SoC01 Ukitumia hii dawa yenye mchanganyiko wa mizizi sita, utavuta wateja kwenye biashara yako mpaka watu washangae (Tazama na sikiliza hii video)

Stories of Change - 2021 Competition
Sep 6, 2021
24
111
Na Elivius Athanas.
0745937016.

Kifungua kinywa cha asubuhi ni chai lakini kifungua kinywa cha waungwana ni salamu.
Salamu kwenu wanafamilia wa JamiiForums, ni imani yangu kuwa mu wazima wa afya na poleni sana mashabiki wa Simba damudamu, kwa shambulizi la risasi moja ya kichwa, mliyofyatuliwa na Wanajeshi wa Yanga kwenye vita ya kombe la Ngao ya Jamii pale Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Ningekuwa mchoyo wa nidhamu na msaliti wa mila na desturi za Kiafrika, endapo ningeanza kuandika makala hii bila kuwasalimu.

"Nasikitika kuwa, hii video niliyosema uitazame, ipo kwenye simu lakini kila nikitaka kuambatanisha video (attach file) inashindikana na haiwezekani kuhariri kichwa cha habari kikishaenda hewani, mtanisamehe".

Baada ya kutimiza jukumu hilo la kinidhamu, niende moja kwa moja kueleza na kufafanua makala yetu tajwa.

Ujasiriamali umekuwa ni chanzo kikubwa cha ajira kwa Watanzania wengi. Wanawake kwa wanaume, vijana kwa wazee, wamekuwa wakijihusisha na biashara ndogondogo ili kuweza kujikimu na maisha. Akina mama wengi, wamefungua migahawa ya kuuza chakula, kutembeza mboga za majani na biashara zingine kadha wa kadha ili kujikimu kimaisha.
Vijana nao hawajabaki nyuma, wamefungua vibanda vya kuuza matunda, kutembeza nguo na bidhaa zingine.

Utafiti wenye viwango vya Kimataifa niliofanya kuhusu Vijana na Ajira, umebaini kuwa, kati ya vijana kumi (10) waliohitimu Vyuo, vijana watatu (3) wamepata au wanaendelea kutafuta ajira maofisini, vijana wanne (4) wanajihusisha na ujasiriamali nikiwemo mimi na vijana watatu (3) waliobaki, wamekimbilia nyumbani kwao na kuendelea na maisha wakiwa nyumbani na wazazi.

BIASHARA NI KITU KIZURI SANA.
JE, UNAZIFAHAMU MBINU ZA KUVUTA WATEJA?

Zifuatazo ni mbinu sita (6) ambazo ukizitumia, utavuta wateja kwenye biashara yako mpaka watu washangae!

1. Toa huduma ya Kifalme na kibunifu kwa mteja wako wa mara ya kwanza ili kumvuta arudi tena. Sawa, mteja ni Mfalme lakini mteja wa mara ya kwanza ni zaidi ya Mfalme. Mfano, kama mgahawa wako una utaratibu wa wateja kunawa nje, ukiona mteja mpya mchangamkie, mletee maji na umunawishe mikono. Atajiona wa thamani sana endapo ataona wateja wengine wananawa nje lakini yeye kaletewa maji kunawishwa. Atafurahi sana na fadhila zake itakuwa ni kurudi tena kwako. Kadri siku zinavyoenda yeye mwenyewe atanawa nje bila kuambiwa na mtu.
Katika biashara yoyote ile, kuwa mbunifu na toa huduma ya Kifalme kwa mteja wako wa mara ya kwanza kwani ukiharibu mwanzo utampoteza mteja huyo.
Kama inawezekana, unaweza kumuongeza kidogo, kumpa ajaribu (kuonja) na ubunifu kadha wa kadha ambao utamfanya mteja wako wa mara ya kwanza arudi tena.

2. Ubora wa bidhaa yako kila siku.
Hata ukitoa huduma ya Kifalme kiasi gani ila kama bidhaa (biashara) yako haina ubora, mteja hawezi kurudi tena.
Ubora wa bidhaa yako ni suala la msingi sana katika biashara yako.
Kama ni chakula kiwe na ubora siku zote, kiive siku zote. Siyo leo ugali haujaiva, kesho chumvi imepelea, kesho kutwa chumvi imezidi. Utapoteza wateja.
Bidhaa yako ikiwa bora, itamshawishi mteja awaambie watu wengine waje kupata huduma kwako.
Wateja wanataka bidhaa zenye hofu na afya zao, wanataka bidhaa halisi na siyo bandia.
Hakikisha ubora wa bidhaa zako kila siku, utapata wateja kila siku.

3. Usafi wa kudumu katika biashara yako ni dawa nyingine ya kuvuta wateja.
Jitahidi sehemu yako ya biashara iwe safi siku zote. Nzi na uchafu mwingine kwenye eneo lako la biashara, vitafukuza wateja na kuwavunja miguu wasirudi tena.
Kama ni genge, hakikisha genge lako ni safi mda wote. Kusiwe na uchafu na wadudu watakaotia kinyaa wateja.
Kama ni mgahawa wa chakula, uwe safi mda wote, vyombo na meza viwe safi mda wote.
Mteja akija akakuta mkutano wa nzi mezani, hatarudi tena.
Ukiwa msafi kwenye biashara yako, utajihakikishia wateja wengi kwani asilimia kubwa ya wateja, wanapenda sehemu za biashara zilizo safi na salama.

4. Ulimi wa mvuto na ukarimu kwa mteja.
Ulimi ni silaha kubwa sana kwenye vita ya biashara. Wafanyabiashara wanaotumia ulimi vizuri, wanajihakikishia wateja wa kudumu. Ongea na mteja kwa bashasha na tabasamu. Mkaribishe kwa maneno matamu na kamwe usimfokee.
Msongo wako wa mawazo na hasira ulizotokanazo nyumbani, usizimalizie kwa mteja, hatorudi tena.
Maneno matamu kwa mteja, humliwaza mteja na kumfanya ajisikie kuwa yupo sehemu salama na sahihi ya kupata huduma.
Karibu na asante vitawale mdomoni kwako.
Nashukuru sana na ubarikiwe, viwe vibwagizo vya wimbo wako wa biashara.
Dawa ya ulimi na ukarimu, vitakusaidia sana kuvuta wateja kwenye biashara yako.

5. Mahudhurio mfululizo kazini kwako.
Hakuna kitu kibaya kinachofukuza wateja kwenye biashara kama mahudhurio yasiyoeleweka.
Leo umefungua, kesho umefunga.
Leo upo, kesho haupo.
Mahudhurio ya aina hii, huwakasirisha wateja na kuwafanya wakukimbie.
Ukiwa na mahudhurio butu kazini kwako, fahamu kuwa unachimba kaburi la kuzika wateja wako mwenyewe.
Jitahidi sana kuwa na mahudhurio chanya katika sehemu yako ya biashara.

6. Weka vivutio vya kihaiba katika sehemu yako ya biashara. Mfano, redio, mziki, runinga, nyimbo za dini, maji ya moto na vivutio vingine vya kihaiba kulingana na aina ya wateja ulionao.
Mfano, kuna wateja wengine wanapenda wawe wanakula chakula cha mchana huku wanasikiliza matangazo ya mchana ya redio "DW". Hivyo akija kwenye mgahawa wako akakuta umewasha redio "DW", ataendelea kuja hapo siku zote.
Kuna baadhi ya wasichana na wanawake wanapenda nyimbo za dini, wakija kula chakula kwenye mgahawa wako wakasikia nyimbo hizo, wataendelea kuhudhuria kwako kwani wakifika kwako wanakula huku wanasikiliza nyimbo wanazozipenda.
Kama wateja wako ni vijana wa mtaani (wahuni), wakija kwenye biashara yako wakakuta miziki ya singeli inapigwa, watatulia hapo na kupata huduma.
Hivyo ni muhimu sana kuweka kivutio cha kihaiba kulinganana aina yako ya wateja.

MWISHO. Ujasiriamali umekuwa na mchango mkubwa katika kuzalisha ajira na kuongeza pato la Taifa. Hivyo, Serikali na Wadau wengine wa sekta ya biashara, waboreshe na kutengeneza mazingira rafiki ya kufanya biashara hasa biashara ndogondogo (ujasiriamali) ili kuwasaidia wajasiriamali kufanya biashara kwa uhuru na wepesi.

Na hiyo ndiyo dawa yenye mchanganyiko wa mizizi sita ambayo ukiitumia, utavuta wateja kwenye biashara yako mpaka watu washangae!

Ahsanteni kwa kunywa dawa.
 
Mambo ya biashara ni magumu sana,na ndio maana wafanyabiashara walio wengi hivi sasa wanatumia madawa na makafara kwenye biashara zao ili wauze bila shida.
 
Ungetumia muda huu kusoma biblia Ungepona
.you can't be serious
IMG_20210924_074847.jpg
 
Mkuu, nimekuja chap kwenye uzi nikijua kuna mchanganyiko wa mizizi na miyegeya ya kuvutia wateja!

Mkuu, hizi mbinu ni ngumu!
 
Back
Top Bottom