Ufisadi uliokithiri na alichokisema mbunge wa CCM Luhaga Mpina juu ya ufisadi wa kutisha serikalini


K

kasema

Member
Joined
Sep 27, 2010
Messages
22
Likes
0
Points
0
K

kasema

Member
Joined Sep 27, 2010
22 0 0
MAELEZO BINAFSI JUU YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI.

Kwa mujibu wa kifungu cha 28(8), naomba kutoa maelezo binafsi juu ya matumizi ya kawaida ya serikali kuwa makubwa kuliko mapato ya ndani na hivyo kupelekea deni la Taifa kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, wakati wa kipindi cha maswali na majibu tarehe 16, Aprili 2013 hapa Bungeni niliuliza swali la nyongeza katika swali la msingi namba 47 la mheshimiwa Thuwayaba Idrisa Muhammed (Mbunge wa Viti maalum) kuhusu deni la Taifa na pia katika mwongozo niliouomba kwako ambapo nilieleza kuwa moja ya sababu ambayo inasababisha deni la taifa kuongezeka ni pamoja na serikali kuwa na matumizi makubwa ya kawaida kuliko uwezo wa mapato yake ya ndani na hivyo imekuwa ikikopa fedha ndani na nje ili kufidia pengo.

Mheshimiwa Spika, Majibu ya naibu Waziri wa fedha Mheshimiwa Saada Mkuya Salum wakati akijibu swali langu la nyongeza alikana kwamba serikali kwa namna yeyote ile haikopi fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida bali inakopa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo pekee. Pia hata wakati akitoa maelezo juu ya mwongozo niliouomba tarehe 24/04/2013 aliendelea na msimamo huo na akaongeza kuwa katika fedha za matumizi ya kawaida (recurrent expenditure) kuna kiasi kikubwa (big chunk) ya fedha za maendeleo zifikiazo trilioni 1.6 kama Human Capital Investment.

Mheshimiwa Spika Kwa kuwa sijaridhika na majibu yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha kwa nyakati zote mbili yaani wakati akijibu swali la nyongeza na hata alipopewa nafasi ya kujibu mwongozo wangu, kwani maelezo yake hayakuweza kujibu hoja mahususi na hii ni kinyume na masharti yaliyowekwa na kifungu cha 46(1) cha kanuni za kudumu za Bunge toleo la 2013, hivyo nimeamua kuwasirisha maelezo binafsi ili nipate ufafanuzi wa kina na kwamba niweze kuishauri Serikali juu ya suala hili.

Mheshimiwa Spika, Majibu yake yameleta mkanganyiko mkubwa kwani badala ya Naibu Waziri wa Fedha kuthibitisha alichokieleza kuwa Serikali haikopi kugharamia matumizi ya kawaida, ameleta tafsiri mpya ya shughuli gani ni matumizi ya kawaida (Reccurent Expenditure) na ipi ni matumizi ya maendeleo (Development expenditure). Amekwenda mbali zaidi kwa kusema hata fedha inayotengwa kulipa deni la Taifa na semina ni fedha za maendeleo, je tafsiri hii ya Naibu Waziri inazingatia viwango gani? Kwani kwa mujibu wa hotuba za bajeti za Waziri wa Fedha zimekuwa zikiyagawa matumizi katika makundi mawili yaani matumizi ya kawaida (Mishahara, Deni la Taifa na matumizi mengineyo) na matumizi ya maendeleo kwa mujibu wa viwango vya kitaifa (Government standing orders) na kimataifa (IMF, World Bank, Accounting International Standards n.k)

Mheshimiwa Spika, upo ushahidi wa kitakwimu unaothibitisha kuwa matumizi ya Serikali ni makubwa kuliko mapato ya ndanina kwamba Serikali imekuwa ikilazimika kutaafuta misaada na mikopo ili kuziba pengo hilo.

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Waziri wa fedha ya mwaka 2011/2012 inaonyesha kuwa mapato ya ndani yalikuwa trilioni 7.3 wakati matumizi ya kawaida yalikuwa trilioni 8.6 hii ni tofauti ya trilioni 1.3, na hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 mapato ya ndani yalikuwa trilioni 9.1 wakati matumizi ya kawaida yalikuwa trilioni 10.6 hii ni tofauti ya trilioni 1.5. Kwa mujibu wa takwimu hizi pengo la mapato linaongezeka kila mwaka na kila mapato ya ndani yanapoongezeka matumizi ya kawaida huongezeka zaidi.

Mheshimiwa Spika, Vilevile katika vitabu vya hotuba ya Waziri wa fedha ya zinaonyesha kiasi cha shilingi trilioni 3.05 (2011/2012) na shilingi trilioni 2.31 (2012/2013) zilikopwa kugharamia Miradi ya Maendeleo, na shilingi trilioni 2.48 (2011/2012) na shilingi trilioni 2.89 (2012/2013) zilikopwa kwa ajili ya kuziba pengo la mapato

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa ya Umasikini na maendeleo ya watu (PHDR -2011) matumizi ya Serikali yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka 15.1% ya GDP (2000/2001) hadi kufikia 26.3% (2009/2010). Pia pengo la mapato ya ndani na matumizi ya kawaida limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka, nakisi ya kibajeti (Fiscal deficit-bila misaada) limekuwa likikuwa kila mwaka kutoka 4.3% (2001/2002) hadi 10.9% (2009/2010) ya GDP na nakisi ya kibajeti ikijumuisha misaada imekuwa toka 0.4% hadi 4.7% (2009/10) ya GDP. Hivi sasa nakisi ya kibajeti (Kujumuisha misaada) limefikia 6.6% ya GDP (2011/12)

Mheshimiwa Spika, ili taifa liweze kutoka hapa lilipo sasa ni lazima tuongeze bidii katika ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima sambamba na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato na matumizi holela. Tumekuwa tukishuhudia ndani ya bunge hili kupitia hotuba ya bajeti ya Waziri wa fedha na Waziri Mkuu kuwa serikali itapunguza matumizi yake yasiyo ya lazima lakini kwa sababu zisizo julikana matumizi haya yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa upande wa kuongeza mapato jitihada mbalimbali zimewekwa lakini mafanikio yake yamekuwa ni ya kusuasua.

Mheshimiwa Spika, Matumizi ya kawaida (Reccurrent Expenditure) ya serikali hujumuisha deni la taifa, mishahara na matumizi mengineyo (OC) ukipitia vipengele hivi vyote utagundua kuwa endapo jitihada madhubuti zitachukuliwa tunaweza kupunguza matumizi ya serikali kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, Matumizi mengineyo (Other Charges-OC) kwa Wizara, Mikoa na Halmashauri; eneo hili limekuwa ni kichaka cha ufisadi. Kumekuwa na manunuzi yasiyokuwa na tija, samani za ofisi zenye gharama kubwa kila mwaka, posho za safari (ndani na nje ya nchi), ununuzi wa magari ya kifahari, mtiririko wa warsha na semina, mafuta, mafunzo, samani, viburudisho, matengenezo hewa ya magari, maonyesho ghali yasiyo na tija, ongezeko la shughuli za kiutawara n.k

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa uchambuzi wa bajeti unaofanywa kila mwaka na shirika la Sikika katika maeneo sita pekee ya bajeti yaani: posho, gharama za safari (ndani na nje), semina (ndani na nje ya nchi), mafuta na vilainisho, viburudisho na ununuzi wa magari. Matumizi haya yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka, kama ifuatavyo: shilingi bilioni 626.3 (2011/2012), shilingi bilioni 681.2 (2012/2013) na mwaka ujao wa fedha (2013/2014) inakadiliwa kuwa shilingi bilioni 714.1.

Mheshimiwa Spika, Uchambuzi huu umekwenda mbali zaidi na kuonyesha kuwa katika mwaka ujao wa fedha (2013/2014) ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Mahesabu ya serikali imepunguza gharama za mafunzo kwa kiasi cha shilingi milioni 888 sawa na punguzo la 38% lakini wakati huo huo Wizara ya Fedha imeongeza mara kumi gharama za mafunzo kutoka shilingi milioni 885 (2012/2013) hadi shilingi bilioni 8.8 (2013/2014).

Mheshimiwa Spika, Posho ni matumizi yenye utata na yanayolalamikiwa sana ndani na nje ya Bunge lako tukufu. Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na Sikika, jumla ya shilingi bilioni 360 zimepangwa kutumika kulipa posho tu katika mwaka wa fedha 2013/14. Kuna ongezeko la 15% ukilinganisha na mwaka 2012/13. Ripoti ya Bunge ya Novemba 2011 iliyochunguza skandali ya Jairo ni mfano na ushahidi tosha jinsi matumizi mabaya ya posho na dizeli kwa magari yasivyo na tija kwa uadilifu na maendeleo ya nchi. Vile vile kwa mujibu wa MTEF 2011/2012-2013/2014 ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii bei ya mafuta ilichajiwa hadi shilingi 4,000/= kwa lita badala ya shilingi 2,200/= iliyoko sokoni. Mambo haya yote Waziri wa Fedha anajua na Waziri Mkuu anajua.

Mheshimiwa Spika, safari za ndani na nje ya nchi pamoja na warsha ni matumizi mengine yaliyogubikwa na ufujaji yaliyolalamikiwa sana hadi kufikia Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuagiza watakaotaka kufanya semina na safari watafute kibali kutoka ofisi yake. Haidhuru bajeti katika maeneo haya imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano mmoja tu kufafanua ufisadi wa semina na safari,Tanzania ilialikwa katika moja ya vikao vya Umoja wa Mataifa katika Tume ya Haki za Kiuchumi, Jamii na Utamaduni (United Nations Commitee for Economic, social and cultural rights) vilivyofanyika Geneva, Uswiss kuanzia tarehe 12-30 November 2012,Tanzania ilipeleka jopo la watu 34 ikiwa ni msafara mkubwa kuliko nchi nyingine zote zilizoalikwa, mfano Bulgaria (16), Ecuado (9), Iceland (6), Mauritania (13) na Equittorial Guinea (8), Pamoja na jopo hilo kutoka Tanzania kuongoza kwa ukubwa lakini wakati wa majadiliano katika kikao hicho Watanzania walishindwa hata kujibu maswali, kwa makadirio ya chini ziara hiyo ilitumia zaidi ya shilingi milioni 400.

Mheshimiwa Spika, taarifa hizi zimenukuliwa kutoka tovuti ya UN
http://www2.ohchr.org/english/bodies/cescr/docs/list/DelegationTanzania_49.pdf
na, Committee on Economic, Social and Cultural Rights - 49th session

Mheshimiwa Spika, ukiacha vipengele hivyo sita hapo juu yapo maeneo mengi yanayosababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma, mfano; ununuzi wa kila mwaka wa samani, ununuzi wa vifaa (sare, stationary n.k) zaidi ya mahitaji na vyenye bei kubwa kuliko iliyopo sokoni, gharama kubwa za pango, gharama kubwa za matengenezo na ukarabati (barabara, majengo na magari) na uhamisho holela.

