Ugiriki: Maelfu ya wakimbizi wameachwa bila makazi baada ya moto mkubwa kuunguza mahema

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
24173cf7b4074c8b82bbc2156564549e_18.jpg
Maelfu ya wakimbizi wameachwa bila makazi baada ya moto mkubwa kuunguza mahema katika kambi kubwa zaidi ya wakimbizi barani Ulaya ya Moria iliyopo katika kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki, kisiwa chenye uwezo wa kuhifadhi wakimbizi 3,000 lakini chenye idadi ya wakimbizi 13,000.​
Chanzo cha moto huo ulioanza usiku wa siku ya Jumanne bado hakijafahamika, huku maafisa wakiripoti kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mahema na makontena yakiwa yameharibiwa kabisa.​
"Kambi ya Moria imeteketea kabisa, nguo zetu na kila tulichokuwa nacho kimeungua moto, kwa sasa nipo barabarani na mke wangu na watoto, hatuna chakula wala maji," anasema Mohammad Hanif Joya, mkimbizi kutoka nchini Afghanistan anayeishi katika kisiwa hicho.​
Maelfu ya waandamanaji wamepanga kufanya maandamano ya amani licha ya polisi kuweka vizuizi barabarani kuwazuia waandamanaji hao kuufikia mji wa karibu wa Mytilene.​
Moto huo umetia chumvi katika tatizo la hali mbaya ya kibinadamu katika kambi hiyo kubwa zaidi nchini Ugiriki ambayo ilikuwa imewekwa karantini kuepusha kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona ambayo yalikuwa yameanza kuongezeka katika kambi hiyo ambapo visa vipya 35 viliripotiwa wiki iliyopita.​
Shirika la Madaktari wasio na mipaka limesema kuwa hawana taarifa za vifo wala majeruhi. Msemaji wa shirika hilo, Faris al-Jawad amesema ipo haja ya kuwahamisha wakimbizi hao kutoka katika kisiwa hicho na kuwapeleka katika nchi zingine za Umoja wa Ulaya.​
"Hali hii ilitarajiwa kutokea kutokana na kuwakusanya wakimbizi wengi kiasi hicho katika sehemu ndogo," alisema al-Jawad.​
Kambi ya Moria katika kisiwa cha Lesbos ilianza mwaka 2011 kama kituo cha dharura cha kupokea wakimbizi waliokuwa wakikimbia hali ngumu ya maisha nchini Afghanistan, kisha kituo hicho kikageuzwa kambi rasmi ya wakimbizi lakini yenye uwezo wa kupokea wakimbizi 3,000 tu. Kambi hiyo kwa sasa ina zaidi ya wakimbizi 13,000, huku ikikosa huduma muhimu za kibinadamu kama vile umeme na maji ya kutosha.​
Chanzo: AlJazeera
 
Back
Top Bottom