Ufisadi wa kutisha TANESCO, Mbunge aliuzia matairi mabovu

mpigauzi

JF-Expert Member
Jul 17, 2012
275
71
Madudu ya TANESCO haya
• Mbunge aiuzia matairi mabovu

na Mwandishi wetu, Dodoma

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, jana aliibua madudu mengine ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambapo ilinunua misumari kwa pauni 50,000 badala ya spea.

Muhongo aliongeza kuwa baadhi ya wabunge wakiwamo wale wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wanafanya biashara na TANESCO, ambapo kampuni ya mbunge mmoja ililiuzia shirika hilo mataili mabovu.

Waziri huyo aliibua madudu hayo alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliochangia hotuba ya bajeti yake kwa mwaka 2012/2013 ambapo alisema serikali haitasita kuiingilia TANESCO pindi inapobaini mambo hayaendi sawa.

Alisema kuna taarifa za siri kutoka kwa wabunge watatu kuwa biashara ya nguzo imekuwa ikifanyiwa mchezo mchafu kwa kuchukuliwa mkoani Iringa na kupelekwa Afrika Kusini na kisha kurejeshwa hapa nchini na kuuzwa bei kubwa.

Aliongeza kuwa TANESCO ina madudu mengi na wamemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi ndani ya shirika hilo.

"Waheshimiwa wabunge naomba tumwachie CAG afanye uchunguzi kama tulivyomuagiza na habari za kamati teule tuachane nazo na kufunga mjadala huu hata kwenye vyombo vya habari tuchape kazi," alisema.

Waziri Muhongo alianza kujenga hoja zake akinukuu kauli mbili za mwanafalsafa na mwandishi wa habari mkongwe kuwa; "Ukweli ni tochi au kurunzi ndani, hivyo kadiri unavyoitingisha ndivyo inavyowaka" na "Ukitaka kujua mafanikio ya kiongozi yeyote aliyefanikiwa ni kutazama yale ya wenzake waliyoyaacha."

Katika hilo aliweka bayana kuwa mtu yeyote anayeitetea TANESCO au wale wote wanaowaumiza wananchi ni mpuuzi, kwa vile shirika hilo limekuwa likifanya kazi tangu mwaka 1930 lakini kwa miaka yote hiyo wameshindwa kusambaza umeme kwa asilimia 20.

"Anayedhani TANESCO haitaingiliwa anajidanganya tu. Hii ni ajabu, maana hatuwezi kuchukua vyanzo vya mapato ya serikali kwenye bia kila mwaka badala ya TANESCO," alisema.

Kuhusu kuunda tume kwa mambo ambayo yanakuwa yametokea ndani ya wizara yake, Waziri Muhongo alisema utaratibu mpya anaoupendekeza sasa ni ule wa watendaji pamoja na yeye kwenda eneo husika na kukutana na wananchi kusikiliza (public hearing.

Tuhuma za Mhando
Kuhusu tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, William Mhando, alisema kuwa amesimamishwa kupisha uchunguzi wa matumizi mabaya ya fedha na madaraka.

Alizitaja tuhuma zinazomkabili Mhando kuwa ni pamoja na kukiuka sheria ya maadili ya umma kwa kuingia mkataba wa kutoa mkopo wa sh milioni 884.5 kwa kampuni ambayo ana masilahi nayo, kwani mkewe Eva ndiye mkurugenzi, na watoto wao wawili (Veronica na Fredy.

Kuhusu hofu ya kuwapo kwa mgawo wa umeme, Waziri Muhongo alisema kuwa ilikuzwa tu na mafaisadi kwa kupitia mawakala wao lakini akabainisha kuwa shirika linao uwezo wa kutosha kuzalisha umeme.

Ni katika mlolongo wa hujuma hizo, waziri alibainisha kuwa madai ya kwamba wizara ilikiuka kanuni ya manunuzi ya umma kwa kuipa mkataba Kampuni ya PUMA Energy wa kusambaza mafuta kwa Kampuni ya IPTL kwamba si za kweli.

"TANESCO haikuwa na fedha, vile vile mafuta, lakini ilitaka iweke masharti kwa kampuni ya kuisambazia mafuta. Siku wanapoweka mgawo hawakunipa taaarifa wala wasaidizi wangu. Watu hao hao waliokata umeme kwa kusingizia kukosa mafuta nilikwenda ofisini kwao kesho yake nikitokea Dodoma, lakini nikakuta bado hawajanunua mafuta," alisema.

