Ukweli kuhusu bajeti ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania 2021/ 2022

Baraka Mina

JF-Expert Member
Sep 3, 2020
581
574
Wahenga walisema "Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha", baada ya mjadala mrefu juzi Juni 22, 2021 Bunge la Tanzania lilipitisha na kuidhinisha Bajeti Kuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania shilingi trilioni 36.68 (36,681,897,765,000) kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo wabunge 361 sawa na 94% walipiga kura ya ndiyo, wabunge 23 sawa na 6% walipiga kura isiyo ya maamuzi (hawajakataa wala kukubali) na wabunge 5 hawakuwepo wakati wa zoezi hilo la upigaji kura. Ikumbukwe kwamba bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 ina ongezeko la 4% ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha wa 2020/2021 iliyokuwa ni shilingi trilioni 34.8.

Nilimsikiliza kwa makini Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wakati akijibu hoja kwa ajili ya kuhitimisha mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali kabla ya Bunge kuidhinisha Bajeti hiyo Bungeni jijini Dodoma, kwa hakika Serikali inahitaji kupewa pongezi za dhati kwa jinsi ilivyojipambanua namna ambavyo itaenda kuitekeleza bajeti hii na kuhakikisha inaleta maendeleo jumuishi na endelevu

Kuna baadhi ya hoja (mambo) wengi wetu tulizielewa vibaya kutokana na tafsiri tofauti zilizoenea sambamba na kukosa taarifa sahihi na huu hapa chini ndiyo ukweli kuhusu bajeti hii.​

KODI YA MAJENGO KUPITIA MITA ZA LUKU
Kodi hii haitatozwa kwa kila mwenye umeme na wala kwa matumizi ya umeme bali maeneo ambayo yatatozwa ni yale yaliyoainishwa yenye sifa kisheria, hivyo namba za mita za luku za wananchi ambao hawatakiwi kulipa zitaondolewa katika mfumo (blacklisted). Sambamba na hilo kodi hii italipwa na mmiliki wa nyumba na sio ya mpangaji. Kama ilivyokuwa inakusanywa kwa njia ya kawaida (physical) ukusanyaji uleule unapelekwa katika njia ya kielektroniki kwa sababu teknolojia imekuja ili kurahisisha kazi.

Serikali imeeleza kuwa kodi hii haitatozwa kwa kila mwenye umeme na wala kwa matumizi ya umeme kwa sababu kodi ingetozwa kwa matumizi ya umeme gharama za uzalishaji wa umeme zingeongezeka na hivyo kuleta adha kwa wananchi.

MAKATO YA SIMU KWENYE MUDA WA MAONGEZI
Makato hayatafanyika kila siku bali ni pale tu mtu anapoweka muda wa maongezi. Makato yataanzia shilingi 5 kwa wanaotumia shilingi 1000/= kwenda chini mpaka shilingi 222 kwa wanaotumia 100,000/= na kuendelea.

Mhe. Mwigulu Nchemba alisisitiza kuwa nchi hii (Tanzania) itajengwa na watanzania wenyewe, ni lazima tubebe majukumu hayo (ulipaji wa kodi) kama watanzania kwa sababu majukumu hayo ni yetu na nchi yetu ina matatizo pamoja na jitihada kubwa ambazo zimefanyika. Kila hatua ya maendeleo tunayoifanya inatuletea changamoto zaidi; ndivyo utaratibu wa maendeleo ulivyo.

WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI
Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 322 kwa ajili ya kufungua maeneo ambayo hayapitiki (hayana barabara) katika maeneo ya mijini na vijijini. Kila jimbo la uchaguzi litapata si chini ya bilioni 1 kwa ajili ya barabara hizi.

Barabara za vijijini zimekuwa ni kilio kikubwa kwa muda mrefu. Kutengwa kwa fedha hizi ambazo zitatumika kujenga barabara za vijijini ili zikae muda mrefu kutasaidia usafiri wa uhakika kwa wananchi, usafirishaji wa bidhaa na kuanza kusogeza huduma karibu na wananchi sambamba na kuiwezesha TARURA kifedha na kiutaalamu ili ifanye kazi kwa ufanisi zaidi.​

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 70 ili kuwapeleka chuo wanafunzi 11,000 waliokosa mkopo mwaka 2020 na wanafunzi 10,000 wanaokadiriwa kuwa wangekosa mkopo mwaka 2021. Kutengwa kwa fedha hizi kutawezesha wanafunzi wote waliodahiliwa katika vyuo vikuu nchini na kuomba mkopo katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuweza kupata mikopo na kutimiza azma yao ya kupata elimu ya juu na kuongeza wasomi wa kada mbalimbali nchini.

Pia Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 125 kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya vyumba vya madarasa (maboma) 10,000 kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza, kila halmashauri itapata maboma yasiyopungua 10. Wanafunzi wengi waliofaulu wamekuwa wanashindwa kwenda kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za Serikali kwa sababu hakuna nafasi au miundombinu haitoshi.

Ikumbukwe kuwa mwaka kesho (2022) taifa linaenda kupata toleo la kwanza la wanafunzi wanaoenda kumaliza darasa la saba na kuanza kidato cha kwanza ambao waliandikishwa kupitia elimu bila malipo kwa shule ya msingi. Fedha hizi ni sehemu ya hatua nzuri kukabiliana na uhitaji wa vyumba vya madarasa nchini.​

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 100 kwa ajili ya zahanati kwenye vijiji na kata (maboma ya afya). Fedha hizi zitahakikisha ujenzi ulioanza na ujenzi mpya unakamilika katika maeneo husika na wananchi hususan maeneo ya vijijini wanapata huduma bora za afya.

Pia Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 50 kwa ajili ya vifaa tiba pamoja na dawa. Utekelezaji huu utaenda sambamba na suala la bima kwa wote.

WIZARA YA MAJI
Serikali imetenga nyongeza ya bilioni 207 kwa ajili ya shughuli za maji na utaratibu wa visima na mabwawa. Kwa sasa Serikali inajielekeza katika utaratibu wa kisima kwa kila kijiji kama ilivyo kwa umeme.

Pia fedha hizi zinatarajia kufanya ununuzi wa magari ya kujimba visima na greda za kuchimba mabwawa.

Mbali na hoja hizo hapo juu, Serikali imesisitiza kuwa inazingatia mambo yote yanayoikabili nchi yetu sambamba na miradi ya kimkakati ambayo ni lazima ipate fedha; Serikali imeona vyema ikafanya utaratibu wa kupata fedha kiasi (fedha za ndani) lakini kwa wakati huohuo itafute mikopo yenye masharti nafuu ambayo haitaipa mzigo mkubwa wa deni kwa taifa letu.

Ndugu watanzania wenzangu kazi ya kujenga nchi yetu lazima ifanywe na sisi sote.​

Nawasalimu kwa jina la Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania.

 
Wale waliokuwa wanapotosha kuhusu tozo ya jengo karibuni mtudadavulie kama ni sahihi au si sahihi
 
Kutenga hayo ma trilioni miaka yote hakunaga shida, hata wakisema ni trilioni 50!!je huwa zinatoka zote?watu miska yote huwa wanashangilia figure kuongezeka, lakini huwa hawajiulizi ile kidogo tu ya mwaka uliotangulia haikufikiwa je hii?!!
Fedha zitatoka zote. Bajeti hii ni ya kimkakati, utekelezaji wa wazi unakuja.
 
Wale waliokuwa wanapotosha kuhusu tozo ya jengo karibuni mtudadavulie kama ni sahihi au si sahihi
Hoja hizo hapo juu ndiyo sahihi. Wengi tulielewa vibaya na kuanza kuishambulia Serikali lakini ufafanuzi umetolewa ambao unatosheleza akili na ufahamu.
 
Hizo ngonjera za kisiasa. Kuna miradi ina zaidi ya mwongo mmoja inatengewa budget na haijakamilika, kila mwaka fungu lipelekwalo ni upembuzi yakinifu.
 
Hizo ngonjera za kisiasa. Kuna miradi ina zaidi ya mwongo mmoja inatengewa budget na haijakamilika, kila mwaka fungu lipelekwalo ni upembuzi yakinifu.
Unaweza kutoa mfano wa hiyo miradi ili tuweze kuijua sote kwa pamoja.
Kazi kubwa imekuwa ikifanyika katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na miradi mingineyo, ni wakati wa kuendelea kusonga mbele bila uoga.
 
Bunge la chama kimoja katu haliweza isimamia serikali. Hata ilete hoja za kienda wazimu watapiga makofi na kuunga mkono hoja.
Mkuu tuache kuwa na mtazamo hasi katika hilo. Bunge lina wabunge wa vyama vingi ikiwemo CCM, CUF, CHADEMA na ACT - Wazalendo. Chama Cha Mapinduzi chini ya ahadi yake namba 8 kinasisitiza juu ya kusema ukweli daima, fitna ni mwiko.

Mara nyingi tumeona wabunge mbalimbali ambao wamekuwa wakiishauri Serikali kwa hoja na Serikali inakubaliana na hoja zao.

Katika Bunge hili la Bajeti Mhe. Nape ni mojawapo ya wabunge ambao hoja zao zimepokelewa na Serikali kwa ajili ya utendaji.
 
Ambazo watawekewa TARURA wajenge barabara au zitaingizwa kwenye ac ya mbunge?kama mbowe alivyokuwa anapigania.
Hizo zinaelekezwa TARURA...ILA HAZITOSHI JAPO KWA KUWA NI MWANZO SIO MBAYA ILA NEXT BAJETI WALAU ZIWE BILLIONI TATU KILA JAMBO ITAKUWA NI HATUA KUBWA
 
Kwa bajeti hii hakuna huo ubabaishaji. Serikali imeazmia kuhakikisha maendeleo jumuishi na endelevu yanapatikana.
Kila mwaka , ngojera hizo zimekuwa zikiimbwa sana!!cha ajabu waziri anasema itabidi tufunge mikanda, huku wazee wa kusifu na kuabudu(wabunge wa ccm) wanatwambia sasa hii ni bajeti ya kurudisha pesa kwa mwananchi, vyuma vimepatiwa grisi wakiongozwa na nape!

Sasa hadi hapo kuna nini!!?huo ubabaishaji utaisha vipi wakati pesa nyingi inaliwa na wajanja!!eti mashine za efd za makusanyo zimepotea! unaingiza 50, zinapotea 70 hapo utegemee maendeleo?ndio maana marais wengi wa Africa wameamua kuwatesa wanyonge ili wapate pesa za bure za IMF/WB kwa kisingizio cha COVID 19!
 
Back
Top Bottom