singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Bibi. Jenista Mhagama (Mb), akifuatilia maelezo ya wajumbe wa kikosi Maalum cha kukagua vibali vya Ajira za Wageni (hawapo pichani) wakati alipokutana nao Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Desemba, 2015, (katikati) ni Naibu Waziri (Kazi, Ajira na Vijana), Anthony Mavunde na Katibu Mkuu (kazi na Ajira), Eric Shitindi.
Serikali imeamua muda wowote kuanzia mwezi huu kuanza ukaguzi wa vibali vya Ajira za Wageni nchini, kufuatia muda wa siku 14 kuisha uliotolewa na serikali katika tangazo la utolewaji wa vibali vya kazi kwa wageni nchini lililotiwa saini Desemba 14, mwaka huu, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Aiira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Jenista Mhagama (Mb), ambaye aliwataka waajiri wote nchini kwa muda wa siku hizo wawe wametekeleza matakwa ya Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya Mwaka 2015.
“Katika taarifa tuliyoitoa mwezi huu, tuliwajulisha waajiri wote wenye waajiriwa wageni ambao wana vibali vya kazi za muda (Carry on Temporary Assignment) na wale wote wasiokuwa na vibali vya ajira vilivyotolewa na kamishna wa kazi nchini kuwa wanatenda kosa. Kamishna wa kazi amepewa mamlaka kutoa vibali vya ajira kwa wageni wanaotaka kufanya kazi nchini. Hivyo hakuna mamlaka nyingine yoyote inayoruhusiwa kutoa vibali vya ajira kwa wageni,” amesema Mhagama
Amesema hayo, Tarehe 29 Desemba, 2015, Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na kikosi maalum kitakachoendesha operasheni hiyo chenye wajumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uhamiaji na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (OSHA), ikiwa lengo ni kufuatilia kama agizo lililotolewa na serikali limefuatwa na kuhakikisha taratibu zinazopaswa kufuatwa katika utoaji wa vibali vya ajira zinazingatiwa.
“Serikali ilitoa muda wa siku 14 kwa waajiri wote wawe wametekeleza matakwa ya Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.” Alisitiza Mhagama.
Mwezi Machi, mwaka huu Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya Mwaka 2015 (The Non-Citizens (Employment Regulation) Act)). Sheria imeanza kutumika rasmi tangu tarehe 15 Septemba, 2015. Sheria hiyo inaanzisha Mamlaka moja yautoajiwa vibali vya ajira kwa wageni na Mamlak ahiyo ni Kamishna wa Kazi.