Prof. Muhongo alifafanua kuwa fedha walizowapatia TANESCO hazijaingilia utaratibu kwani hawakuingia huko kuwashawishi waipe zabuni PUMA Energy.

Alisema kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na serikali kwa asilimia 50, hivyo kununua mafuta kwake wanapata unafuu na gawiwo la hisa, lakini pia walibaini ujanja kwamba hata kampuni iliyokuwa ipewe zabuni ya kuuzia mafuta TANESCO kwa sh 1,800 kwa lita, nayo inayanunua kwa PUMA Energy kwa bei ndogo ya sh 1,460.

"Tumepata barua ambayo tungeitumia kama nondo ya kutuokoa humu ndani kama wabunge msingeshutukia mchezo uliokuwa ukifanyika dhidi yetu. Hii ndiyo ingetuokoa maana inaonesha kuwa kwa vile IPTL ipo chini ya mufilisi, mkataba unabainisha wazi kuwa Wizara ya Nishati na Madini ndiyo yenye mamlaka ya kuinunulia TANESCO mafuta," alisema.

Kuhusu Bodi ya TANESCO nayo kuvunjwa kutokana na kukosa uhalali wa kimaadili, waziri alisema wanaelekea huko na hivyo kubainisha kuwa hata wajumbe wake kuanzia sasa watapaswa kuomba kazi na kusailiwa kwa kulingana na sifa zao.

Katika hatua nyingine, Waziri Muhongo amaeanza kutekeleza maagizo ya kupunguza matumizi ya serikali kwa vitendo ambapo amepiga marufuku watendaji wake kutumia magari ya anasa, maarufu kama mashangingi na kwamba viongozi wakuu watatumia magari yasiyozidi CC 3000, ambayo watakopeshwa.

Alisema kwa kufanya hivyo, wizara yake itaokoa kiasa cha sh bilioni 1.4 kila mwaka, fedha ambazo zitaelekezwa kwenye matumizi mengine ya maendeleo.

Pia alikubaliana na hoja ya msemaji wa kambi ya upinzani, John Mnyika, ya kuitaka serikali kuweka akiba ya dhahabu, akisema jambo hilo ni la msingi na kama kuna mchumi atalikataa itabidi wamtilie shaka.

"Kwa mfano, unaweza kuona wenzetu wa mataifa makubwa walivyojizatiti katika hilo, mathalani Marekani inaongoza kwa kuweka akiba ya tani 8,133.5, ikifuatiwa na Ujerumani 3,396.3, IMF tani 2,811.1, Italia 2,451.8, Ufaransa 2,435.1, China 1,054 wakati Afrika Kusini inashika nafasi ya 29 ikiwa na tani 125," alisema.

Wezi wa umeme waanikwa
Waziri Muhongo pia aliwataja wezi sugu wa umeme ambao wamekuwa wakitumia nishati hiyo kwa kutumia luku za wizi ambazo hazijasajiliwa na TANESCO ambapo katika orodha hiyo imo shule maarufu ya kimataifa ya St. Mary's inayomilikiwa na mmoja wa wabunge wa Viti Maalumu, Mchungaji Gertrude Rwakatare.

Alisema kuwa shule hiyo imetumia umeme wa sh milioni 10.5 huku wezi wengine wa Dar es Salaam wakitajwa kuwa ni Access Benki ya Tabata sh milioni 13.8, Shree Shalim sh milioni 8.1 na Hoteli ya Akubu Paradise mali ya Philip Ngunda iliyoko eneo la Kariakoo.


Source: Tanzania daima
 
Du safi sana muhongo,nimekukubali hasa hapo kwa kupunguza matumizi ya serikali,pia yale mashangingi V8 za kijani zile waziuze kabisa,pia hii ifanyike kwenye wizara nyingine hizo fedha zinunue hyo mashine ya uchunguzi wa magonjwa mwilini na ujenzi wa mabweni,wapunguze na paye coz fedha nyingi watakua wanaokoa wasitegemee walevi tu na wavuta tumbaku ndio waendeshe nchi,je watu wakiokoka je?(By Kafulila)
 
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, jana aliibua madudu mengine ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambapo ilinunua misumari kwa pauni 50,000 badala ya spea.
Muhongo aliongeza kuwa baadhi ya wabunge wakiwamo wale wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wanafanya biashara na TANESCO, ambapo kampuni ya mbunge mmoja ililiuzia shirika hilo mataili mabovu.........

Mzee EL (Mamvi) ni mkali kweli (Strategist). Mwizi akikimbizwa kwenye umati wa watu naye huweza "kupotezea" kwa kuita "mwizi, mwiziii". Je yale maazimio 26 ya kamati ya Mwakyembe kuhusu Richmond ndo "yamepotezewa hivyo" na hii kashfa mpya? TAFAKARI
 
"Pia alikubaliana na hoja ya msemaji wa kambi ya upinzani, John Mnyika, ya kuitaka serikali kuweka akiba ya dhahabu, akisema jambo hilo ni la msingi na kama kuna mchumi atalikataa itabidi wamtilie shaka.
“Kwa mfano, unaweza kuona wenzetu wa mataifa makubwa walivyojizatiti katika hilo, mathalani Marekani inaongoza kwa kuweka akiba ya tani 8,133.5, ikifuatiwa na Ujerumani 3,396.3, IMF tani 2,811.1, Italia 2,451.8, Ufaransa 2,435.1, China 1,054 wakati Afrika Kusini inashika nafasi ya 29 ikiwa na tani 125,” alisema."

jamani nisaidiea hapo kwenye red: kama hivi haya madhahabu ya buzwagi, geita, nyamongo, geita,nk. ni sawa na Tani ngapi? je na hawa jamaa wenye hizo tani za akiba wanazitoa wapi?wanachimba wenyewe au wananunua?
 
Halafu madakitari wakigoma kuhusu mazingira na vifaa duni,pia hata boresho la mishahara mnawapeleka mahakamani....wakati kumbe akina ulimboka wanajua kua nchi hii inafedha na inaweza kulipa hata hizo milioni 3.

Kama mtu mmoja na familia yake wanajikusanyia limbikizo la milioni 800,kwanini madakitari wasigome.

JK jitahidi kuwa mwenye hekima kama ulivyo fanya sasa kwa kuwapa support Filed Marshal Muhongo na strategist wake Maswi,Ninaimani kwenye hii battlefield watashinda tu.

AMANI IWE JUU YENU
 
Hongera sana Prof . Muhongo na Maswi kwa utendaji uliotukuka . Safisha uozo ndani ya Tanesco...Sasa nimeamini kwamba kumbe Waziri bora asiwe Mbunge , ila atokane na uweze wake wa kuchapa kazi na kupambana na maamuzi magumu kwa usahihi zaidi wenye kuleta tija kwa maslahi ya Taifa .
 
Ila kuhusu bodi nadhani nayo washitakiwe kwa matumizi mabaya ya madaraka kwani siyo kweli kwamba hawakujua kuhusu kampuni ya mkewe Mhando au kuhusu nguzo za umeme na pia mkataba wa kununua mafuta.

Moja ya kazi ya bodi ni kusimamia utendaji wa MD na uendeshwaji wa shirika, na pia kupitia na kujiridhisha na maamizi au mapendekezo yaliyofanywa na MD.

Sasa ili la kumpa mkewe tenda walitakiwa walione toka mwanzo ila kwa sababu wakurugenzi wetu wanafuata posho na maslahi binafsi tu hawawezi kuona penye tatizo.
 
"Pia alikubaliana na hoja ya msemaji wa kambi ya upinzani, John Mnyika, ya kuitaka serikali kuweka akiba ya dhahabu, akisema jambo hilo ni la msingi na kama kuna mchumi atalikataa itabidi wamtilie shaka.
"Kwa mfano, unaweza kuona wenzetu wa mataifa makubwa walivyojizatiti katika hilo, mathalani Marekani inaongoza kwa kuweka akiba ya tani 8,133.5, ikifuatiwa na Ujerumani 3,396.3, IMF tani 2,811.1, Italia 2,451.8, Ufaransa 2,435.1, China 1,054 wakati Afrika Kusini inashika nafasi ya 29 ikiwa na tani 125," alisema."

jamani nisaidiea hapo kwenye red: kama hivi haya madhahabu ya buzwagi, geita, nyamongo, geita,nk. ni sawa na Tani ngapi? je na hawa jamaa wenye hizo tani za akiba wanazitoa wapi?wanachimba wenyewe au wananunua?
Wanachimba kutoka wapi kama sio kwenye makoloni yao Tanzania ikiwa the leading colonized producer. SHTUKA.
 
Wanachimba kutoka wapi kama sio kwenye makoloni yao Tanzania ikiwa the leading colonized producer. SHTUKA.

kwa hio sie kuzipata na kuweka akiba hiyo (kama walivyoshauri) inatakiwa kununua au kuzipata wapi? wakati zipo tayari huko Buzwagi, n.k? au deposits zetu zote hazifikii hizo tani walizonazo wenzetu
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom