Ufisadi: Truth and Reconciliation

Mpanda Merikebu

Senior Member
Dec 27, 2007
170
2
Hivi karibuni kumekuwa na ufunuo (usio kamili) wa ufisadi uliondelea huko Benki Kuu. Katika ufunuo huo, wananchi tulielezwa kuwa Rais amekasirishwa na ufisadi huu na akaamua mambo kadhaa, ikiwemo kutengua uteuzi wa Gavana wa wakati huo. Ukichambua jambo hili kwa haraka haraka, utapata burudisho la moyo na kupata imani iliyotoweka katika serikali yetu. Lakini, ukifanya uchambuzi yakinifu, utagundua kuwa hatua ya Rais ni ndogo sana na kihistoria, hata wale waliofikishwa mahakamani huachiwa. Basi ili kutokupotezeana muda na kikubwa zaidi, kutokufanywa wapumbavu na kuleweshwa na kiini macho cha kumfanya Ballali ndio kuhani wa mafisadi, ningependekeza kuundwa kwa chombo cha kutafuta ukweli na usuluhishi wa madhambi yote yaliyofanyika.

Kabla sijazungumzia chombo hiki ambacho kiundwe kwa nguvu ya pamoja kati ya serikali kuu, mahakama na bunge (katu isiwe ya wateuliwa wa Rais pekee), ningependa nichambue tuhuma zenyewe za ufisadi na wahusika wake.

Mambo haya ya ufisadi yalianza kutangazwa na vyombo kadhaa vya mawasiliano na habari zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Kwa hakika wale waliokuwa wameeneza habari hizi walikuwa wamefanya kazi yao ya uchunguzi na walijua wanachokiongelea. Ikatokea kwamba viongozi wa vyama vya upinzani ndio waliozungumzia ufisadi huu kwa uwazi. Kati ya ufisadi uliozungumziwa ni wizi katika Benki Kuu, mikataba mibovu ya madini, uuzwaji holela na kinyume cha maadili wa makampuni, mikataba mibovu ya kampuni za uzalishaji umeme na mengineyo mengi. Kwa kifupi, ufisadi umepelekea kwa rasilimali za nchi kuibwa na wageni huku wakisaidiwa na viongozi wachache serikalini kwa manufaa yao binafsi.

Ufisadi huu (kama ufisadi mwingine wowote) ni mbaya sana na huna budi kukemewa. Kukemewa pekee sio suluhisho; inatakiwa wale wahusika wote, wakubwa na wadogo, wachukuliwe hatua za kisheria na urithi wa nchi yetu ukombolewe. Zaidi ya hapo, zichukuliwe hatua ili kuanika maovu yote yaliyotokea na kutafuta suluhisho la kudumu lenye kuzuia ufisadi huu kutokea tena. Watanzania wameporwa urithi wao, jasho letu limetutoka katika kujenga taifa letu, kodi tumetozwa kuendesha serikali yetu hivyo basi serikali inawajibika kutueleza kiunagaubaga ni kwa namna gani pesa zilivyoibiwa, ni nani alihusika, na hatima ya wahusika ni ipi. Hii ni haki ya kila Mtanzania ambayo serikali haiwezi kutunyima.

Tukirudi kwa suala la Ballali, nilitaja mwanzoni kuhusu kiini macho kilichotolewa na Rais na wasaidizi wake. Ripoti ya kampuni ya uhasibu ya Ernst and Young imewakilishwa kwa Rais lakini haijawekwa wazi kwa wananchi. Swali la kujiuliza ni kwanini kumekuwa na usiri wa ripoti hiyo? Kwanini ripoti hiyo isitolewe kwa wananchi ili nao waichambue na kutoa tathmini zao wenyewe? Wanataaluma, wanasheria, wafanyabiashara au hata wananchi tu wa kawaida, tungependa kuisoma hiyo ripoti ili tutoe tafsiri zetu wenyewe pia.

Kitu kingine kinachoonesha kutokuwajibika kwa serikali, ni kauli ya waziri wa fedha Mh. Meghji. Mama waziri ameliambia taifa kuwa alijulishwa na Katibu Mkuu wake Bw. Mgonja juu ya uongo wa Gavana Ballali ili waziri ahalalishe malipo. Imechukua zaidi ya mwaka mmoja kabla ya serikali kuchukua hatua yoyote ya nidhamu kwa Gavana. Hivi kweli Mh. Meghji aliwezaje kufanya kazi na Ballali na kumwamini angali akijua alikuwa amedanganywa? Kwa nini mheshimiwa waziri hakusema chochote kwenye kamati ya Bunge iliyoongozwa na Mh. Kigoda na iliyotoa ripoti safi ya BoT? Kwa mtaji huu, ni mangapi ambayo yanaendelea sasa hivi ambayo hayajaripotiwa na pengine hatutayajua mpaka Slaa au Zitto wayaseme mwakani?

Sihitaji kuwa mwanasayansi wa anga kujua kuwa Sh. 130 + bilioni ni nyingi. Kwenye dunia yangu, kiasi hiki cha pesa kingeleta maji na umeme kwenye vijiji vingi ambavyo mpaka sasa karibu miaka 50 ya uhuru, hivyo vitu vya msingi ni anasa. Kwa pesa hiyo, hata shule nilizosoma zingepata maji, mabweni yangeboreshwa na walimu wangelipwa vema. Kwa pesa hiyo, zahanati zingepata madawa zaidi, barabara zingejengwa, wakulima wangepata pembejeo na ruzuku kujiendeleza na kilimo chao, na watoto wengi zaidi wangekwenda shule na kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu kwani kungekuwa na walimu na vitabu.

Kulingana na taarifa hizi zilizotoka, binafsi sijaridhishwa na hatua ya Rais. Yeye kama mkuu wa nchi, ana mamlaka ya kufanya makubwa kuliko aliyoyafanya. Naamini Ballali hakuwa mwenyewe na washirika wake wakubwa bado wako serikalini au bado wanasaidia chama tawala kwa hali na mali. Wengine, imeamuliwa kuwa Rais atawastahi ili wastaafu kwa amani. Hii si haki kwetu sisi wananchi wa Tanzania,walipa kodi na wapiga kura. Magereza yamejaa watu ambao wamefanya wizi mdogo kulinganisha na mafisadi haya.

Tukizingatia ukweli wa kuwa Ballali hakuwa peke yake, kuna wasiwasi kuwa haki haitapatikana. Sababu inayonipelekea kuwa na fikra hii ni kutokana na ukweli kuwa wahusika ni wengi na wenye nafasi za juu serikalini na katika jamii. Hivyo basi, kufuatia mfano uliofanyika kwa ndugu zetu wa Afrika Kusini na Liberia ambapo wale waliofanya maasi ya ubaguzi na mauaji waliletwa mbele ya chombo cha amani, kweli na mapatano, ningependekeza nasi tufanye vivyo. Siasa iachwe pembeni, ukweli upatikane na haki ipatikane. Kwa mtaji huo, ningependekeza yafuatayo:

i) Chombo hiki kiwe cha huru chenye wataalam mbalimbali na wananchi wa kawaida
ii) Mahojiano yawe ya wazi, yatangazwe moja kwa moja kwa redio au televisheni
iii) Wahusika wote wafilisiwe mali walizozipata isivyo kihalali. Mali hizi ni pamoja na zile walizoziwekeza kwa wake/waume zao, washirika wa biashara, familia au marafiki
iv) Wahusika walio na pasi za kusafiria za nchi nyingine au wakiwa ni raia wa kuhamia wafukuzwe na mali zao kutaifishwa
v) Ikibainika kuwa taarifa walizotoa kwenye mahojiano haya ni za uongo au zisizo kamili, wapate kifungo bila ya uwezekano wa kupata msamaha
vi) Wahusika wasiruhusiwe, katika maisha yao yote, kuwa wajumbe wa bodi, mashirika na taasisi zozote za serikali na umma
vii) Wahusika wapelekwe kwenye mikoa yote bara na visiwani, kwa gharama zao wenyewe, ili wananchi wawaone na kuwahoji
viii) Kama kutakuwa na viongozi wastaafu wanaohusika, wanyang’anywe hadhi, marupurupu na kinga ambazo watakazokuwa nazo kwa nyadhifa walizokuwa nazo
ix) Wahusika watakaoonyesha ushirikiano wapewe ulinzi wa maisha yao na familia zao katika kipindi hiki, ikidhihirika kuwa watuhumiwa wengine wanawatishia
x) Serikali kuu, Bunge na Mahakama zitunze kumbukumbu hizi ziwe za kudumu ili iwe sehemu ya historia yetu kwa vizazi vijavyo

Japo wahenga walisema amani haiji bali kwa ncha ya upanga, lakini pia naamini kuwa kama tutakuwa na upeo mkubwa na kutaka suluhisho la kudumu, basi kuna njia nyingine zaidi ya ncha ya upanga. Cha msingi ni kwamba, ukweli uanikwe, Ballali alindwe wakati akitoa utetezi wake na kufichua mafisadi wengine na kama wako serikalini, basi wafukuzwe kazi mara moja. Pia, rasilimali ya nchi irudishwe kwenye mikono ya wananchi na Bunge liombe radhi wananchi kwa kushindwa kuwafichua mafisadi na badala yake kuwatetea mafisadi hawa.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania na watu wake!
 
Mpenda Merikebu:

Tukizingatia ukweli wa kuwa Ballali hakuwa peke yake, kuna wasiwasi kuwa haki haitapatikana. Sababu inayonipelekea kuwa na fikra hii ni kutokana na ukweli kuwa wahusika ni wengi na wenye nafasi za juu serikalini na katika jamii. Hivyo basi, kufuatia mfano uliofanyika kwa ndugu zetu wa Afrika Kusini na Liberia ambapo wale waliofanya maasi ya ubaguzi na mauaji waliletwa mbele ya chombo cha amani, kweli na mapatano, ningependekeza nasi tufanye vivyo. Siasa iachwe pembeni, ukweli upatikane na haki ipatikane. Kwa mtaji huo, ningependekeza yafuatayo:

Kwa kweli hii ni hoja nzito sana: Nimeamua tu kuchukua kifungu hicho kidogo ili kuanzisha gurudumu la huo mchakato. Kama kwa namna fulani hili likawezekana,itakuwa ni very serious NATIONAL REFORMATION ever taken place in our beutifull country Tanzania. Hili likitokea likakuwa jambo kubwa kuliko linavyoonekana kwenye maandishi haya. Mabadiliko ambayo yangetokea hapo kwa kweli yangekuwa ya kimsingi na ya kiutu. Yangekuwa ya kutuondoa kwenye makosa mengi mazito tangu taifa kuasisiwa...kabala sijaendelea...!

Labda nikuulize. Unafikiri litafikiwaje jambo kama hilo. Nani ataanza hicho kitakachokuwa cha kwanza kukianza, ambacho ni kipi? tafadhali hebu tukumbushe au tupe mwelekeo kwa nchi zilizowahi kupitia hili zoezi lilifanyika vipi?
 
3562108-8ca.gif
 
MV Mapenzi (Merikebu),

Naam, ni busara na hekima pekee ambazo zittawez sawazisha haya mambo. Mkondo wa kuleta mageuzi si lazima maneno makali na matusi yatumike. Ndio maana katika waraka wangu kwa Mh. Raisi Kikwete, ninamsihi azinduke na kulinda Utaifa na si Chama!

JC,

Habari hii yafanana sana na "Hoja ya Afya"! We need to change our thinking even in search for justice. We need to pe positive rather than negative. A positive influence is a thousand times better than a million negative forces!
 
JC,
Nashukuru kwa kuwa na mawazo endelevu kuhusu jambo hili. Kifupi, the Truth and Reconciliation Commission ilikuwa ni kama mahakama iliyoanzishwa na serikali ya Afrika Kusini ili kupata suluhisho la amani. Tume hii ilikuwa kama mahakama kwa vile ilikuwa na uwezo wa kumwita mtu (subpoena) kujibu tuhuma, kutoa adhabu, kupendekeza mafao n.k. Tume hii iliongozwa na Askofu Mkuu Desmond Tutu na iliendeshwa kwa namna ya watu kuja mbele ya tume hii kwa hiari na kupeleka malalamiko yao kwa jinsi walivyoona wameonewa, kudhulumiwa, kubaguliwa au kunyanyaswa kwa namna yoyote ile. Kwa ufafanuzi zaidi, angalia link hii http://www.doj.gov.za/trc/legal/act9534.htm yenye kutoa kifungu cha sheria ya kuanzisha tume hii na kazi yake

Kama ilivyo mambo mengi, huwezi kuwafurahisha watu wote. Kwa mfano, katika tume hii ya Askofu Tutu, kuna watu walioipuuzia kama vile Rais wa zamani wa nyakati za ubaguzi, Bw. P.W. Botha. Lakini pia kuna watu wengine waliona kuwa hii tume imewasitiri wale wenye madhambi...mfano mzuri ni familia ya mpigania ukombozi Steve Biko, ambao waliona kuwa kwa kutoa ukweli wa kilichompata Biko, walinyimwa haki na polisi waliomuua wameishia wakipeta.

Kwa upande wetu, tukumbuke kuwa tunachotaka ni kujenga kwani yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Hivyo changamoto ya wana JF ni hii: Je tukubali ukweli utuweke huru na kukubali kuwa na msamaha (wenye masharti) kwa wahusika, ili mradi rasilimali na fedha za taifa zinarudishwa na wahusika kufilisiwa? Najua ni jambo gumu kwani baadhi yetu wangependa kuona hawa mafisadi wanapelekwa Isanga, Karanga na Ukonga; lakini pia kuna hatari ya kutopata ukweli wa undani na baada ya maji kupoa (miaka michache ijayo), kutakuwa na skendo nyingine na hawa watu watakuwa wametoka jela na kwenda kutumbua maisha! Je tuko tayari?
 
Rev. Kishoka,

Nashukuru kwa uchangiaji wako wa mada hii. Ni kweli, hamaki, matusi na mud slinging hazimaanishi zitaleta matokeo yanayopendelewa. Waraka wako kwa Mh. Rais unayasema haya na natumaini Rais atasoma na kuelewa nyaraka zetu hizi kwenye JF.

Haya mapambano (ambayo si lazima yawe ya silaha au matusi) ndio kwanza yameanza. Vijana Jazz Band waliimba "Daima mbele, haturudi nyuma sisi vijana", vivo hivyo, JF itaendelea kusonga mbele na Inshallah Rabuka Mtukuka atatuongoza kwenye Dar es Salaam mpya!
 
Back
Top Bottom