Mheshimiwa Spika, Kwa takwimu hizi ahadi ya serikali ya kupunguza matumizi yasiyokuwa na tija haina ukweli wowote. Ushauri wa CAG, Wabunge na wadau mbalimbali hauzingatiwi na Serikali kwani bajeti zimekuwa zikiwasiriswa kwa sura ileile. Mimi binafsi niliikataa bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13 ilipowasirishwa kutokana na miradi ya maendeleo kutengewa fedha pungufu huku matumizi yasiyokuwa na tija kutengewa fedha lukuki.

Mheshimiwa Spika, Aidha kwa hatua nyingine katika mwaka ujao wa fedha baada ya serikali kushinikizwa na Wabunge imekubali kupunguza Matumizi Mengineyo (OC) na kuongeza fedha za Maendeleo katika Wizara mbalimbali, Mfano, Maji (shs.bilioni 184.5), Uchukuzi (shs.bilioni 30), Viwanda (shs.bilioni 30) na Vijana (shs.bilioni 9). Swali la kujiuliza ni kwanini Serikali kwa muda mrefu imekuwa na kigugumizi cha kupunguza matumizi haya? Kwani kwa muda mrefu miradi ya maendeleo imekuwa ikitengewa fedha kidogo na Taifa kuingia mikopo isiyo ya lazima na kuzidi kuongeza mzigo mkubwa wa madeni. Hii si sawa kuendekeza matumizi ya namna hii wakati watanzania wengi wakifa kwa kukosa huduma muhimu za afya, elimu, barabara na maji. Endapo eneo hili litadhibitiwa vizuri tunaweza kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 700.

Mheshimiwa Spika, Mishahara; katika eneo hili tumeshuhudia mishahara hewa kwa muda mrefu sasa. Kwa mujibu wa taarifa CAG shilingi bilioni 1.8 (2009/2010) na shilingi milioni 142.7 (2010/2011) zimelipwa kwa watumishi hewa katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, mishahara mipya imekuwa ikitengwa katika bajeti wakati kibali cha ajira hakijatolewa, vilevile kumekuwapo na ongezeko kubwa la umbile la serikali (Government structure) usiozingatia uwezo wa mapato ya ndani. Mfano, utitili wa Mashirika ya Umma ambayo kwasasa yanafikia zaidi ya 200 na mengi yakifanya kazi zinazofanana, katika mwaka wa fedha 2012/2013 ruzuku ya mashirika ya umma katika matumizi ya kawaida ilifikia shilingi trilioni 1.7. Hii ni sawa na 11.3% ya bajeti ya serikali.

Mheshimiwa Spika, Pia ukubwa wa wizara zinazofanya kazi zinazofanana mfano TAMISEMI na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hata baada ya shughuli za Elimu ya msingi na Sekondari kuhamishiwa TAMISEMI ukubwa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi umebaki vilevile.

Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa, ifahamike kwamba serikali imekuwa ikikopa ndani na nje ya nchi ili kugharamia Miradi ya Maendeleo (Development Expenditure) pamoja na kuziba Pengo la mapato (Recurrent Expenditure) na kwamba hivi sasa Deni la Taifa limefikia shilingi trilioni 21 sawa na 47% ya Pato la Taifa (GDP). Hii inamaanisha kwamba karibia nusu ya pato la Taifa liko kwenye Deni.

Mheshimiwa Spika, nchi kukopa siyo dhambi ila tatizo linaanzia pindi tunapokopa kwa ajili ya matumizi makubwa yanayoweza kuepukwa, kupunguzwa na kugharamiwa na fedha za ndani. Pia kumekuwa na tatizo la kutokulipa marejesho ya mikopo kwa wakati na kusababisha malimbikizo makubwa ya riba kunakopelekea kuongezeka kwa deni la Taifa kila mwaka, mfano hadi kufikia Septemba 2012, malimbikizo ya riba yamefikia dola za kimarekani milioni 781.06 (Tsh trilioni 1.27).

Mheshimiwa Spika, Vile vile kumekuwapo na kasi kubwa ya ongezeko la dhamana za Serikali (Excessive use of Government Guarantees) kwani hii inaongeza Deni kwa Serikali pindi mzaminiwa anaposhindwa kulipa (Contigent Liabilities), hadi Disemba 2011 dhamana za Serikali zilifikia shilingi trilioni 1.4, ipo mifano mingi ya makampuni ambayo hayafanyi vizuri katika biashara baada ya kupata dhamana ya Serikali. Pia kwa mujibu wa CAG madeni mengine hayana maelezo na hivyo ni mikopo hewa, hii ni hatari kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, licha ya kitendo hichi kupelekea kuweka rehani mapato ya siku za usoni lakini pia ni mzigo mkubwa unaolielemea Taifa. Ni lazima Nchi yetu sasa iwe na mtazamo mpya katika ukopaji na udhibiti wa ongezeko la Deni la Taifa.

Mheshimiwa Spika, Matumizi ya Maendeleo (Development Expenditure); Serikali hutegemea misaada, mikopo na fedha za ndani katika kugharamia eneo hili. Kutokana na fedha za ndani kuzidiwa na matumizi ya kawaida, serikali imekuwa ikitenga fedha kidogo sana za ndani katika eneo hili na zimekuwa hazitolewi kutoka hazina kwa wakati, pindi zinapotolewa huwa pungufu ya kiwango kilicho idhinishwa katika bajeti na wakati mwingine hazitolewi kabisa.

