Ukweli wa Jenerali Ulimwengu uwatoe tongotongo wanazuoni!

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,903
Ukikutana na Jenerali Ulimwengu kwa mara ya kwanza, unaweza kudhani kuwa uko na mtu mkimya, mtulivu na msikivu – lakini ukikaa naye nusu saa utakubaliana nami kuwa uko mbele ya mtu anayeijua dunia vizuri, anayeijua nchi yake kwa mapana na hasa kujua inapaswa kwenda wapi. Jambo lingine utakalojifunza kwa Ulimwengu ni ujasiri na kujiamini, nadhani wakati mwanaharakati huyu alikuwa anazaliwa – uoga ulikuwa haupo kabisa duniani.

Hivi majuzi katika mwendelezo wa makongamano makubwa yaliyoandaliwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere pale Ukumbi wa Nkrumah Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Jenerali ulimwengu aliwaacha midomo wazi wasomi nguli wa Vyuo mbalimbali na wananchi waliokuwa wakifuatilia mjadala ule kwenye vyombo vya habari. Ulimwengu alihoji kwa utashi mpana kwa nini taifa letu linazidi kudidimia, akahoji mathalani kwa nini mabilioni ya fedha yalitapanywa kutafuta “katiba feki” na hasa akahoji kwa nini pamoja na juhudi za rais wa sasa, ukitizama kwa picha kubwa unagundua kuwa hafanyi vizuri kwenye eneo la upanuzi wa Demokrasia. Jenerali anayesema haya mbele ya Mgeni Rasmi, Rais wa awamu ya nne, Mzee Ben Mkapa.

Najua kuwa wakati anatamka haya baadhi ya maprofesa walikuwa matumbo joto, wakiinama chini ili wasionwe kama walitabasamu kufurahia ujumbe alioutoa moyoni. Jenerali aliitengeneza siku yangu kuwa murua kabisa kwa sababu alisema ukweli, na ukweli una upande – hauwezi kuwa vuguvugu, ni ama moto au baridi.

Nimeamua kuandika waraka huu ili kuwagutusha wasomi na wanazuoni wetu nguli hapa Tanzania – maprofesa, madaktari na wahadhiri wa kila namna. Jukumu kubwa la wataalamu hawa ni kufanya tafiti na kuzitetea ili wanasiasa na wafanya maamuzi wazifanyie kazi zilete tija kwa jamii. Wanasiasa wanao muda mdogo sana na siyo watu wa kutulia mahali fulani ili kutumia muda mrefu kabisa kuchunguza jambo fulani, wao ni watu wa kuletewa na kueleweshwa “hiki kikifanywa hivi na vile nchi itapiga hatua kubwa…”. Sisemi kuwa wanazuoni wetu hawafanyi kazi hiyo, la hasha! Wanafanya sana na wamefanya kwa miaka mingi tu.

Tatizo ambalo naliona kwa hatua ya sasa ni wasomi kushindwa kusimamia yale waliyoishauri serikali, wanasiasa na wafanya maamuzi. Wanazuoni na wataalamu wa Tanzania kazi yao kubwa ni kufanya utafiti fulani na kuikabidhi serikali au mamlaka na kisha wananawa na kujitoa, wanajiweka mbali kabisa na haiwahusu. Wasomi na wanazuoni wa nchi nyingine wanajitambua zaidi, wako ‘aggressive’ wanajua ni haki na wajibu wa serikali kufuata yaliyo sahihi kwa maendeleo ya taifa – na kwa hiyo wasomi wa nchi hizo husimama hadharani na kidete na kuisukuma serikali itekeleze masuala ya msingi iliyoshauriwa.

Kasumba ya wasomi na wanazuoni wetu ni kuishia kukabidhi na “kulala mbele kwa mbele”, yatakayofuata hayawahusu. Hii ni kasumba mbovu sana na ndiyo imewaendekeza wanasiasa na kuwafanya waendelee kujilimbikizia madaraka makubwa na kutosikiliza vilio na mahitaji au vipaumbele vya wananchi. Lazima tuambiane ukweli, kama Profesa wa Chuo Kikuu hawezi kuihoji serikali, akipewa kipaza sauti anatetemeka na kuishia kulalamika na kuomba “naomba…naomba…napendekeza…ni maoni yangu….” vipi kule kijijini ambako kuna baba mzazi wa Profesa, kuna wadogo zake ambao hawakusoma n.k. hawa wakikutana na mkuu wa wilaya si watapiga magoti na kumsalimia?

Sibezi aina ya uongeaji wa wasomi wetu nguli, hapana. Nahoji uwezo wao wa kuhoji na kutuonesha kwa maneno na vitendo kwamba wanataka jambo fulani lifanyike. Sisemi kuwa wasomi hawa wawe wanaharakati na wanasiasa, nasema hawa wasomi wetu wanatusaidiaje kupenyeza ajenda kubwa na za kitaifa kwa wanasiasa ikiwezekana kwa kuwasukuma hadharani na bila woga? Kwa nini kipande cha video cha hojaji za Jenerali Ulimwengu kinasambaa sana kila kona ya nchi, ni kwa sababu yale aliyoongea ndiyo ulitegemea yaongelewe na maprofesa nguli! Lakini kwa bahati mbaya wakubwa hao wamejiweka pembeni, jamii haisikii sauti zao na kwa hivyo inaibidi iendelee kutii sauti za dhamira mbovu za watawala wenye malengo mabaya,wasioambilika na wasiosikia la mtu.

Wasomi hukutana kila mwaka kujadili falsafa za Mwalimu Nyerere, mchango wake na kama tunauishi, umajumui wa kiafrika n.k. lakini hawayaongei kwa uwazi na bila hofu kama alivyofanya Jenerali Ulimwengu. Ulimwengu hana shahada nyingi za Chuo Kikuu na wala hana mamlaka yoyote katika nchi, lakini ni raia anayethubutu kusema kile ambacho jamii pana inahisi kinaendelea. Hana hofu na ajira maana ajira yake ni maarifa yake na kichwa chake, hana hofu na mishahara kwa sababu mshahara wake ni maarifa yake na kichwa chake.

Wanazuoni wetu nguli hutufundisha kusema kweli, na kweli kabisa lakini wanapokuwa kwenye mazingira ambayo wanaweza kunukuliwa na jamii nzima ikiwemo watawala, huishia kulalama na kugumia tumboni, hawatamki maneno kama ya Jenerali ambayo si matusi hata kidogo – bali ni ukweli ambao watawala hawapendi kuusikia. Ukirejea dhana ya msomi au mtu aliyetumia kodi za wananchi wenzake kupata elimu, ni kwamba mtu huyo anapaswa kurudisha yale aliyopewa – kwa vitendo, kwa kuonesha njia, kwa kuonesha ujasiri, kwa kuonesha kuwa ni wajibu wa serikali kufanya hiki na kile na wananchi hiki na kile. Huyu ni mtu ambaye lile asemalo linapaswa kusikilizwa na kuwatikisa watawala, kuwaogofya wenye mamlaka na kuwafanya watambue kuwa wao siyo mabosi, bali wananchi ndiyo waajiri.

Wakati nahitimisha hoja hii, nikakumbuka kuwa – kama nchi hii ingekuwa na kina Jenerali Ulimwengu 1,000 peke yake. Watawala wote wangelikuwa wanajua wajibu wao na kuutekeleza ipasavyo – lakini kwa hali iliyopo, sidhani kama tunao kina Jenerali 100.

Makala hii imechapwa kwenye DARUBINI YA MTATIRO katika Gazeti la Mwananchi la Jumapili 19 Juni 2016.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii na Kisiasa, Mtafiti na Mwanasheria Simu; +255787536759/ Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com/ Tovuti; juliusmtatiro.com.
 
Hao wanaoitwa wasomi na wahadhiri hawajitambui! Ni bora wasiokuwa na kiwango hicho cha kukariri darasani angalau wengi wao wanauthubutu na kujiamin kuliko wasomi ambao sofa yao kuu ni uoga!
 
Back
Top Bottom