Uhuru wa fikra za Rais Magufuli wabadili taswira ya Tanzania Kimataifa

blix22

JF-Expert Member
Jun 23, 2013
213
645
Na Rubaba Protas

Mpango wa mataifa ya kimangharibi kujitanua kiuchumi katika mataifa yanayoendelea, huja kwa kiasi kikubwa na mbinu za kubadilisha fikra za watu ili iwe rahisi kuwatawala, kuchukua mali zao kiulaghai, kuharibu tamaduni na kuharibu mfumo mzima wa maisha katika jamii husika.

Makala hii inajikita katika kuangalia namna mifumo mbalimbali ya baadhi ya nchi za kiafrika na nchi nyingi zinazoendelea hubomolewa na mataifa makubwa kwa lengo la kuendeleza utawala wa kimangharibi kifikra na hata kiuchumi.

“Ukitaka kuangamiza taifa lolote duniani, haribu mfumo wa elimu”, ni msemo ambao wanaharakati na watetezi wa elimu huutumia. Kwa kuazima maana kuu iliyopo katika msemo huu, kwenye makala hii msemo utabeba maana; ukitaka kuangamiza taifa lolote duniani, haribu mfumo wa kufikiri, haribu tamadumi au haribu falsafa inayoendesha maisha ya jamii. Kwa muktadha huo; ukitaka kuharibu kasi ya maendeleo yanayoendelea sasa nchini Tanzania, haribu falsafa ya hapa kazi tu.

Baada ya vita kuu ya pili ya mwaka1945, dunia iliingia katika vita nyingine ambayo iliigawa dunia katika pande kuu mbili kwa tofauti za kifikra, mitazamo na falsafa iliyokuwa ikiongoza jamii za wakati huo. Mataifa tajiri ya Mangharibi yalipambana dhidi ya yale ya Mashariki. Vita ikawaacha vijana wanamapinduzi wa Afrika wa miaka hiyo: Mwalimu Julius Nyerere, Kwame Nkuruma na wengine wengi, kama watazamaji wa vita kubwa kuwahi kutokea duniani.

Naitaja kama vita kubwa kuwahi kutokea duniani kwasababu, licha ya madhara makubwa kutokea, hakuna silaha hata moja ya moto iliyotumika. Katika vita hii mashambulizi yalielekezwa kwenye fikra na mitazamo mbalimbali. Upande mmoja wa vita hiyo ulitawaliwa na fikra za kibepari chini ya Marekani kama kiranja wa nchi za Ulaya na baadhi ya zile za Amerika. Huku upande mwingine ukiongozwa na fikra za kikomunisti chini ya uongozi wa muungano wa nchi za Kirusi, Cuba, Venezuela na nyinginezo.

Mmarekani na washirika wake walijua wazi ya kuwa wakienda Moscow na teknolojia ya silaha za kivita za wakati huo,zingeweza kukutana na upinzani wa kiwango cha juu toka kwa Warusi. Ndege zao za kivita zingeweza kudondoshwa kabla hata ya kufanya maangamizi katika ardhi ya kikomunisti. Mrusi kwa upande mwingine alitambua ya kuwa akirusha ndege zake za kivita kuelekea New York, huenda hata zisingefanikiwa kuvuka bahari ya Atlantiki kabla hazijatunguliwa na Wamarekani.

Kama vita hii ingekuwa ya kutumia mtutu wa bunduki, kila upande ulikuwa dhaifu kwa mwingine. Kimantiki, vita ya silaha za moto isingeweza kutoa ushindi mwepesi kwa upande wowote ule. Na kupelekea kila upande kutafuta mbinu mbadala yenye nguvu na iliyo imara kumshinda mpinzani wake. Vita hii iliyojulikana kama vita baridi mara tu baada ya vita kuu ya pili ya dunia ndio msingi wa Makala hii. Ilikuwa vita iliyopiganwa kila mmoja akiwa ofisini au nyumbani kwake bila kuvaa.

kombati wala mandege makubwa. Ilikuwa ni vita ambayo kila upande ulilenga kuharibu falsafa za maisha ya upande mwingine.

Ni vita yenye taswira kama hii baina ya Wamarekani na Warusi ndio ilitufanya Watanzania kwa hiyari yetu, kuruhusu makampuni ya madini kutoka kwa mabeberu kuchimba dhahabu, Tanzanite, Gesi, Almasi na madini mengine na faida kubwa kwenda kwao huku tukiachiwa mashimo. Hii ndio vita ya kifikra ambayo msingi wake ni kuharibu falsafa na mitazamo ya mtu au taifa. Ndio vita tuliyoshindwa kupigana kwa miaka mingi na kutufanya watanzania kuwa wanyonge kiuchumi licha ya utajiri mkubwa tulionao.

Ni vita yenye mtazamo kama huu ambayo kwa miaka mingi Watanzania tulinyoosha mikono kuashiria kushindwa hata kuendesha bandari zetu kwasababu tuliliamini kundi la walaghai na majambazi wa kiuchumi lililotusadikisha kwamba hatuna wataalamu wala uwezo wa kiuchumi kuendesha bandari hizo.

Kwa miaka mingi vita ya kifikra imekuwa ngumu sana kwetu Watanzania kwasababu hata pale tulipoona fursa ya kuwa na umeme wa kutosheleza mahitaji ya nchini, alijitokeza mtu na mawazo tofauti kwamba tutaangamiza vyura na viumbe wengine kwenye maporomoko kule Kihansi, Stiglers (Bwawa la Mwalimu Nyerere) na sehemu nyingine. Na wale tuliowapa dhamana ya kutuwakilisha kama taifa, wakageuka kuwa wasaliti kwa kukubaliana na mawazo ya Mabeberu. Tanzania ikaendelea kubaki gizani, huku akili na ubunifu wetu wa juu ukiishia kwenye kubadilisha aina ya makopo na rangi kwenye utengenezaji wa vibatari.

Kama wahenga wanastahili kuheshimiwa na kupewa sifa kwa mafundisho yao, basi Mheshimiwa Jakaya Kikwete anastahili heshima kubwa kwa usemi wake: “Akili za kuambiwa, changanya na za kwako.” Hakika tulishindwa kuchanganya akili zetu pale tulipoletewa hadithi za kihuni na ujanja mkubwa. Viwanda vingi vilivyojengwa kwa mabilioni ya pesa viliuzwa kwa milioni kadhaa, huku udalali ukifanywa na baadhi ya wataalamu wa kitanzania waliosomeshwa kwa kodi za wananchi.

Tusisahau kwamba tafsiri ya diplomasia ya uchumi inasura nyingi kutegemeana na uwezo wa nchi kiuchumi, ushawishi wa nchi katika hoja za kimataifa, na nafasi ya nchi katika makundi mbalimbali ya kimataifa. Kwa nchi za ulimwengu wa kwanza (kama zinavyojiita), diplomasia ya uchumi huweza kumaanisha vita, ukandamizaji na hata utapeli wa kiwango cha juu. Tulijiingiza kwenye diplomasia hii ya uchumi kabla ya kujijengea heshima kwenye utajiri wa rasilimali tulizonazo, tukawapa mtaji waliokuwa tayari wanaifahamu diplomasia hiyo.

Watanzania wana wajibu mkubwa wa kuwashukuru Maraisi Wastaafu kwa kukisimika ‘Chuma’ kwenye utawala wa nchi. Mhe. Jakaya Kikwete alipotueleza habari za kutuletea chuma tukaanza kujua ni ule ule utani wake ambao hupenda kuutoa hata ndani ya hotuba zake. Leo hii watanzania wengi wamegundua ukweli ndani ya msemo wa kukileta chuma.

Hakika Rais John Pombe Magufuli ni Chuma ambacho mabeberu wameshindwa hata kukikwangua. Hiki ni chuma tena chuma cha pua chenye fikra na mitazamo sahihi kwa mustakabali wa Taifa la Tanzania. Tumekitumia Chuma kwenye makinikia, ukuta wa Mererani,

ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa na kila aina ya kazi za maendeleo ya taifa, na bado kiko imara. Chuma kimepambana na kila aina ya maadui wa taifa la Tanzania.

Tulidanganywa na kutapeliwa kwamba nguzo za umeme lazima zitoke nje ya nchi, licha ya nchi yetu kuwa na misitu minene yenye miti ya kila aina. Hii ilichelewesha maendeleo hata katika jamii. Ili upate umeme toka TANESCO kulikuwa na namna mbili za kufanya: moja kusubiri nguzo kwa zaidi ya miezi sita na mbili ni kuilipia nguzo hiyo hiyo nje ya utaratibu wa kawaida ili ipatikane kwa haraka. Mhe. Rais Magufuli, ni kweli ‘tumenyanyasika sana ndani ya nchi tajiri’. Hongera kwa mawazo mbadala na yaliyohuru, leo hii nguzo za umeme zinatengenezwa mpaka Wilayani Kasulu, tena kwa kutumia miti ya mikaratusi.

Tulidanganywa na kutapeliwa ya kwamba hatuna uwezo wa kuliendesha Shirika la Ndege la Tanzania, tukawapatia wajanja. Eti tukasadikishwa kwamba kuendesha shirika kwa ndege za kukodi kungeleta tija na ufanisi. Hii ilikuwa ni ngumi nyingine ya kichwa kwa Shirika iliyozidi kulidondosha nje ya ulingo wa mashirika ya ndege dunia. Chuma kwa mawazo yake huru tunamiliki ndege 11 zikiwemo ndege mbili za ajabu (dreamliners).

Tulidanganywa na kutapeliwa kwamba kuzalisha umeme wa maji mto Rufiji kutahatarisha maisha ya wanyamapori na viumbe wengine. Mabeberu wakageuka kuwa nyuki wakali na kila mtu akitaka kujaribu kwenda huko anafurushwa na makundi ya nyuki hao wa kigeni. Kumbe wajanja wanafurahia maisha kwa kuwinda Wanyama wetu na kuishi kwenye hoteli sawa na zilizopo huko kwao. Mawazo huru yametupenyeza Rufiji tukiwa na bilioni sita za kodi za watanzania, na sasa tunaibuka na Mradi wa Megawati 2115 kutoka bwawa la Julius Nyerere.

Tulidanganywa na kutapeliwa eti hatuwezi kuendesha bandari, tukawapatia wajanja wachache na wasaliti miongoni mwetu wakawa wanakusanya mapato na kuweka matumboni mwao. Wengi tukawa wahanga wa wizi uliotamalaki bandarini na tukaibiwa mpaka vipuri vya magari tuliyoagiza kutoka nje ya nchi. Bandari ikapoteza mvuto na wateja wengi wakakimbilia kaskazini na kusini kukwepa huduma mbovu za bandari ya Dar es Salaaam. Mawazo huru ya chuma yamesafisha kila uozo ndani ya bandari.

Kwa hakika tulitapeliwa kwa udanganyifu wa kiwango cha mwendo kasi kwamba akili zetu hazikuwa na uwezo wa kuendesha Shirika la Reli (TRC). Tulikuwa kama ‘mazuzu tunaopewa kioo kinachong’aa’ kwenye ile hadithi ya Mwalimu Nyerere, ‘na sisi tukawapatia dhahabu’. Baadhi yetu tukahujumu miundombinu ya reli ili malori ya mizigo yapate kutamalaki kwenye uharibifu wa barabara zetu. Hatimaye Shirika la Reli likaingia mikononi mwa wawekezaji wa kigeni. Uhuru wa fikra za Rais Daktari Magufuli umeirudisha TRC katika sekta ya usafirishaji kwa kishindo. Bado muda mfupi watanzania wataanza kupanda zile treni walizokuwa wakiziona kwenye sinema.

Chuma kimetufumbua macho na masikio, tumefuta mawazo ya umasikini vichwani mwetu ndani ya nchi tajiri. Hakika uhuru wa fikra za Rais Magufuli umebadilisha Taswira ya nchi ya Tanzania Kimataifa. Hatimae Julai mosi ya mwaka 2020, benki ya dunia inaitambua na kuitangaza Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za uchumi wa kati duniani. Hongereni watanzania kwa kuchapa kazi na kuifikisha nchi katika hatua hii muhimu, hongera Rais Magufuli kwa kuliongoza vema jahazi kuelekea Tanzania yenye asali na maziwa.
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom