Ufisadi mpya waibuka; Vigogo waingia ubia na gereji bubu mtaani kuchota mamilioni

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797


Mwandishi Wetu

Toleo la 271
5 Dec 2012
​


  • Vigogo waingia ubia na gereji bubu mtaani kuchota mamilioni


LICHA ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuripoti kuhusu ufisadi unaofanyika kupitia matengenezo ya magari ya Serikali, sheria zimeendelea kuvunjwa, baadhi ya vigogo wanaomiliki baadhi ya gereji za mitaani wamekuwa wakijichotea mamilioni kifisadi, kupitia matengenezo hayo, Raia Mwema, limeelezwa.

Kwa mujibu wa mwongozo wa matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya Serikali, jukumu la kusimamia matengenezo hayo limewekwa kisheria chini ya Wizara ya Ujenzi, kupitia kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).


Katika utekelezaji wa majukumu yake, TEMESA kupitia karakarana yake, hupaswa kukagua na kuidhinisha matengenezo ya magari ya Serikali, na hata kuruhusu magari hayo kwenda kutengenezwa katika gereji binafsi, lakini imebainika hilo halifanyiki kwa sasa.


Vyanzo vyetu vya habari kutoka TEMESA na baadhi ya madereva wa magari ya Serikali vinadokeza kwamba magari mengi yamekuwa yakipelekwa katika gereji za mitaani kinyemela, bila kibali cha TEMESA, sambamba na ukiukwaji wa taratibu nyingine.


Baadhi ya taratibu nyingine zinazokiukwa kwa lengo la kujichotea mamilioni ya fedha katika matengenezo ya magari ya Serikali ni namna ya kuteua gereji za mitaani.


Mwongozo wa matengenezo ya magari ya Serikali unaelekeza: "Karakana (gereji) teule zitapatikana kwa mujibu wa sheria ya ununuzi wa umma." Kwa maana ya utaratibu wa zabuni itakayosimamiwa na TEMESA.


Hata hivyo, taarifa kutoka TEMESA zinaeleza kuwa mwongozo huo umekuwa ukikiukwa na baadhi ya maofisa waandamizi wa Serikali, wanaotajwa kuwa na ubia na baadhi ya gereji zinazopewa kazi ya kutengeneza magari ya umma.


Mbali na hayo, mchakato wa malipo kwa gereji hizo za binafsi umekuwa, kwa sehemu kubwa, ni wa kuvunja taratibu.


Mwongozo unaelekeza kwamba malipo ya matengenezo kutoka idara au wizara, lazima yathibitishwe na TEMESA, lakini utekelezaji wa matakwa hayo ni kitendawili.


Kipengele hicho kinachotaka malipo yahakikiwe na TEMESA kwanza, kimekuwa kikikukwa na baadhi ya vigogo, ikidaiwa wamekuwa wakifanya malipo makubwa ili kujipatia fedha ya ziada, jambo ambalo lisingewezekana kama TEMESA ingehusishwa moja kwa moja.


Raia Mwema limeelezwa kwamba idadi kubwa ya gereji zinazotumika kufanikisha wizi huo kupitia matengenezo ya magari ya Serikali ni gereji bubu, zisizosajiliwa rasmi kwa kazi hiyo jambo ambalo pia ni kinyume cha sheria.


Baadhi ya madereva wa viongozi wa kitaifa waliozungumza na mwandishi wetu kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini, wamekiri wakati mwingine kupeleka magari hayo kwenye gereji binafsi mitaani bila kufuata taratibu za kiserikali.


"Kuna hujuma zinafanywa dhidi ya karakana ya TEMESA ili iendelee kutokuwa na uwezo kutengeneza magari ya Serikali. Wapo viongozi wameanzisha gereji mitaani na wengine wameingia ubia maalumu na wamiliki wa gereji hizo," anasema dereva wa mmoja wa makatibu wakuu katika moja ya wizara nchini.


Anaongeza: "Magari yaliyopo chini ya usimamizi wake (TEMESA) yanapelekwa gereji hizo kwa matengenezo na malipo yanafanyika kwa kiwango cha juu zaidi ili fedha za ziada wagawane.


"Kwa hiyo mhusika anakuwa amepata fedha ya ziada kutokana na malipo makubwa yaliyofanywa. Pili, anakuwa amepata faida kupitia ubia wake na mmiliki wa gereji, kwa sababu gereji hiyo inajiendesha kibiashara."


Maelezo ya dereva huyo yanaungwa mkono na mmoja wa Mameneja wa Karakana ya M.T Deport (jina linahifadhiwa) ambaye anakiri kwamba kwa muda mrefu, Serikali imekuwa ikipoteza kiwango kikubwa cha fedha kwa uzembe wa watu wachache wenye kujali maslahi yao.


"Hii ndiyo karakana kuu ya serikali (Motor Transport Deport) iliyoanzishwa mwaka 1947, imechoka kiasi cha kutia aibu na huenda ndiyo maana magari mengi ya Serikali yanatengenezwa kwenye gereji za uraiani bila ya hata kufuata taratibu husika," anasema Meneja huyo na kuongeza: "Ushiriki wa gereji teule za binafsi katika matengenezo ya magari una taratibu zake, si kila gereji inao uwezo huo.


"Kabla ya kupewa kazi, karakana inahakikiwa kama imejitosheleza katika vifaa na wataalamu waliobobea katika ufundi wa magari. Karakana teule zinapatikana kwa njia ya zabuni inayosimamiwa na TEMESA. Lakini hili limekuwa halifanyiki."


Ubia wa vigogo

Kuhusu tuhuma kwamba baadhi ya gereji zinamilikiwa au kuwamo katka ubia na baadhi ya viongozi wa Serikali, Meneja huyo anakiri kufahamu jambo hilo.
"Hilo lipo na ndiyo maana baadhi hawataki gereji ya Serikali kujengewa uwezo zaidi kwa upande wa vifaa na watalaamu kwa sababu wanajua gereji zao zitakufa huko mitaani," anasema.

Meneja huyo aliungwa mkono na mtumishi mwenzake katika karakana hiyo aliyemgeukia mwandishi wetu na kumwambia: "Tumekuwa tukilalamika karakarana ya Serikali kutelekezwa, hatupati mahitaji kwa kiwango cha kuridhisha. Jiulize;

Serikali wamekuwa wapesi katika kununua magari, tena ya kisasa kabisa, lakini hawataki kuboresha gereji ya uangalizi wa magari yao. Majibu unayo wewe mwenyewe, ni ufisadi mtupu. Watu wamejitengenezea gereji zao mitaani."


Juhudi za kumpata Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli hazikuweza kuzaa matunda kutokana na kuwapo katika shughuli za kikazi nje ya ofisi yake. Magufuli pia hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya mkononi.


Ripoti ya CAG

Katika ripoti ya CAG kuhusu ukaguzi kwa kipindi kilichoishia Machi 31, mwaka huu, suala la matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya Serikali lilijitokeza.

Uchunguzi wa CAG ulihusu pamoja na mambo mengine, idadi vyombo vya moto vya Serikali ambavyo ni zaidi ya 200 pamoja na matengenezo yake.


Ilibainika kwamba kati ya magari na pikipiki 65,252 zilizosajiliwa, hakuna kumbukumbu kamili inayoonyesha ni magari yapi yanafanya kazi na ni yapi bado yanamilikiwa na Serikali.


"Wizara ya Ujenzi, kama wizara husika katika usimamizi wa magari ya Serikali, haijaweka mfumo bora wa kusimamia matengenezo ya magari ya Serikali. Hakuna sera ya matengenezo ya magari ya Serikali. Kuna upungufu wa miongozo juu ya usimamizi wa matengenezo ya magari ya Serikali," inadokeza ripoti hiyo.


Inaendelea kueleza: "Uteuzi wa gereji binafsi kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa magari yanayomilikiwa na Serikali, umekuwa ukichelewa kila mwaka na mara nyingi TEMESA imekuwa haihusishwi kwenye mchakato mzima.


"Utendaji wa gereji na karakana binafsi, haufuatiliwi kwa kiasi cha kutosha. TEMESA haina utaratibu wala mipango, katika mpango wake wa kila mwaka wa jinsi gani itafuatilia utendaji wa gereji binafsi.


"Karakana za TEMESA zilizopo Dar es Salaam (MT Depot na Vingunguti) vifaa vyake vingi ni chakavu ama havifanyi kazi. Vifaa muhimu kwa shughuli za karakana vipo kwenye hali mbaya."


Wizara, Idara kuhujumu TEMESA

Ripoti ya CAG ilieleza kuwa licha ya TEMESA kutoa huduma ya matengenezo ya magari ya taasisi na idara za Serikali, idara hizo zimekuwa hazilipii huduma hiyo.

"Deni la matengenezo ya magari TEMESA limefikia Shilingi za Tanzania bilioni 3.9 hadi Desemba 2010. Wizara ya Ujenzi haijaweka mfumo sahihi wa kusimamia matengenezo ya magari ya serikali."











 
mfumo ambao hauna check and balance unaruhusu ubadhirifu kila kona kwa sababu hakuna mtu wa kuangalia kinachotokea na hata kama yupo hakuna mtu anayemwangalia mtazamaji kama anafanya kazi kweli kama inavyotakiwa na kama hafanyi kazi hakuna mwajibishaji na kama yupo hakuna wakumungalia mwajibishaji kama anafanya kazi yake.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom