Ukosefu wa Mbinu za Kibiashara bado ni tatizo kwa Wakulima kufikia masoko Nchini

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99
WADAU wa uzalishaji wa mazao ya Viungo, Mboga na Matunda Zanzibar wamesema ukosefu wa taaluma na mbinu sahihi za kibiashara bado ni kikwazo kikuu kinachokwamisha wakulima wengi nchini kushindwa kuyafikia masoko na kupelekea kukosekana kwa uhakika wa uendelevu wa biashara za mazao ya kilimo kwa wakulima.

Walieleza hayo wakati wa mafunzo ya biashara na masoko kwa wazalishaji wa mazao kupitia mradi wa VIUNGO Zanzibar yaliyolenga kuwajengea uwezo wazalishaji hao kutambua mbinu bora za kibiashara katika kuyafikia masoko na kukuza vipato vya wakulima nchini.

Walisema licha ya wakulima kutumia muda na nguvu kubwa katika uzalishaji wa mazao mbalimbali lakini nguvu hizo zinashindwa kuleta tija kwao kutokana na mazao mengi yanayozalishwa hukosa soko la uhakika kwa wakati na kusababisha hasara kwa wazalishaji.

Kibano Omar Kibano, mzalishaji wa mazao ya Viungo kutoka Wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba alieleza kuwa kutokana na changamoto ambazo wakulima wanakabiliana nazo wakati wa kutafta masoko imepelekea wengi wao kukata tamaa kuendelea na uzalishaji.

“Wakulima wengi tunazalisha sana lakini tunakosa uelewa wa namna ya kuyafikia masoko baada ya kuzalisha nahii inapelekea kupata hasara kubwa kwani mazao mengi yanaharibikia shambani kwa kukosa wanunuzi jambo ambalo kwakweli linaturejesha nyuma,” alisema Kibano.

Nae Hamida Khamis Faki mkulima wa Mboga alieleza matumaini yake na mradi wa VIUNGO kuwa kupitia mafunzo ambayo wakulima wanapatiwa ya uzalishaji bora wa mazao na namna ya kufikia masoko itasaidia kuondoa kikwazo hicho cha muda mrefu kwa wakulima nchini.

Alieleza, “tunashukuru mradi huu unaanza kuonesha mwanga na kurejesha matumaini kwetu kwani kwa muda mrefu tumekuwa tukiumia kwa kutumia nguvu nyingi kuzalisha pasipo kuwa na faida jambo ambalo hutukatisha sana kuendelea na shughuli hizi.”

Omar Mtarika, afisa biashara na masoko wa mradi wa VIUNGO Zanzibar unaotekelezwa kwa mashirikiano ya taasisi za People’s Development Forums (PDF), Community Forests Pemba (CFP) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, (TAMWA Zanzibar) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) alihimiza wakulima kujenga utaratibu wa kufaya utafiti wa mahitaji ya soko kabla ya kuzalisha ili kuepukana na changamoto za ukosefu wa soko kutokana na kuzalisha bidhaa zisizoendana na mahitaji.

Alisema wakulima kuzalisha mazao kwa mazoea bila kufuatilia mahitaji ya bidhaa sokoni bado ni kikwazo na ndicho hupelekea wakulima wengi kupata hasara katika mazao wanayozalisha.

Alifahamisha kuwa kutokana kubainika kuwepo kwa changamoto hiyo, mradi umeandaa mafunzo hayo kwa lengo la kuwawezesha wakulima kuwa na ujuzi wa kutambua mbinu za kibiashara ili ziwasaidie kuondokana na vikwazo vinavyowarejesha nyuma katika shughuli za kilimo.

Alisema, “mradi umeandaa mafunzo haya kwa lengo la kuongezea uelewa wa kibiashara kwa wakulima kufahamau taratibu za mauzo ili kufanya biashara ya kilimo kuwa endelevu na zenye uhakika wa mapato kwao.”

Alitaja changamoto nyingine inayowakabili wazalishaji nchini kuwa ni ukosefu wa mbinu na taaluma ya utunzaji bora wa mazao wakati wa mavuno jambo linalopelekea mazao mengi kuathiriwa na kuharibika katika kipindi cha mavuno na utunzaji.

“katika utafiti ambao tumefanya tumegundua bidhaa nyingi za wakulima huanza kuharibika na kupoteza ubora wake kipindi cha mwisho hasa wakati wa uvunaji na utunzaji wake kwaajili ya kupeleka sokoni, na hii ni kutokana na wakulima wengi hawana taaluma ya utunzaji bora wa bidhaa za kilimo kwa kuzingatia viwango stahiki,” alisema Mtarika.

Alifahamisha kuwa ili bidhaa iweze kukidhi vigezo kuingia katika soko la ushindani hasa kimataifa ni lazima izingatie viwango vya ubora na usalama wa bidhaa husika ambapo upatikanaji wake huanzia kwenye uzalishaji na utunzaji wake na hivyo mradi unatoa mafunzo kwa wakulima kuwa na ujuzi wa kuzingatia vigezo sahihi ili kuwa rahisi kwao kuyafikia masoko kwa ubora unaotakiwa.

Alieleza, “kupitia mradi huu, wakulima wanahimizwa kufuata mbinu bora za uzalishaji na uvunaji wa mazao bora ili kuwezesha bidhaa zenu kufika sokoni zikiwa katika ubora wake, kwahiyo wakati tunaenda kwenye kilimo cha biashara ni lazima tuzalishe kwa kuzingatia mahitaji na vigezo vyote vya usalama wa chakula.”

Mafunzo ya biashara na masoko kwa wakulima Pemba yameshirikisha vikundi 15 vya wazalishaji wa Mboga, Matunda na Viungo ambapo pia washiriki wamepata fursa ya kujifunza mbinu za kutambua gharama za uzalishaji, upangaji wa bei Pamoja na mfumo wa mpango biashara kwa wakulima hao.

Mradi wa VIUNGO ni mradi wa kilimo cha Mboga, Matunda na Viungo, ambao unatekelezwa Zanzibar kwa mashirikiano ya taasisi za People's Development Forums, (PDF), Community Forest Pemba (CFP), na Chama Cha Waandishi Wa Habari Wanawake Tanzania, (TAMWA Zanzibar kupitia mpango wa AGRICONNECT kwa ufadhili wa Umoja Wa Ulaya (EU).
 
Back
Top Bottom