Mheshimiwa Spika, upande wa misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo imekuwa ya kusuasua hususani tangu mdororo wa uchumi uikumbe Dunia mwaka 2008, kumekuwa na masharti magumu na maswali yasiyokuwa na majibu kutoka kwa wahisani na wakati mwingine wahisani wamekuwa wakijitoa kutokana na kukosekana kwa nidhamu na uadilifu wa matumizi ya fedha za umma nchini.

Mheshimiwa Spika, Pia fedha zimekuwa zikitolewa kwa kuchelewa na pungufu ya kiwango kilicho ahidiwa. Kutokana na kusuasua kwa upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo kumepelekea miradi mingi kutokamilika kwa wakati na hata kutotekelezwa kabisa. Mfano, miradi ya maji ilitengewa fedha za ndani kiasi cha shilingi bilioni 140 katika mwaka wa fedha 2012/2013 lakini hadi kufikia robo ya pili fedha iliyokuwa imetolewa ni shilingi bilioni 29 sawa na 20.7% tu ya fedha iliyoidhinishwa; Wizara ya Kilimo chakula na Ushirika ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 120.4 lakini hadi kufikia machi 2013 ni shilingi bilioni 22.96 tu sawa na 19% ya fedha zilizoidhinishwa ilikuwa imetolewa, pia katika halmashauri na mashirika mengi nchini hadi bajeti inafikia mwisho yanakuwa yamepokea fedha chini ya 50% ya fedha zilizoidhinishwa.

Mheshimiwa Spika, Waheshimia Wabunge ni muda sasa kuwaeleza watanzania ukweli kwamba Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP-1) unadalili zilizo wazi kutokutekelezeka hata PAMANDU (President's Delivery Bureau) iliyoanzishwa haitaleta mabadiliko yoyote tusipo kutatua tatizo la ukosefu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Mapato ya Ndani: Mapato ya ndani hutegemea mapato yatokanayo na kodi na yasiyo ya kodi yaani maduhuli. Mapato yote ya kodi hukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati maduhuli hukusanywa na Wizara, Taasisi na Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, Wigo wa mapato; Kwa mujibu wa TRA ni watu milioni 1.6 tu wanaolipa kodi ya mapato kati ya watu milioni 14.2 ambao wanastahili kulipa. Hii ni idadi ndogo sana ya walipa kodi ikilinganishwa na nchi jirani ya Kenya ambayo walipa kodi wake wamefikia zaidi ya milioni 10.

Mheshimiwa Spika, Uwezo wa TRA kukusanya mapato; Licha ya TRA kufikia malengo na wakati mwingine kuvuka malengo ya kukusanya mapato lakini kumekuwa na hisia kuwa malengo mara nyingi yako chini ikilinganishwa na ukuaji wa uchumi na mahitaji muhimu ya Taifa. Mwenendo wa makusanyo ya kodi kwa miaka mitatu shilingi trilioni 5.2 (2010/2011), shilingi trilioni 6.2 (2011/2012) na inakadiriwa shilingi trilioni 8.1 (2012/2013). Makusanyo haya ni madogo mno ikilinganishwa na raslimali za Taifa na idadi ya watu iliyofikia milioni 44.9 (Sensa, 2012).

Mheshimiwa Spika, Uwezo wa Wizara, Taasisi na Halmashauri kukusanya Maduhuli; ukusanyaji wa maduhuli umekuwa wa kusuasua kwani licha ya raslimali zilizopo, mapato yasiyokuwa ya kodi ni chini ya 10% ya makusanyo ya mapato ya serikali,mwenendo wa makusanyo wa maduhuli shilingi bilioni 442.9 (2010/2011), shilingi bilioni 911.7 (2011/2012) na inakadiriwa shilingi bilioni 644.6 (2012/2013). Hii inaonyesha dhahili kuwa hakuna usimamizi thabiti wa ukusanyaji wa mapato nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali ikiwemo Kamati Maalum ya Spika (Mapato- 2012) zinaonyesha udhaifu mkubwa uliopo wa ukusanyaji kodi na maduhuli.

Mheshimiwa Spika,
mfano Madini mengi yamekuwa yakitoroshwa na kuuzwa nje ya Nchi kwa njia za panya na hivyo kukwepa kodi, pia makampuni ya madini yamekuwa yakikwepa kodi kiasi cha shilingi bilioni 525 kila mwaka kwa kuingiza katika hesabu matumizi yasiyo ruhusiwa, licha ya TMAA kuthibitisha ukwepaji huu lakini TRA haijakusanya mapato hayo.

Mheshimiwa Spika, Makampuni ya Simu kuendelea kukwepa kodi kwa kuficha taarifa muhimu za kukokotolea kodi, gharama kubwa za matangazo zisizokuwa na kikomo, gharama zisizokuwa na ukomo za management na service fee, pamoja na misamaha lukuki ya kodi. Inakadiliwa kuwa kila mwaka makampuni ya simu hukwepa kodi kiasi kisichopungua bilioni 600. Tanzania inakusanya kodi ya mapato kidogo sana katika sekta ya simu kuliko nchi nyingine yeyote Afrika Mashariki, mfano mwaka 2010 Kenya (USD 79.3 Milioni), Uganda (USD 31.3 Milioni), Rwanda (USD 14 Milioni) wakati Tanzania ilikuwa na USD 1.7 Milioni tu.

Mheshimiwa Spika, Bandari; katika Bandari mapato mengi yamekuwa yakipotea kutokana na ucheleweshaji wa kupakia na kupakua mizigo, wizi wa mizigo, rushwa ambapo baadhi ya wafanya biashara huungana na watendaji wa serikali kuibia serikali mapato. Kwa mujibu wa Taarifa za Benki ya Dunia (Opening the Gate, 2012) zinasema zaidi ya mapato yapatayo USD bilioni 1.8 (TSH trilioni 2.9) yalipotea bandarini kwa kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika, katika sekta nyingine kama Uvuvi serikali inakosa mapato ya shilingi bilioni 362 kila mwaka kutokana na udhibiti hafifu wa uvuvi haramu pamoja na kukosekana takwimu za kukokotolea mapato. Katika sekta isiyo rasmi kila mwaka tunakosa mapato ya shilingi trilioni 1.3 kutokana na kushindwa kuwatambua walipa kodi katika sekta hii na kwamba mfumo wa kodi uliopo unawaacha nje. Pia sekta ya Misitu na Nyuki tunapoteza shilingi bilioni 93 kila mwaka kutokana na rushwa na utoroshaji wa magogo ghafi nchi za nje, wakati Mashirika ya umma hupoteza zaidi ya shilingi bilioni 50 kila mwaka n.k.

Mheshimiwa Spika, Utoroshaji wa fedha nje ya nchi, kwa mujibu wa tafiti za hivi karibuni Utoroshaji wa fedha nje ya nchi umeoungezeka na umefikia wastani shilingi bilioni 600 kila mwaka. Pia kwa mujibu wa mwenyekiti wa United Nations High Level on Illicit Financial Flow from Africa, Hon.Thabo Mbeki anasema kuwa utoroshaji wa fedha nje ya bara la Afrika umefikia USD billion 50 (TSh trilioni 81.5) kila mwaka. Pamoja na ongezeko hili linalolitishia kufirisika kwa Taifa na bara zima lakini kwa sababu zisizo eleweka serikali imenyofoa kipengere cha utoroshaji wa fedha nje ya nchi katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano (FYDP-1).

Mheshimiwa Spika, Hata vyanzo vipya vya mapato vilivyoainishwa katika mpango wa maendeleo ukurasa 82-96 yaani: Superprofit tax on minerals, controlling Ilicit Outflows, Taxation on Financial Transactions, Tanzania in the Diaspora n.k havijaanza kufanyiwa kazi. Wakati huohuo Tanzania hivi sasa tunajitegemea kibajeti kwa 54%-60% tu ikilinganishwa na nchi jirani ya Kenya ambayo inajitegemea kibajeti kwa 98%.

Mheshimiwa Spika, Misamaha ya kodi; Misamaha ya kodi inayotolewa na serikali kama vuvitio vya uwekezaji nchini ni mikubwa mno kiasi cha kuathili wigo wa mapato nchini, kutokana na mapato madogo ya ndani Taifa limeshindwa kugharamia miradi ya maendeleo, kulipa watumishi wake mishahara mizuri pamoja na kugharamia shughuli mbalimbali za uendeshaji wa serikali. Hali hii imelifanya Taifa kuendelea kutegemea misaada na mikopo kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, Katika hotuba za bajeti za serikali za miaka mitano mfululizo zimeonyesha nia ya serikali kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia 1% ya pato la Taifa na hata katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano (FYDP-1) ilikubalika kuwa misamaha ya kodi ishuke hatua kwa hatua hadi kufikia 1% ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2015/2016. Katika taarifa za CAG za kila mwaka wa fedha amekuwa akishauri misamaha ya kodi ipunguzwe ili kuongeza wigo wa mapato ya serikali.

Mheshimiwa Spika, Licha ya ushauri na ahadi hizo za serikali na makubaliano katika mpango wa maendeleo hakuna jitihada madhubuti za kupunguza misamaha ya kodi nchini kwani badala yake misamaha imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, mfano kwa mujibu wa taarifa za CAG mwaka wa fedha 2009/2010 (bilioni 680.6), 2010/2011 (trilioni 1.01) na mwaka 2011/2012 (trilioni 1.8). Kwa mujibu wa takwimu hizi misamaha ya kodi imepanda toka 2.9% (2010/2011) hadi 4.3% (2011/2012). Vilevile misamaha ya kodi imepanda toka 19% hadi 27% ya makusanyo ya kodi. Hivyo utaona kuwa endapo tu serikali isingeongeza misamaha katika mwaka wa fedha 2011/2012 serikali ingepata mapato ya ziada ya shilingi bilioni 800.

Mheshimiwa Spika, Jedwali la 3 la ongezeko la thamani (VAT) lilikuwa na makundi 5 mwaka 1997 lakini hivi sasa jedwali limefikia makundi 26 tofauti na nchi nyingine kama Uganda, Malawi na Kenya ambazo hazina jedwali lefu kama letu. Tanzania inatoa misamaha mikubwa ya kodi (4.3%) ikilinganishwa na nchi zingine za Afrika mashariki, mfano Kenya (1%) na Uganda (0.4%) tu.

Mheshimiwa Spika, Udhibiti na usimamizi wa fedha za umma; tafiti mbalimbali na taarifa za CAG na PPRA zimekuwa zikionyesha ufujaji, wizi na rushwa kubwa katika matumizi ya fedha na raslimali za umma.

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imekuwa ikitoa taarifa kuhusu manunuzi ya umma, aidha imekuwa ikibainisha jinsi wakaguliwa (procurement entities-PE) zinavyokiuka manunuzi kwa makusudi, mfano kulipa zaidi ya mkataba, kulipa kazi ambayo haikufanyika, kulipa kwa bei kubwa zaidi ya bei iliyoko sokoni na miradi kutokuwa na thamani halisi (value for money); mfano, katika ukaguzi wa viwango na thamani (Value for money) ambapo miradi 137 ilikaguliwa ni mikataba 63 tu sawa na 46% ndiyo iliyokuwa na thamani halisi na mikataba iliyobaki ilikuwa imechakachuliwa. Kwa mujibu wa CAG na PPRA ni zaidi ya 70% ya bajeti ya mwaka inatumika katika manunuzi ya bidhaa na huduma, serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi sana katika eneo hili. Endapo eneo hili litasimamiwa kikamilifu ili kila shilingi ifanye kazi yake stahili tutaokoa zaidi ya 10% ya fedha zilizoidhinishwa katika manunuzi. Mfano, bajeti ya mwaka 2012/2013 tungeweza kuokoa kiasi kisichopungua shilingi trilioni 1.1 ambazo zingeweza kugharamia maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, Licha ya unyeti wa suala zima la manunuzi lakini serikali imekuwa mpinzani namba moja wa kukwamisha udhibiti wa raslimali za umma kwani chombo hichi (PPRA) kimekuwa hakitengewi fedha za kutosha kukiwezesha kutekeleza majukumu yake ya ukaguzi. Mamlaka hiyo katika mwaka wa fedha 2011/2012 iliweza kukagua wakaguliwa 121 tu kati ya zaidi ya 400 ambao walipaswa kukaguliwa hii 30% tu. Sheria ya manunuzi ya Mwaka 2004 ilifanyiwa marekebisho mwaka 2011 ili kuipa uwezo zaidi wa kulinda na kudhibiti manunuzi ya umma na tukatunga sheria mpya ya Manunuzi (PPA, 2011). Mheshimiwa Rais alikwisha saini sheria hii mpya tangu tarehe 30, Desemba 2011 lakini cha kushangaza ni karibia miaka 2 sasa kanuni hazijatolewa na hivyo sheria haijaanza kutumika.

Mheshimiwa Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG), CAG pia amekuwa akitoa taarifa na mapendekezo yake dhidi ya mwenendo wa mapato na matumizi ya serikali, aidha amekuwa akibainisha ubadhilifu mkubwa wa fedha za umma kama; malipo hewa, kutumia fedha zaidi ya zile zilizoidhinishwa kwenye bajeti, upotevu wa vitabu vya mapato, malipo bila vielelezo n.k lakini inasikitisha taarifa zake hazipewi nafasi ya kutosha kujadiliwa ndani ya Bunge na kwamba hoja za ukaguzi zimekuwa hazijibiwi na kuletwa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, Pia mwaka huu serikali imeleta marekebisho ya sheria ya Ukaguzi (Public Audit Act, 2008) vifungu namba 37, 38, 39 na 40 vya sheria ya Ukaguzi wa Umma kukataza taarifa ya CAG kujadiliwa Bungeni hadi serikali ijibu hoja hizo, upo ushahidi wa kutosha katika Bunge hili, tumeomba mara kwa mara taarifa ya majibu ya hoja za CAG toka serikalini tangu waka 2009/2010, 2010/2011 lakini hadi sasa majibu hayajaletwa.

Mheshimiwa Spika marekebisho haya hayajawahusisha maafisa masuuli ambao hawajibu hoja za ukaguzi kwa wakati hadi CAG anapokuwa amekamilisha ripoti yake, badala yake sheria inatetea uzembe huo kwa kuhalalisha mianya ya ufujaji wa fedha za umma.
Mheshimiwa Spika, Ushiriki wa Bunge katika mchakato wa bajeti; kwanza nikupongeze kwa kusimamia na kukubali mabadiliko ya mzunguko wa bajeti (Budget Cycle) kuanza mapema na kumalizika kabla ya mwezi Julai sambamba na kuanzishwa kwa kamati ya bajeti.

Mheshimiwa Spika, Ili kamati ya bajeti na Bunge hili lipate fursa nzuri ya kuchambua mapendekezo ya bajeti lazima iende sambamba na uanzishwaji wa ofisi ya bajeti (Parliamentary Budget Office). Kwani hivi sasa licha ya kuwapo kwa kamati ya bajeti haina nyaraka muhimu (Budget Analysis) zitakazo wawezesha waheshimiwa wabunge kuwa na taarifa za kutosha kuhusu bajeti. Taarifa zilizopo ni kwamba suala hili linapingwa na serikali pasipo sababu zinazoeleweka na zipo taarifa kwamba hata uanzishwaji wa kamati ya bajeti ulipigwa vita na serikali.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ni masikini sana na hivyo ni lazima kila fedha na raslimali tulizonazo zitumike kwa uangalifu na kikamilifu. Taifa limeshindwa kufikia Malengo ya Milenia ya kupunguza umasikini na kufikia 19.5% ifikapo mwaka 2015 ikiwa kabla ya miaka miwili tu na umasikini Tanzania bado ni 33.4%, pia kwa mujibu wa ripoti ya nchi masikini sana duniani ya mwaka 2012 iliyotolewa na shirika la biashara na maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) jiji Geneva-Uswiss imebainisha nchi 48 zinazoingia katika kundi la nchi masikini sana (LDC), na Tanzania ni moja wapo kati ya nchi 33 za Afrika, katika orodha hiyo wenzetu wakenya hawapo katika kundi hili, hii ni aibu kubwa na haikubaliki.

Mheshimiwa Spika, Mapendekezo;

 1. Serikali ipunguze na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima katika posho, gharama za safari (ndani na nje), mafunzo (ndani na nje ya nchi), mafuta na vilainisho, viburudisho, ununuzi wa magari, ununuzi samani, ununuzi wa vifaa (sare, stationary n.k), upangaji holela (Dodoma na Dar es salaam), gharama kubwa za matengenezo na ukarabati (barabara, majengo na magari), uhamisho holela, pia serikali ikomeshe mishahara hewa na kuepuka malimbikizo ya riba na matumizi mengine ya mfano huu. Kabla ya kuwasilishwa kwa bajeti ya mwaka 2013/2014 serikali iwasilishe Bungeni taarifa ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ikiainisha kiasi kilicho okolewa na matumizi yake mapya.
 2. Kabla ya kuwasilishwa kwa bajeti ya mwaka 2013/2014 taarifa ya kamati Maalum iliyoundwa na Mheshimiwa Spika kwa ajili ya kuishauri serikali katika namna bora ya kuongeza mapato iwasilishwe Bungeni ili kutoa wigo mpana zaidi kwa wabunge kuishauri serikali kuhusu mapato na matumizi.
 3. Serikali izibe mianya yote ya upotevu wa mapato, ifuatilie na kutoza kodi na maduhuli yote yaliyokwepwa kulipwa miaka ya nyuma na ilete mpango mkakati wa kuongeza mapato ya ndani kabla ya kuwasirisha bajeti ya mwaka 2013/2014.
 4. Kabla ya kuwasirishwa kwa bajeti ya mwaka 2013/2014 serikali iwasirishe taarifa ya mchanganuo (detailed) wa Deni la Taifa lililofikia trilioni 21 sasa, sambamba na madeni ya wazabuni na wakandarasi.
 5. Kwa kuwa serikali imeahidi mara kwa mara kupunguza misamaha ya kodi Na Kwa kuwa tulikubaliana katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, hivyo katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2013/2014 serikali ilieleze Bunge na Watanzania imepunguza misamaha ya kodi kwa kiasi gani? Punguzo hilo lazima liashirie kufikia 1% ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2015/2016.
 6. Kwa kuwa suala la ugawaji wa fedha (Disbursment) linamkanganyiko mkubwa kati ya Hazina na watumiaji yaani Wizara,Taasisi na Halmashauri, Serikali iwasirishe taarifa ya ugawaji fedha katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012 na 2012/2013 na sababu za kwanini fedha hazipelekwi kama zilivyoidhinishwa na Bunge.
 7. Ofisi ya bajeti ya Bunge (Parliamentary Budget Office-PBO) inayohusisha wadau zaidi ya wabunge ianzishwe sasa ili kuwasaidia Wabunge kuichambua bajeti kwa kina na kwa sekta ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji wa Bunge na serikali. Bila uchambuzi ni vigumu kuifahamu bajeti kwa kina.
 8. Sheria ya Ukaguzi wa Fedha za Umma (Public Audit Act, 2008) pamoja na sheria zingine za usimamizi wa fedha yaani Public Finance Act, 2001 na Local Government Finance Act, 1982 ziletwe Bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ili kuzipa uwezo zaidi wa kulinda, kusimamia na kudhibiti matumizi (utilization) ya raslimali za Taifa.
 9. Wizara ya fedha iweke rasimu za bajeti kwenye tovuti yake wakati ikiendelea kujadiliwa Bungeni. Rasimu hiyo iwe na mchanganuo wa kila wizara (MTEF). Hii itawezesha wananchi wengi kufuatilia na kutoa maoni wakati bajeti ikijadiliwa, pia itarahisisha uchambuzi wa bajeti wa kitaalam (Budget Analysis) na pia Bajeti iliyopitishwa na Bunge iwekwe kwenye tovuti ya Wizara ya fedha ili wananchi waweze kufananisha iliyopendekezwa na iliyopitishwa.
Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasirisha

LUHAGA JOELSON MPINA
MBUNGE-KISESA

28/05/2013
 
Kitaturu

Kitaturu

JF-Expert Member
Joined
Apr 13, 2013
Messages
4,786
Likes
3,355
Points
280
Kitaturu

Kitaturu

JF-Expert Member
Joined Apr 13, 2013
4,786 3,355 280
Nammunga mkono kwa 100% kwani inawezekana kabisa kupunguza matumizi ya serikali yasiyo ya lazima na fedha zikaelelekezwa katika shighuli za maendeleo,kuboresha huduma za jamii kama afya,elimu,barabara vijijini nk bila kusahau kuboresha mishahara ya watumishi ambako ndiko kuliko na malalamiko sana zaidi kwa sasa!.

MFANO;
 1. Kuna maana gani kila kuchao maeneo ya utawala km mikoa mipya,wilaya mpya kuongezwa? Mfano kuna umuhimu na ulazima wowote kwa sasa kuwaza kuligawa jiji la Mbeya eti?....Ktk hili tafsiri yake ni moja tu kuwanufaisha watu flani kisiasa zaidi kuliko manufaa ya mapama ya kiuchumi.....maana yake baadhi ya watu wapate umeya, udiwani au U-DC au U-RC nk
 2. Kulikuwa na umuhimu gani kuinyang'anya wizara ya elimu mamlaka kamili ya kusimamia sekta ya elimu kikamilifu na kuwapa jukumu hilo TAMISEMI kusimamia jambo hilohilo na wakati huo wizara hiyo kubaki na muundo na jukumu hilohilo??.....Kwa sababu TAMISEMI kuna idara maalumu inayohusika na elimu na hapo pana Naibu waziri mmoja Bw. Kassim Majaliwa eti yeye ni maalumu kwa elimu tu TAMISEMI wakati huohuo kuna wizara kamili ya elimu yenye waziri na naibu waziri na watendaji wengine kibao......Huu ni upuuzi kwa sbb hapa ni sawa na kulipa mishahara watu wa4 kwa kufanya kazi moja. Na haya ndiyo yanayoleta matatizo katika sekta ya elimu hata elimu(ufaulu) yetu kuporomoka mwaka hadi mwaka tangu kuingia kwa Kikwete madarakani!!.
 3. Halafu mimi imeniuma sana kwamba ni watu 1.6m tu wanalipa kodi katika taifa hili kati ya zaidi ya 14milioni wenye uwezo wa kulipa kodi!!!??....Aisee hili ni tatizo na udhaifu wa hali ya juu wa serikali hii ya CCM!!. Mbaya zaidi kidogo hiki kinachopatikana kinapigwa juu kwa juu na hao wenye nafasi zao za kuchukua tu na kukihamisha nje ya nchi!!......Ndiyo maana hawa washkaji hawataki kuondoka madarakani hata kama ni kulazimika kung'oa watu kucha,meno na hata kuua kabisa!!

HOJA ya Mpina makini sana, lakini kwa mambo yalivyo katika serikali ya CCM najua watakuja na porojo na kejeli kibao kwa mleta hoja na ni lazima watamwambia mwenzao ametumwa na CHADEMA kuivua nguo serikali
!!.
 
C

Chikaka Sumuni

JF-Expert Member
Joined
May 16, 2013
Messages
1,339
Likes
5
Points
0
C

Chikaka Sumuni

JF-Expert Member
Joined May 16, 2013
1,339 5 0
Shida ya Mpina naye ameamua kutoa ngonjere kama kweli anayo dhamira ya kuwatetea wananchi wa Tanzania hawezi kufanya hivyo akiwa ndani ya CCM aamue ajiunge na Makamanda wa ukweli, Mimi ninao ushauri kwa ndugu zangu hao wa rangi ya kijani,

Kama CCM wanataka kuendelea kutawala kama wanavyodai wafanya yafuatayo:-
1. Wawe wanafunzi wazuri wa sera, itikadi, malengo na mtazamo wa Mwl. Nyerere
2. Waiangalie Katiba na Mwongozo wa CCM wakati wa Mwl.
3. Wawaondoe wafanya biashara wote kwenye chana chao CCM kwani alama zao ni Jembe
na Nyundo (Wakulima na Wafanyakazi)
4. Wasikilize hotuba za Mwl kwa makini hata kabla ya kuzunguka mikoani ili wale wote
ambao Mwl aliwatilia mashaka wawaondoe CCM kama alivyomtimua Malecela na kuandika
kitabu kuelezea Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania.
5. WAafute mikataba yote ya kuwaibia watanzania raslimali zao za asili alizowajalia
Mwenyezi Mungu.
6. Wawaombe radhi hadharani watu waliouawa katika mazingira ya kutatanisha na hasa
pale ambapo vyombo vya dola vilipohusika, mfano mauaji ya Mwangosi.
7. Mambo ya EPA, Kifo cha Gavana Balali na wote walioshiriki kuuza nyumba za serikali
wawajibishwe mahakamani.
8. Waturudishie ti zile za USWISS bila shida wala hatutawashitaki.

TAFAKARI!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!! !
 
C

Chikaka Sumuni

JF-Expert Member
Joined
May 16, 2013
Messages
1,339
Likes
5
Points
0
C

Chikaka Sumuni

JF-Expert Member
Joined May 16, 2013
1,339 5 0
Kula pini tu KAMANDA hawa ndo CCM wanavyo tuaga tayari make Nyerere aliwahi kusema yafuatayo:-
 • Tumepuuzwa kiasi cha kutosha,
 • Tumeonewa kiasi cha kutosha,

 • Tumenyanyaswa kiasi cha kutosha,

 • [*=left]Unyonge wetu ndo uliosababisha yote haya sasa ni wakati wa kujenga Umoja wetu Imara ili kujikomboa kutoka mikononi mwa mkoloni na mdhalimu.
​Tafakari!!!!!!!!!!!!!!!!!!
 
S

Shackshake

Senior Member
Joined
May 27, 2013
Messages
187
Likes
5
Points
0
Age
38
S

Shackshake

Senior Member
Joined May 27, 2013
187 5 0
Piiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiipoooooooooooooz,..,,,......samahani lakini
 
mwenyenchi

mwenyenchi

JF-Expert Member
Joined
Nov 10, 2011
Messages
658
Likes
31
Points
45
mwenyenchi

mwenyenchi

JF-Expert Member
Joined Nov 10, 2011
658 31 45
CCM bado kuna wabunge wachaaaaaache makini (Mpina) ; weeeeeengi wao ni wazinzi (Chemba), majambazi na walarushwa (EL), wanafiki, dhaifu, waongo, wapenda starehe, wambea, wamejaa mipasho na maneno ya kwenye khanga (Makida, Mizengwe, Komba) ndio maana nchi imekwama baada ya miaka 52 ya Uhuru!
Baba Riz ndio kiboko yoa, yupo Japan anacheza na watoto wa chekechea!
 
K

Kisimbusi

Senior Member
Joined
Jan 27, 2013
Messages
128
Likes
0
Points
0
K

Kisimbusi

Senior Member
Joined Jan 27, 2013
128 0 0
Ndefu lakini worth the read. Shukrani nyingi kwa Mpina
 

Forum statistics

Threads 1,273,088
Members 490,268
Posts 30,470,878