ufisadi ni wito wa kuwa mwaminifu ili ukomboe taifa na watu wake. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

ufisadi ni wito wa kuwa mwaminifu ili ukomboe taifa na watu wake.

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Shayu, Nov 19, 2011.

 1. Shayu

  Shayu Platinum Member

  #1
  Nov 19, 2011
  Joined: May 24, 2011
  Messages: 506
  Likes Received: 720
  Trophy Points: 180
  Kwanza ningependa kumshukuru mungu muumba kunipa nafasi hii ya kuandika waraka huu kwenu ndugu zangu. Namuomba anielekeze fikra nilizonazo zitoke kama ninavyokusudia kutoka kichwani kwangu na kuwafikia ndugu zangu kwa faida ya taifa letu. Aniongoze niendelee kutafakari kuhusu uhuru, uzalendo na mwelekeo wa taifa letu. Mimi kila wakati ninaamini tuna uwezo wa kuwa kama taifa lolote lile duniani. Ni jitihada zetu na umoja wetu ndio utakaotufikisha huko.

  Nimekuwa nikitafakari kuhusu uwepo wa mataifa na tawala mbalimbali duniani na asili zake. Kama ilivyokuwa kwetu kabla ya kuja kwa mjerumani hatukuwa na Tanganyika. Tulikuwa na makabila tu mbalimbali yaliyokuwa yanajitawala yenyewe. Ukoloni ndio uliotuleta pamoja, ndio uliotukusanya.

  Mwaka wa 45 baada ya kifo cha yesu kristo uingereza ilikuwa kama taifa letu. maskini wa kutupwa. walikuwa wanaishi kwenye nyumba za udongo na kulikuwa na makabila mbalimbali hawakuwa taifa kama sasa. Wamekuwa taifa baada ya warumi kuwavamia na kuwatawala. Warumi walikuwa wameendelea sana kitechnologia, silaha zao zilikuwa bora zaidi ya waingereza na walikuwa na elimu zaidi ya waingereza.

  Baada ya kutawaliwa na warumi walijua usalama wao utakuwepo tu pale watakapojishughulisha katika kutafuta maarifa na uvumbuzi. Ni ukweli usiopingika kwamba taifa lolote lililoendelea kitechnologia ndilo taifa ambalo lina nafasi kubwa ya kutawala mataifa mengine.

  Nina waelezea historia hii nataka kuonyesha kwamba hakuna kitu ambacho kinashindikana tukiamua kama taifa. kama tukiwa na jitihada za pamoja kubadilisha hii hali tuliyonayo sasa hivi na kuliletea taifa letu heshima.

  Inahitaji uzalendo na mapenzi kwa taifa letu kubadilisha hali hii.

  Serikali lazima iwe na agenda ya kuleta mapinduzi kwa watu wake. Ili tuondokane na hali hii. Ili tujenge heshima kwa taifa letu. Bunge, serikali na mahakama lazima vifanye kazi kwa pamoja ili kuleta mapinduzi. Mahakama lazima itende haki ili watu wetu waendelee kuwa wamoja. Wananchi lazima watii sheria kwa moyo wao wote na wajishughulishe katika ujenzi wa taifa lao wenyewe kwa kufanya kazi kwa bidii na kujitolea katika masuala yahusianayo na Taifa. Watumishi wa umma wajue wapo pale kutumikia umma na si vinginevyo na wafanye hivyo kwa dhati kabisa. Hatutaweza kujenga umoja wetu kama hatutatendeana haki kati yetu. Wabunge lazima waishi majimboni kwao. wayaelewe vizuri majimbo yao na kuwawakilisha vyema waliowatuma. Tutaendelea ikiwa vyombo hivi vitafanya kazi kizalendo na ufanisi mkubwa.Kama vyombo hivi havifanyi kazi ipasavyo kwa uzalendo na kwa kujitolea hatutafika popote.

  Watu wetu lazima wajue agenda ya taifa letu ni nini? Tuhakikishe akili za watu wetu ziko huko. Nchi yetu imekuwa haina agenda imekuwa nchi ya matukio hatuwezi kuendelea namna hiyo agenda za taifa lazima zimee mioyoni na akilini mwa watu wake. hii inahitaji umoja na uzalendo wa watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama. Shuleni na vyuoni lazima wajue ajenda na dira ya taifa lao ni nini. Na wajitolee kwa dhati kabisa kufanikisha dira hiyo huu ni wito wa kizalendo wa kuamsha hisia za watu kuhusu utaifa na dira na mwelekeo wetu kwa pamoja.

  Bunge letu limekuwa likibadilisha agenda na watu wa taifa hili hatujui agenda ya taifa letu ni nini. Tunakosa mwelekeo, tunabaki kuwa mashabiki. Lazima tuwe na agenda kama taifa na ni lazima zizame akilini na mioyoni mwa watu wetu kama tunataka kufanya mapinduzi katika taifa hili.

  Tunaweza kufanya mapinduzi makubwa katika uvumbuzi na katika mambo mengine mengi tu. Ni utayari wetu, umoja wetu na kujitolea kwetu kutakako tufikisha huko. Bado naamini na nitaendelea kuamini maisha yangu yote tuna uwezo wa kuwa taifa kubwa duniani. Ni kujipanga kwetu tu sisi na familia zetu na makabila yote tuamue kupambana na kutengeneza jina letu duniani. Hii inawezekana kabisa. Kama tutaweka taratibu katika vyama vyetu vya kisiasa ambazo zitazingatia maslahi ya taifa kwanza na watu wake.

  Naongea haya wakati nchi yetu ikiwa na mgawanyiko mkubwa uliotokana na ubinafsi na ufisadi. Watu wetu wamegawanyika. Hakuna tumaini katika taifa. Uzalendo umepungua. Ni wakati wetu kuzungumza matatizo yanayotukabili kama taifa kama watu wenye akili na busara ili tusiligawae Taifa letu.

  Tutafakari upya kuhusu mwelekeo wetu kwa pamoja. Vijana na wazee wa taifa hili, wapi tumekosea. Tujue chimbuko la ufisadi na ubinafsi. Tuangalie upya malezi katika familia zetu na mahusiano yetu kama watu tunaoishi taifa moja. Mimi naamini kuna sehemu tumekosea.

  Umaskini wa taifa hili unatokana na maadili na watu wetu kutokuwa na discipline, uzalendo na uwajibikaji kwa taifa letu wenyewe na kukosa vipaumbele kama taifa na kutokuwa wamoja kwetu katika malengo.

  Tuwafundishe watoto wetu kuhusu umuhimu wa taifa hili walipende na walitumikie tukijua kwamba hatuna ardhi nyingine zaidi ya hii ya Tanzania. Tulinde maliasili zetu na vitu vingine ambavyo ni vya pamoja kama taifa.


  Wito wangu kwenu tuangalie maneno yanayotoka midomoni mwetu kama yanajenga au kubomoa taifa letu. Tutahukumiwa Vinywa vyetu. Tutaitwa wazalendo au wasaliti kwa vinywa vyetu pia. Matendo yetu na yaonyeshe uzalendo wetu kwa taifa. kwa kujitolea kwa nafsi kwa ajili ya watu wengine.

  Mimi nimezaliwa katika taifa hili. Siijui nchi nyingine zaidi ya ardhi hii. Nimekula matunda na chakula kinachotokana na ardhi hii. Nimekula nyama na maziwa ya mifugo inayokula nyasi zilizoota katika ardhi hii. Mimi ni mwana wa taifa hili. limenikuza na kunilea. Sitakubali yeyote avuruge amani na umoja wetu kama taifa.

  Imani yangu ni siku moja taifa hili litanyanyuka kutoka hapa lilipo na kuwa taifa kubwa. Watu wenye busara hujenga taifa lao kwa umoja na mashirikiano wajinga hulibomoa taifa lao kwa ubinafsi.

  Taifa hili la Tanzania likisambaratika tutakuwa kielelezo cha ujinga na upumbavu. Tunaweza kukaa chini na kujadili mambo yetu kama binadamu. Ndugu zangu tutakapovunja umoja wetu na mapenzi yetu kama watu wa taifa moja tumevunja nchi. hatutaepuka kupigana. Kama unalipenda taifa hii utampenda raia mwenzako na utalitumikia taifa hili kwa uaminifu. Nchi hii tutaiharibu wenyewe kwa ujinga wetu na tutaijenga kwa maarifa na busara zetu.

  Tamaa hazitatujenga kama taifa. Hatuwezi kuendelea kama taifa ikiwa kila mmoja atajiangalia mwenyewe, ikiwa kila mmoja atatafuta umaarufu wake mwenyewe au utukufu wake mwenyewe na sio utaukufu wa taifa. Kuna mataifa wanalitamani sana taifa letu. Tusichezee stability ya nchi yetu. Tutakapokuwa sio wamoja nchi yetu itakapokuwa sio stable hata mataifa dhaifu yataingia nchini kwetu na kuiba maliasili na kubaka dada zetu.


  Ufisadi umekuwa kero masikioni mwetu kila mtu haupendi. kila mtu anauchukia. Hii ni dalili ya kuporomoka kwa maadili na uzalendo katika taifa letu. Ni wajibu kwa kila mzalendo kwanza kuwajibika yeye binafsi kwa kuwa mazalendo na mwaminifu lakini pili kuongea madhara ya ufisadi katika jamii na kupambana nao. Hatutaweza kuushinda ufisadi wala rushwa pasipo kuelimisha jamii na kubadilika sisi wenyewe tunaochukia ufisadi. Tuongee ukweli kuhusu taifa letu bila ushabiki. Tufanye harakati la kujenga taifa hili liwe imara na madhubuti hatujawa taifa ili tuondoe umaskini tuu. Tumekuwa taifa ili tutawale na tujenge heshima yetu mbele ya mataifa mengine katika kila nyanja hilo ndilo tumaini langu ya kwamba kila mtu ajitolee katika kila field aliyopo ili kuliletea sifa taifa hili.
   
 2. Shayu

  Shayu Platinum Member

  #2
  Nov 17, 2012
  Joined: May 24, 2011
  Messages: 506
  Likes Received: 720
  Trophy Points: 180
  Tafakari kuhusu huu ujumbe kwa kina. Nimeamua niurudie.
   
Loading...