Ukaguzi wa majengo pale linapotokea tishio la jengo kuanguka unatia shaka

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Edsimba.jpg

Maoni ya Katuni



Hivi sasa katika miji mikubwa, likiwemo Jiji la Dar es Salaam, ujenzi wa majengo makubwa ya ghorofa umeshamiri karibu kila kona. Hii ni hatua nzuri ya maendeleo ya makazi na vitega uchumi.
Lakini pamoja na umuhimu wake, inatia shaka kama ujenzi huu unafuatiliwa ili kuhakikisha kuwa unafanyika kitaalamu na kwa viwango vya ujenzi vinavyokubalika.
Matukio ya majengo kuanguka au hatarini kuanguka kutokana na nyufa kujitokeza katika hatua mbalimbali za ujenzi, yameripotiwa sana miaka ya nyuma hasa katika Jiji la Dar es Salaam hata kufikia hatua ya kuundwa kwa tume kufuatilia ujenzi huo.
Ikashauriwa kwamba ufanyike ukaguzi wa mara kwa mara kwa majengo yote yanayojengwa kabla ya kuanza kutumika. Hata hivyo, inavyoonekana ni kwamba ukaguzi haupo na ndiyo maana bado ujenzi unafanyika kiholela jambo ambalo ni hatari sana kwa maisha ya watu na mali.
Kwa mfano, wiki hii katika jiji la Dar es Salaam serikali imesitisha ujenzi wa jengo moja la makazi na biashara lenye ghorofa nane kwenye kiwanja namba 8/33 kilichoko makutano ya barabara za Swahili na Mafia.
Ni hatua iliyokwenda sambamba na kuhamishwa kwa wafanyabiashara wote na wapangaji wa jengo hilo kwa ajili ya usalama wao.
Hatua hiyo ilitokana na jengo hilo linalomilikiwa na Hamisa Mohamed kujengwa chini ya kiwango na kupasuka nyufa kuanzia ghorofa ya kwanza hadi ya tatu na kuashiria kuwa halitaweza kuhimili uzito wa ghorofa zinazoendelea kujengwa.
Kwanza tunawapongeza wale wote walioona nyufa hizo na kutoa taarifa mara moja. Pili, tunaipongeza serikali ya mkoa wa Dar es Salaam kwa kusitisha ujenzi huo ambao tayari umeashiria hatari baadaye.
Hata hivyo, sisi tunajiuliza, hivi matukio ya huko nyuma ambapo mengine yalisababisha vifo kutokana na ujenzi wa kiwango duni hatujifunzi kutokana na makosa? Ukaguzi ule tulioambiwa utafanyika mara kwa mara katika hatua mbalimbali za ujenzi uko wapi?
Kinachoshangaza zaidi ni kwamba ipo Bodi ya Usajili wa Wakandarasi Nchini(CRB) ambayo ina wajibu wa kukagua majengo yote nchini kubaini uimara wake kwa usalama wa watu na mali zao.
Haipendezi chombo hiki kiwe kinakurupuka pale tu linapotokea tatizo kama hilo la ghorofa kuwa na nyufa kabla hata halijatumika.
Kama nyufa hizo zingejitokeza mara baada ya jengo kujaa watu ingekuaje? Balaa hilo angelaumiwa nani? Mungu apishilie mbali, lakini kama kipo chombo cha ukaguzi lakini hakifanyi kazi yake inavyotakiwa, hili ni kosa kubwa la jinai.
Bodi hii baada ya jengo hilo kusitishwa ujenzi, imeibuka na kusema eti imeanza kufanya ukaguzi kila siku katika majengo yanayojengwa ili kutambua ubora wa vifaa vinavyotumika kwa ujenzi. Je, kwa jengo hilo la ghorofa nane, wakaguzi wake walikuwa wapi hadi karibu linakamilika?
Inawezekana kabisa yapo majengo mengi yaliyo katika hatua mbalimbali za ujenzi ambayo yamejengwa chini ya kiwango lakini hakuna anayeshughulika nayo. Hivi tunasubiri hadi maafa yatokee ndipo tuanze kukimbizana na kutupiana lawama?
Ni muhimu vyombo vya serikali vilivyopewa dhamana ya kusimamia maendeleo pamoja na huduma za jamii kutimiza wajibu wao wa kila siku badala ya kukurupuka pale tu linapotokea tatizo.
CRB inapaswa kuwa makini hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote kutokana na maeneo mengi kujengwa majengo makubwa ya kisasa ambayo kama hayatasimamiwa vema katika hatua zote za ujenzi, maafa makubwa yanaweza kulighubika taifa bila sababu.



CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
 
Back
Top Bottom