Ukosefu wa uongozi: Maadili na miiko ya uongozi

Mwamba Usemao Kweli

JF-Expert Member
Oct 5, 2012
744
225
MAADILI ya uongozi ni mwenendo au tabia njema inayokubalika na jamii katika kazi ya kuongoza. Kwa kuwa uongozi ni kazi ya kuwaelekeza watu kwenye kujiletea maendeleo yao kwa utashi wa uhuru, haki na usawa; viongozi lazima wazingatie maadili ya uongozi yanayokubaliana na utashi wa utu, heshima ya binadamu na usawa katika matumizi ya rasilimali za nchi katika kufikia malengo ya ujenzi wa jamii ya watu waliyo sawa na huru.
Hivi ndivyo ilivyodhaniwa kwenye Azimio la Arusha la 1967 na ndio maana uongozi wa awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius K. Nyerere na chama cha ukombozi (TANU) uliamua kwa pamoja kuweka maadili na miiko ya uongozi kama sehemu ya Azimio la Arusha (1967).
Mabadiliko ya sura ya uongozi tangu uhuru (Desemba 9, 1961) hadi wakati huu umeifanya kada ya uongozi wa siasa Tanzania kuwa kazi ya kipato, kama zilivyo kazi nyingine ambazo baadhi ya watu ndani na au nje ya mfumo wa kada ya uongozi wamekuwa wakipigana vikumbo kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi za uongozi kwenye mfumo wa vyama na au wa kushika madaraka ya kuongoza nchi kwenye nafasi zake zote.
Maadili ya uongozi kama dhamana inayotoka kwa wananchi yamegeuka na kuwa satwa ya ujasiriamali wa kisiasa. Wanasiasa wenye uoni wa kijasiriamali wanaodhani kwamba uwekezaji kwenye siasa ni wenye kulipa wamechukua nafasi kubwa kwenye mchakato wa siasa na uandaaji wa nafasi za uongozi ndani na au nje ya mfumo wa siasa, jamii na uchumi.
Kukosekana kwa maadili ya uongozi kwa sehemu kubwa kumesababishwa na hali angavu ya roho iliyochafuka na kushikwa na uchu unaoongozwa na tamaa ya kishetani katika kutafuta “ukubwa” na mamlaka yenye satwa (nguvu) katika kutawala fursa zote zenye taathira katika mchakato wa maisha ya watu na mazingira. Viongozi wa siasa wamepoteza utu na heshima yao kama binadamu anayehitaji utulivu wa nafsi yenye matumaini juu ya kuwatumikia wengine.
Kwa ujumla, kama alivyoandika Sayyid Mujtaba Musawi Lari (1992) kwenye kitabu chake kinachoitwa “Uchunguzi wa Matatizo ya Kimaadili na Kinafsi” binadamu anahitaji kuishi kwa kufuata maadili yaliyokamilika. Lari (1992, ukurasa wa 75) anasema, “mojawapo kati ya misingi na shuruti za maisha ya kijamii na ukamilifu wa kila taifa ni maadili.”
Ndio kusema, hata Azimio la Arusha (1967) lilisisitiza sana “maadili” na miiko ya uongozi ambayo ndiyo yaliyokuwa sehemu ya maisha ya viongozi wa TANU (na CCM baina ya miaka ya 1967 hadi 1992).
Lari (1992) anaonyesha kwamba kama taifa litakosa maadili basi kuna kila dalili ya taifa hilo kuangamia na au kupoteza mwelekeo wa maisha ya saada kimaanawi, kiroho na kimaada. Kwa kuwa binadamu haishi kwa mkate peke yake; bali, kama kiumbe wa kijamii, lazima afuate njia ya uhuru, haki na usawa katika kuelekea kwenye uchaji Mungu ili kwa uchaji huo ipatikane nafasi ya baraka za kiroho katika kufikia malengo makuu na mhsusi ya kuumbwa kwake katika kufanya dunia mahala pa ustawi wa maisha ya sasa katika kuyaendea maisha ya baadaye.
Kwa mtazamo wa uchunguzi wa kisayansi na kwa utumizi wa mantiki ya hoja tunaweza kukubaliana kwamba uongozi (na hususan, uongozi wa siasa) umekosa maadili ya uongozi kwa vile sehemu kubwa ya uongozi wetu na viongozi wengi wamekosa maadili ya uongozi na kuongoza.
Mara kadhaa wametokea watu kuukosoa uongozi wa nchi yetu. Japokuwa ukosozi huo huonekana kana kwamba ni chuki binafsi zinazoelekezwa kwa watu binafsi kwenye mfumo wa uongozi kutokana na inda (chuki ya mtu dhidi ya mafanikio ya mwingine).
Hata kama, kwa sehemu fulani wapo wanaodhani kwamba ukosefu wa uongozi wenye maadili ya uongozi na ukosozi wake huchukua sura ya chuki binafsi; kuna ukweli wa moja kwa moja na wa kisayansi unaoonekana kwa kushindwa kwa uongozi unaoongoza shughuli za serikali kufika utashi wa uongozi bora.
Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kuandika kitabu juu ya uongozi na hatma ya Tanzania wakati wa mgogoro wa uongozi wa awamu ya pili kipindi cha miaka ya 1990 na 1995.
Mwalimu Nyerere alijaribu kuonyesha upungufu uliyojitokeza kwenye sehemu ya pili ya awamu ya pili kutokana na kutelekezwa kwa Azimio la Arusha la 1967 na siasa kugeuzwa “ujasiriamali.” Hata hivyo, ukosozi wa Mwalimu Julius K. Nyerere haukuchukuliwa kwa vile “kitabu chake kilikwishapita, na enzi hiyo ilikuwa na kitabu kingine.”
Siasa iliendelea kuwa mwendo mdundo kila kiongozi akitafuta kuwekeza kwenye ujasiriamali wa kisiasa (political entrepreneurship) kwa kuwa ilishaonekana wazi kwamba uongozi wa siasa utachukua nafasi muhimu kwenye miaka ya kuanzia 2005 na kuendelea; hali tunayoishuhudia sasa!
Mwaka 2008, kama miaka mitatu tangu kuanza kwa awamu ya nne, Profesa Ibrahimu Haruna Lipumba na yeye (kama mwanafalsafa na mwanasiasa) aliandika hotuba juu ya “ukosefu wa uongozi na hatma ya Tanzania.”
Kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere ndivyo ilivyokuwa kwa Profesa Lipumba, ukosozi wake ulionekana pumba na kama kawaida uongozi wa chama tawala uliendelea na mwenendo uleule usiyozingatia mabadiliko ya uongozi wenye tija kwa kuzingatia utashi wa watu na maendeleo yao kwa kuzingatia uongozi wenye maadili yaliyotukuka.
Hali tete ya ukosefu wa maadili imeendelea kuishika Tanzania. Hata sasa, hali ya ukosefu wa maadili ya uongozi imechukua sura mbaya zaidi kwa vile viongozi wengi wamepoteza maadili ya utu na heshima ya binadamu imemezwa na shetani anayewaongoza kwenye ufisadi mpevu.
Kwa muhtasari, tujaribu kufuatana katika kuangalia matatizo ya kimaadili na kinafsi yanayowakabili viongozi wengi wa Tanzania waliyekabidhiwa dhima ya kuongoza shughuli za serikali ya watu kwa niaba ya wananchi.
Katika matatizo ya kimaadili kumi na sita (16) kama yalivyoainishwa na Lari (1992) kwenye kitabu chake; sehemu ya matatizo kumi na moja (11) ya matatizo hayo yanapatikana kwa viongozi wa Tanzania!
Hili linaweza kukusitua msomaji; hata hivyo, hiyo ndio hali halisi! Kama tutayachukua matatizo ya kimaadili yanayowakabili vongozi wengi ndani na au nje ya mfumo rasmi wa uongozi wa serikali tunaweza kuona kwamba asilimia 68.75 (kama 69%) ya matatizo aliyoyaorodhesha na kuyachambua Lari (1992) yangalipo. Huu ni msiba mkubwa kwa taifa!
Viongozi wengi ni waongo! Pasipokuwa na chembe ya kuogopa dhambi ya uongo, wengi wa viongozi wamekuwa wakichukua viapo vya uongo na kushindwa kutafakari madhara yake.
Uongo wa viongozi wengi, kwa mujibu wa uchunguzi na mantiki, unasababishwa na tamaa au tabia chafu ya mazowea ya kudanganya! Wanatumia uongo kwa vile haijawahi kushuhudiwa viongozi wakiwekwa mtu-kati katika kuthibitisha tabia hii ambayo ndio inayowafanya wananchi wengi kuishi kwa kutegemea uongo kama sehemu ya mila na dasturi kwa vile wanawaona viongozi wao wakishiriki na kunufaika na uongo wa kimaslahi. Viongozi wengi wamekuwa wahaini kwa nchi na watu wake kutokana na uongo!
Unafiki, kama ugojwa mbaya wa kimaadili, umewashika viongozi wengi wa Tanzania! Kwa ujumla, kama falsafa ya unafiki ilivyo; viongozi wengi ni wepesi wa kutoa ahadi lakini si watekelezaji. Uongozi wa Tanzania umekuwa hodari wa kutoa ahadi nyingi kuliko uwezo wa utekelezaji wa ahadi hizo kutokana na ufinyu na au matumizi mabaya ya rasilimali.
Kutokana na ahadi za kinafiki zinazotolewa na viongozi wa siasa wakati wa kampeni za uchaguzi wananchi wamekuwa wakiwapa ridhaa ya kushika nafasi za uongozi kwa dhana kwamba yale yaliyoahidiwa kwenye ilani za uchaguzi yatafanyiwa kazi.
Kinyume chake, viongozi wengi wamekuwa wakifanya hiana pamoja na kuchukua ahadi ya kutekeleza ahadi na viapo vyao. Viongozi wengi hawasemi ukweli; isipokuwa husema uongo! Uongo umekuwa sehemu ya maisha ya uongozi wa siasa; na ndio maana wapo baadhi ya wanafalsafa wameshaanza kuiona siasa kuwa “mchezo mchafu.”
Sifa nyingine mbaya ya kimaadili waliyonayo viongozi wengi wa siku hizi ni udhalimu. Wengi wa viongozi wa serikali katika ngazi zote wana tabia ya kuwakandamiza wanyonge wanaohitaji huduma kama sehemu ya haki ya wananchi kutoka kwa viongozi (na watendaji) waliyepewa dhamana ya kuwatumikia kwa uhuru, haki na usawa.
Hali hii, pamoja na mambo mengine, ndio chanzo cha ufisadi wa kimfumo na wa ndani ya mfumo. Chimbuko la rushwa, hongo, chirimiri, kadhongo, na kuzunguka mbuyu ni kutokana na udhalimu wa moja kwa moja katika kukandamiza uhuru, haki na usawa wa kutoa huduma bora kwa wananchi kwa mujibu wa utashi wa sheria, kanuni na taratibu za kazi ya kusimamia menejimenti ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kutokana na hali ya kutokuwepo upendo baina ya viongozi na wananchi, roho mbaya na kinyongo miongoni mwa viongozi na wananchi wanayedhulumiwa huamsha chuki na uadui ndani ya jamii.
Kwa kutamani hali ya kukomaa kwa chuki na uadui kwa maslahi ya kibinafsi kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa, kijamii na kiuchumi wamekuwa mstari wa mbele katika kuchochea sintofahamu, songombingo au sokomoko za kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kwa hali hiyo wapate kujijenga kisiasa na kuchukua nafasi ya kutawala kwa kutumia matukio!
Mchezo huu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa siasa ni wa hatari kwa vile wananchi wanatumiwa kama kondoo wa kafara katika kufikia malengo ya kisiasa!
Uchunguzi wa mwandishi (kwenye mazingira ya demokrasia ya siasa za vyama vingi) umegundua kwamba sehemu kubwa ya viongozi wana ugonjwa wa kinafsi wa hamaki!
Wengi wa viongozi wa siasa hawana uwezo wa kudhibiti hasira zao; na mara nyingi, viongozi waliyeghadhibika huonyesha hasira hadharani na hata wakati mwingine kushindwa kutumia busara na kuishia kutukana matusi (ya nguoni) au kutoa lugha chafu na kashfa! Hapa ndipo walipofika wengi wa vingozi wengi wanaotegemewa kuwa wakomavu na wenye uwezo wa hali ya juu kwa kudhibiti hamaki! Ifahamike hapa kwamba, “mwanzo wa hasira ni wendawazimu na mwisho wake ni majuto.”
Wapo baadhi wa viongozi waliyejikuta wakihamaki na kufanya maamuzi yasiyozingatia uhuru, haki na usawa na kujikuta wakijiingiza kwenye migogoro ya kimaadili.
Kwa kuwa viongozi wengi wa Tanzania ni watu wanaopenda sana kuchuma na kulimbikiza mali kama mtaji wa ujasiriamali wa kisiasa; wengi wao, kama wanavyoshuhudiwa siku hizi, wamekuwa na tamaa ya hali ya juu katika kuvuna na kuhifadhi utajiri hususan kwa njia haramu na za kifisadi.
Hali hii inawafanya wengi wao kuwa na tabia ya ubahili na kushindwa kuwasaidia wananchi wanaowaongoza katika kujinasua kutokana na umasikini wa kipato. Hakuna kiongozi anayefanyakazi ya kuwatafutia wananchi suluhisho la kudumu la matatizo na au changamoto za hali mbaya ya uchumi.
Kama wapo, ambao ni wachache, ni wale wanaowapa wapiga kura wa maeneo yao misaada midogo wanapopatwa na majanga ya asili na au kutoa usaidizi wa elimu, mtibabu au maji pale wanapoombwa kufanya hivyo.
Tamaa ya kupenda sana na au kutaka sana ndiyo inayowafanya viongozi wengi kufanya vyovyote na kwa “liwalo na liwe” katika kutafuta uwezo wa hali na mali katika kujenga uwezo wa kutawala mchakato na mfumo wa siasa na upatikanaji wa viongozi ndani ya na au nje ya chama na hatimaye serikalini.
Kutokana na sababu za kimaumbile; tamaa ya kupita kiasi katika kutafuta uongozi kwa jinsi yoyote iwayo ndiyo inayowavuta wengi wanaotafuta nafasi za kungia kwenye msongo wa uongozi wa chama (kinachotawala) na ndani ya uongozi wa utendaji wa serikali kuwa kama mbwa-mwitu au tai anayesubiri kurarua!
Hata kama, wananchi wenye mamlaka ya kuwapa madaraka viongozi nafasi za kuongoza, wakitumia nafsi yao ya kisheria, viongozi wenye tamaa iliyopitiliza hutumia ushawishi wa nguvu ya fedha zilizochumwa kifisadi kupora nguvu ya kisheria waliyonayow ananchi.
Mwenendo huu wa kijamii, kisiasa na kiuchumi ndio unaoifanya Tanzania ya leo iwe kama “shamba la bibi.” Kila mwenye nafasi ya kutamani kushika nafasi ya juu kwenye uongozi wa ndani ya chama kinachotawala na au ndani ya mzingo wa utendaji wa kiserikali katika menejimenti ya uchumi na jamii atatafuta nafasi ya kuvuna mali nyingi na kutafuta umaarufu kwa njia yoyote iwayo alimuradi apate nafasi ya kuwa “bwana mkubwa.”
Mchakato wa kutafuta “ukubwa” na “uheshimiwa” umewaroga viongozi wengi wa siasa, jamii na uchumi hadi kutaka wasujudiwe na wananchi masikini!
Huu ni ushenzi wa kimaadili uliyopitiliza! Si ajabu kuwakuta vijana wachanga (mabwana wadogo) watoto wa viongozi (vigogo) ndani ya chama na au serikalini wakitafuta utajiri (wa hali na mali) katika kulinda na au kutetea nafasi za wazazi wao ndani na au nje ya mfumo wa uongozi!
Baba anarithisha ushenzi wa kimaadili kwa kizazi chake; na mama na yeye anafanya vivyo hivyo, kama baba afanyavyo! Kama chama kinageuzwa kampuni la wenye hisa, na wale wenye hisa nyingi ndio wanakuwa wamiliki wa uongozi kwa jinsi wanavyoweza kununua nafasi za uongozi au kuwanunulia watu wanaowataka kuwa viongozi kwa vile wapendavyo wao (wenye ushawishi wa hali na mali). Uongozi umefanywa sehemu ya kinyang’anyiro cha hila na mizungu ya uharibifu wa kimaadili usiyozingatia uhuru, haki na usawa wa kiakili, kiroho na kimaanawi.
Binadamu hakuumbwa aishi kama mnyama wa porini; hata wanyama (wa porini) wamewekewa sheria, kanuni na taritibu za kimambile ambazo shuruti (lazima) wazifuate katika kuyaendea maisha yao kama wanyama, sembuse binadamu?!
Sura ya viongozi wengi inaonyesha kwamba wengi wamebobea kwenye uwongo, unafiki, takaburi (kiburi na jeuri), udhalimu, chuki na uadui, hamaki, hiana, ubahili, tamaa, na mabishano.
Matatizo haya yote ya kimaadili ndio yanayoufanya uongozi wetu ushindwe kufikia malengo ya usimamizi mzuri wa menejimenti ya rasilimali za Tanzania katika kuendesha mapambano dhidi ya maadui wa taifa ambao ni: umasikini; ujinga; maradhi; na ufisadi. Inawezekana kubadilisha hali ya uongozi wetu; wananchi wanapaswa kuchukua nafasi yao. Uongozi wa kiroho ni wajibu kufundisha kwa uhuru, haki na usawa juu ya dhima ya viongozi kwa wananchi. Kwa jinsi hiyo, tamko la kichungaji lililotolewa tarehe 18 Agosti, 2010 mjini Dodoma na viongozi wa dini lilihitaji usimamizi makini na madhubuti.
Kwa ujumla, viongozi wengi wa siasa wamekosa sifa zilizoainishwa na viongozi wa dini, yaani: (1) ucha Mungu; (2) kujali na kuwastahi watu; (3) kupenda haki na kuwajli wanyonge; (4) kuijua na kuitetea Katiba ya nchi; (5) ukweli wa maneno na matendo; (6) kushirikiana na wananchi wote bila ya ubaguzi; (7) uwezo wa kuongoza na upeo mpana; (8) kupenda amani na utulivu; (9) uadilifu; na (10) moyo wa uzalendo na kulipenda tiafa lake! Sifa zote hizi; zaidi ya silimia 60 hazipo! Tuna wajibu wa kutafakari tulipokosea; nasisitiza, tulikosea, na ni wajibu tutafute njia ya uhuru, haki na usawa katika kutafuta ufumbuzi wa uadilifu kama taifa. Hatujachelewa sana; japokuwa tumeshaumia kwa miaka 30 sasa; tujiandae kuleta mapinduzi ya fikra.


WADAU:​

Mwandishi wa makala hii anaitwa Bakari M Mohamed anapatikana kwa simu +255 713 593347 au barua Barua pepe: maligwa1968@yahoo.com


SOURCE: TANZANIA DAIMA

MY TAKE: 100% VEMA nimempa huyu mtaalamu wetu kwa uchambuzi makini ulioenda shule na kama viongozi wetu watajaribu kutafuta chanzo cha mmomonyoko wa maadili ambacho kinafahamika sana kwa wasiasa wetu, na kupambana nacho, tutafanikiwa kulikomboa taifa letu la Tanzania kutoka katika umaskini.

Naomba mchangie wadau.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom