Ufisadi TCRA

Kinto

Senior Member
Apr 22, 2008
109
12
Waungwana nimeisoma hii ikanipa shock, huu wimbo utaisha lini, sioni dalili ya kufikia hata kibwagizo, hebu check huu ubeti

Mabilioni ya TCRA yaibua utata bungeni

Mwandishi Wetu Juni 25, 2008

  • Ni za mahujaji, barabara ya Msata, Uwanja wa Ndege wa Mwanza
UTATA umeibuka serikalini kuhusu mabilioni ya fedha zilitolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) baada ya baadhi ya wabunge kuhoji zilivyotumika na sheria waliyotumia mawaziri kuagiza kutolewa kwa fedha hizo.

Habari zinaeleza kwamba Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POC) imejipanga kuhakiki matumizi ya fedha hizo zilizoelekezwa katika miradi ambayo haijafahamika kwa hakika kama imekwisha kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Habari zinaeleza kwamba TCRA ilitoa zaidi ya Sh bilioni 15 kwa maelekezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Miundombinu na Wizara ya Fedha, kwa ajili ya miradi mbalimbali ambayo haikuwa katika bajeti ya mamlaka hiyo.

Akichangia Bajeti ya Serikali wiki iliyopita, Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Susan Lyimo, alitaka maelezo kuhusu maagizo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu yalivyotumika kutoa fedha kutoka TCRA kwenda katika miradi ya barabara na uwanja wa ndege wa Mwanza, miradi ambayo haiko katika sekta ya mawasiliano. Lyimo ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.

TCRA imeelekezwa kutoa fedha hizo na viongozi wa juu wa serikali kwa kuwa mamlaka hiyo ni mali ya Serikali na fedha hizo ni za Serikali.

Viongozi wanaotajwa kushiriki vikao vya kuidhinisha na kuomba fedha hizo ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Mawaziri waliowahi kuongoza Wizara ya Miuondombinu, Andrew Chenge na Basil Mramba na aliyekuwa Naibu Waziri, Wizara ya Fedha, Abdisalaam Issa Khatib.

Miongoni mwa miradi iliyoombewa fedha kutoka TCRA ni mradi wa barabara ya Msata kwenda Bagamoyo kwa kiwango cha lami uliopatiwa Sh bilioni 7 kati ya Sh bilioni 10 zilizoombwa, mradi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza uliochotewa Sh bilioni 7.1 na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) waliopewa Dola za Marekani milioni 1 (Sh Bilioni 1.2).

Lowassa, Mramba na Abdisalaam walikutana na watendaji wakuu wa serikali akiwamo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Goodluck Ole Medeye, Machi 10, 2006 na kuelekeza mamlaka hiyo na idara nyingine kutoa fedha za haraka kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Msata hadi Bagamoyo.

"Kwa vile barabara kuu kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya kaskazini ni muhimu sana kwa uchumi, Waziri Mkuu ameelekeza kwamba barabara kutoka Msata kwenda Bagamoyo ipewe kipaumbele na iwekwe lami haraka iwezekanavyo kwa kutumia fedha za TCRA na vyombo vingine vya serikali ambavyo fedha zake zinaweza kutumika," ameeleza mtoa habari wetu akinukuu mawasiliano ndani ya Serikali.

Kwa mujibu wa mtoa habari huyo Serikali ilijenga hoja hiyo kipindi cha matatizo ya usafiri katika barabara iendayo mikoa ya kaskazini baada ya daraja la Lugoba wilayani Bagamoyo kuzolewa na mafuriko na Waziri Mkuu aliagiza utekelezaji wa mradi huo uliopangwa kugharimu Sh bilioni 35, uanze mara moja.

Hata hivyo, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POC) chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Mbunge wa Mbarali (CCM), Esterina Kilasi, ilishitushwa na maelezo ya TCRA walipokutana na menejimenti ya mamlaka hiyo Dar es Salaam hivi karibuni baada ya kuwa na wasiwasi kama kweli fedha zilizotolewa zimefanya kazi iliyokusudiwa.

Habari kutoka serikalini zinaeleza kwamba tayari TCRA wamekwisha kutoa maelezo ya jinsi walivyoshinikizwa kutoa fedha hizo wakiegemea kifungu cha 56 cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ya mwaka 2003, inayompa Waziri mhusika kuingilia utendaji wa mamlaka hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya maofisa wa Serikali wamepinga tafsiri ya sheria hiyo wakieleza kwamba Waziri mhusika ama kiongozi yeyote hana mamlaka ya kuingilia mambo ya fedha ya mamlaka hiyo bali anachoruhusiwa ni kusimamia mambo ya kisera zaidi na kutoa ushauri wa kiutawala na masuala mengine pale tu panapotokea utata mambo ambayo hayakutokea.

Kuhusu mradi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, habari zinaeleza kwamba mwishoni mwa Desemba 2006, Wizara ya Miundombinu chini ya Chenge iliialiagiza TCRA kutoa Sh 7,130,000,000/- kukarabati uwanja wa ndege wa Mwanza kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Uganda.

Kutokana na msukumo kutoka serikalini, TCRA ililazimika kukopa benki ya Stanbic kuweza kutoa fedha za awali zilizotakiwa kwa haraka kutoa malipo ya awali ambayo kuna habari kwamba fedha zake zilitumwa nje ya nchi zikielezwa kutumika kumlipa mkandarasi wa uwanja huo ambao sasa utalazimika kufanyiwa ukaguzi kuona kama fedha zilizotolewa zilitumika kwa kazi iliyokusudiwa.

Habari zinaeleza kwamba Kamati ya POC imepanga kufanya ukaguzi maalumu kutembelea miradi iliyopewa fedha na TCRA ili kujiridhisha kama fedha zilizotolewa zimefanya kazi iliyokusudiwa, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo baada ya kukutana na watendaji wa mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Dodoma.

Gharama za Uwanja wa Ndege wa Mwanza uliopangwa kukamilika Novemba 2007, zilielezwa kuwa ni Sh bilioni 8.2 ikiwa ni pamoja na gharama za mkandarasi (Sh bilioni 7.7) na msimamizi mkuu aliyepangiwa kulipwa Sh 501,879,531.

Kwa mujibu wa habari hizo, TCRA iliagizwa tena na serikali kupitia Wizara ya Miundombinu kutoa dola za Marekani milioni moja (Takriban Sh bilioni 1.2), kwa ajili ya kugharamia safari ya mahujaji wa Tanzania na nchi nyingine waliokwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kutokana na matatizo ya kiutendaji ndani ya ATCL.

Fedha hizo zilizoingizwa katika akaunti ya ATCL zilielezwa kugharamia mahujaji hao kwa ajili ya kulipia mafuta ya ndege; uongozaji na paking ya ndege; huduma za vyakula na malazi kwa wahudumu wa ndege; na huduma za uwanja wa ndege Dar es Salaam na Jeddah.

Hata hivyo, tofauti ya fedha nyingine fedha zilizotolewa kwa mahujaji zilielezwa kwamba zingelipwa serikali katika kipindi ambacho hakijaelezwa kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Enos Bukuku.

Habari zinaeleza kwamba TCRA ililalamika kukwama kutekeleza miradi yake muhimu inayolenga kuboresha utendaji wake kama mamlaka nyeti kutokana na kulazimika kuchangia miradi iliyo nje ya majukumu yake katika sekta ya mawasiliano lakini serikali iliendelea kulazimisha kuchota.

TCRA ilielezwa kutoa ahadi ya kuchangia Sh bilioni 27.54 kwa ajili ya 'ujenzi wa makao makuu' uliotajwa kugharimu Sh bilioni 30.6 lakini inaelezwa kwamba hadi sasa mamlaka hiyo imetoa chini ya Sh bilioni 10 hadi Mei mwaka huu kutokana na majukumu mengine yanayoikabili ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mitambo ya kusimamia masafa.

Hii ni mara ya kwanza kuibuliwa kwa siri ya utolewaji wa fedha kutoka asasi mbalimbali pamoja na kuwapo taarifa kwamba asasi nyingi za serikali na umma pamoja na makampuni binafsi yamekua yakichangia kwa hiari ama kushinikizwa na serikali ama wanasiasa kuchangia miradi ama shughuli mbalimbali.
 
Ufisadi mwingine halafu kumbe nimegundua bongo kuna pesa yaani mabilioni yanatoka kila sehemu. Halafu nimeona Chenge pia. Unategemea nini?
 
+
ni chenge, lowassa na mgonja. interesting..
Hapo umemaliza mkuu, haiwezekani kiongozi wa nchi kama Lowassa/Chenge/Mgonja hata Yona wawe matajiri hivi hivi na kusingizia sijuwi ng'ombe au mashamba!
Lazima wawe wanaiba serikalini tu, hela za mlipa kodi, hela za wale 95% walio vijijini...
 
Ndo anataka kila mtu awe tajiri yeye anauchukia umaskin yaan kila mtu aibe ili awe tajiri halafu asingizie mifugo
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom