Uko wapi uaminifu na uadilifu?

Mar 3, 2008
13
0
Na Mwandishi Maalum

NIMEFUATILIA kwa siku nyingi sana kelele zinazopigwa na viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu kile kinachoitwa kuwa ni "kashfa" ya Richmond na ile ya kuchotwa kwa shilingi bilioni 133 kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kinyume cha taratibu.

Sina sababu ya kuhadithia upya kuhusu kashfa hizo, bali ninataka kuzungumzia hatua ya viongozi wa CHADEMA ya "kuzishikia bango" na kutumia kivuli hicho kuficha ubadhirifu wa mamilioni ya fedha wanaofanya katika chama chao.

Wanachama waliojazwa imani kuwa chama chao kinaongozwa na viongozi waadilifu katika matumizi ya mamilioni ya fedha za ruzuku na zile zinazotoka kwa wahisani na wafadhili wamekuwa mstari wa mbele kushangilia kila tamko linalotolewa kwa namna moja ama nyingine na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Aikaeli Mbowe; Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Peter Slaa; Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Zitto Zuberi Kabwe na Mkurugenzi wa Taifa wa Vijana, John John Mnyika.

Tathmini ya uhakika inaonyesha kuwa viongozi hao wanne ndio wamekuwa vinara wa kutengeneza na kuhubiri kila aina ya uzushi na uongo dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, na pia wanataka wanaonekane wajuzi na wataalamu mabingwa wa kutetea raslimali za taifa na Watanzania.

Pamoja na kufanya hivyo mara kwa mara kwa kutumia majukwaa ya siasa mikutanoni, vyombo vya habari na intaneti, ukweli kuwa lengo lao hasa ni kutaka sifa kwa faida zao wenyewe unaweza kuthibitishwa kwa namna nyingi, moja kati ya njia hizo ukiwa "udandiaji" wa kila "ishu" inayofanywa na serikali na kuipotosha kwa kadri wawezavyo.

Ndivyo alivyofanya Mbowe alipowahutubia akina mama wa CHADEMA kwenye ukumbi wa Urafiki, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati akiwahutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hivi karibuni.

Si lengo langu kuwasemea wanachama wa CHADEMA kuhusu vilio vyao vya chini chini kutokana na woga wanaojazwa, lakini ukweli kuwa chama hicho hakina nidhamu ya matumizi ya fedha za ruzuku na wahisani yamewahi kulalamikiwa hadharani na Mwenyekiti wa Chama hicho wa mkoa wa Mara, Chacha Zakayo Wangwe mwishoni mwa mwaka uliopita.

Pamoja na mambo mengine, Wangwe alikuwa akipigania ruzuku iende kwa wanachama katika matawi, kata, wilaya na mikoani zikaijenge CHADEMA kuliko hali iliyopo hivi sasa ambapo fedha hizo za walipa kodi zimekuwa "zikitafunwa" na viongozi waandamizi utadhani zinaliwa na mchwa katika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.

Nakubaliana kwa asilimia 100 na hoja hiyo ya Wangwe ambaye hata hivyo inasikitisha kuona alipochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kelele zake hizo zimekwisha, badala yake ameungana na kundi hilo ambalo wakati akiwania nafasi hiyo alikaribia kulisambaratisha kama kishada kilichokwenda harijojo.

Je, yuko wapi Wangwe aliyekuwa mpinzani mkubwa wa matumizi ya helikopta inayoonekana kuwa ya Mbowe zaidi badala ya CHADEMA ingawa inakodiwa kwa shilingi milioni tatu kwa siku zinazolipwa na chama, lakini ambayo kama Mbowe hayupo nchini haikodiwi hata kuruka kwa dakika tano tu?

Yuko wapi Wangwe aliyekuwa kinara wa mapambano dhidi ya matumizi mabaya ya ruzuku inayofujwa kwa idhini ya Ofisi ya Katibu Mkuu, yule ambaye anapokwenda Karatu ama bungeni anajifanya ana uchungu mkubwa na fedha za walipa kodi, lakini anapokuwa Makao Makuu ya CHADEMA anasimamia ubadhirifu anaodai kuupinga mikutanoni?

Yuko wapi Wangwe aliyekaribia kusababisha Zitto na Dk. Slaa wajiuzulu nyadhifa zao wakidai wamedhalilishwa, yule ambaye alipokuwa akitafuta achaguliwe kuwa Makamu Mwenyekiti alikuwa na ujasiri mkubwa wa "kupasua" ukweli na kuanika maovu yote yanayofanywa katika chama chake?

Je, inawezekana kwamba amenyamaza baada ya jina lake kuingia katika orodha ya "vigogo" wanaolipwa fedha nyingi za mishahara katika Makao Makuu ya CHADEMA huku wakidai ni posho ili kuwazubaisha wasiolipwa hata senti tano waliopo kwenye matawini, kata, wilaya na mikoani?

Mbali na kaka yangu Wangwe, nashindwa pia kujua kinachosababisha Mkurugenzi wa Taifa wa Vijana, John John Mnyika asipinge wala kusema chochote kuhusu matumizi ya ovyo ya fedha za ruzuku, lakini kama Wangwe inawezekana pia anafanya hivyo kwa sababu naye ni mmoja wa wakurugenzi wanaolipwa malaki katika mishahara yao huku wakicheza "danganya toto" kwa kudai eti kwamba wanajitolea!

Wanaodhani Mnyika ni kiongozi mwenye uchungu wa kweli na fedha za walipa kodi anapopiga kelele za EPA, Richmond ama mkataba wa Buzwagi na kuanza kumshangilia kwa nderemo na hoihoi hawajui kwamba ni mjumbe wa vikao vyote vya Sekretarieti, Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Taifa huku pia mara kwa mara akikaimu Ukatibu Mkuu wa Chama; lakini hata siku moja tu hajawahi kupendekeza kuwa mamilioni ya fedha hizo za ruzuku "yanayotafunwa" kwa fujo yatengenezewe mfumo wa kutumika mpaka matawini.

Simwelewi Mnyika anapopiga kelele nyingi magazetini akitangaza "utakatifu" wa kisiasa huku akishindwa kuzuia ubadhirifu uliokithiri katika chama chake, akashiriki kudhulumu wanachama na viongozi wanaosota matawini, kata, wilaya pamoja na mikoa ingawa ni wao waliofanya kazi kubwa zaidi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na hatimaye kukiwezesha kupata ruzuku inayokaribia shilingi milioni 100 kila mwezi.

Wakati akiwa sehemu ya wateule wachache kabisa wanaofaidika na fedha hizo, Mnyika mwenyewe ni shahidi kwamba hakuna cha maana anachowafanyia vijana wa CHADEMA iwe Dar es Salaam, Kigoma, Arusha, Ruvuma, Tanga, Pemba na kadhalika.

Kama anabisha atuambie mwaka jana alifanya ziara ngapi za kikazi katika na mikoa ipi ili tuone iwapo kweli ni Mkurugenzi wa Taifa wa Vijana wa CHADEMA na siyo Mkurugenzi wa Taifa wa Mafaili Ofisini, kisha aseme katika ziara hizo alibeba agenda zipi za kukijenga chama hicho ili tujue kama anapokea mshahara kwa haki hata bila kuhoji posho nyingine.

Aseme amekwenda wilaya zipi nchini katika kipindi angalau cha miezi sita tu iliyopita ili kuwahamasisha vijana wa CHADEMA wazidi kushikamana, vinginevyo atueleze amehutubia mikutano mingapi ya hadhara katika kipindi hicho kama hashindi tu ofisini "akicheza" na intaneti akidhani atamwezesha rafiki yake Mbowe kushinda urais mwaka 2010.

Hata kwa siasa dhaifu kiasi gani haiwezekani kwa kiongozi mwandamizi kama yeye ategemee kujenga chama ili baadaye kije kushinda uchaguzi mkuu kwa makala za intaneti huku takribani zote zikisheheni uongo na uzushi dhidi ya CCM na serikali yake.

Ni Watanzania wangapi wanaoishi mijini wanatumia intaneti iwe kwa shughuli zao wenyewe ama za kikazi ili awe na imani ya wapiga kura kuzisoma makala zake anazoandika huko na kutarajia ushindi mwaka 2010? Au, ni kijiji gani nchini ambako wananchi wamewahi angalau tu kusikia neno linaloitwa intaneti achilia mbali kujua maana au hata shughuli zake?

Wanaodhani Mnyika ana mchango mkubwa kwa CHADEMA hawapembui mambo kwa upana, na pia inawezekana ni wavivu wa kufikiri na hivyo wao wenyewe ni kama usiku wa giza.

Inawezekana wanachama na viongozi wa CHADEMA waliopo kwenye matawi, kata, wilaya pamoja na mikoa hawajui kama chama chao kinapata mamilioni ya fedha za ruzuku, yale ambayo badala ya kukijenga "yanatafunwa" na viongozi na maofisa wa makao makuu huku wakidanganywa na kuaminishwa kuwa chama kinaendeshwa kwa kufadhiliwa na Mbowe, Edwin Mtei, Philemon Ndesamburo na matajiri wengine rafiki.

Kama Mbowe na Dk. Slaa ni viongozi waadilifu na waaminifu katika pesa waonyeshe mgao wa ruzuku ya karibu shilingi milioni 100 inavyotumika katika chama chao, waseme makao makuu inatumia kiasi gani kila mwezi na mikoani zinakwenda kiasi gani ili kulipia kodi za ofisi na mahitaji mengine, vinginevyo wamsute uso kwa uso Chacha Wangwe kuwa ni muongo aliposema hakuna chochote kinachopelekwa.

Nasema kifua mbele na bila mashaka yoyote kwamba kitu pekee kinachosaidia kuficha ufisadi uliopo CHADEMA ni ukweli kuwa chama hicho "kipo kama hakipo", kwamba ukiondoa pale panapoitwa makao mkuu kulikobaki kote ni sawa na sufuri.

Endapo kingekuwa kikubwa kama CCM, ukweli kuwa mamilioni ya fedha za ruzuku "yanayotafunwa" na viongozi wa makao makuu utadhani zaka ungekuwa umeshafichuka.

Ndiyo maana ukifika hapo hakuna agenda yoyote ya kukijenga chama ili kiwe na nguvu isipokuwa watu wako "bize" kuandika makala za uzushi katika intaneti, na pia hakuna mkakati wowote wa muda mrefu wala mfupi unaolenga kukiinua kiuchumi ili kisiwe ombaomba kupita kiasi. Kubwa linalofanywa na viongozi waliopewa madaraka ya kitaifa ni kujijenga wenyewe ikiwemo kujilipa mamilioni ya fedha za ruzuku pamoja na kutoka kwa wahisani na wafadhili.

Wanaobisha kuhusu ukweli huu wamuulize Wangwe imekuwaje ageuke bubu muda mfupi tu baada ya kuchaguliwa kwake kuwa Makamu Mwenyekiti miezi mitatu iliyopita. Aseme kwa nini ameachana kabisa na mapambano ya kupinga kwa nguvu zake zote ubadhirifu mkubwa wa ruzuku unaozidi kushika kasi katika makao makuu ya CHADEMA.

Wahoji inakuwaje chama kinakodi helikopta kwa shilingi milioni tatu kwa kila dakika 60 inazoruka angani huku wakati huohuo kikishindwa kupeleka angalau tu shilingi elfu tatu kwa mwezi katika kila mkoa hata kama ni mara mbili kwa mwaka.

Waulize ni nani ameidhinisha maofisa wa makao makuu ya chama hicho wanaotaka kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 wajigawie kabisa majimbo watakayokwenda kuwania nafasi hiyo utadhani wanachama wote waliopo huko hawana mbele wala nyuma.

Waulize kikao gani kiliketi na kuidhinisha wawe wanalipwa shilingi milioni moja kila mmoja kwa kufanyiana zamu utadhani wake wenza kwa mume wao huku wanachama waliopo kwenye matawi, kata, wilaya mpaka mikoa wakitengwa katika mgao huo wa ruzuku ambayo mwaka 2005 walishiriki kwa nguvu zao zote kuihangaikia.

Waombe kuonyeshwa sheria ya ruzuku inayoruhusu fedha hizo zitumiwe na viongozi wa makao makuu kwenda katika majimbo wanayotoka na kufanyia maandalizi ya kuwania ubunge mwaka 2010.

Wakati hayo yakifanyika kwa siri na tahadhari, "vigogo" wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Aikaeli Mbowe; Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Peter Slaa pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Zitto Zuberi Kabwe wamekuwa wakiwadanganya Watanzania eti kwamba hawana mawaa.

Mpaka hapo uko wapi uaminifu na uadilifu wao katika chama chao kwanza ili tuweze kuziamini kauli zao wanapozungumza kwa ukali kuhusu Richmond au EPA?

SOURCE: GAZETI LA TAZAMA

Nakufagilia Mwandishi Maalum. Endelea kuwapasha ukweli kina Mbowe, Dk. Slaa, Zitto na Mnyika ambao wanajifanya vinara wa kupigia kelele EPA na Richmond ili kuwa kichaka cha kufichia uovu wanaowafanyia wanachama na viongozi wa Chadema waliopo nje ya makao makuu.

Mfano mwingine mzuri ni majuzi tulipoona Mbowe alivyokopa fedha kutoka NSSF, lakini badala ya kulipa kulingana na masharti ya mkopo aliyoyakubali mwenyewe wakati anachukua fedha hizo mwaka 1990 hivi sasa analeta ujanja wa kutumia mahakama akitaka imwidhinishie matakwa yake ya kifisadi ya kutotaka kulipa.

Kama riba anayopaswa kulipa siyo ya kawaida, ina maana alitia saini mkataba wa mkopo huo akiwa amelala usingizi au alikuwa hajui kusoma na hivyo hakuelewa nini kimeandikwa, akasomewa na kudanganywa, kisha akaweka tu dole gumba?!


Na Mwandishi maalum
 
Naomba niseme tu kwamba mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa hapa TZ.Ninachotaka kusema mimi ni kwamba haya malumbano yasiyokua na miguu wala kichwa hayajeni TZ tunayoitaka sisi.

Vyama vyote mimi navifahamu katika level ya taifa hadi huko vijijini na mimi ni mzaliwa wa kijijini pure.Unaposema CHADEMA hawapeleki pesa vijijini hili mimi nalikubali kwa asilimia miamoja.Lakini tufanye kazi kama msumeno,CCM ndio inapeleka ruzuku yake vijijini au tunakulupuka tu kusema CCM inapeleka ruzuku yake vijijini.Hivi hali ya wenyeviti huko vijijini mnaijua au?

Kama kuna mwana ccm mwenye data kwamba mshahara kwa wahusika ni kiasi fulani aseme kama moto hautawaka.Mimi nadhani tungelenga sana maslahi ya taifa kwa ujumla wake.Lakini kama ni kuoza kwa vyama nadhani CCM inaongoza.

Huko vijijini kwa vyama vyote vya siasa mnatufanyia usanii tu.Hebu angalieni samani zinazotumika mijini na vijijini ni tofauti kabisa.Ni chama gani kimepeleka Shangingi kijijini basi hata kama sio shangingi,ni chama gani kimepeleka hata baiskeli kwa wenyeviti wao huko vijijini..Jamani tusidanganyane,vyama vyote huko vijijini ni uozo tu.IPO SIKU MOTO UTAWAKA.
 

Attachments

  • image008.jpg
    image008.jpg
    29.4 KB · Views: 50
Naomba niseme tu kwamba mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa hapa TZ.Ninachotaka kusema mimi ni kwamba haya malumbano yasiyokua na miguu wala kichwa hayajeni TZ tunayoitaka sisi.

Vyama vyote mimi navifahamu katika level ya taifa hadi huko vijijini na mimi ni mzaliwa wa kijijini pure.Unaposema CHADEMA hawapeleki pesa vijijini hili mimi nalikubali kwa asilimia miamoja.Lakini tufanye kazi kama msumeno,CCM ndio inapeleka ruzuku yake vijijini au tunakulupuka tu kusema CCM inapeleka ruzuku yake vijijini.Hivi hali ya wenyeviti huko vijijini mnaijua au?

Kama kuna mwana ccm mwenye data kwamba mshahara kwa wahusika ni kiasi fulani aseme kama moto hautawaka.Mimi nadhani tungelenga sana maslahi ya taifa kwa ujumla wake.Lakini kama ni kuoza kwa vyama nadhani CCM inaongoza.

Huko vijijini kwa vyama vyote vya siasa mnatufanyia usanii tu.Hebu angalieni samani zinazotumika mijini na vijijini ni tofauti kabisa.Ni chama gani kimepeleka Shangingi kijijini basi hata kama sio shangingi,ni chama gani kimepeleka hata baiskeli kwa wenyeviti wao huko vijijini..Jamani tusidanganyane,vyama vyote huko vijijini ni uozo tu.IPO SIKU MOTO UTAWAKA.

Makala hii niliisoma kwenye gazeti la TAZAMA ikiwa na mwandishi Charles Charles ambaye ni katibu wa vijana wa CCM wa uenezi. Hongera Charles, naona unafanya vizuri kazi yako mpya. Zephania, kwanini umeamua kuondoa jina la Charles badala yake umeandika mwandishi maalumu? Hivi gazeti la TAZAMA liko kwenye mtandao? Kama hapana, hizi habari wewe unazipataje ndugu yangu. Au uko TAZAMA?

Ni vyema mwandishi angetuambia na ruzuku ya CCM inatumikaje ili tuweze kulanganisha vizuri.

PM
 
Makala hii niliisoma kwenye gazeti la TAZAMA ikiwa na mwandishi Charles Charles ambaye ni katibu wa vijana wa CCM wa uenezi. Hongera Charles, naona unafanya vizuri kazi yako mpya. Zephania, kwanini umeamua kuondoa jina la Charles badala yake umeandika mwandishi maalumu? Hivi gazeti la TAZAMA liko kwenye mtandao? Kama hapana, hizi habari wewe unazipataje ndugu yangu. Au uko TAZAMA?

Ni vyema mwandishi angetuambia na ruzuku ya CCM inatumikaje ili tuweze kulanganisha vizuri.

PM

CCM inapokea ruzuku ya milioni kama 2000, pamoja na vitega uchumi vyote. CHADEMA inapokea milioni kama 50, CUF zaidi ya milioni 100. Je, kila chama kinatumiaje? Je, hivi vyama vina vyanzo vingine vya mapato? Vyanzo vipi na zinatumikaje?

PM
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom