Ukistaajabu ya China Utayaona ya Tanzania

mgt software

JF-Expert Member
Nov 1, 2010
13,767
7,115
Na BWANKU M BWANKU

Wiki hii nzima naendelea kustaajabu sana kusoma habari moja kuhusu nchi ya China. Nchi tunayoambiwa inakuja kwa kasi sana kuja kutawala Uchumi wa Dunia. China imetangaza uamuzi wake wa kuvibadirisha nusu ya Vyuo vikuu vyake nchi nzima takribani Vyuo Vikuu 600 na kuwa Vyuo vya Ufundi yaani Polytechnics Kama lengo na mpango wa China kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi wanaohitimu Shahada (Degrees) na kuwa na nadharia tu ya kukariri (Academic theory) isiyo ya vitendo isiyokuwa na uwezo wa kumpa kazi Mwanafunzi wa China.

China wanaona elimu ya Vyuo vikuu imejikita kuzalisha tu Wahitimu wanaokariri nadharia (Academic theory) wanaoshindana na kuwaza tu kutafuta Kazi yaani Job Seekers bila ya kuwa na uwezo wa kivitendo kuvumbua na kutengeneza fursa yaani Job creators.

Katika kukazia Mpango huo tayali Naibu Waziri wa Elimu wa China Lu Xin ameshatangaza mpango wa Serikali ya China kuvibadirisha Vyuo Vikuu vya Umma vya China vipatavyo 600 Kuwa Vyuo vya Ufundi vitakavyojikita katika kuwaandaa na kuwapika Wachina Kwenye Kada za Uhandisi (Engineering), Mafundi Wakubwa (Senior Technicians) na Wataalamu wa teknolojia. China inaona mpango huu ni wa kuanza kutekelezwa mapema sana mwaka huu kwani utasaidia kuwapika vijana wa China wenye ujuzi na maarifa ya Juu sana kwenye uzalishaji na Kutafsiri fursa zinazowazunguka Wenyewe (Market relevance).

Serikali ya China inaona ongezeko la tatizo la ajira nchi kwao linalozunguka asilimia 15 kwa sasa linasababishwa na Mifumo ya Vyuo vikuu vyao kuandaa wanafunzi waliokaririshwa na kujikita kwenye nadharia tu ya madarasani bila ya kuwa na Ujuzi wa Yale yanayowazunguka kwa hivyo wanaona suluhisho sahihi ni Kubadirisha tu mfumo wa elimu yao unaomfunga mwanafunzi.

Wadau mbalimbali Wa Elimu China wakiongozwa na Rais wa Kituo cha Ufundi kutokea Kituo kilichopo Kusini mwa China Lao Hansheng wanapendekeza na kutaka kuwaona Wanafunzi wa China wenye Ujuzi na wanaoendelezwa Vipaji vyao na sio wale wanaohaha kukariri ili wapate madaraja ya kwanza Kwenye mitihani yao.

Kwa hakika ni Mjadara mpana sana na China imepania haswa kutekeleza hilo na ndio maana Serikali imeshatangaza uamuzi wa kulifanyia mabadiriko Baraza la Mitihani la China (The Gaokao) liwe linatunga Mitihani ya kiufundi na Ufundi na kuachana na Mitihani ya nadharia ambayo inafahamika kwa kukaririsha wanafunzi. China wamepania haswa.

Taifa kubwa na linaloendelea kwa kasi kubwa sana duniani kwa sasa kama Uchina inaona elimu ya Vyuo vikuu imejikita kutengeneza kundi kubwa la wasomi waliojaza manadharia pekee vichwani mwao wanaohaha ofisi za Umma na binafsi kutafuta kazi badala ya wao wenyewe kutengeneza ajira. Yani elimu ya Vyuo vikuu ni kwa ajili ya kazi za kuajiriwa yaani Job Seekers na sio kumuandaa kijana kutafsiri fursa na kujiajiri (Job creator). Ni stori tamu ukiifatilia kule China.

YA TANZANIA.

Wakati Wachina wakiendelea na mpango na mchakato wao wa kubadirisha mfumo wao wa elimu ili uendane na mazingira ili wapunguze tatizo la ajira linaloikumba China, ninaiona nchi yangu Tanzania ikiendana na hadithi ya China. Hadithi ya Vijana wa Vyuo vikuu wanahitimu kila Mwaka na kuingia Kwenye soko la ajira na Uwezo wa Vijana hao kutafsiri fursa zinazowazunguka na Kujiajiri (Job Creation).

Tanzania kama ilivyo China imekuwa na Mfumo wa elimu unaoendana ambao China wanauona kama ni Janga kwa mustakabali kwa taifa lao. Hapa pamekuwa na Mjadara mkubwa na mpana sana kuhusu uwezo wa wanafunzi wanaohitimu kila mwaka Kwenye Vyuo Vikuu na kama Kweli ni Qualified kuzalisha na Kujiongeza.

Hapa nchini kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na changamoto kubwa sana ya ajira kwa wahitimu wengi wanaohitimu kila mwaka vyuoni na kuhoji kama uwezo wa wahitimu hao kiujuzi na maarifa ukoje katika kujiajiri baada ya malengo ya asili ya kuajiriwa kukwama. Ukistaajabu ya China utayaona ya Tanzania. Ni Kweli Mfumo wetu wa Vyuo Vikuu unawaandaa vilivyo Vijana wa Vyuo vikuu kuwa na mawazo stahiki nje ya kuajiriwa na kujiajiri?

Mjadara mkubwa ni kama ule ule wa China. Hapa ni kupima Ujuzi wanaoupata wanafunzi madarasani na uhalisia wake kwa mazingira ya Tanzania na dhana nzima ya Maendeleo.

Ni kweli Ujuzi wanaotoka nao wanafunzi wetu vyuoni unaendana na Mazingira halisi ya Tanzania? Ujuzi huo hasa unaweza kumsaidia kijana wa Kitanzania kutafsiri fursa za mazingira yake na kujiajiri?

Majuzi nimesikia Uongozi wa Chuo Kikuu kimoja ukiongelea tatizo la ajira nchini na wakisema wana mpango wao kama Chuo kufanya utafiti wa kubaini tatizo la ajira na namna ya kukabiliana na tatizo hili hasa kwa Vijana wanaohitimu Vyuoni. Natamani kuiona hiyo tafiti ikifanyika na Kuja na Matokeo (Findings)

Nawiwa kuona Mjadara wa China ukihamia kidogo Tanzania. Je tutaweza kuvibadiri baadhi ya Vyuo Vikuu vyetu kuwa Vyuo vya Ufundi (Polytechnics) ili kuwapata vijana wenye Sifa stahiki stadi za Ujuzi wa Kujiajiri? Jamani tutafakari kidogo..........

Ukistaajabu ya China Utayaona ya kwetu Tanzania.
 
Back
Top Bottom