia yeye hajui kukanda chapati, masikini. Nilimuonea huruma kwani nilijua anasikia aibu. Aihofia kuonekana yeye sio mke bora.

Punde kina mama walitoka na kutusalimia. Kisha wakamuita Mchumba wangu wakimwambia anasubiriwa kwenye chapati watu wanatakiwa wanywe chai saa mbili. Hapo Mchumba wangu akaitikia looh!

Mchumba wangu aliboronga vilivyo, alipika chapati nzito na ngumu sana. Hakuna aliyeweza kuzila, kila mmoja alizilaumu, huku wenye uvumilivu mdogo wakitoa maneno ya karaha yaliyomchoma mchumba wangu.

Hilo likapita, baada ya kunywa chai ya mapolopolo, kilichofuata ni kudeki nyumba, looh! Mchumba wangu hakuweza kupiga deki. Hakujua namna ya kukausha sakafu hali iliyopelekea sakafu kubaki na vidimbwi vya maji. Hiyo nayo ilikuwa fedheha kwani ilisababisha minong'ono kwa kinamama; Hata kudeki pia hajui. Walimsengenya.

Hilo nalo likapita. Muda wa kuosha vyombo ndio kizaazaa. Masikini Mchumba wangu hakuweza kuosha vyombo. Unajua kule kwetu kijijini vyombo vya kulia chakula siajabu ukavikuta na masizi. Hivyo kuviosha mpaka masizi yaondoke ilihitaji muoshaji asiyembabaishaji. Mchumba wangu hilo likamshinda. Vyombo vyote vilikuwa na masizi. Hayo masufuria alishindwa kuyasugua. Yalikuwa kama hayajaoshwa. Looh!

Hilo nalo likapita, Muda wa kupika chakula cha mchana ukawadia. Mchumba wangu akaambiwa akawashe moto, asubuhi aliwashiwa na Dada yangu. Masikini mtoto wa watu, aliwasha jiko mpaka akalia. Jiko la kuni halihitaji uhuni. Lahitaji ujuzi na makuzi yasiyoyakipuuzi. Alichukua nusu saa kuwasha jiko la kuni. Basi moshi wa kuni ulimfanya kila mara atoe ,machozi. Alipuliza akapuliza mapaka mashavu yakalegea masikini.

Chakula hakikuiva, wali ulikuwa mbichi kabisa, tena mboga ambayo ilikuwa ni kuku ilikuwa inanuka moshi na chumvi nyingi. Labda kwenye moshi angejitetea hajazoea jiko la Kuni lakini je mafuta alivyozidisha pamoja na chumvi. Ilikuwa ni aibu, mchumba wangu hajui kupika jamani.

Hilo nalo likapita, watu wakala chakula cha korokoroni. Muda wa kufua ukawadia. Alipewa nguo afue, zilikuwa nguo za vitambaa vya sebuleni. Mchumba wangu hakuwa anajua kufua. Alitoa nguo ikiwa haijatakata. Nilisikia aibu sana. Lakini ningefanya nini ikiwa aibu imeshaingia. Looh!

Basi Mke wangu akanambia anaondoka, nikambembeleza lakini ikashindikana. Alitoroka bila kuonekana. Nilikuta sms iliyosema " Nimeondoka, nimechoka na mikazi yenu"
Dooh!

Basi hayo ndio mambo yaliyotokea siku zile Mchumba wangu alipokuja nyumbani kwetu kutambulishwa.

Mchumba wangu alijifunza kupika, kuosha vyombo, kufua nguo, na kazi zingine za nyumbani, pia amejifunza kuishi katika mazingira yoyote.

Baadaye tulipanga siku ya harusi. Siku ya Harusi ilifika. Je ilikuwaje?
Kama unataka kujua ilikuwaje, like, na kushare page yetu. Kisha nitadondosha uhondo wote wa siku ya harusi ilipofika.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
069332300
 
Nimesoma yote n nzuri kwa hapo ilipofika

Kama mlimfundisha kazi inapendeza sana
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom