Ukihusika na dawa za kulevya Zanzibar kifungo cha maisha jela

John Haramba

JF-Expert Member
Feb 4, 2022
365
1,373
Baada Rais wa Zanzibar, Dr. Hussein Ali Mwinyi kuidhinisha sheria mpya ya kudhibiti dawa za kulevya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya, leo Ijumaa Februari 4 2022 amezungumzia sheria hiyo ambayo imeanza kutumika.

“Kama Kamishna Mkuu au Afisa ambaye amehidhinishwa, kwa sababu za msingi akihisi kuna sababu za msingi kwa nyumba, gari au chochote ambacho kinahisiwa kimebeba madawa ya kulevya, atapewa ruhusa na haki kwa mujibu wa sheria kupekua na ikiwezekana kuvunja au kufungua mlango au kuondoa kizuizi.

“Hii ni nguvu ambayo atakuwa amepewa na mamlaka, vilevile mtu yeyote ambaye atakutwa na hatia ya kuingiza au kusafirisha dawa za kulevya, ikithibitika atakuwa na hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa mujibu wa sheria hii,” amesema Dkt. Saada Mkuya.

====

MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU SHERIA YA KUANZISHWA KWA MAMLAKA YA UDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA ZANZIBAR

Ndugu Katibu Mkuu OMKR,

Watendaji wa OMKR,

Watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Ndugu waandishi wa Habari,

Assalam aleikum.

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenye Enzi Mungu Mwingi wa Rehma kwa kutukutanisha hapa leo hii, tukiwa wazima wa afya na tukitimiza majukumu ya kulipeleka mbele Taifa letu.

Ndugu waandishi wa Habari, lengo kuu la kuwaita hapa ni kuutarifu umma kupitia kwenu kuwa SHERIA YA KUANZISHWA KWA MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA ZANZIBAR imeshatiwa Saini na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na imeanza kutumika rasmi baada ya kutiwa Saini.

Sheria hii inajulikana kama Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Namba 8 ya mwaka 2021.

Mantiki na Madhumuni ya sheria hii;

Madhumuni ya sheria Namba 8 ya 2021 ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar ni kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya yenye na uwezo kamili wa kupeleleza, kukamata, kuchunguza na hatimae kupeleka Mahkamani mashauri yanayohusiana na dawa za kulevya Pamoja na makosa mengine yanayofanana nayo. Aidha sheria hii imefuta taasisi iliokuwa ikisimamia Uratibu wa masuala ya dawa za kulevya nchini ambayo ni Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya na kuanzisha taasisi inayojulikana kama Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, itakayoongozwa na Kamishna Mkuu na itakuwa chini ya Baraza la Taifa la Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ambalo linaongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Tofauti ya Sheria hii na ya zamani;

Tofauti ya Sheria hii na ya zamani;

Kwa ujumla Sheria hii mpya kwanza, imeanzisha Mamlaka yenye nguvu ya kisheria na thabiti ya kusimamia udhibiti wa dawa za kulevya nchini ambapo, Taasisi hii mpya ina uwezo wa kuchunguza, kukamata, kupeleleza na kufungua mashtaka mahakamani;

Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa anaweza kuhoji, kupeleleza au kufanya ukaguzi kwa mtu yeyote au kikundi chochote cha watu kadri atakavyoona inafaa;

Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa, atakuwa na uwezo wa kukagua, kupekuwa, kuzuia, kukamata, kuweka kizuizini na kufanya uchunguzi kuhusiana na makosa yaliyo chini ya Sheria hii;

Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa ambaye ana sababu za msingi za kuamini kwamba gari, ndege, meli, chombo cha kubebea mizigo au chombo chengine chochote cha usafiri kimetumika au kinatumika katika kutenda kosa chini ya Sheria hii, anaweza kukisimamisha, kuingia na kuifanyia upekuzi gari, ndege, meli, chombo cha kubebea mizigo au chombo chengine cha usafiri na anaweza kwa madhumuni hayo kuvunja au kufungua mlango na kuondoa kizuizi cha kuingia ndani ya chombo;

Endapo mtu anachunguzwa au anashitakiwa kwa kosa chini ya Sheria hii, Kamishna Mkuu anaweza, pale ambapo anaamini kwamba ushahidi wowote unaohusiana na kosa au mali unapatikana katika akaunti ya benki, kufanya maombi mahkamani ya amri ya kuzuia akaunti ya benki;

Bila ya kujali masharti ya sheria yoyote, Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa anaweza wakati wowote kwa madhumuni ya Sheria hii kufanya uvamizi na kuingia katika jengo lolote ambalo anaamini kwamba kosa limetendeka au litatendeka ndani ya jengo hilo;

Sheria imeanzisha Baraza la Taifa la Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ambalo linaongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Baraza litasimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na litakuwa ndio chombo kikuu cha maamuzi na lenye usimamizi wa jumla kwa Mamlaka hii jambo ambalo tunaamini kuwa janga hili la dawa za kulevya litaweza kudhibitiwa kwa haraka na ufanisi zaidi na pia kutakuwa na usimamizi madhubuti katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini;

Kwa sheria hii, Mamlaka inaweza kutoa maelekezo pale itakapohitajika kwa taasisi yoyote ya Serikali au idara katika kutekeleza masharti ya Sheria hii, na taasisi au idara hiyo itawajibika kutekeleza maelekezo hayo;

Sheria hii pia imetoa majukumu ya jumla kwa taasisi za umma katika kuzuia na kupambana na dawa za kulevya nchini, Baraza litapokea na kuzipitia taarifa za taasisi za umma juu ya majukumu yao katika kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Taasisi hizo ni:

(a) Idara ya Usalama wa Taifa Zanzibar;

(b) Jeshi la Polisi Zanzibar;

(c) Chuo cha Mafunzo Zanzibar;

(d) Ofisi ya Uhamiaji Zanzibar;

(e) Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar;

(f) Shirika la Bandari Zanzibar;

(g) Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali;

(h) Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu; na

(i) Taasisi nyengine yoyote kama Baraza litakavyoona inafaa.

Kwa kuzingatia kwamba kila mmoja anatimiza wajibu wake katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini, na kwa kuhakikisha kuwa kwa kiasi kikubwa makosa yanayohusiana na utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya yanazibitiwa kwa njia zote, hali itakayopelekea kupunguza athari zitokanazo na dawa za kulevya nchini, sheria hii imeanzisha Kamati za Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya katika kila Mkoa ambazo zitaongozwa na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa husika;

Lengo la ujumla la sheria Namba 8 ya 2021 ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar;

Sheria hii imelenga kudhibiti makosa mbali mbali yanayohusu uhalifu wa dawa za kulevya na makosa yanayo fanana nayo ambapo jumla ya vifugu 26 vimekataza moja kwa moja uhalifu huu wa dawa za kulevya pamoja na makosa yanayofanana nayo kama:

 Sheria inaharamisha mambo mbalimbali ikiwemo kilimo cha bangi, mirungi, kulima, kumiliki, kusafirisha, kuuza na kununua mbegu zinazoweza kuzalisha dawa za kulevya kwa kutoa adhabu ya kifungo cha maisha.

Kufadhili biashara ya dawa za kulevya adhabu ya kifungo cha maisha na kutaifisha mali zote.

 Inaharamisha usafirishaji wa dawa za kulevya, kujihusisha kwa namna yoyote kinyume cha Sheria na kemikali zinazoweza kuzalisha dawa za kulevya kwa kutoa adhabu ya kifungo cha maisha.

 Inaharamisha kumiliki mashine, vifaa na maabara kwa lengo la kutengeneza dawa za kulevya kwa kutoa adhabu ya kifungo cha maisha na kutaifisha kifaa hicho Pamoja na mali.

 Mmliki wa jengo kuruhusu jengo litumike kwa uhalifu wa dawa za kulevya, adhabu ni Faini isiyopungua milioni 10 au kifungo kisichopungua miaka 30 au adhabu zote mbili.

 Sheria imekataza bila ya kuwa na kibali kuingiza, kutoa, kusambaza, kumiliki na kutengeneza kemikali bashirifu, adhabu ni kifungo kisichopungua miaka 30.

 Sheria imetoa adhabu kwa mtu yoyote atakekataa kutoa taarifa ama ushahidi unaohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya au kutoa taarifa za uongo kulipa faini isiyopungua shilingi milioni 30 na isiyozidi shilingi milioni 50 au kifungo kisichopungua miaka 15 na kisichozidi miaka 30 au adhabu zote mbili.

 Sheria imekataza kwa namna yoyote ile kusaidia au kusababisha kutendeka au kutenda uhalifu wa dawa za kulevya na kutoa adhabu sawa sawa na mtenda kosa mwenyewe.

 Sheria imekataza kutoa dawa tiba zinazotumika kwa matibabu ambazo zinaweza kutumika kama dawa za kulevya zinazozibitiwa kisheria kinyume cha utaratibu, inadhibiti matumizi ya dawa adhabu ni faini isiyopungua Shilingi Milioni Hamsini za Kitanzania au kifungo kisichopungua miaka thelathini au vyote viwili.

 Sheria imekataza kutumia dawa za kulevya, na akitiwa hatiani, atalipa faini isiyopungua Shilingi Milioni Tano za Kitanzania au kifungo cha mwaka mmoja au vyote viwili.

 Endapo mtu atajitayarisha au atajaribu kufanya au kutokuzuia kitu kinachosababisha utendaji wa kosa chini ya Sheria hii, atapewa nusu ya adhabu ambayo angestahiki kupewa endapo angetenda kosa hilo.

 Mtu atakayekiuka masharti ya kifungu chochote cha Sheria hii, kanuni yoyote au amri yoyote iliyowekwa chini ya Sheria hii ambapo adhabu yake haikutajwa, ametenda kosa, na akitiwa hatiani atatumikia kifungo kisichopungua miaka kumi na tano na kisichozidi miaka thelathini.

Endapo daktari wa binaadamu, daktari wa meno au daktari wa upasuaji wa wanyama, ametiwa hatiani chini ya Sheria hii, bila ya kujali masharti ya sheria nyengine yoyote, jina lake litafutwa katika daftari la usajili na hatofanya kazi ndani ya Zanzibar.

 Endapo kosa limefanywa na kampuni chini ya Sheria hii, mtu ambaye, wakati kosa linafanyika, alikuwa dhamana na ana jukumu la kusimamia uendeshaji wa shughuli za kampuni, atachukuliwa kuwa ametenda kosa na, akitiwa hatiani atawajibika.

 Pale ambapo kosa lolote limefanywa na kampuni na imethibitishwa kwamba kosa limefanywa kwa kuridhiana au kukubaliana au limechangiwa na uzembe wowote kwa upande wa mkurugenzi, meneja, katibu au ofisa mwengine wa kampuni, mkurugenzi, meneja, katibu au ofisa mwengine huyo wa kampuni atashtakiwa na kuadhibiwa ipasavyo na kampuni hiyo itafutiwa usajili au kutaifishwa.

 Mmiliki, mkaazi au mtu anayehusika na usimamizi wa eneo atatakiwa kutoa taarifa haraka iwezekanavyo kwa Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa juu ya uwepo, ndani ya eneo lake, wa mimea ya dawa za kulevya, mazao ya dawa za kulevya au dawa za kulevya ambazo huenda zimelimwa, zimezalishwa au zimetengenezwa isivyohalali.Ikiwa mmiliki, mkazi, au mtu anayehusika na usimamizi, ameshindwa kutoa taarifa, ametenda kosa, na akitiwa hatiani, atalipa faini isiyopungua Shilingi Milioni Kumi za Kitanzania na isiyozidi Shilingi Milioni Hamsini za Kitanzania au kifungo kisichopungua miaka kumi na tano na kisichozidi miaka thelathini au vyote viwili.

 Mtu ambaye kwa makusudi au kwa nia ovu anatoa taarifa za uongo zinazosababisha ukamataji au upekuzi chini ya Sheria hii, ametenda kosa, na akitiwa hatiani, atalipa faini isiyopungua Shilingi Milioni Kumi za Kitanzania au kifungo kisichopungua miaka miwili au vyote viwili.

 Ufilisi wa Mali; Endapo mtu yoyote ametiwa hatiani kwa kosa chini ya Sheria hii, au atatiwa hatiani kwa kosa linalofanana nalo, na Mahakama ya jinai nje ya Zanzibar, mali

anazomiliki yeye mwenyewe au mshirika wake, alizozipata kutokana na dawa za kulevya katika tarehe ya mashtaka au baada ya tarehe hiyo zitafilisiwa na kuwa mali za Serikali.

Endapo mtu atatiwa hatiani na Mahakama nje ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria yoyote inayofanana na masharti ya Sheria hii, atashughulikiwa kama vile ametiwa hatiani na Mahakama yenye uwezo Zanzibar.

 Kitu chochote kilichotumika kwa ajili ya kufichia dawa za kulevya ambazo zinatakiwa kutaifishwa chini ya Sheria hii, kitu hicho kitataifishwa.

 Endapo mtu ameuza dawa za kulevya ambazo anafahamu au ana sababu ya kuamini kwamba dawa za kulevya zinatakiwa kutaifishwa chini ya Sheria hii, mapato ya mauzo yatataifishwa.

 Endapo mtu atamiliki kitu au mali iliyopatikana isivyo halali ikiwa yeye mwenyewe au mtu mwengine yoyote kwa niaba yake kinyume na sheria hii, kitu au mali hiyo itafilisiwa na Serikali.

 Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa anaweza kutoa amri ya kuzuia kitu au mali wakati wa kufanya uchunguzi, upelelezi au ufuatiliaji chini ya sheria hii, ikiwa anayo sababu ya kuamini kwamba kitu au mali yoyote kuhusiana na uchunguzi, upelelezi au ufuatiliaji uliofanyika imepatikana isivyo halali na kitu au mali hiyo kinaweza kufichwa, kuhaulishwa au kutumiwa kwa namna ambayo inaweza kuharibu utaratibu wa utaifishaji wa kitu au mali hiyo chini ya Sehemu hii.

Tiba

Sheria hii imetupa uwezo wa kuanzisha vituo vya utambuzi, tiba, elimu, uangalizi, urekebishaji wa tabia ili kuweza kuwarudisha kwenye jamii watumiaji wa dawa za kulevya kwa kuzingatia masharti na kwa namna kama itakayoelekezwa katika kanuni.

Tayari kituo chetu cha Tiba na Marekebisho ya Tabia kilichopo Kidimni kimeanza rasmi kutoa huduma hizo, kituo kinatarajiwa kuwa na mafunzo ya ujasiriaamali kwa wale ambao watakuwa wanapata huduma ndani ya kituo hicho.

Wito kwa Jamii

Kutokana na sheria hii kuwa kali sana, nawanasihi wana jamii ya kizanzibari kujiepusha kwa kila hali na uhalifu huu wa dawa za kulevya kwani madhara yake kiafya na kisheria ni makubwa sana kwa mtenda kosa Pamoja na jamii yake husika.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Zanzibar bila ya Dawa za Kulevya inawezekana.
3I8A5420.JPG
3I8A5388.JPG
 
Waache upuuzi hio sio solution, kama wakitoa ajira vijana hawatatumia au watapunguza wimbi la vijana kutumia na kuuza madawa hayo, wanawatia stress za maisha wakivuta bangi kupunguza mawazo wanawalaumu pumbaaavvv watoe ajira waache kupambana na upinzani
 
Salaam,

Kumekwa na ongezeeko kubwa la vijana wetu kuharibikiwa kutokana na utumiaji wa mihadarati na ulevi wa kupindukia. Hii inatokana na changamoto za kimaisha kama vile kuvunjika kwa ndoa wakati wa utotoni, Malezi ya mzazi mmoja, Kufiwa katika umri mdogo, Kunyanyaswa hasa kunyanyaswa kingono, Kushindwa kukabiliana na hisia, kuvamiwa na misukumo ya marafiki na mabadiliko ya kitabia.

Tunatoa huduma ushauri na semina kwa vijana. Endapo wewe ni Mzazi au mlezi, Kiongozi wa dini, Mwalimu, Daktari au muuguzi na unae kijana au unafahamu familia yenye kijana anaetaseka, wa kike na wa kiume basi unaweza kuwasiliana nasi,

AMKA SIMAMA USIONE AIBU HAUKO PEKE YAKO

Karume

Kigamboni Sober House: MRC Tanzania
+255742550551
samsonkarume@gmail.com

Upatapo Ujumbe huu, Share na wengine
 
Waache upuuzi hio sio solution, kama wakitoa ajira vijana hawatatumia au watapunguza wimbi la vijana kutumia na kuuza madawa hayo, wanawatia stress za maisha wakivuta bangi kupunguza mawazo wanawalaumu pumbaaavvv watoe ajira waache kupambana na upinzani
hakuna taifa lililofanikiwa kuzuia uenezaji wa madawa ya kulevya kwa kuweka sheria kali.uwe masikini au tajili huu uhuni wa madawa ya kulevya ukiingia tu basi jamii haina dawa ila ni kudorora tuu, china kaua sana , saudia kakata vichwa sana Nigeria mtuhumiwa anachimba kaburi lake ndipo auwawe lakini kote huko hakukufua dafu dampo linazidi kunuka tuu.unapowawekea sheria kali ndipo wauzaji nao huloga{recruits} vyombo vya dola viwalinde.
 
hakuna taifa lililofanikiwa kuzuia uenezaji wa madawa ya kulevya kwa kuweka sheria kali.uwe masikini au tajili huu uhuni wa madawa ya kulevya ukiingia tu basi jamii haina dawa ila ni kudorora tuu, china kaua sana , saudia kakata vichwa sana Nigeria mtuhumiwa anachimba kaburi lake ndipo auwawe lakini kote huko hakukufua dafu dampo linazidi kunuka tuu.unapowawekea sheria kali ndipo wauzaji nao huloga{recruits} vyombo vya dola viwalinde.
Something is better than nothing !! Usipoweka sheria Kali kila MTU ataingia kwenye kazi hiyo !! Usipoweka sheria Kali ujue baada ya muda mfupi Taifa litakuwa lina idadi kubwa ya watu wanaonesa nesa barabarani na mate yanadondoka mdomoni !! Tutapata watalii wengi sana kuja kuwaona watoto wetu wanavyonesa nesa !!! HONGERA RAIS MWINYI HUKO ZANZIBAR !!
 
Dawa kubwa ya kulevya ni Pombe...watu hawaelewi tu.
Dunia nzima sio wajinga kuyapiga vita madawa ya kulevya !! Wanajua madhara yake kuwa ni makubwa sana tena sana kulinganisha na madhara yatokanayo na unywaji wa pombe !!!
 
Back
Top Bottom