Ufisadi utakwisha tukiondoa mgongano wa Maslahi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ufisadi utakwisha tukiondoa mgongano wa Maslahi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by kingwendu, Jan 12, 2009.

 1. k

  kingwendu Member

  #1
  Jan 12, 2009
  Joined: Feb 24, 2007
  Messages: 30
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Ufisadi utakwisha tukiondoa mgongano wa Maslahi?

  Bila ya shaka wengi wetu tumechoshwa na ufisadi, na ili tuweze kusonga mbele tunahitaji viongozi ambao kweli wakisema wanauchukia ufisadi tushawishike kwa kauli zao na matendo yao kwamba kweli wao si mafisadi.

  Naambatanisha article iliyonigusa kutoka raia mwema... Tujadili...

  Mgongano wa kimaslahi na ufisadi unaoitesa Tanzania.

  Mwandishi Wetu Januari 7, 2009
  MARA kadhaa tumesikia viongozi wetu waandamizi na hata mkuu wa nchi Rais Jakaya Kikwete akielezea dhamira ya Serikali yake kupeleka mswada bungeni unaozuia kuchanganya siasa na biashara.

  Hili pengine linaweza kuwa ni jibu muafaka kwa matatizo yanayolitesa Taifa; ulaji wa rushwa, matumizi mabaya ya ofisi za umma na ufisadi unaotishia amani, umoja na utulivu wa nchi.

  Mara kadhaa mimi na wengine pia hupenda kusema nchi yetu ipo njia panda; yale yanayotokea sasa hayajawahi kushuhudiwa kwa muda mrefu au hayajawahi kutokea kabisa katika historia ya nchi. Ni njia panda, kabla hatujafika huko tunapotaka kufika katika Tanzania ile yenye neema na maisha bora kwa watu wake.

  Kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri baada ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu na viongozi waandamizi na wafanyabiashara mashuhuri kusimamishwa mahakamani ni dalili ya kile nilichokisema hapo juu. Hakika tu njia panda na Mungu akipenda na kwa jitihada zetu wenyewe, nchi itafika pale tunapotamani kufika.

  Makala hii itazungumzia dhana ya mgongano wa kimaslahi na kwa namna gani tunaweza kupunguza au kukwepa kabisa athari zake. Maana bila ya shaka ni huu mgongano wa kimaslahi ndio haswa kitovu cha mikikimikiki tunayoiona katika wakati huu; ufisadi wa kupindukia unaolitesa Taifa.

  Kitafsiri mgongano wa kimaslahi ni ile hali inayojitokeza pale mtu aliye katika nafasi fulani ya kuaminiwa (mfano; mwanasiasa, mwanasheria, mhandisi n.k) anapokuwa na maslahi yanayokinzana, baina ya maslahi yake binafsi na nafasi aliyokuwa nayo.

  Kukinzana huko kwa maslahi kunamuweka katika nafasi ngumu ya kufanya maamuzi bila ya kufanya upendeleo unaosukumwa na maslahi ya kibinafsi. Ikumbukwe mgongano wa kimaslahi unaweza kujitokeza hata pale ambapo hakuna uvunjwaji wa sheria au hata kukiukwa kwa maadili.

  Mgongano wa kimaslahi unaweza kutengeneza picha ya upendeleo hata pale mhusika pengine hakuwa na nia ya upendeleo na hivyo basi kuiweka taaluma yake au cheo chake katika hali ya kutiliwa shaka.

  Athari za mgongano wa kimaslahi wakati mwingine zinaweza kupunguzwa kwa kuwa na chombo huru kitakachochunguza na kuhakiki katika suala husika kama kulikuwa na namna yoyote ya kukiukwa kwa taratibu, mathalani Kamati za Bunge zinavyofanya kazi, mfano hai ni ile kamati ya Dk. Harrison Mwakyembe katika sakata la Richmond.

  Mgongano wa kimaslahi unaweza kujitokeza si kwa wanataaluma na wanasiasa pekee bali pia kwa waajiriwa wa kada nyingine kazini, mfano, kama ikitokea meneja ununuzi wa shirika alishiriki katika kutoa maamuzi ya ushindani wa tenda fulani ambayo pengine ndugu yake au rafiki yake naye alikuwamo katika ushindani ule na mtu yule au kampuni ile ikashinda na kupata tenda ile basi hapo kunakuwa na kiwingu cha mgongano wa kimaslahi.

  Wanazuoni wa taaluma mbalimbali wanakubalina kwamba suala zima la mgongano wa kimaslahi wakati mwingine ni suala ambalo si jepesi kuepukika na hii ni kwa sababu lipo ndani ya asili yetu kama wanadamu. Maana ni hulka ya nafsi ya mwanadamu kujipendelea au kupendelea wale walio karibu yake. Ni watu wachache waliojaliwa kuwa na nafsi za kupendelea wengine na kwa hivyo kuzishinda tamaa za nafsi zao na hawa ndio wanaoitwa waliofaulu kwa maksi za hali ya juu.

  Kwa hivyo basi kitu cha msingi cha kujiuliza ni kwa namna gani tunaweza kuidhibiti hali hii ya mgongano wa kimaslahi na pengine kuziba nyufa zilizopo katika mapungufu yetu ya kibinadamu na mengineyo. Njia zifuatazo zinaweza kutumika:

  Kuepuka kabisa mgongano wa kimaslahi

  Njia bora kabisa ya kupambana na mgongano wa kimaslahi ni kuuepuka moja kwa moja kwa kuepuka kujihusisha kabisa na biashara yoyote au taaluma yoyote baada ya kuteuliwa kushika ofisi ya umma.

  Mfano, mwanasiasa aliyeteuliwa au kuchaguliwa kushika wadhifa fulani anaweza kuuza hisa zake zote katika mashirika au kampuni alizokuwa akishiriki. Au kwa namna nyigine anaweza kuzihamisha hisa hizo kwenda katika chombo cha udhamini kitakachokuwa kinaendelea na biashara bila ya ufahamu wake au yeye kuwa na ushawishi wa namna yeyote.

  Kuwa na uwazi zaidi katika kutangaza mali

  Njii hii ni maarufu na inatumika sana nchini ingawa ufanisi wake bado unazaa maswali mengi kuliko majibu kutokana watu wengi kuendelea kuhoji ukweli wa mali zile zinazotajwa na watumishi wetu na uhalisia wa mali zenyewe anazomiliki mtu mhusika.

  Wengi pia hawaridhiki na utaratibu uliopo kwamba mtu yule aliyetangaza mali zake wakati anaingia madarakani hatangazi wakati anapoachia nafasi husika.

  Kujitoa katika maamuzi kunapokuwa na mgongano wa kimaslahi

  Wale wanaoona kwamba panaweza kutokea mgongano wa kimaslahi kwa wao kuwapo katika nafasi ya kimaamuzi au ushawishi inashauriwa ni bora wakakaa pembeni, na mtumishi muadilifu na mkweli ni yule ambaye pia atakuwa tayari kusema kwa uwazi kwa wenzake kuwa anajitoa katika kujadili suala husika kwa sababu kutakuwa na mgongano wa kimaslahi.

  Haya hutokea, ndiyo maana majaji au mahakimu hawatakiwi kutoa maamuzi au kushiriki katika mwenendo wa kesi ambazo wao wanaweza kuwa na mgongano wa kimaslahi.

  Ushirikishwaji wa chombo huru katika uhakiki

  Chombo huru kinaweza kutumika katika uhakiki wa kuangalia kama kulikuwa au kutakuwa na mgongano wa kimaslahi na kutoa mapendekezo. Kwa mfano, chombo huru kinaweza kutumika kutangaza bei halisi ya kukodisha jengo la mheshimiwa fulani ili majengo yale yatumike kwa shughuli za shirika au hata serikali kwa kuangalia uhalisia wa bei iliyopo sokoni na hadhi ya majengo husika na namna mkataba mzima ulivyo pasi na kuwapo kiwingu au mizengwe yeyote.

  Njia nilizozitaja hapo juu ni baadhi tu kati ya zile zinazoweza kuwa ni suluhisho la mgongano wa kimaslahi. Naamini zipo nyingine ambazo pia zinaweza kutumika lakini kwa uchache niseme nimefungua mlango katika mjadala wa njia muafaka za kuepuka mgongano wa kimaslahi haswa katika kuisubiri ile ahadi ya kupeleka bungeni mswaada wa kuzuia kuchanganya siasa na biashara ili kuleta ufanisi na tija katika kutumikia umma.

  Cha muhimu hapa kutambua ni kwamba umma wa Tanzania umeamka, si sawa na ule wa miaka ya nyuma. Yanayotokea sasa katika medani za siasa za Tanzania na sheria kuonekana kuanza kufuata mkondo wake iwe ni somo kwa wale wote wanaotaka kuitumikia nchi kwamba hatutajali shahada zao za uzamili au uzamivu kutoka UDSM, Oxford, Harvard au kona yeyote duniani. Ukiwa fisadi sheria zitakubana.


  w.kindamba@citybankingcollege.co.uk
   
Loading...