UFISADI: Viongozi wameiweka CCM kwenye Auto-Pilot?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
UFISADI: Viongozi wameiweka CCM kwenye Auto-Pilot?

Johnson Mbwambo Mei 7, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

WENGI wetu tunafahamu kwamba ndege kubwa ya abiria inayosafiri masafa marefu, mathalan London hadi New York, kuna wakati rubani hutegesha mitambo ili ijiendeshe yenyewe (Automatic Pilot).

Kwa kawaida rubani na msaidizi wake hufanya hivyo ili nao wapate nafasi ya kunyoosha miguu, kunywa kahawa au hata kwenda maliwatoni.

Lakini si kila safari unaweza kuiweka ndege katika Auto-Pilot. Ni shurti safari iwe ya masafa marefu. Aidha, ndege haiwezi kuwekwa Auto-Pilot kabla rubani hajaielekeza mambo fulani fulani; kama vile kule anakotaka ielekee, iende kasi gani na iruke umbali gani kutoka usawa wa bahari.

Kwamba safari ya chama tawala cha CCM ya kuwaondoa Watanzania katika umasikini ni ya masafa marefu, si jambo la kujadili. Kwamba katika safari hiyo ya masafa marefu viongozi wameamua kuiweka katika Auto-Pilot (kwa sababu ya kuchoka?) pia si jambo la kujadili.

Pengine jambo la kujadili ni iwapo marubani wetu hao waliielekeza ndege ielekee wapi na kwa mwendo-kasi upi, kabla ya kuiweka katika Auto-Pilot. Najua wapo watakaosema kwamba walifanya hivyo, lakini najua pia kwamba wapo watakaosema kuwa hawakufanya hivyo.

Lakini kwa mtazamo wangu, viongozi wa juu wa CCM wameiweka ndege katika Auto-Pilot bila kwanza kuipa mwelekeo, na sasa ndege inajiendea hovyo kwa mwelekeo iliyojichagulia yenyewe!

Yapo matukio mengi yanayonifanya niamini hivyo; lakini la hivi karibuni ambapo Andrew Chenge, Waziri wa Miundombinu aliyejiuzulu kwa sababu ya kuhusishwa na ufisadi, alipokelewa kwa mbwembwe na vifijo wakati akirejea katika jimbo lake la Bariadi Magharibi, limeifanya imani yangu hiyo iongezeke.

Taarifa za vyombo vya habari zinasema kwamba safari hiyo ya Chenge ya kurejea jimboni ilikuwa kama kufuru; kwani katika kila kijiji alichosimama kuhutubia, alichinjwa ng’ombe kwa ajili ya kuwalisha wananchi waliofika kumpokea.

Jambo la kusikitisha na kukatisha tamaa ni kwamba mbwembwe na kufuru yote hiyo ilipata baraka za CCM mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Ripoti zinasema kwamba miongoni mwa magari 70 yaliyoshiriki katika mapokezi hayo, yalikuwemo ya chama tawala na pia ya serikali, na kwamba kinara wa mapokezi hayo jimboni alikuwa ni Katibu wa CCM wilayani Bariadi, Masunga Lyabuyenze.

Ukitafakari tukio hilo la aina yake, hakika, unapata hitimisho moja tu kubwa; nalo ni kwamba mapokezi hayo yalilenga kuwakejeli wale wote wanaomtuhumu Chenge kwa ufisadi na pia wale wote waliomwekea shinikizo la kujiuzulu uwaziri. Na hapa ndipo hatari yenyewe ilipo.

Kumwandalia mapokezi kamambe kama hayo kiongozi anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi na ambaye baada ya yeye mwenyewe kuzipima ameamua kujiuzulu, na Rais Jakaya Kikwete naye baada ya kuzipima akamkubalia kujiuzulu, ni kuwakejeli wale wote ambao, kwa njia moja au nyingine, walihusika na kujiuzulu kwake uwaziri.

Lakini si hivyo tu, mapokezi hayo pia ni kejeli kwa wote wanaopambana na ufisadi, na dhahiri ni mapokezi ambayo si heshima kwa Rais na Mwenyekiti wa Chama aliyepania kupambana na ufisadi. Si heshima; hasa kwa sababu Rais alimkubalia ajiuzulu kwa kuzingatia uzito wa tuhuma zenyewe.

Ndiyo maana sote tumebaki na mshangao mkubwa; huku tukijiuliza maswali mengi. Ni nini ambacho wenzetu hawa wa Mwanza, Shinyanga na hasa jimbo la Bariadi Magharibi wanakifurahia baada ya mbunge wao huyo kutuhumiwa kwa ufisadi wa kiwango ambacho hakijapata kuonekana nchini?

Au ndiyo tumeishiwa na viongozi mashujaa kiasi kwamba hata kiongozi anayetuhumiwa kwa ufisadi kwetu sisi anatosha kuwa shujaa wetu? Au ni njaa tu na umasikini uliowafanya wananchi wajitokeze kwa wingi kila kijiji alikopita; ili angalau wapate kula nyama ya ng’ombe zilizochinjwa?

Lipo pia swali jingine linalodai jibu. Wakati Chenge alipolaumiwa kwa kusema kwamba dola milioni moja alizoziweka benki Uingereza ni ‘vijisenti’, aliwaomba radhi Watanzania wote kwa kauli yake hiyo isiyo ya kiungwana, lakini wakati wa mapokezi hayo ya Bariadi aliirudia tena kauli yake hiyo kwa kusema kwamba hawezi kujiua na kuacha ‘visenti’ vyake.

Je, hii ina maana kuomba radhi kwake kwa awali, kwa mjumbe huyu wa Kamati Kuu ya CCM, kulikuwa ni mzaha kwa Watanzania? Tangu lini uongozi umegeuka kuwa jambo la mzaha?

Lakini swali zito zaidi pengine ni hili: Je, mapokezi hayo ya Bariadi Magharibi yalikuwa na baraka za makao makuu ya CCM? Na kama ndiyo, baraka hizo leo zinamweka wapi Rais wa nchi (Jakaya Kikwete) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM?

Au tatizo la ufisadi ni tatizo la Serikali tu, na halipaswi kuikosesha usingizi CCM; japo ndicho chama tawala? Na kwa nini viongozi wa juu wa CCM waruhusu Chama wilayani na majimboni kugeuka kuwa kimbilio la viongozi wake wanaotuhumiwa kwa ufisadi? Je, huku si kujenga ukabila kidogo kidogo na kuigawa nchi?

Ikumbukwe kwamba hiyo si mara ya kwanza kwa kiongozi mtuhumiwa wa ufisadi, anayeachia ngazi, kukimbilia jimboni na kupokelewa kama hero.

Tuliiona hiyo kwa Edward Lowassa wakati wa mapokezi yale ya Monduli baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu kutokana na kuhusishwa na kashfa ya ufisadi ya Richmond. Na Chenge anaweza asiwe ndiye wa mwisho.

Tuliona hivyo pia kwa Mbunge Harrison Mwakyembe wakati naye alipopokelewa kwa shangwe siku aliporejea Kyela; japo mapokezi yake ni kwa sababu ambazo ni tofauti kabisa na hizo za Lowassa na Chenge. Mapokezi yake yeye yalikuwa ni chanya (kwa wengi wetu) kwa sababu yalilenga kumpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Bunge iliyochunguza suala la Richmond na kutoa ripoti makini.

Lakini je, mapokezi ya Lowassa baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu, na hayo ya Chenge ni ya kuwapongeza kwa kufanya lipi jema? Lojiki ingekuwa kuandaa maandamano ya kuwalaani kwa kuyatia aibu majimbo yao; maana mbunge kutuhumiwa tu kwa ufisadi mkubwa kiasi hicho ni aibu kwa jimbo zima.

Lakini kuwaandalia watuhumiwa wa ufisadi mapokezi kamambe ya kuwapongeza badala ya maandamano ya kuwalaani; maana yake ni kwamba tumeanza kuwa insane na kwamba hatuishi tena katika dunia ya lojiki.

Nimetumia mifano ya mapokezi hayo ya majimboni ya Lowassa, Mwakyembe na haya ya karibuni ya Chenge kuonyesha tu jinsi ambavyo viongozi wa juu wa CCM wamekiweka chama hicho katika Auto-Pilot.

Nasema hivyo kwa sababu nina hakika CCM makao makuu haijatoa mwangozo kuhusu suala hili linaloidhalilisha; na hivyo kwa kukosa mwongozo toka juu, CCM wilayani na CCM majimboni huamua kufanya wanavyoona ni sahihi au wanavyotaka wao kwa kuwa hakuna wa kuwaongoza. Tuliliona hilo Monduli, tukaliona Kyela na sasa Bariadi Magharibi.

Na kote huko ambako mapokezi hayo yamefanyika, CCM iko vipande vipande. Arusha (kwa Lowassa) upo mgawanyiko katika chama. Mbeya (kwa Mwakyembe) CCM imegawanyika katika makundi mawili – moja ni la Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa na jingine ni la Mwakyembe na Profesa Mwandosya.

Mkoani Mwanza nako ambako ‘Mzee wa vijisenti’ alipokewa kwa mbwembwe, hali ni hiyo hiyo. Kumekuwepo na mgawanyiko mkubwa CCM mkoa wa Mwanza na suala la hivi karibuni la ubomoaji wa Uwanja wa Nyamagana limezidi kutia chumvi kwenye kidonda cha mgawanyiko huo. Hata Shinyanga nako mambo si shwari.

Kimsingi, kama uongozi wa juu wa CCM usingekuwa umekiweka Chama katika Auto-Pilot, ungekuwa umeshayashughulikia haraka matatizo ya uongozi wa CCM katika mikoa hiyo mitatu, na pengine tusingeshuhudia maandamano na mapokezi hayo ya kejeli ya kina Chenge. Lakini ndege iko kwenye Auto-Pilot, matatizo yameachwa yajitatue yenyewe!

Lakini hata ukiangalia jinsi CCM kinavyobabaika katika suala la mwafaka na CUF au kinavyolichukulia suala la kuhusishwa kwa viongozi wake katika skandali za ufisadi za EPA, Richmond, Kiwira, Twin Towers, Meremeta na nyingine nyingi, utagundua tu kwamba hakina kabisa mwongozo wa namna ya kuyashughulikia matatizo hayo, au namna ya ‘kuwashughulikia’ viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Na ndiyo maana umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) mkoa wa Tanga unatoa tamko la kuwataka viongozi wote wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi kujiuzulu uongozi; lakini punde tu wanajibiwa na CCM wilaya ya Bariadi Magharibi kwamba waache kuupigia debe “upuuzi huo.” Sura hii inathibitisha kwamba Chama hakina mwongozo kuhusu suala hili.

Kwa nini chama ni kimoja lakini kila mkoa unapuyanga kivyake? Ni kwa sababu ndege iko kwenye Auto-Pilot, na wakati rubani anaondoka kitini kwenda kunywa kahawa, hakuipa ndege mwelekeo wa wapi pa kwenda!

Na ndiyo maana naamini kwamba kama ndege hii itaendelea kuwa kwenye Auto-Pilot, tutaendelea kuona vituko vingine vikubwa zaidi vya viongozi wa CCM kutukuzana wenyewe kwa wenyewe kwa ufisadi.

Tafakari.
 
Back
Top Bottom