Uhenga haambiwi mwana, dhoruba ilipo - shwari ipo!

Jul 18, 2020
14
12
Na: Norbert Mporoto.
Tanzania.
20180603

Wakati huu tulionao ni matokeo ya matukio ya kihistoria, ama kwa ubaya au uzuri. Na ukweli utakaosalia milele na kubaki kuwashangaza wengi ni kwamba historia ya mtu, jamii, kikundi cha watu au taifa ndiyo hutoa dira na mwelekeo wenye mwafaka salama utaoijenga kesho yao. Historia huweka alama isiyofutika na inayoeleza mahali ambapo kitu au jambo fulani lilianzia ili kuwasaidia wataokuja baadaye kurejea mwanzo wa safari yao na kuwawezesha kufanya tathimini kuona kipi kinapaswa kifanyike ili kuijenga kesho yao kwa ufanisi mkubwa na kwa manufaa ya wote.

Historia huenda sambamba na kutunza thamani ya mtu, ikiwemo utamaduni, desturi, mila na matendo yote ambayo hubeba mwenendo wa jamii husika. Lakini historia pia hubeba kumbukumbu ya mambo mabaya kwa lengo la kutoa funzo, kwani dhamiri yake huwa si kupotosha kwa kutaka watu wajifunze mambo mabaya.

Maisha yetu mpaka kufikia hapa na kuendelea ni mfano wa mbio za vijiti. Tulipokea kijiti toka kwa watangulizi wetu ambao kwa nafasi yao walijitoa kutengeneza kesho yetu ambayo ndiyo hii tunayojivunia huku tukisahau wajibu wetu kwa manufaa ya vizazi vijavyo. Nachelea kusema ujanja au werevu wetu umevuka mipaka kiasi cha kuikumbatia mifumo mipya ya maisha ambao ni kinyume na historia yetu.

Mapokezi au ubunifu wa mfumo mpya wa maisha haya yana asili mbili, moja ikiwa ni janga la kutengenezwa. Hii inaturejesha karne kadhaa nyuma na kuakisi dhamiri ya ukoloni katika mataifa yetu ya kiafrika. Ni wazi kwamba wakoloni hawakutaka kabisa tuitunze na kuifahamu historia yetu bali yale mageni waliyotaka tuyafahamu, lakini kubwa ikiwa kuletewa utamaduni mpya kwa kila jambo ili tuisahau historia adhimu iliyobeba thamani yetu. Hivyo walifanikiwa kutufanya wageni katika uafrika wetu.

Asili ya pili ya mfumo huu dhalimu wa maisha yetu ni matokeo ya uzembe, upuuzi na ujinga tulio au tunaokazana kujivika mara tu baada ya kupokea kijiti toka kwa watangulizi wetu. Na hili ndilo tatizo kubwa kwani tunaonekana watu wa ajabu kuendelea kulia vilio visivyokwisha huku tukinyoshea watu vidole wakati ndani yetu tunafurahishwa na namna machozi yanavyotububujika. Ukweli ni kwamba weledi na ufahamu wa kung’amua ni kipi tunapaswa kufanya toka kwenye historia hiyo ya kututaka tuishi usingizini milele tunao. Ila tu imefikia mahali tumeridhika na mfumo huu mpya. Niwakumbushe kwamba, ni vigumu kupata tiba ya wazimu ambao asili yake imeanzia ndani ya familia. Huu ni uzembe usiofaa kukumbatiwa na ni msiba wa kujitakia.

Kwa wachache wanaoweza kurejea historia yetu wana wa Afrika ni wazi wataafikiana nami kwamba historia yetu haikutuandaa kuwa kizazi cha watu waoga kiasi hiki. Mapambano ya kulikomboa bara hili yametokana na ujasiri na uthubutu wa watu wachache waliokubali kupoteza muda, nguvu, na maisha yao tena katika umri mdogo wakiamini kwamba hatma ya bara hili itakuwa ni nzuri kuendana na uzalendo waliouwekeza. Nani hivi sasa anatathimini maisha na jitihada za watu kama Xola Tyamzashe, Ahmed Kathrada, Peter Abrahams, Mathew Goniwe, Ndeh Ntumuzah ama Victoria Mxenge?

Aina ya woga huu ni tamaa tu ya kuishi huku tukifanywa watumwa chini ya mwamvuli wa wale wale ambao tumewabadilisha jina. Watangulizi wetu katika historia yao hawakutaka kabisa kufungamana na ukoloni kwa namna yoyote ile. Ajabu miaka michache tu tangu watukabidhi silaha za mapambano tumejisahaulisha mwelekeo tunaopaswa kwenda hata kuwakaribisha maadui zetu ndani bila hofu. Historia vichwani mwetu imekataa kumjua mkoloni kwa jina lake halisi, ila imeweza kumbatiza jina jipya la mfadhili na mwekezaji. Na historia hii mpya imefurahishwa na utandawazi na kuchukizwa na ubeberu. Labda! Sababu wazimu huu tumeukaribisha kuanzia ndani ya familia zetu.

Chembechembe za uadui na chuki zinazotugawa leo hii sio chimbuko wala mfumo wa maisha wetu wa awali. Historia ya bara la Afrika imetokana na misingi ya umoja, udugu na mshikamano. Waliotangulia waliishi kama ndugu, mipaka ya taifa moja na jingine haikuwa kikwazo kwao, imani yao ilidumu kwa kuamini wao ni wamoja. Leo hii uko wapi umoja walioturithisha? Tumetoa wapi uadui na chuki? Kwanini tunagawika kwa sababu za kisiasa, kabila au utaifa wetu? Je tumeridhika kuwafaidia wale wanaoazimia kunufaika na utengano wetu? Akili yangu hainiaminishi kwamba kuna jitihada za kutaka kujibu maswali hayo kati yetu.

Ila kila mmoja anaamini katika kuurithi uadui, chuki na mgawanyiko uliopo akiamini na kusimamia kujipambanua na kukita mizizi ya mabavu ili kuwa bora zaidi ya nduguye. Inaumiza sana kuona miaka hamsini au sitini baada ya wachache wetu kumwaga damu yao ili kutuletea umoja, mafanikio yale yamegeuka na kurudi hatua nyingi nyuma zaidi. Afrika inagawika kisa tofauti za ukabila na udini, siasa na tamaa za madaraka. Ukweli ni kwamba Afrika haipikiki katika chungu kimoja, waafrika tunazikana kila kukicha kinyume na matarajio ya wazee wetu.

Tutakubaliana ya kuwa kumchokoa Mamba katika pango lake kunataka utaratibu! Mfumo wa maisha tulionao unawafurahisha watu wengi ndani na nje ya nchi. Wapo wanaofurahishwa na ujinga tuliojibebea na kubebeshwa, kwani wana uhakika wataendelea kunufaika juu yetu. Wapo wanaopendezwa na namna tunavyojitenga na maarifa ya kukuza ufahamu wetu, na kushadadia upuuzi usio na mbele wala nyuma katika kulijenga bara letu. Hivyo, zoezi la kuwasitisha watu hawa ni lazima litugharimu sawasawa na gharama tulizotumia kuwaruhusu watuchezee akili.

Vita pekee tunayopaswa kupigana ni kuyatafuta maarifa kadri ya uwezo wetu. Tunahitaji vizazi vitavyojitambua ili kuepusha kupumbazwa na kufanyika kuwa kizazi cha kuridhia kila jambo. Thamani yetu haiwezi kupatikana ndani ya vazi la unyonge tulilojivika, ujinga tuliojibebesha au usasa wa kipuuzi tunaoukumbatia kwa kuamini kuwa ndiyo maisha tunayopaswa kuishi. Lazima tujiulize tutawakabidhi nini watoto wetu na vijukuu vyetu mara baada ya kufika ukomo wa pumzi zetu? Ni lazima panapobidi tuifundishe historia yetu ili tuiweke bayana heshima tuliyonayo katika ulimwengu huu, hiyo itawezesha kuangaza nuru njema kwa walio gizani.

Katika vitu adhimu ambavyo historia yetu itabaki kufundisha ni pamoja na kuwa kasuku hazai utumwani. Ila cha kustaajabu ni kwamba hapa nyumbani tumeshindwa kufugika hata kuona ugeni ni jambo jema kiasi cha kupotelea katika lindi la ugeni huo. Nadhani ni mwendelezo uleule wa kukosa maarifa unaofanya tushindwe kutathimini uzuri tulionao hapa kwetu. Afrika inajitosheleza kushinda hao wanaotufanya watumwa wao, historia yetu imebeba kila neno zuri kulielezea bara hili, ni wakati sasa wa kurejea na kuirejesha heshima ya mataifa yetu. Ikiwa uchi utajitokeza kutupatia mavazi ni lazima tuwe na tahadhari ya kutathimini jina la mtoa zawadi kabla ya kuipokea kwani kuchutama jangwani hakunayo ahueni!

#UhuruniFkra #Uhengahaambiwimwana #Dhorubailiposhwariipo #Mporotowrites #Tanzania #afrikanyumbani
IMG_20161026_184249.jpg
 
Back
Top Bottom