Ukiguswa nawe Gusa - Ushauri

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,731
40,836
Wawili wapendanapo, si ajabu kugusana,
Popote pale walipo, wazee hata vijana,
Ije mvua na upepo, mikono watashikana,
Fumbo kubwa la mguso, unapoguswa gusika!!

Wengine wanashituka, pale wao wanaguswa,
Pembeni wakaja ruka, kama wamekoswa koswa,
Wakabakia kucheka, hawajui la kupaswa,
Ni utamu wa mguso, unapoguswa gusika!!

Wapo wapenda mgongo, wakakigusa kiuno,
Kwa mbwembwe na kwa maringo, wakikenua na meno,
Wamejawa na usongo, yamewatoka maneno,
Mtetemo wa mguso, unapoguswa gusika!!

Wapo wapenda kifua, wakaligusa na tumbo,
Lengo lao twalijua, wanaamsha majambo,
Haraka wakipumua, utadhania mgambo,
Ladha kubwa ya mguso, unapoguswa gusika!!

Wapo wependa kugusa, visoguswa hadharani,
Wakayafanya makosa, wakajaitwa wahuni,
Mkitaka kuvigusa, mjifunguie chumbani,
Ni fahari ya mguso, unapoguswa gusika!!

Uguse aliye wako, karibu mshikilie,
U mguse atakako, asije akachukie,
Wa mwenzako huyo mwiko, tamaa usiwakie
Siri kubwa ya mguso, unapoguswa gusika!!

Ninawasihi wenzangu, msiogope kugusa,
Ni kipaji chake Mungu, ukiguswa nawe gusa,
Ukaondoa machungu, na machozi kupangusa,
Ni uhondo wa mguso, unapoguswa gusika!!

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)
 
Back
Top Bottom