SoC01 Ukatili na Unyanyasaji wa Kingono kwa watoto na vijana: Madhara na jinsi ya kukabiliana na vitendo

Stories of Change - 2021 Competition

BAAJUN POET

Member
Jul 15, 2021
6
11
Makala hii ikufikie wewe Mzazi, Mlezi, Kaka, Dada na Ndugu wote ambao mnao wadogo zenu au watoto wenu ambao wapo mashuleni au Vyuoni. Na bado hujui kuhusiana na jambo kubwa na la hatari linalowasibu ambalo ni tishio kwa maadili yao, utu wao na maisha yao kwa ujumla.

Nianze kwa kunukuu ya kuwa:
"Hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya kuwa hayapo." -Mwalimu J. K. Nyerere. (Mwisho wa kunukuu)

Mimi ni kijana wa Miaka 21 ambaye leo hii nimeona bora niliongelee suala hili ambalo bila shaka kwa wazazi, walezi, serikali na jamii kwa ujumla imekuwa ikilifumbia macho kutokana na uzito wake. Suala ambalo linawatesa watoto na vijana wengi hasa Mashuleni na Vyuoni (ambapo nikiwa kama mwanafunzi nimeshuhudia haya).

Si suala jengine bali Ukatili na Unyanyasaji wa Kingono kwa watoto na vijana wa Kike na Kiume; ikiwemo Ubakaji na Uingiliaji Kinyume na Maumbile!

Binafsi yangu, haikuwa rahisi kuamua kuingia katika utafiti wa jambo hili; kwani ni miongoni mwa mambo yanayo ogopwa kuongelewa.

Swali ni Je, kwanini nimepata ujasiri wa kuliongelea? Ni kwasababu tatizo hili linazidi kukua kwa kasi sana hasa Mashuleni na Vyuoni, na pengine linagusa watu wengi na familia nyingi. Kusudi kuu la simulizi na makala hii ni kuisaidia jamii kwa kuipa maarifa juu ya mzizi wa tatizo na nini kifanyike kupunguza kasi ya tatizo hili sugu katika ngazi za familia, taasisi za elimu kama shule, vyuo na Jamii kiujumla.

Kutatua hili, ni vizuri kwanza tukubali kuwa tatizo hili lipo, japo ni zito na linatia ukakasi linapoongelewa mbele za watu.

Katika kuuanza utafiti wangu nilianza kuipitia Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania, ya mwaka 2018. Ambapo takwimu zinaonesha ya kuwa hadi mwaka 2018 kumekuwa na ongezeko la watoto 2,365 waliofanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono. Huku kila mwezi pakikadiriwa idadi ya watoto 394. Na idadi ya watoto wa kiume wanaofanyiwa vitendo hivyo ikiongezeka mara 45 zaidi kuanzia mwaka 2017/2018.

Aidha, ripoti hiyo haikukinzana na taarifa ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe, alipoliambia bunge ya kuwa; kesi zinazoripotiwa za ukatili wa kingono kwa watoto kati ya mwaka 2012/2015 hufikia wastani wa kesi 19 kila siku! Huku watoto wa kiume wakifikisha jumla ya kesi 2,031 kwa mwezi Januari hadi Machi, 2016!

Katika utafiti wangu nimegundua ya kuwa, licha ya kuazishwa kwa madawati mengi ya kijinsia, kesi za ukatili na unyanyasaji wa kingono kwa watoto na vijana (hasa wa kiume) zimekuwa zikiripotiwa kwa uchache sana na familia husika, au haziripotiwi kabisa! Ukilinganisha na kesi za watoto au vijana wa kike ambao walau wao kesi zao huripotiwa.

Swali ni kwanini kesi za watoto na vijana wa kiume wanaopitia unyanyasaji na ukatili huu wa kingono zimekuwa zikifichwa na wanajamii hasa wanafamilia?

Kuna machache yaliyosemwa na wananchi:
"Kutokana na jamii zetu kulichukulia suala hili ni fedheha, inawalazimu kuficha na kuwa kimya, hapo huyamaliza masuala haya kifamilia ili kulinda heshima ya familia na heshima ya vijao wao." Alisema mmoja wa wananchi hao.

"Hata hivyo hakuna mzazi asiyependa kuona haki inapatikana kwa unyanyasaji wowote wa kingono anaofanyiwa mtoto wake. Lakini iwapo alichofanyiwa mtoto huyo kitaripotiwa, kisha kesi kufikishwa mahakamani, bila shaka jambo litakuwa kubwa na litajulikana na watu wengi, na hofu yetu ni kuwa, mtoto huyu ataonekanaje katika jamii? Na hapo ndipo unapoona wazazi wengi huyamaliza masuala haya kifamilia. Jambo ambalo pia lina changamoto zake kwani huchochea wahalifu wengine kuendelea zaidi na kutenda makosa."


Kutokana na maelezo hayo, nilipendelea kujua sababu kuu za tatizo hili ambazo baadhi ya maoni ya wachangiaji yalikuwa kama ifuatavyo:

1. Malezi na Makuzi ya Mtoto: Mzazi au mlezi kushindwa kufuatilia makuzi ya mtoto wake, hata kwa kumkagua. Mzazi kushindwa kumsikiliza mtoto na kuwa bize na kazi. Lakini pia mzazi au mlezi kuwa Mkali sana. Ukali unaopelekea hofu kwa mtoto au kijana huyo hivyo kushindwa kuongea na mzazi wake kuhusu yanayomsibu.

2. Vishawishi: mashuleni (hasa Boarding Schools) na vyuoni kuna ushawishi mkubwa sana. Vishawishi kutoka kwa marafiki pamoja na watu wa nje ya shule na vyuo. Ni vema wazazi wakawatimizia haja zao watoto wao. Na kuwajengea watoto hao misingi mizuri ya kimaadili na kiuchamungu.

3. Mazingira: Kuna mazingira huchochea vitendo hivi hasa kama mazingira aliyopo mtoto au kijana yana mjumuiko wa shughuli hatarishi kama uuzaji na utumiaji wa pombe, bangi na madawa ya kulevya, kadhalika na masuala mengine ya anasa.

4. Mila na desturi: Vijana wengi wamekuwa wakihofia kusema yanayowasibu sababu pengine kuongelea kuhusu masuala hayo kama ubakaji na ulawiti yamekuwa ni Mwiko kuongeleka katika jamii zetu. Hivyo unamkuta kijana amefanyiwa ukatili huo ila anakaa kimya.

5. Matatizo ya Kiakili: wengine hufanya vitendo hivi wakiwa hawajitambui kiakili.

6. Umasikini: hii imekuwa sababu kubwa ambapo watoto na vijana wengi (hasa wanafunzi) wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za maisha na mahitaji yao ya msingi, hali inayowalazimu kuingia katika vitendo hivi bila ya kujua kuwa vitendo hivyo kwao ni ukatili wa kijinsia na ni hatari kwa afya zao. Pia kuna baadhi ya watoto na vijana hufanya vitendo hivyo wakiwa na nia ya kusaidia uchumi wa familia zao; huku familia hizo zikiwa ima zinajua au hazijui.

7. Rushwa na Ubinafsi: Hii hutokea ambapo matatizo haya huchukuliwa kawaida sana katika vyombo vya sheria. Huwezi kushangaa kuona Kesi imefikishwa pahala husika lakini baadhi ya maofisa wasio na utu wakila rushwa na kuishauri familia kulimaliza suala kindugu. Kwasababu tu Pengine aliyefanya kitendo hicho ni mtu mzito au tajiri mwenye pesa na mali nyingi.
Imeonekana ya kuwa kwa familia masikini nyingi imekuwa ni vigumu kwao kuendesha kesi hizi kwa kuhofia gharama na vitisho.

MADHARA YA VITENDO HIVYO NI YAPI?

Kuna madhara kadha wakadha, anayokutana nayo mtoto au kijana anayefanyiwa ukatili na unyanyasaji wa kingono ikiwemo kubakwa au kulawitiwa kama ifuatavyo:
1. Magonjwa
2. Kifo (kujiua)
3. Kupotezewa heshima na utu wake
4. Kupotezewa ndoto na malengo yake
5. Kuvunjiwa haki zake za msingi
6. Kupungua kwa ujasiri wake
7. Kuelemewa na mawazo
8. Kuwa na hali ya kutokujiamini
9. Kuwa ni mtu wa kujutia
10. Udumavu wa kimwili na kifikra

NINI KIFANYIKE KUKABILIANA NA TATIZO HILI?

A) Kwako mzazi, mlezi, ndugu, jamaa na marafiki, ni vema kufuata yafuatayo ili kuepukana au kumuepusha ndugu yako au mwanao kutokana na kufanyiwa vitendo hivyo:

1. Kuwa na ukaribu na kijana wako. Mfanye ajihisi amani awapo na wewe hata akuelezee lolote linalomsibu.

2. Mpe malezi bora ya kiuchamungu na kiutambuzi kijana wako. Mfanye awe mwerevu, mpe ujasiri na mfanye awe na misimamo mikali na asimamie ndoto zake.

3. Chagua pahala salama pa kumsomesha kijana wako. Epuka boardings schools kama hakuna ulazima. Si vibaya kumpeleka boarding mwanao, lakini usimtelekeze kwa kipindi chote cha masomo yake.

4. Kuwa na tabia ya kufiatilia mienendo na makuzi ya mtoto wako. Muepushe na yasiyostahili kwake kwa kutumia njia nzuri. Na sio ukali. Chunga malazi yake pia! Hakikisha kuna utaratibu mzuri juu ya wale anaoshinda nao au kulala lao.

5. Muoneshe wapi anahitajika kwenda. Na muoneshe wanaomfaa. Kisha Mpongeze inapobidi.

B) Kwa serikali, sekta binafsi na Jamii kwa Ujumla:
1. Itolewe elimu ya kutosha kwa watoto na vijana kupitia vilabu vya mashuleni na vyuoni, mitandao ya kijamii, vyombo vya habari, madawati ya jinsia, pamoja na majukwaa ya sanaa na vikundi vya vijana.

2. Kufanyike maboresho ya sheria juu ya adhabu na kufanyike kampeni za kutosha za kupinga vitendo hivyo na kuwabaini wote wanaowafanyia watoto vitendo hivyo na wale wanaopokea rushwa kuficha maovu hayo.

3. Mila na desturi zinazopinga kuongelea masuala ya afya ya uzazi na yale ya uelimishaji rika halikadhalika masuala ya unyanyasaji wa kingono zinapaswa kupingwa vikali kuanzia ngazi ya Familia. Masuala haya yanapaswa kuonekana ni Jambo la kawaida kuongeleka katika jamii.

Mabadiliko ni sisi! Kwa pamoja tunaweza! Jukumu hili ni letu sote!

images (1).jpg

MWISHO.

Imeandaliwa na,
OMARY BAAJUN (21)
Mwanafunzi, Chuo Cha Utumishi wa Umma (TPSC), DSM.
0684-956-676
29 Julai 2021.
 
Ahsante kwa and iko Zuri.. Lakini pia kuna haja ya kuangalia suala la usiri wa taarifa hasa uendeshaji wa mashitaka na kesi mahakamani ili kulinda utu wa mhanga wa vitendo vya ukatili. Ama sivyo kuwe na utaratibu wa kuwa na package ya Counseling kwa wahanga wote ili kuwaweka sawa kiakili.
 
Back
Top Bottom