Uhondo katika simulizi za kusisimua

Jumakidogo

R I P
Jul 16, 2009
1,851
0
Mzee wa shamba


Baada ya mduao huo Ben Roja akabaki akijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, maswali ambayo yalikuwa yakijiumba na kusambaa ubongoni mithili ya kiumbe chenye uhai.
Akaendelea kuvuta hatua kuelekea ofisini kwa inspekta Wabongo. Stella akiwa ofisini mwake alishangaa kuona Ben akiingia ofisini humo akiwa amebeba mkoba wa kike mkononi mwake, ikamchukua nukta tano tu kuutambua mkoba huo.
Ulikuwa ni mkoba wake yeye mwenyewe, mkoba wa mtumba ambao yeye mwenyewe kwa mikono yake aliununua maeneo ya sabasaba miezi minne iliyopita. Mkoba ambao Ben aliikuta bahasha yake ilyokuwa imeibiwa ikiwa imewekwa humo.
Macho ya mshangao yakamtoka huku akijiuliza kimya kimya mkoba ule ambao aliporwa na kibaka muda mfupi uliopita umefikaje mikononi mwa Ben Roja.
Lakini Ben baada ya salamu hakusema chochote akaingia ofisini kwa bosi wake huku akimwacha stella ndani ya wimbi kubwa la mshangao.
Kama kawaida mzee wabongo alikuwa amekaa nyuma ya meza yake ile ile ya siku zote, sura yake ilionyesha kuwa imechoka kupita kiasi.
Uso wake ulionyesha makunyanzi na mikunjo mingi iliyokuwa ni uthibitisho wa uzee aliokuwa nao.
Akamtizama Ben aliyekuwa akiingia taratibu ofisini mwake huku mkononi akiwa ameshika kitu, kitu ambacho inspekta Wabongo alikitambua mara moja, ulikuwa ni mkoba, mkoba ambao alikuwa akiufahamu sana, mara kwa mara alikuwa akimuona nao Stella ambaye ndiye katibu wake mukhutasi
Mambo yalikuwa yanamchanganya vibaya sana Ben Roja, matukio ya kimazingara pamoja na mauzauza yaliyokuwa yakiendelea kwa pamoja ni mambo ambayo yalikuwa yakimuweka katika wakati mgumu sana na kushindwa kuamua aanze kutatua tatizo lipi na kumalizia lipi.
Mtu aliyekuwa anajiita
‘’Mzee wa shamba’’
tayari alikuwa kesha mpiga bao na kumzidi alama nyingi sana.
Kama ni mtihani wa darasani basi mtu huyo anayejiita mzee wa shamba alikuwa akiongoza, kama ni ligi ya mpira wa miguu basi mzee wa shamba alikuwa na pointi nyingi zaidi kumzidi yeye.
Kwa ujumla Ben alikuwa kazidiwa maarifa na muuaji huyo, wakati yeye hapajui hata mahali ambapo muuaji huyo hunywa soda, lakini muuaji huyo tayari kesha fika mpaka mahali anapoishi na kumuibia makaratasi yake yote ya muhimu.
Wakati yeye Ben alikuwa anakula ugali wa matembele, mwenzake alikuwa anakula ugali kwa kuku wa kubanikwa.
Kwa ujumla walikuwa na tofauti kubwa sana kati yao, tofauti ambayo ingemlazimu Ben kutumia akili nyingi ya ziada kupata ulinganifu. Alijaribu kupanga mfululizo wa matukio tangu alipowasili kwa mara ya kwanza nchini akitokea huko Somalia bila ya kupata jawabu aanzie wapi.
Tukio lake la kwanza lenye utata mkubwa ni kutoweka kwa nyaraka muhimu alizokuwa amekabidhiwa na inspekta Wabongo kwa ajili ya kuanzia uchunguzi.
Hizi ziliibiwa nyumbani kwake katika mazingira yasiyo ya kawaida na yenye utata mkubwa.Ajabu lingine likafuatia, nyaraka hizohizo akazikuta kwenye mkoba wa Stella baada ya kuukamata mikononi mwa kibaka baada ya kumtilia mashaka.
Mkoba wa stella ambaye ni mfanyakazi wanayefanya nae kazi katika ofisi moja. Tukio hilo lilisababisha kuitishwa kwa kikao cha dharula ofisini mwa Inspekta Wabongo, kikao cha aina yake ambacho kilihudhuliwa na watu watatu tu, wajumbe hao walikuwa ni Inspekta Wabongo, Ben Roja na, Stella.
Kikao hicho kilikuwa na ajenda mbili tu. Ajenda ya kwanza ilikuwa ni kuhusu mtu aliyeokotwa akiwa ameuwawa asubuhi hiyo ambapo kwa taarifa za awali mtu huyo alitambuliwa kuwa alikuwa afisa mtendaji wa kijiji cha Matumbulu.
Ajenda ya pili ilikuwa ni kukutwa` nyaraka zilizomhusu Ben katika mkoba wa Stella. Maafisa hao wa usalama walikuwa wametulia kwa kipindi kirefu kila mmoja akiwa kimya kabisa huku akiwa amezama katika bahari ya fikra akijaribu kutafakari na kupambanua hiki na kile.
Kati ya wote hao Stella ndiye aliyekuwa na wakati mgumu zaidi kuliko wenzake akijaribu kukumbuka mazingira yaliyopelekea kuwepo kwa ile bahasha juu ya meza katika sebule yake.
Kila alipokuwa akijaribu kuvuta kumbukumbu kuwa aliichukua kutoka ofisini na kurudi nayo nyumbani. Ubongo wake ulikuwa ukifuta kumbukumbu zote za nyuma na kuanzia palepale mezani alipoikuta ile bahasha kwa mara ya mwisho kabla ya kuitumbukiza kwenye mkoba wake. Pamoja na bahasha hiyo pia suala la mauwaji ya afisa mtendaji ndilo lililokuwa likimpasua kichwa zaidi kuliko mengine.
Kwa mara ya mwisho kijana huyo alikuwa mgeni wake, mgeni ambaye alifika kwake jana jioni na kumweleza matatizo chungu nzima yaliyokuwa yakikiandama kijiji alichokuwa akikiongoza..
Tena alimkaribisha kulala katika chumba chake cha kufikia wageni, hata asubuhi kulipopambazuka alienda kumgongea ili kumjulia hali lakini kwa mshangao mgeni huyo hakuwepo.
Jambo hilo hakulitilia maanani sana kwani mgeni wake huyo alikuwa ni mtu mzima na akili zake, ni kipindi ambacho aliamua kufanya maandalizi yake ya kawaida kwa ajili ya kwenda kazini.
Lakini wakati akienda kazini alifika mahali na kukuta kundi la watu wakiwa wamekusanyika huku wakishangaa kuokotwa kwa mtu aliyeuawa. Kama maiti hiyo ingekuwa haijafunikwa kwa kanga basi kuanzia hapo ndipo ujumbe maalumu kuwa mtu aliyeuwawa ni mgeni wake ungekuwa umemfikia rasmi Stella kwa mara ya kwanza, lakini haikuwa hivyo.
Hapo hapo katika mkusanyiko huo ndipo lilipo tokea lile tukio la kuporwa mkoba wake na kibaka ambaye alijichanganya katika mkusanyiko wa watu na kutoweka nao. Mkoba ambao tena ukajikuta ukiangukia mikononi mwa Ben Roja.
Roho ilikuwa ikimuuma sana kwa kuuwawa kwa mgeni huyo akiwa mikononi mwake, hata hivyo ilibidi afiche hisia zote za kuonyesha kuwa alikuwa akimfahamu marehemu huyo.
Kwa upande wa Ben yeye hakuwa akihitaji kitu chochote zaidi ya maelezo ya kina kutoka kwa Stella. Alitaka kujua jinsi bahasha yake ilivyofika mikononi mwa dada huyo hali ya kuwa kwa mara ya mwisho ilikwa mikononi mwake.
Tena katika nyumba anayoishi, nyumba ambayo hakuna mtu yeyote aliyekuwa akiingia humo zaidi yake yeye Ben.
Kimya kiliendelea kutawala. Kiliendelea kutawala huku watu hao watatu wakiendelea kutizamana kama majogoo yaliyokosa mwamuzi katika pambano kali la kupigania temba, yaani kuku jike.


Aliyekuwa wa kwanza kuvunja ukimya huo alikuwa ni Insepkta Wabongo kwa kusema
‘’Nadhani umefikia wakati sasa wa kuamua nini cha kufanya kwa kutumia maamuzi mazito hata kama yatakuwa na athari kwa watu wachache, lakini yawe na faida kwa watu wengi. Mimi binafsi mambo haya yananichanganya sana, yananichanganya kwa sababu nimefanya kazi ya upolisi kwa miaka mingi sana iliyopita.
Nimekumbana na kesi nyingi sana, nimepambana na wezi pamoja na majambazi waliobobea katika fani hiyo. Nimepambana na wauwaji wa makusudi na wale wa bila kukusudia.
Pia nimevunja rekodi ya kuwatia ndani vibaka, wazurulaji na, wahuni wadogowadogo wanaosumbua raia kila siku bila ya sababu. Lakini katika umri wangu huu kazini sijawahi kupambana na kesi yenye utata na mauzauza kama hii.
Kesi ambayo haina pa kuanzia wala haijulikani pa kuishia, kesi ya kumsaka mchawi na mwanamazingaombwe stadi tena aliyebobea anayejiita ‘’mzee wa shamba’’ ni mzee wa shamba huyu huyu anayeendelea kutuchezesha kindumbwendumbwe kama mtoto kikojozi aliyejikojolea usiku wakati wa usingizi mnono.
Wewe Ben bado hujashuhudia mambo kwa sababu ni kama mgeni kwa sasa, usimlaumu sana huyu binti kuwa na bahasha iliyoibiwa nyumbani kwako, kumbuka kuwa hapa kuna miujiza mbele yetu.
Ikiwa mimi mwenyewe nimeibiwa nyaraka zangu katika mazingira tata, wewe pia umeibiwa kwa maajabu. Mwizi huyo hawezi kushindwa kuacha hii bahasha katika sebule ya huyu binti katika mazingira ya kimaajabu pia.
Jambo hilo si lakushangaa sana kwa sasa.’’
Maneno hayo ya Inspekta Wabongo yalionekana kumwingia vema Ben Roja na alikuwa amekaa kimya akisikiliza vipande hivyo vya maneno kwa umakini mkubwa na uangalifu wa hali ya juu. Wakati huohuo Inspekta akaendelea
‘’Inatubiti tulazimishe mambo haya ikibidi kwa kuyaunga unga vipande vipande ili kutengeneza kitu ambacho kinaweza kuleta maana na ufumbuzi wa mafumbo haya yaliyo mbele yetu.’’
Inspekta Wabongo akamaliza hotuba yake hiyo fupi na kuwatizama Ben na Stella katika nyuso zao kwa zamu. Ben akavuta pumzi ndefu na kuzishusha kwa mkupuo kisha kinywa chake kikawa tayari kuongea,
‘’maneno uliyoongea mzee nimeyasikia na kuyaelewa vizuri lakini na mimi pia ninayo machache ya kusema’’
Inspekta akatingisha kichwa kuonyesha kuwa anakubaliana naye na yupo tayari kumsikiliza, Ben akaendelea.
‘’Kwa upande wangu kuna kitu kimoja tu ambacho naweza kufanya kwa sasa ili upelelezi wetu uende kwa haraka. Baada ya kufanya utafiti na upelelezi wangu wa awali, mashaka yangu nayaelekeza kwa huyu mgeni wako anayekusumbua kila siku’’
aliposema maneno hayo Stella akamkazia macho na kuongeza umakini katika kumsikiliza.
Aliongeza umakini kwa sababu kipengele hicho kilikuwa kikimgusa kwa namna moja ama nyingine.
Kilimgusa kutokana na kuwa alikuwa amejiingiza katika penzi la mgeni huyo aliyekuwa ametajwa na Ben. Mgeni ambaye alikuwa akifahamika kwa jina la Bosco Majaliwa.
Ben akaendelea kuongea,
‘’Nasema hayo nikiwa na ushahidi wa baadhi ya mambo ambayo yananifanya nimtilie mashaka. Kwa mfano jana wakati nikiwa katika jitihada za kumtafuta afisa mtendaji ambaye kwa bahati mbaya sasa ni marehemu, katika hangaika yangu hiyo baada ya kupata maelekezo kutoka kwa raia wema.
Karibu kabisa na ofisi yake nilikutana naye akiwa katika mbio kali sana lakini kwa bahati mbaya sikumtambua mara moja kuwa ndiye mtu niliyekuwa nikihitaji kuonana naye.
Jambo hilo lilitokana na kuwa sikuwa nimewahi kukutana naye hapo kabla, japo nilishangazwa sana na ukali wa mbio zake, nilipuuza na kusonga mbele kuzielekea ofisi ambazo ndizo nilizoelekezwa kuwa zilikuwa za afisa huyo.
Nilipofika karibu na jengo hilo nikamuona mtu akitoka ndani ya ofisi hiyo. Mtu huyo alikuwa amebeba shoka kubwa mkononi, nilipomtizama kwa makini sana nikamtambua mara moja, alikuwa ni huyu huyu mgeni wako anayekutembelelea mara kwa mara.
Mgeni ambaye tayari tunao uhakika kuwa ndiye anayetuchezea kwa mambo yake ya kishirikina.
Kutokana na mbwembwe pamoja na matukio yake yalivyo ninao uhakika kuwa huyu ndiye anaweza kuwa ‘’mzee wa shamba’’ Ninao uhakika kuwa huyu Bosco Majaliwa diye mzee wa shamba muaji wetu anayetupeleka puta.
Kutokana na kuonekana kwake katika ofisi ya marehemu muda huohuo ambao nilikutana nae katika mbio kali ninayo mashaka kuwa huo ndio wakati ambao alikuwa amepanga kumuua kijana huyo lakini inaonyesha aliponyoka kutoka katika mikono ya muaji, muuaji ambaye nina uhakika ni Bosco Majaliwa.
Kwa vyovyote vile kijana huyo ilikuwa ni lazima auwawe kwani baada ya kumponyoka muuaji inamaanisha kuwa tayari alikuwa amebaini na kumtambua mtu anayesababisha matatizo katika kijiji chake.
Hapo ndipo muuwaji huyo akaanza kufuatilia nyayo zake na kumsaka kwa udi na uvumba kabla siri hiyo haijavuja kwa mtu yoyote. Nahisi mtendaji amekufa akiwa na siri yake moyoni ambayo hatukupaswa kuijua kwa kuhofia kutibuliwa kwa mipango ya muuaji.
Tangu sasa naanza kumsaka huyo mzee wa shamba, naapa kuwa mahali popote nitakapokutana naye itakuwa ni sawa na vita, yaani ama zake ama zangu’’
Maelezo hayo mafupi ya Ben yalimchanganya sana Stella, hasa ile sentesi ya mwisho aliposema ‘’nikimpata ama zake ama zangu’’ tamko hilo alilichukulia kama tangazo la shari lililokuwa limeashiria hatari kwa mpenzi wake mpya Bosco Majaliwa.
Mtu aliyetokea kumpenda sana kuliko kitu chochote. Baada ya kauli hiyo kutolewa Stella alibadirika ghafra na kuwa kama mtu aliyepooza na kuyatupa mawazo na fikra zake mbali sana nje ya ofisi hiyo.
Ulikuwa ni umbali hewa, umbali wa kufikirika ambao si rahisi kufikiwa na chombo chochote cha wanasayansi hata vile viendavyo kasi. Alikuwa akijaribu kuipima tabia na mwenendo wa mpenzi wake huyo mpya kama zipo alama zozote za kumfanya aonekane kuwa ni muaaji wa kutisha anayetingisha vyombo vya usalama nchini.
Hata hivyo hakupata alama zozote ambazo zilikuwa zikimuweka Bosco katika sifa ya uuaji. Bosco alikuwa na muonekano wa kipalokopaloko, tena alikuwa na muonekano wa wale mapadri wenye nyadhifa kubwa za kiroho katika parokia zao.
Upole na utulivu wake hakuna mtu yeyote ambaye angetokea kumshuku kuwa ndiye muuaji anayeisumbua jamii.
Stella aliendelea kuwaza na kuwazua akitafuta majibu, akapitisha uamuzi kuwa ikiwa itathibitika kuwa ni kweli Bosco ndiye muuaji, itambidi yeye binafsi ahame nchi kwa aibu ya moyo na nafsi yake.
Ahame aende akaishi huko ulaya, nasikia huko watu wanaishi maishi mazuri sana wakifurahia kila kitu. Chakula, starehe na, hata hali ya hewa, nasikia huko hata muwako wa jua ni tofauti na huku kwetu.
Kwa kufanya hivyo atakuwa amekimbia na kuepuka kashfa na lawama ambazo angepata. Pamoja na hayo pia kulikuwa na kitu kingine cha ziada ambacho kilikuwa kikigonga na kupasua kingo za ubongo wake wa kufikiri na kumuongezea ukubwa wa mzigo katika akili zake.
Kitu hicho ni mambo ya kichawi na miujiza iliyokuwa ikifanywa na huyohuyo Bosco Majaliwa. Ni kweli katika jamii mambo ya kichawi huwa hayakosekani na yalikuwepo tokea enzi za mababu.
Tangu enzi hizo walikuwepo mabingwa ambao ni mfano mzuri sana wa kuigwa katika sanaa hiyo. Alikuwepo Ngwanamalundi mchawi kutoka huko kanda ya magharibi, Kinjikitile Ngwale na, wengine wengi.
Mbali na hao walikuwepo pia wataalamu wa kuonyesha miujiza, hawa walikuwa ni manabii waliotokea kujizolea umaalufu na sifa kemkem, mfano Mussa na Yesu ambaye nasikia aliwahi kulisha kipande cha samaki kwa watu zaidi ya 2000 nao wakala mapaka wakasaza.
Hivyo kwa Stella mtu kufanya miujiza haikuwa jambo la ajabu sana kwake kiasi cha kufanya asiwe mpenzi wake.
Mbaya kwake iliyomuuma sana ni kuhusishwa mpenzi wake Bosco na muuaji mwenye kichaa. Hali hiyo hakuipenda na ilikuwa imekaa vibaya sana kwa upande wake.
Hadi kikao chao hicho kifupi kilipokuwa kinamalizika Stella alikuwa bado hajategua kitendawili cha nini afanye baada ya hapo.
Je aongee na Bosco kuhusu suala hilo? Au auchune huku akisubiri mwisho wake utakuwaje. Baada ya kuwaza sana yote hayo hatimaye akajilazimisha kuyasahau na kuendelea na kazi zake kama kawaida


*********************
Hutokea mara chache sana kwa mwanamke kushika tama. Hali hiyo ilimkuta mwanamke ambaye naweza kusema ki umri alikuwa jirani sana kuufikia utu uzima, lakini si uzee. Umri huo waswahili wameupa jina wanasema ‘’mtu wa makamo’’ aina hii ya umri ni ule ambao upo kati kati ya uzee na ujana.
Ni umri ambao ukimkuta mtu akiwa katika hali ngumu ya maisha unaweza kudhani kesha zeeka na, ukimkuta katika hali nzuri ya maisha unaweza kufikiri kuwa mtu huyo bado ni kijana mdogo sana.
Lakini pamoja na umri huo wa makamo muonekano wa mwanamke huyo kwa hali ya mawazo aliyokuwa nayo sasa alionekana kama mzee tayari. Uso wake ulikuwa umejikunja na kusinyaa ndani ya siku moja tu.
Moyo wake haukuwa na raha wala furaha na baadala yake ulikuwa umejenga udugu wa karibu na ujirani mwema na kitu kinachoitwa hofu.
Hofu inayoambatana na mashaka, mashaka ambayo yaliunda kero rasmi mwilini mwa mwanamke huyu. Mwanamke ambaye amejitafutia matatizo makubwa kutokana na penzi.
Penzi ambalo limemkolea na kumfanya achanganyikiwe mithili ya mtu mgeni katika tasnia hiyo. Mwanamke huyo alikuwa ni Stella, jioni hii baada ya kutoka kazini na kufanya shughuli ndogondogo za nyumbani anjikuta akiwa juu ya kochi lake dogo miongoni mwa yale mengine yaliyokuwepo pale sebuleni kwake, macho yake alikuwa ameyaelekeza kwenye runinga iliyokuwa pale sebuleni.
Yalikuwa yakitizama kwa makini sana lakini japo runinga hiyo ilikuwa imewashwa, macho hayo hayakuona chochote zaidi ya fikra hewa katika ulimwengu pweke wenye mauzauza kibao.
Yalikuwa hayaoni kwani yalikuwa yamepoteza dira na mwelekeo wake kwa ujumla na kujikuta akimfikiria sana Bosco Majaliwa.
Alikuwa anamkumbuka kwa mengi sana mtu huyo.
Japo uhusiano wao ulikuwa umedumu kwa muda mfupi sana, kubwa katika yote lililofanya amkumbuke sana ni uwezo wake wa kufanya mapenzi ambapo raha ya mwanaume huyo hajawahi kuipata popote tangu alipoanza kufaidi tendo hilio kwa mara ya kwanza.
Bosco Majaliwa alikuwa na ufundi wa aina yake, ufundi na utamu ambao kama mwanamke yeyote angeuonja abadani asingekubali kuachana na mwanaume hata kwa mtutu wa bunduki. Bosco alikuwa katia fora,yawezekana alikuwa amewazidi wanaume wote duniani.
Wakati Stella akiwaza na kufikiria hayo, mlango wake mkubwa wa kuingilia sebuleni ukaanza kugongwa taratibu na mtu ambaye alionyesha kuwa hakuwa na haraka. Mlango haukuwa wazi, kitu kilichofanya Stella anyanyuke mwenywe kwenda kuufungua. Mtu aliyemkuta pale mlangoni alikuwa akihitaji sana kumuona lakini si kwa muda huo, ni kama alikuwa amewahi sana kujileta mwenyewe kwake.
Bosco Majaliwa alikuwa amesimama mlangoni huku uso wake ukionekana kuachia tabasamu pana lenye mvuto.
Tabasamu ambalo pia lilipokewa kwa tabasamu kutoka kwa Stella, japo lilikuwa tabasamu la kivivuvivu lakini lilikuwa limebeba ujumbe mzito ulioonekana katika macho ya Stella yaliyolegea ghafra.
Macho hayo ni kama yalikuwa yakitamka ‘’nakupenda sana’’ Jioni hii Bosco alikuwa amevalia suruali matata sana aina ya kodrai ya rangi ya udongo, pamoja na suruali hiyo pia alivalia fulana mkato ambayo watoto wa mjini walipenda kuiita ‘’form six’’ Mavazi hayo yalifanya aonekane mtanashati, nadhifu na, maridadi sana. Alionekana kuwa ni miongoni mwa watu wenye pesa waishio mjini, tena waoshio bila ya kufikiria kuwa kuna kitu kinachoitwa njaa.
Kwa hakika alikuwa hafanani kabisa na sifa za ‘’ Mzee wa shamba’’ Mafanikio haya ya ghafla yalitokana na fedha nyingi alizokuwa amekwiba benki. Wizi ambao uliwaacha watu wote katika fadhaa na mshangao mkubwa.
Hiyo haikuwa jioni yenye giza la kutosha kwani miali ya jua yenye rangi ya dhahabu ilikuwa bado ikionekana kwa mbali katika hali ya kufifia ili kufanya maandalizi ya kila siku katika kuukaribisha usiku.
Majira kama haya Stella hakupenda kuonekana akiwa na mgeni wa aina ile nyumbani kwake kutokana na hali halisi ilivyokuwa, hivyo alimkaribisha mgeni wake moja kwa moja chumbani. Pamoja na sababu hiyo pia, Stella hakupenda mtu yeyote yule ajue kuwa anaye bwana, hiyo ilikuwa tabia yake ya kawaida.
Hivyo ndivyo alivyoumbwa. Stella hakuwa na furaha kama siku zote, jambo hilo Bosco alilitambua mapema sana.
Hakuwa mtu mwenye furaha na uchangamfu kama alivyozoea kumuona siku zote. Hilo likamfanya aulize, huku akimpapasa sehemu mbalimbali za mwili wake, kitendo hicho akakisindikiza na swali dogo kumuelekea Stella.
‘’Vipi mpenzi, leo naona haupo katika hali yako ya kawaida au kuna tatizo?’’
Swali hilo ni kama lilimzindua Stella na akajitahidi kurudi katika hali yake ya kawaida. Hali iliyozoeleka na Bosco majaliwa.
‘’Oop hapana mpenzi, kuanzia mchana najisikia kichwa kinagonga sana’’
Stella akajibu ili kumpteza maboya Bosco Majaliwa.
‘’ Eee hali hiyo inasababishwa na uzito wa majukumu yenu ya kila siku, unatakiwa kutumia dawa za kutuliza maumivu kila siku utokapo kazini na kupumzika katika mazingira yaliyotulia’’
Kimya cha nukta kadhaa kikapita kisha Bosco Majaliwa akaendelea kuongea baada ya kuvuta pumzi ndefu na kuzishusha kwa mkupuo.
‘’Kesho ni siku yako ya mapumziko, nimeamua nikupeleke kijijini ili ukayaone mashamba yangu. Mashamba ambayo mazao yake hunipatia kipato ambacho ndicho hufanya maishi yangu yaonekane bora siku zote. Ni mashamba yenye historia ndefu sana ambayo kisa chake nitakuhadithia siku moja’’
Stella alivutiwa sana na habari hiyo, alivutiwa kwa sababu aliona kuwa ni habari ambayo inaweza kumfumbua macho kutokana na yale yaliyokuwa yakihisiwa na Ben kuhusu mpenzi wake huyo.
Safari hiyo ingekuwa ni moja ya kipengele ambacho kingefanya aanze kuyajua maisha ya Bosco kwa undani zaidi. Mtu ambaye alikuwa akihisiwa kuwa yeye ndiye muuaji, mtu aliyekuwa akihisiwa kuwa yeye ndiye ‘’Mzee wa shamba’’ Safari hiyo aliisubiri kwa hamu sana.
Baada ya kupewa ujumbe huo akatamani masaa yaende mbio au yaruke kama ndege ili asubuhi ifike haraka aende akayashuhudie hayo mashamba kama alivyoahidiwa. Wakati Stella akifikiria hayo Bosco akaomba maji ya kuoga bafuni, kitendo ambacho Stella alikitekeleza bila kipingamizi kwani kwa wakati huo giza tayari lilikuwa limeshatanda angani.
Bosco alipoenda kuoga bafuni stella yeye akabaki pale sebuleni akiendelea kuangalia runinga, kama ilivyo kawaida kwa nyumba za kiswahili choo na bafu hujengwa kwa uani hivyo ilimbidi Bosco kutoka nje kabisa.
Dakika chache baada ya Bosco kutoka nje mlango mkubwa wa kuingilia sebuleni kwa Stella ukaanza kugongwa na mtu aliyekuwa kasimama kwa nje.
Stella hakuhitaji mgeni nyumbani kwake wakati Bosco Majaliwa akiwa maeneo hayo, hivyo japo mlango ulikuwa haujatiwa komeo akainuka ili kwenda kuangalia ni nani aliyekuwa akigonga mlango usiku huo.
Baada ya kufungua mlango Stella nusura azimie palepale kwa hofu na mashaka kwani mtu aliyekutana naye pale mlangoni hakumtegemea, alikuwa ni Ben Roja, kijana hatari anyeogopwa na kila mtu katika idara yao. Mtu aliyetoa tangazo la vita dhidi ya mpenzi wake Bosco Majaliwa.
Leo itakuwaje kama Bosco atatoka bafuni na kumkuta pale, Ben alikuwa ni kijana mwelevu na msomi mzuri wa saikolojia ya mwanadamu, ule ubabaikaji wa Stella alitumia nukta moja kuutambua na nukta iliyofuata akamuweka sawa kwa kusema,
‘’ vipi dada naona umeshituka sana ama hukutegemea kabisa ujio wangu huu wa ghafra’’ ‘’Aaa hapana usihofu kaka Ben karibu ndani’’
Stella akajibu huku mikono na mwili wake wote ukitetemeka mithili ya mtu aliyemwagiwa mapande ya barafu.
‘’Hapana dada usihofu ntakaribia siku nyingine na samahani sana kwa usumbufu, nimekuja ghafra kutokana na shida ya muhimu iliyonipata. Nimejaribu kupiga simu ya mzee lakini kwa bahati mbaya haipatikani, tafadhari naomba unipe namba za simu ya afande Gallusi nahitaji kuongea nae sasa hivi’’
Stella bila kusema chochote akarudi ndani haraka haraka na kutoka akiwa na simu mkononi, akabonyeza bonyeza baadhi ya vitufe katka simu hiyo kisha akaanza kutaja namba za simu kwa kituo wakati huo huo Ben naye alikuwa akizirekodi katika simu yake.
Baada ya kumaliza zoezi hilo Ben Roja akaaga na kwenda zake. Pamoja na kutokomea gizani kwa kijana huyo lakini Stella hakuamini mpaka alipohakikisha kuwa mtu huyo ametoweka kabisa katika upeo wa macho yake.
Stella jasho lilikuwa limelowesha mwili wake mzima, alilowa mpaka nguo zake za ndani zikawa chapachapa kama aliyezivaa bila ya kuzianika baada ya kuzifua.
Alirudi kochini asiamini kama ni kweli ujio wa kijana yule ulikuwa ni kwaajili ya namba za simu tu ama kulikuwa na kitu kingine alichokuwa akikitafuta, mawazo hayo yalimshinda nguvu na kujikuta akikimbilia kitandani kwenda kulala. Hata Bosco alipotoka bafuni kuoga alikuta mpenzi wake huyo keshajifunika shuka gubigubi.

*****************​
Siku kadhaa zilkuwa zimepita tangu walipotembelewa kwa mara ya mwisho na mtu aliyejiita kuwa yeye ni mzee wa shamba. Mtu ambaye alikuwa mgeni kwao na hata katika kijiji chao kwa ujumla.
Mtu huyo hakuwa mkazi wa maeneo hayo, alikuwa mgeni akitokea mahali kusikojulikana.
Tangu alipoanza kuonekana katika kijiji hicho kumekuwa na mikosi ya mara kwa mara pamoja na mauaji ya ajabuajabu yanayokiandama kijiji chao. Tangu mara ya mwisho kutembelewa na mgeni huyo hali ya hewa kwa upande wao ilikuwa imechafuka vibaya, tena aliyechafua alikuwa huyohuyo mgeni wao wa maajabu.
Amani yao pia ilitoweka kwa kiasi kikubwa sana, amani ambayo ilimfanya Mdoe awe na woga wa kutembelea hata mashamba yake kwa hofu ya kuuawa.
Hata mama yake mzazi alishindwa kurudi kijijini kwake mapema kutokana na muda mwingi kuutumia kwa kumfariji mwanawe. Mtihani walioachiwa na Bosco Majaliwa walikuwa bado hawajaupatia majibu.
Hilo ni jambo ambalo lilikwa likimuumiza sana Mdoe,mashariti waliyopewa yalikuwa magumu sana kuyatimiza.. Kukabidhi mali yote kwa mtu huyo na kuondoka zao au mama yake mzazi akubali kuolewa na mtu huyo ama vinginevyo wauwawe.
Ni sharti moja tu ambalo Mdoe aliona kuwa lina unafuu kwao, nalo ni kukubali mama yake arithiwe na mzee wa shamba. Shariti ambalo mama yake alilipinga kwa madai kuwa yeye umri wake tayari umekuwa mkubwa.
Sababu ambayo Mdoe aliona kuwa haina msingi, ni dhahili Mdoe na mama yake maji yalikuwa yamewafika shingoni na kuanza kuwazidi kimo polepole.
Hata mwili wa Mdoe ulipungua sana, hakuwa yule Mdoe mwenye miraba minne ambaye alikuwa ni miongini mwa wanaume wachache sana waliokuwa na mwili kama wa kwake yeye.
Matatizo yalikuwa yamemwandama kama kupe na mbwa, matatizo yalimfanya apoteze hata hamu ya kula.
Mwili wake ulipururuka kama puto lililotobolewa na msumali wenye ncha kali. Watu wenye ndimi na vinywa visivyokuwa na breki wakaanza kueneza ujumbe usiokuwa rasmi kuwa Mdoe kesha kanyaga mawaya.
Yaani kesha uvaa ukimwi na tayari umeshaanza kumtafuna, hawakujua ugonjwa rasmi uliokuwa ukimsumbua MdoeFUATILIA KATIKA kidogo2009
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom