Ujamaa umempofusha Mukama; Wafanyabiashara wakiondoka CCM itanusurika?

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
*Wafanyabiashara wakiondoka CCM itanusurika?
*Atakiwa kuangalia mazingira ya sasa yalivyo duniani
*Armando Guebuza, Mwai Kibaki ni wafanyabiashara
Na Waandishi Wetu


Alianza Nape Nnauye
Mapema, Katibu wa Idara ya Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye, akiwa ziarani mjini Iringa wiki mbili zilizopita, alikaririwa na vyombo vya habari, likiwamo gazeti hili, akiwataka wafanyabiashara wote waondoke ndani ya chama hicho, ikiwa ni moja ya hatua ya kujivua gamba, kwa maelezo kwamba chama sasa kinarudi katika misingi yake ya kuwa mtetezi wa wakulima na wafanyakazi.

Katika hotuba yake kwa wafuasi wa chama hicho mjini Iringa, Nape alikaririwa akisema chama hicho sasa hakihitaji misaada ya wafanyabiashara kwa kuwa kinayo miradi inayoweza kukiingizia fedha nyingi endapo itasimamiwa vizuri.

Wiki iliyopita, Katibu Mkuu, Wilson Mukama, alirudia kauli ya Nape ya kuwataka wafanyabiashara waondoke ndani ya chama hicho wakati alipoanza ziara ya siku nane katika Mkoa wa Mara, mkoa ambao ni mara ya kwanza kuutembelea tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo mwezi uliopita. Mukama ni mwenyeji wa mkoa huo.

Mukama achochea tafakuri zaidi
Hata hivyo, tofauti na Nape, kauli ya Mukama, pengine kutokana na nafasi yake kama mtendaji mkuu wa chama, imesababisha kuibuka kwa hoja mbalimbali kuhusiana na mustakabali wa kisiasa wa Chama Cha Mapinduzi na wanachama wake, baadhi wakisema maadam kauli hiyo si msimamo ulioafikiwa katika vikao rasmi vya chama, unaonyesha mgongano wa kiitikadi miongoni mwa viongozi, wanachama na wafuasi wa chama hicho.

“Unajua Mukama ni mtu mwenye mrengo wa wastani uliogemea kushoto (centre leftist) na pengine ndio maana anaona kuwa njia pekee ya kukijenga chama ni kuugeukia mfumo wa kijamaa. Hiyo ndiyo nadharia yake. Si makosa kuwa na nadharia kama hii, lakini wakati wa sasa kiongozi lazima awe pragmatic, huwezi kuwaondoa wafanyabiashara katika chama kwa kuwa utakuwa unalitenga kundi muhimu na linalokua na kuongezeka kila siku,” anasema mfanyabiashara mmoja wa Dar es Salaam ambaye ni mwanachama wa CCM.

Kuibuka kwa tabaka la wafanyabiashara
Katika hali ya kawaida, mfanyabiashara huyo anasema, Chama Cha Mapinduzi, ambacho kwa kipindi cha miaka karibu 20 sasa kimejipambanua na wafanyabiashara kupitia misimamo na sera zake za kuinua uchumi, itakuwa ni vigumu kuamka siku moja na kusema hakitaki kuwa na wanachama na viongozi ambao ni wafanyabiashara.

Kauli ya mfanyabiashara huyo inatokana na ukweli kwamba ingawa chama hicho kilianzishwa kikiwa na lengo kubwa la kuwatumikia wakulima na wafanyakazi wa Tanzania, mageuzi makubwa ya kisiasa, kijamii na kichumi yaliyotokea duniani, yamekifanya chama hicho kugeuka na kuwa nguzo kubwa ya kuibuka kwa kundi jingine kubwa la wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo miongoni mwa viongozi na wanachama wake.

“Wengi wa wafanyabiashara waliopo hawajatoka nje ya CCM, hawa ni zao la sera zilizohuishwa ndani ya chama hicho kutokana na mageuzi makubwa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi yaliyotokea kote duniani mwishoni mwa miaka ya themanini. Ukitazama nyuma na kufikiria kurudi kule tulikotoka bila ya kuangalia mazingira ya sasa ya Tanzania na dunia, huwezi kubaki na mtu kwa kuwa kila mtu ndani ya chama anafanya biashara ya aina fulani,” anasema Mbunge wa CCM kutoka kanda ya magharibi, ambaye pia alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina na kisha kuongeza:

“Katika dunia ya leo ni Korea Kaskazini tu inayozungumzia Ujamaa wa mrengo wa kushoto. Hata Cuba na Venezuela sasa zimeanza kufungua milango kwa ajili ya uwekezaji. Hii ina maana kwamba biashara sasa inakuwa sehemu ya uchumi wa nchi na kwa maana hiyo kundi la wafanyabiashara linanza kujijenga taratibu. Hata dola kuu la Urusi (USSR) lililokumbatia Ujamaa na Usoshalisti mkongwe sasa halipo tena.”

Azimio la Zanzibar na athari zake
Na kwa hakika tangu kupitishwa kwa Azimio la Zanzibar mwaka 1992, lililoruhusu viongozi wa chama kujihusisha na biashara, CCM imejikuta ikijenga tabaka la wafanyabiashara wa aina zote, wakiwamo wakubwa na wadogo, huku wachache waliokuwa nje ya mkondo wa chama, wakivutiwa kujiunga na chama hicho.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa za Tanzania wanalitazama Azimio la Zanzibar kama ndio kaburi lilimozikwa Azimio la Arusha la Februari 5, 1967 ambalo liliweka masharti magumu kwa viongozi, likiwataka wasijihusishe na biashara ya aina yoyote, ikiwamo hata ile ya kumiliki nyumba za kupangisha.

Kwa kuwakataa wafanyabiashara, chama hicho huenda kikajikuta katika mgongano mkubwa wa kiitikadi na wanachama wake maarufu, baadhi yao wakiwa ni wale ambao kwa miaka yote hiyo, wametumia muda na rasilimali zao nyingi katika harakati za kukijenga chama kwa kufadhili mikutano, chaguzi na shughuli nyingine mbalimbali za chama hicho.

Wafanyabiashara makada wa CCM
Miongoni mwa wafanyabiashara hao ni kama wafuatao:

Abdulrahman Kinana: Mmoja wa makada wakubwa ndani ya CCM ambaye mchango wake kwa chama ni mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuwa msimamizi mkuu wa kampeni za wagombea wa urais wa chama hicho kuanzia mwaka 1995 wakati wa Rais Benjamin Mkapa hadi 2010 wakati wa Rais Jakaya Kikwete.

Baada ya kuamua kuacha utumishi wa Serikali mwaka 1995, Kinana amekuwa akijishughulisha na biashara mbalimbali na hajawahi kutumikia nafasi yoyote ya utendaji ndani ya chama hicho, ukiacha nafasi ambayo anaishikilia hadi sasa ya ujumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Biashara za Kinana ni matokeo ya kuhuishwa kwa msimamo wa CCM kulingana na mazingira ya kisiasa na kiuchumi duniani.

Rostam Aziz: Huyu ameingia rasmi katika siasa baada ya kuwania ubunge wa Igunga katika uchaguzi mdogo uliofanyika 1994, kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Charles Kabeho. Amekuwa akiendesha biashara ya kifamilia kwa muda wote huo, huku naye akiwa mhimili mkubwa ndani ya chama hicho katika siasa za ushindani, hasa kwa kutoa mchango mkubwa katika kampeni za Mkapa katika vipindi vyote viwili na hata kwa Rais Jakaya Kikwete katika vipindi vyote viwili.

Mbali ya kuwahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu na sasa Halmashauri Kuu ya Taifa, amewahi pia kukitumikia Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa mmoja wa wajumbe wa sekretarieti iliyokuwa chini ya Mzee Yusuf Makamba, akisimamia Idara ya Fedha na Uchumi.

Nimrod Mkono: Mmoja wa wanasheria mashuhuri na pengine anayemiliki kampuni kubwa ya kisheria kuliko zote Tanzania, ikiwa na ofisi katika nchi mbalimbali duniani, zikiwamo Uingereza na Marekani. Pamoja na kufanya biashara na wateja mbalimbali ndani na nje ya nchi, Kampuni ya Mkono Advocates anayoimiliki, imefanya kazi kwa karibu na Serikali katika kesi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania. Hivi sasa ni Mbunge wa Musoma Vijijini, ambako anafanya vema katika kuinua maisha ya wakazi wa huko na hivyo kuwa mmoja wa makada wa kupigiwa mfano wa chama hicho.

Mwita Chacha Gachuma: Ni mmoja wa wafanyabiashara maarufu katika Kanda ya Ziwa, anayemiliki vitega uchumi mbalimbali na ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa Chama Cha Mapinduzi katika shughuli mbalimbali za chama. Mpaka sasa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na mchango wake wa hali na mali unahesabika kuwa moja ya michango adhimu kwa chama katika Kanda ya Ziwa.

Anthony Diallo: Huyu ni mfanyabiashara mwingine katika Kanda ya Ziwa ambaye hadi siku za karibuni, alikuwa akihesabika kuwa mmoja wa magwiji wa siasa katika kanda hiyo, akitumia rasilimali zake katika kuuza sera na mafanikio ya CCM kwa Watanzania kupitia vyombo vya habari anavyovimiliki, vikiwamo redio, televisheni na gazeti. Amekuwa katika siasa za CCM tangu mwaka 1995 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Mwanza Vijijini, jimbo ambalo baadaye lilibadilishwa jina na kuitwa Ilemera.

Salim Abri: Huyu ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa katika Mkoa wa Iringa, lakini wakati huo huo akiwa mmoja wa makada mashuhuri ndani ya chama hicho. Misaada yake kwa Chama Cha Mapinduzi mkoani Iringa ni mkubwa pengine kuliko wafanyabiashara wengine wote mkoani humo, wakiwamo hata wale waliowahi kushika nyadhifa nzito serikalini. Ni mmoja wa watu wanaoheshimika sana ndani ya CCM katika Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.

Azim Suleiman Premji: Huyu ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma ambaye naye ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa mkoani humo na ambaye kwa miaka mingi, amekuwa mmoja wa wachangiaji wakubwa katika chama chake.

Deo Kasenyenda Sanga: Huyu ni mfanyabiashara maarufu mkoani Iringa, akijulikana na watu wengi kwa jina la Jah People, ambaye mchango wake katika kukisaidia chama umemfanya apendekezwe na hatimaye kushinda katika kinyang’anyiro cha Mwenyekiti wa CCM Mkoa, akiwaangusha wanasiasa wakongwe na wazito kama Philip Mangula, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM enzi za utawala wa Benjamin Mkapa. Sanga pia ni Mbunge wa Njombe Kaskazini.

Mohsin Abdallah Sheni: Huyu pia ni mfanyabiashara maarufu mkoani Kigoma, ingawa pia wakati mwingine huweka makazi yake jijini Dar es Salaam. Wanachama wa CCM Mkoa wa Kigoma wanajua namna mfanyabiashara huyo, ambaye sasa ni mjumbe wa NEC, anavyojitolea kusaidia harakati na shughuli mbalimbali za chama na anaelezwa kuwa alikuwa msaada mkubwa kwa wagombea wote wa CCM, kuanzia wale wa udiwani na ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Nawab Mulla: Ni mfanyabiashara maarufu mkoani Mbeya ambaye sasa ndiye Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa. Huyu amekuwa mmoja wa makada maarufu na waaminifu kwa chama hicho, ambaye pamoja na kukumbana na vikwazo na mitikisiko mbalimbali katika siasa, hajawahi kukisaliti chama chake bali ameendelea kukisaidia katika kunadi sera zake kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya. Yeye mwenyewe anasema uadilifu ndio kitu kinachotakiwa kizingatiwe katika harakati za kujivua gamba zinazoendelea ndani ya chama badala ya kumwangalia mtu kutokana na mali anazomiliki.

Kisyeri Chambiri: Huyu ni mwanasiasa na mfanyabiashara wa siku nyingi mkoani Mara, ingawa sasa amechaguliwa kuwa Mbunge wa Babati Mjini. Amewahi kuwa Mbunge wa Tarime kwa kipindi cha miaka kumi tangu 1995 kabla ya kuangushwa na Chacha Wangwe mwaka 2005. Familia ya Chambiri mkoani Mara ni moja ya familia zinazotambulika kwa juhudi zake katika biashara na imekuwa moja ya nguzo kuu za CCM katika mkoa huo kutokana na mchango wake wa hali na mali katika kukiimarisha chama.

Abdul-Aziz Mohamed Abood: Ingawa amechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka jana kuwa Mbunge wa Morogoro Mjini, mfanyabiashara huyo aliyejikita zaidi katika sekta ya usafirishaji, amekuwa mmoja wa makada wa muda mrefu wa Chama Cha Mapinduzi mkoani humo, akijitokeza kusaidia pale chama kinapokuwa na shida. Hatimaye mwaka jana alifanikiwa kuukwa ubunge wa Morogoro mjini, nafasi ambayo amekuwa akiipigania kwa zaidi ya miaka 15 sasa. Anamiliki pia redio na kituo cha televisheni mjini Morogoro.

Reginald Mengi: Mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini Tanzania na kada wa CCM ambaye si tu amekuwa akikisaidia chama hicho kueneza sera zake kupitia mtandao wa vyombo vya habari anavyovimiliki, bali pia kutoa misaada mbalimbali kwa makundi ya walemavu, vijana na wanawake na hivyo kuchangia kwa vitendo utekelezaji wa sera za CCM.

Frederick Sumaye: Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania ambaye anaedsha ufugaji wa kisasa wa kibiashara baada ya kumaliza miaka kumi ya uwaziri mkuu chini ya Benjamin Mkapa. Amekisaidia sana chama chake kusimamia utekelezaji wa ilani za uchaguzi za Serikali ya Awamu ya Nne na mpaka sasa ameendelea kuwa kada muhimu katika chama hicho.

Wabunge wengine wafanyabiashara
Ukiachilia mbali wafanyabiashara hawa waliotajwa, chama hicho pia kinao wafanyabiashara wengi wanaoshikilia nafasi mbalimbali na ambao wamekuwa msaada mkubwa katika kufanikisha harakati za kisiasa za chama hicho. Baadhi yao ni pamoja na Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji, Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga (huyu ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia), Mbunge wa Ilala Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge na Mbunge wa Mikumi, Abdulsalaam Seleman Amer.

Wengine ni Mbunge wa Kwimba, Mansoor Shanif Hiran, Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya, Mbunge wa Handeni, Dk. Abdallah Kigoda, Mbunge wa Kibaha Mjini, Sylvestry Koka, Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Ramadhan Madabida, Mbunge wa Kibaha Vijijini, Abuu Hamoud Jumaa na Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji.

Wabunge wengine ambao pia ni wafanyabiashara wanaokitangaza na kukipigania chama chao ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum, Dk. Getrude Rwakatare, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza, Mbunge wa Solwa, Ahmed Ali Salum, Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby, Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Esmail Hassan Shah, Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Vijral Soni na Mbunge wa Kishapu, Suleiman Masoud Nchambi.

Mawaziri nao wana biashara zao
Ukiachilia mbali idadi hiyo ya wabunge wanaofanya biashara za aina mbalimbali, karibu mawaziri wote katika Serikali ya Awamu ya Nne, wanafanya biashara ya aina moja au nyingine, biashara ambazo baadhi yao wanazisimamia wao wenyewe na wengine familia zao.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema katika hali kama hiyo, si rahisi kwa Chama Cha Mapinduzi kuwataka wafanyabiashara wajiondoe katika chama kwa sababu kama kweli wakiamua kuitikia wito huo, chama kinaweza kikajikuta kikisambaratika kwa kuwa tayari kimeshajenga kada hiyo miongoni mwa wanachama na viongozi wake.

Mazingira ya kisiasa Tanzania
Wengine pia wanajaribu kuangalia mazingira ya ndani ya Tanzania kwa kuilinganisha CCM na vyama vingine, pamoja na msukumo wa sera za chama katika kupiga vita umaskini miongoni mwa Watanzania.

“Ukisema humtaki mfanyabiashara katika chama, utakuwa unamtaka nani? Unataka watu maskini ndiyo wawe wanachama na viongozi wa chama. Ni wazi hapa kwamba kuna mkanganyiko, kwamba wakati sera za chama zikianisha juhudi za kuondoa umaskini miongoni mwa Watanzania, wakati Serikali ikihimiza uwekezaji wa ndani na nje, wewe unataka chama chako kisiwe sehemu ya mageuzi haya. Huu ni mkanganyiko,” anasema mfanyabiashara mmoja kutoka Kanda ya Ziwa ambaye pia ni mmoja wa viongozi na makada wa CCM.

Mfanyabiashara huyo anasema hata viongozi wa vyama vingine vikubwa vya siasa Tanzania ni wafanyabiashara, akimtaja Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP), John Cheyo, huku akienda mbali zaidi kwa kuwataja wafanyabiashara maarufu kama Philemon Ndesamburo na Edwin Mtei ambao ni miongoni mwa watu wanaoheshimika katika Chadema.

“Unapokuwa Mwenyekiti wa CCM kuanzia ngazi ya mkoa hadi shina, unakuwa huna mshahara, na hii ina maana kwamba lazima uwe na kazi ya kufanya ili kujiingizia kipato. Kwa uzeofu wangu, viongozi wengi katika ngazi hizo wana biashara zao zinazowaingizia kipato cha kila siku.

Unapowafukuza hawa unategemea nini? Sheria za nchi zinakataza mwanasiasa kufanya kazi serikalini.

Majirani zetu nao vipi?
“Nenda kwa majirani zetu, kuanzia Kenya mpaka Msumbiji, Chama cha Frelimo ni chama rafiki wa CCM, lakini Rais wa Msumbiji, Armando Guebuza, anayetokana na chama hicho ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini Msumbiji. Rais Mwai Kibaki wa Kenya na hata Raila Odinga ni wafanyabiashara wakubwa. Leo hii ukiwakataa wafanyabiashara unaelekea wapi? Ni nadharia ambayo imepitwa na wakati,” anasema mfanyabiashara huyo na kuongeza kuwa hata chama rafiki cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini, kimejenga kada ya wafanyabiashara wakubwa kama Cyril Ramaphosa.

Wosia wa Nawab Mulla
Katika mazungumzo yake na Rai, Mulla (Nawab, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya) anasema lazima CCM iwe makini katika kujivua gamba na kwamba viongozi wasichanganye wafanyabiashara na watu wasiokuwa waadilifu.

“Chama kimeamua kufanya mabadiliko ili kurejesha imani ya wananchi. Katika hili tusichanganye mambo, suala linalotakiwa kusisitizwa hapa ni uadilifu, sio utajiri au umaskini wa mtu. Kuna matajiri ambao ni waadilifu, lakini pia kuna watu wasiokuwa matajiri lakini wamekosa uadilifu. Hili ndilo tunalipaswa kulizungumza kwa nguvu zetu zote.

“Halafu tunapomnyooshea mtu kidole kwamba si mwadilifu, lazima tuwe na ushahidi wa kutosha, tusijiingize katika malumbano ambayo hatuna uhakika nayo. Kama kuna watu wasiokuwa na uadilifu, bila kujali kama ni wafanyabiashara matajiri au la, na tukiwa na ushahidi wa kutosha, basi tuwawajibishe, lakini kama hatuna ushahidi tutajikuta tukiwahukumu watu wasiokuwa na hatia,” anasema Mulla.
 
  • Thanks
Reactions: FJM
I'm kinda agree with the RAI Journalist about business men in politics; everywhere in the world business people joins politics and some do wonders in thie country i.e Italy, US, Russia, UK etc...

What i can say is thoughts lead on to purposes; purposes go forth in action; actions form habits; habits decide character; and character fixes our destiny.
 
alikuwa anajifurahisha tu.

ka,a kuna kitu kinampofusha siyoni, labda upara anaouficha kwenye kapelo
 
si wataje majina tu! Hii ya kuwaita wafanya biashara ni woga. Wawaseme wasiwowataka kwa majina tuwajue na kisha wakikaidi wawafukuze, katiba yao inaruhusu. Nape mwenyewe mfanyabiashara!
 
nafasi muhimu kama hizo hushikwa na watu intellectual balaa, sasa mukama anaonyesha hajiwezi kabisa, naweza sema ni mzigo ndani ya chama.
 
What we need as a country is to find the common ground, it's beyond my comprehension why business people are being demonised while they are the biggest sources of our revenue.

Kuwa mfanya biashara hakumnyimi mtu haki ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa na kuwa kiongozi wa umma. Kinachotakiwa kuweka sheria itakayoweza kuwafanya wafanya biashara walio kwenye uongozi wasitumie vibaya nafasi za uongozi wa umma kwa manufaa binafsi. Tukiendelea na tabia hii ya kuwawaona wafanya biashara kama ni watu wenye dhambi kiasi cha kutositahili uongozi, tunawakatisha tamaa vijana wajasiliamali wasiendelee na shughuli hizo kwa kuwa wataonekana hawafai katika jamii, na hatima yake ni umasikini wa milele kwa nchi yetu.
 
Nadhani mjadala siyo kuwa wafanyabiashara tu. Ni muhimu kuangalia usafi wa jinsi utajiri wa wafanyabiashara hao unavyopatikana. Wengi wapo kwenye kundi la wahujumu uchumi na mafisadi tu. Nchi nyingi zilizotoka kwenye mfumo wa kijamaa kwenda ubepari kunakuwa na ufisadi mkubwa. Wengi wanaoibuka ni mabepari uchwara waliotumia nafasi zao kisiasa au kiserikali kujinufaisha. Mchango wao kwa jamii na uchumi ni kama hakuna.
 
CCM ndio walioweka AZIMIO LA ZANZIBAR na kweli sio Wafanyabiashara wote ni Mafisadi
 
Biashara na Siasa; this is the concept that has been abused by Tanzanian political made b'nessmen, not vice versa.
 
Makala haya ya Rai is well calculated kutetea mafisadi. Makala hayafafanui fasili ya kinachoitwa "wafanyabiashara"; iwapo ni wachuuzi, private professionals, merchants, shopkeepers, roadside sellers, hawkers, industrilialists, investors au wengineo.

Hawa wanaoitwa wafanyabiashara, lakini hawako competitive wala competent kiasi kwamba kila wakati wanategemea mipango ya kugema pesa kutoka serikalini kupitia njia za kifisadi huwezi kuwaita wafanyabishara wa kutegemewa na chama chao, but the other way round. Mfanyabiashara hawezi kuwa mkubwa kuliko kampuni yake, ikiwa hivyo, basi huyo ni mgemaji wa mali ya umma anayetumia "kampuni yake" kujipatia mali kupitia mikataba "feki" na makampuni dumavu.

Vivyo hivyo, chama chochote cha siasa hakiwezi kuwa na wanachama wanaitwa "maarufu" kiasi kwamba wako juu ya chama chao. Uanachama una hadhi kubwa kuliko biashara, hali hii ni sahihi iwapo lengo kuu la kuwa mwanachama ni kupata fursa ya kushiriki siasa. Vinginevyo tutegemee kuendelea kusikia hoja feki za wafanyabiashara na wananchama maarufu wa chama fulani (sema CCM).

Mfano halisi: Kampuni za Milambo (sema Rostam Aziz), Alfatel (sema Edward Lowasa) na Shivacom (sema Mnunuzi wa radar ya BaE) kila siku iendayo kwa Mungu consortium ya makampuni hayo matatu inaingiza shs billion 12 kutokana na mauzo ya vouchers/scratch cards za Vodacom. Lakini chunguza hadhi na visibility ya makampuni tajwa. Hizo bilioni 12 hazionekani! Kwa nini? Jibu ni rahisi; hakuna mwenye interest ya kuifanya kampuni kuwa kubwa kuliko "mmilliki". Hivyo ndivyo mapacha watatu wanavyotaka chama chao (sema CCM) kifanane/kiwe. Wao wawe juu (wananchama maarufu), chama chao kiwe chini yao ili, kama wananvyotumia makampuni yao, wakitumie chama chao kukamilisha "biashara"/"tenda" zao serikalini.

Rai linapotosha wasomaji. Uchambuzi wao ni mufilisi. Habari njema ni kuwa wahariri wake [Mihingo na Balile] tunawafahamu kwa tabia na kwa matendo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom