Ukitafakari utagundua kuwa Serikali, CCM hawataki Katiba mpya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ukitafakari utagundua kuwa Serikali, CCM hawataki Katiba mpya

Discussion in 'KATIBA Mpya' started by BAK, Apr 13, 2011.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Apr 13, 2011
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,691
  Likes Received: 82,611
  Trophy Points: 280
  Ukitafakari utagundua kuwa Serikali, CCM hawataki Katiba mpya Tuesday, 12 April 2011 20:21

  Na George Maziku
  Mwananchi

  UKIWASIKILIZA kwa makini viongozi wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM, utagundua kirahisi kabisa kuwa watu hawa lao moja, wanazungumza lugha moja, wana maelekezo kutoka chanzo kimoja, wanatetea msimamo mmoja, yaani kuhakikisha watanzania hawapati katiba mpya.

  Kauli ya rais Jakaya Kikwete kwamba anakubaliana na maoni ya watanzania ya kutaka kuwa na katiba mpya itakayokidhi mahitaji na mazingira ya sasa na yajayo, inapingana na hatua za utekelezaji zilizoanza kuchukuliwa na serikali yake.

  Kwa mfano, Muswada wa serikali wa kuanzisha vyombo vya kuratibu na kusimamia utengenezaji wa katiba mpya, hauonyeshi dhamira ya rais Kikwete ya kuipatia nchi yetu katiba mpya itakayotokana na wananchi, badala yake muswada ule unampa rais mamlaka makubwa ya kisheria ya kuhodhi mchakato mzima wa kutunga katiba ya nchi.

  Waziri Katiba na Sheria, Celina Kombani anakiri kuandaa muswada wa sheria unaompa rais nguvu za kuhodhi mchakato mzima wa kutunga katiba mpya, na anajaribu kuhalalisha kitendo hicho kwa maelezo kuwa rais ndiye mkuu wa nchi na serikali kwa mujibu wa katiba ya sasa, hivyo “haiwezekani” kumwacha nje ya mchakato wa kupata katiba mpya.

  Hayo ni mawazo hodhi, ni mawazo mgando, ni uzamani wa fikra, viongozi serikalini wanaona kitendo cha kutomhusisha rais katika kutengeneza katiba mpya ni sawa na kumpoka madaraka yake ya urais, ni sawa na kumpindua kutoka madarakani.

  Wao bado wanaamini kuwa rais ndiye yote katika yote, yeye ni Alpha na Omega, ni wa kwanza na wa mwisho, hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika bila ushiriki na usimamizi wake, kwao wao, rais ni kama “mungu” wa Tanzania.

  Halafu ukimsikiliza vema waziri Kombani utabaini wazi kabisa kuwa viongozi wa serikali hawataki kabisa suala la katiba mpya, wao wanataka marekebisho ya katiba ya sasa, wanataka kuingiza mambo machache tu mapya katika katiba ya zamani na kisha kuitangaza kuwa hiyo ni katiba mpya.

  Dhamira zao zinathibitishwa na kauli zao na maandishi yao yaliyomo kwenye muswada waliouandaa kwa ajili ya kuunda vyombo vya kuratibu na kusimamia mchakato wa kutengeneza katiba mpya.

  Hata wabunge wa CCM wapo pamoja na serikali yao, nao hawataki kuwepo katiba mpya, wanahofu na hatima yao kama kutakuwa na katiba mpya, wana wasi wasi kuwa huenda katiba mpya itasaidia vyama vya upinzani kukiondoa madarakani chama chao-CCM.

  Msimamo wa wabunge wa CCM unadhihirishwa na mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na utawala ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pindi Chana aliyekuwa akisimamia vikao vya kamati hiyo vya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu muswada wa serikali, vilivyofanyika jijini Dar es salaam, kuanzia Aprili 7 mpaka 9, mwaka huu.

  Katika vikao hivyo Pindi Chana alionyesha wazi kuwa upande wa serikali, alikuwa akiongea kana kwamba yeye ni mtendaji wa serikali, alionyesha wazi kutounga mkono mtazamo wa kuwa na katiba mpya, bila shaka anataka tuendelee kutia viraka kwenye katiba ya zamani.

  Pindi Chana alionyesha hali ya kutokuwa na utashi thabiti wa kufanya shughuli ile, ni kama alikuwa amelazimishwa tu kuja kuwasikiliza wananchi.

  Nasema hayo kwa sababu mwenyekiti alikuwa amejaa ubabe, fikra za ukubwa, na udikteta. Nilisikitika na kukata tamaa nilipomsikia mwenyekiti wa kamati hiyo akitamka hadharani eti wananchi tunapaswa kujiheshimu kwa sababu katika mkutano ule palikuwa na "watu wakubwa sana."

  Nilijiuliza na bila shaka Watanzania wenzangu waliokuwa kwenye kikao hicho nao walijiuliza swali hili: “Hivi ni nani aliye mkubwa kuliko wananchi?”

  Naamini mwenyekiti wa kamati alimaanisha watu kama waziri mkuu mstaafu Joseph Warioba, viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa kama vile Profesa Ibrahim Lipumba wa chama cha wananchi (CUF), Katibu mkuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia na wengine wengi waliohudhuria mkutano huo.

  Kama hivyo ndivyo, kwamba watu hawa ni wakubwa kuliko wananchi, sasa kulikuwa na haja gani ya kuwakaribisha wananchi wote kuja kutoa maoni kuhusu muswada ule? Kwanini hawakuwaalika viongozi hao tu ili kupata maoni yao ? Hii ni tabia mbaya ya viongozi wa nchi yetu kujiona wakubwa kuliko wananchi waliowachagua.

  Kiroja kingine ni pale mwenyekiti huyo alipotaka kuendesha kikao kile kwa kufuata kanuni za bunge kwa watu ambao si wabunge, akitaka wananchi wasizungumze jambo wasilo na ushahidi nalo, kutolitaja jina la rais wa jamhuri kwa dhihaka, kutotumia lugha ya kuudhi wengine na mambo mengine mengi kana kwamba tuko bungeni!

  Hata kauli na vitendo vya viongozi wa CCM wakati huu watanzania wengi wanapopaza sauti zao kutaka kutungwa katiba mpya, ni ushahidi wa wazi kwamba wenzetu hawa hawako pamoja nasi, mawazo yao na ya watanzania wengine yanaachana umbali wa mbingu na ardhi.

  Viongozi wa serikalini na katika CCM wana fikra tofauti kabisa kuhusu suala la katiba ya nchi, wenzetu hawaamini kama katiba ni mali ya wananchi, wenzetu hawaamini kama katiba lazima itokane na wananchi, wenzetu wanaamini katiba ni ya rais na lazima itokane na yeye.

  Katika hali hii, hoja ya Watanzania ya kutaka katiba mpya ni ngumu mno kutekelezeka, kwasababu wenye kuwezesha mchakato ufanikiwe hawana dhamira ya dhati ya kuwa na katiba mpya, vinginevyo watanzania watumie nguvu ya umma kuwalazimisha watawala kuachana na ubabe na udikteta wao.
   
Loading...