Uhitaji wa Kizazi Kipya cha Uongozi wa Upinzani haukwepeki?

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Sep 20, 2021
3,214
3,587
Uhitaji wa kizazi kipya kabisa cha upinzani chenye agenda mpya, dira mpya na mwelekeo mpya wa kisiasa haukwepeki tena kutokana na kwamba CCM chini ya Mwenyekiti wake rais JPM kilichukuwa mwelekeo mpya kabisa wa kujihuisha kama chama kongwe duniani kilichobeba dhima ya uhuru wa nchi yetu na wa bara la Afrika ambapo baada ya uhuru huo wa Tanzania na Afrika sasa kinajikita kuulinda kwa gharama zote kupitia serikali inazoweka madarakani ambazo zimeshiriki pia kulinda amani na uhuru wa nchi za Afrika. Moto unaowaka kwa jirani yako usipokuwa makini nao basi unaweza kukuathiri pia, ni afadhali ushiriki kuuzima ungali huko huko kwa jirani yako kuliko kusubiri kuuzima ukiishaingia nyumbani kwako.

Upinzani wa mazoea na mapokeo (yaani usiotokana na mahitaji halisi ya mazingira ya nchi yetu na uliokosa ubunifu) toka kwa akina Raila Odinga, Kiiza Besigye, Agathon Rwasa, Etiene Tshishekedi, Malema nk hauwezi kamwe kuamua hatima ya nchi yetu kimaendeleo. Hii ni kwa sababu upinzani unarudiarudia nyimbo zilezile zilizokifu wapiga kura na zisizoleta tija. Wananchi hawawezi kula demokrasia ya kususa bunge la katiba na la JMT wala maandamano na mikutano ya hadhara. Wapinzani wanatakiwa wajuwe kuwa kazi pekee ndiyo inaweza kuwapa wapiga kura mkate wa kila siku. Harakati za upinzani zinagharimu mahusiano mazuri ya enzi na enzi yaliyokuwepo kati ya raia na Polisi. Wapinzani wa Tanzania wanafanya kazi kwenye mazingira salama ukilinganisha na wenzao wa Burundi, Sudan Kusini, Uganda, Rwanda, DR Congo nk wanaofanya kazi toka msituni/ughaibuni (mafichoni) na ambako huko mafichoni ughaibuni pia bado wanafuatwa kijasusi na ama kukamatwa au kuuawa.

Upinzani wa Tanzania unahitaji kuzaliwa upya na kuishi kwa kutambua ukweli kuwa demokrasia ya mabadiliko ya uongozi wa dola toka CCM haiwezi kuchagizwa na upinzani kwa ufanisi ilhali ndani yao demokrasia hiyo haikuwahi kuwepo hata pale ilipodaiwa na wafuasi wao basi ilibadilika na kuwa shubiri kwao na kuishia kuonyeshwa mlango wa kutokea. Upinzani unafukuza makada na makamisaa wenye tija na kukaribisha walioasi kwenye vyama vyao (yaani unatema karanga kwa Big G ya kuonja). Wapinzani wanauchukulia uchaguzi kama mchezo wa bahati nasibu, wanashiriki hata wakiwa hawana uhakika wa kushinda. Hata halmashauri walizowahi kuongoza hazina ubunifu mpya (ulioainishwa kwenye ilani zao) kwa ajili ya ufumbuzi wa matatizo ya wananchi wala hazijawa mfano wa kuigwa badala yake zimeendelea kupata vyeti vya ukaguzi vya mashaka tu. Wanaziongoza halmashauri hizo kwa mtindo uleule wa chama tawala na hivyo kukosekana utofauti na mantiki ya siasa za ushindani.

Chini ya awamu ya 5, upinzani ulitakiwa uiache nchi izaliwe upya na wao pia wajipange kuzaliwa upya, na siyo lazima nchi izaliwe upya katika mazingira na kwa vigezo na masharti watakayo wao wapinzani. Lakini pia vigezo na masharti siyo lazima vifanane kwa nchi zote, kuna nchi zimepata maendeleo baada ya kupigwa bomu hatari lililokuja kupigwa marufuku duniani la atomiki na nchi ikawa inazaa mapooza (Japan), zingine zimeendelea zikitumikia adhabu ya kulipa fidia kubwa ya kusababisha vita kuu ya pili ya dunia (Ujerumani), zingine zimeendelea baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda wa miaka mingi (Marekani). Wapinzani hawakutakiwa kufisha ndoto za wapiga kura kuiona paradiso kupitia awamu ya 5 ya uongozi wa nchi chini ya rais JPM. Nchi haiwezi kujengwa kwa maandamano na kususasusa bali kwa kufanya kazi tu kwa bidii. Imewapasa kujuwa kuwa Tanzania wanayowania kuiongoza haikuwahi kupata uhuru wala kubadili demokrasia toka chama kimoja kwenda vyama vingi kwa makabiliano ya kutumia mitulinga na kutoga damu za raia wake.

Aidha ieleweke kwamba Mwl JK Nyerere kama Mwanafalsafa yeyote aliyebobea kwa viwango vya juu, Watanzania wengi hata na walimwengu wengi hawakumuelewa vizuri pale aliposema kuwa mpinzani wa kweli atatoka CCM, wengi walipoona wale waliomeguka CCM mwaka 2015 kwenda upinzani na kwa kuangalia msisimko mkubwa walioleta kwenye medani za siasa za Tanzania; basi walidhani unabii wa Mwl JK Nyerere ulimaanisha upinzani kuchukuwa dola, hili limebaki likitesa wengi waliofasiri kinyume unabii huo wa Mwl JK Nyerere na unabii unapokosa kutimia wengi hukata tamaa na kusema huo ni unabii wa uongo. Kimsingi unabii wa Mwl JK Nyerere ni wa kweli na umetimia kwa asilimia 100.

Kwa vipi? Ukweli ni kwamba alichomaanisha Mwl JK Nyerere ni kuwa upinzani wa kweli utatukia pale ambapo mwana-ccm atameguka na kwenda upinzani kuleta msisimko (siyo kuleta ushindi) wa tofauti na ule uliozoeleka kwa miaka mingi, hiki ndicho alichomaanisha Mwl JK Nyerere, na kwamba hakutoa unabii kuwa mpinzani wa kweli atakayetoka CCM ndiye atakaye tamalaki uongozi wa nchi (alimaanisha siye atakayeshinda uchaguzi wa kiti cha urais bali atawapa Watanzania Upinzani wa msisimko tu), kwa mantiki hii ni kuwa hakuna wa kuweza kumfunga Mwl JK Nyerere kuwa alijichanganya katika unabii wake la hasha!

Alichokitabiri kimetimia, kama kawaida ya kanuni za unabii wa kweli, ni kuwa hakuna cha kuongeza wala cha kupunguza kwenye unabii huo wa Mwl JK Nyerere. Lakini Mwl JK Nyerere bado aliamini na Mungu wa Mbinguni alimpandisha cheo kwenda kwenye utukufu (kutwaliwa) akingali anaamini kuwa CCM kutoka madarakani kwa kipindi hicho alichotoa unabii huo na hata kwa kipindi ambacho kingefuata hicho ni ndoto ya alinacha kabisa. Huyu ndiye Mwl JK Nyerere ambaye kila mtu wakiwamo wapinzani na wana-ccm wameendelea kusisitiza kumuenzi na mara kwa mara wamemrejea kwa falsafa zake kila linapozuka jambo lenye taathira kwa jamii na lenye sura ya agenda ya kitaifa, sasa ile falsafa yake kuwa zidumu milele fikra sahihi za Mwenyekiti wa chama (Mwl JK Nyerere) imeendelea kuenziwa na kila mtu hata wale ambao hapo awali wakati siasa za upinzani zinaanza mwaka 1992 walieneza propaganda kuwa falsafa hiyo imepitwa na wakati huku wakiikana kwa kila dhihaka, sasa imedhihiri kuwa falsafa hiyo ya zidumu fikra sahihi za Mwenyekiti wa chama kweli inaishi milele.

Waliomeguka CCM kwenda upinzani na hatimaye kurudi CCM ni mashuhuda na mashahidi wa ukweli wa unabii huo wa Mwl JK Nyerere kwamba watapeleka msisimko tu lakini siyo ushindi, kwanza ieleweke kwamba siwalaumu kwa kitendo hicho cha kuhamahama maana kwa hakika wametimiza haki yao ya msingi sana ya kidemokrasia na kikatiba, ila ninachotaka kusema hapa ni kuwa wamekuta huko upinzani hali ya demokrasia labda ni tete kuliko CCM na kwamba suluhu ni kurudi CCM tu ambako bado kuna uafadhali kuliko upinzani, hii ndiyo sababu inayofanya niamini kuwa tunahitaji kizazi kipya cha upinzani kizaliwe na siyo hiki tulichonacho ambacho hakiwezi kuchagiza mabadiliko ya kweli hata kwenye halmashauri walizoshika uongozi. Ni bahati mbaya sana kuwa madai haya ya mabadiliko ya uongozi ndani ya upinzani kila yanapoibuliwa basi lazima ziwagharimu sana wanaoyaibua na kuleta hofu, sintojuwa na kila dalili za udikteta na hupelekea hata jamii ya Watanzania kuamini kuwa demokrasia ndani ya upinzani ni ndoto isiyoweza kutimia.

Sitegemei kuwa CCM kingeshindwa uchaguzi wa 1995 basi chaguzi za 2000, 2005, 2010 na 2015 wangemrudisha mgombea yuleyule ambaye angeendelea kushindwa alafu wategemee kushinda chaguzi hizo. KANU hawakufanya hivyo ingawaje wapinzani wake walirudisha wagombea walewale walioendelea kushindwa. Republican cha Marekani hakikuwahi kurudisha wagombea walioshindwa kwenye chaguzi na Marekani ndiyo demokrasia kongwe duniani. Zimbabwe upinzani uliokuwa na mazingira mazuri ya kushinda huku wakiungwa mkono na robotatu ya dunia wameendelea kushindwa kwa sababu wameendelea kuminya demokrasia ndani ya upinzani yenyewe kwa kuendelea kumsimamisha Morgan Tshangirai (sasa hayati) ambaye hatoi maziwa.

Ukomavu wa demokrasia ni kama wa Marekani ambapo chama kinamsimamisha mgombea kwa kura lakini hakioni haya kumpinga wakisema hafai kuongoza Marekani, hapa ndipo demokrasia imemfikisha Donald Trump. Kwanini Republican wanamsuta Trump ambaye wao ndiyo walimpa kura? Sababu ni kwamba kwa Wamarekani kinachoangaliwa ni maslahi ya Amerika na siyo uchu na hamu ya mtu kutawala Amerika. Sasa wapinzani hapa nyumbani wanapotuambia tuandamane hata pale ambapo vyombo vya dola vina taarifa za kijasusi kuwa maandamano hayo yana viashiria vya amani na usalama kutoweka, yatosha tujiulize hawa wapinzani wana maslahi ya Tanzania ndani yao au wana maslahi yao tu yanayotokana na uchu mkali wa kutawala? Hivi masikini wa Burundi, Somalia, Darfur, Syria, Mashariki ya DR Congo, Sudan Kusini, Afghanistan wakiambiwa wabadilishane uraia na masikini wa Tanzania watakataa? Mimi ninasema Tanzania kwanza vyama baadaye, Tanzania kwanza wanasiasa baadaye, Tanzania ni zaidi ya vyama na ni zaidi ya wanasiasa wasiotaka kutii mamlaka halali iliyowekwa kwa mujibu wa katiba. Wanapotaka kuifanya Tanzania kuwa Syria wanasahau kuwa wana mali zao ndani ya Tanzania? Usalama wake utahakikishwa na nani? Dola hiyo hiyo wanayoisuta au waasi watakaokuwa wanapora kila kitu pasina kujali ni cha nani? Ni cha chama gani?

Wenzetu Kenya wamekuwa kama Wazungu, wanapozua vurugu huwa wanakuwa waangalifu wasiharibu miradi ya maendeleo ya binafsi na umma, hata vita vya mwaka 2008 uchumi haukuyumba (labda kwa watalii tu) kwa sababu hawakuhujumu miradi ya maendeleo na ndiyo maana baada ya vita wakaendelea kupaa kiuchumi hadi kufikia uchumi wa pato la kati. Sisi Tanzania bado hata leo tunamenyana na taathira za vita vya Kagera vilivyoisha miaka 36 iliyopita.

majwalaoriko@yahoo.co.uk
 
Back
Top Bottom