Ufisadi mpya kuitikisa Dar! Ni wa bilioni 600/= upanuzi wa Bandari

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Mwandishi Wetu Raia Mwema


bandari216.jpg



Bandari ya Dar es Salaam


Ni wa bilioni 600/= upanuzi wa Bandari


MRADI mkubwa wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, unaotarajiwa kugharimu takriban Sh. bilioni 600, umeingia dosari ikidaiwa kwamba tayari wakubwa serikalini, akiwamo mmoja wa mawaziri, wameanza mipango ya kifisadi itakayochelewesha mradi huo kuanza, Raia Mwema limeelezwa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, katika mipango yao, vigogo kadhaa wamepanga kutafuta kampuni itakayoendesha shughuli za ujenzi bandarini kinyume cha makubaliano ya awali, hali inayoashiria kuweza kuchelewa kuanza kwa mradi husika.

Taarifa kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), zimeeleza kwamba Serikali ya China, kupitia Benki ya Exim ya nchini humo, imekubali kutoa fedha za upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam lakini kumekuwa na vikwazo kadhaa kutoka baadhi ya vigogo hao wa Serikali, wakilenga kujinufaisha na mchakato huo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Waziri mmoja (jina linahifadhiwa kutokana na kutopatikana kwa sasa kujibu tuhuma) amefunga safari hadi China kutafuta mwekezaji "atakayempendeza" ambaye atafanya kazi ya upanuzi wa bandari hiyo eneo la gati namba 13 na namba 14, karibu na gati la mafuta (KOJ).


Uamuzi wa waziri huyo kutafuta kampuni itakayofanya shughuli za upanuzi bandarini, unatajwa kuingilia uamuzi uliofikiwa wa kutoa jukumu hilo kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambayo ndiyo iliyopewa fedha kutoka China, na ambayo ndiyo yenye majukumu ya kupata kampuni husika ya ujenzi.


Kwa mujibu wa habari hizo, awali Waziri huyo katika juhudi zake za ‘kujitafutia' ulaji alikuwa akifanya mawasiliano na kampuni moja ya Falme za Kiarabu (UAE),
ambayo nayo imeelezwa kuwa na uhusiano mkubwa na wanasiasa kadhaa nchini.


Hata hivyo, aliahirisha juhudi zake hizo za Falme za Kiarabu baada ya kuzingatia
ukweli kwamba fedha zinazogharimia shughuli hizo ni kutoka China na kwa hiyo, ni busara kwake kutafuta kampuni ya kichina, ili kupunguza kile kinachoelezwa kuwa ‘kelele' za wadau.

"Waziri huyo baada ya kuona ukubwa wa mradi, ameamua kuingilia majukumu ya Bandari kuhusu kazi hizi, anatafuta kampuni ambayo ndiyo itafanya shughuli za upanuzi. Kwa hiyo Bandari itabaki mtazamaji tu, huyo Waziri anataraji maslahi yake yataingizwa kwenye hiyo kampuni atakayoipa kazi.

"Mwanzo akishirikiana na baadhi ya wanasiasa nchini alitafuta kampuni kutoka Falme za Kiarabu lakini wenzake wakamwambia, tutafute kampuni ya China kwa sababu fedha (mkopo) zimetoka huko China, tukitafuta kampuni isiyo ya China kelele zitakuwa nyingi," kinaeleza chanzo chetu cha habari.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Benki ya Exim ya China kwa maelekezo ya Serikali ya nchi hiyo, imekubali kutoa fedha hizo kwa TPA inayomilikiwa na Serikali ya Tanzania, kwa njia ya mkopo wa muda mrefu na wenye masharti nafuu ya riba ya asilimia mbili tu, lakini kwa masharti kuwa kampuni ya ujenzi ya China ndiyo itakayojenga mradi huo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Serikali ya Tanzania kupitia kwa Wizara ya Fedha, ilikwisha kutoa hati ya dhamana kwa ajili ya mradi huo ambao ulianza kuasisiwa mwaka 2008, wakati huo, Dk. Shukuru Kawambwa akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi.


Raia Mwema
ilifanya mawasiliano na Waziri huyo bila mafanikio. Hata hivyo, kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Waziri wa Uchukuzi, Omari Chambo, naye hakupatikana kueleza kuhusu masuala hayo.


Hata hivyo, gazeti hili lilifanikiwa kumpata Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraem Mgawe, na kueleza kuwa, hana taarifa za kigogo yeyote kuingilia mchakato huo.

Alisema mradi huo ni moja ya miradi muhimu kwao na kwamba inapewa kipaumbele cha juu, lakini bado hawajapata fedha walizoomba serikalini.

Alikanusha kuwa tayari wamepata fedha kutoka Benki ya Exim ya China na badala yake anasema walichopata ni barua kutoka serikalini ambayo itawawezesha kupata fedha.


Kuhusu kuwapo kwa vigogo serikalini na wanasisa wanaokwamisha, Mgawe alisema hana taarifa hizo kwa kuwa wako katika mchakato wa kuanza kwa mradi.


Mradi huo uliorodheshwa katika miradi muhimu ya TPA mwaka 2008 ukiwa na gharama za Dola za Marekani milioni 525, ambazo zitawezesha kupanuliwa kwa Bandari ya Dar es Salaam ili kuweza kushindana na Bandari ya Mombasa, nchini Kenya

Kumekuwa na madai kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi wakiwamo wamiliki wa kampuni za meli, mawakala na hata watumishi wa umma kwamba, matatizo makubwa katika sekta ya bandari yanatokana na ukiritimba uliopo kwa Kitengo cha Makontena ambacho kinaendeshwa na Kampuni binafsi ya Tanzania International Container Terminal Services Limited (TICTS).


Madai hayo pamoja na mengine ndiyo yameisukuma Serikali kuanza mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo inategemewa na nchi kadhaa kupokea mizigo yao, zikiwamo nchi za Rwanda, Burundi na Kongo (DRC).


TICTS ambayo iliingia nchini katika mazingira tata, imekuwa katika migogoro ya mara kwa mara na wadau na hasa wafanyakazi wake kutokana na kile kinachoelezwa ya kwamba kuna mkono wa wanasiasa wachafu, ambao wamekuwa wakiendelea kuyumbisha sekta ya uchukuzi nchini.


Katika eneo hili la Afrika Mashariki, taarifa zinasema, ni Tanzania pekee, katika hatua inayotafsiriwa kuwa ya kujinyima mapato, ndiyo imekabidhi uendeshaji wa biashara kubwa ya kupakia na kupakua mizigo bandarini kwa kampuni binafsi.








 
Taarifa hizi ni sahihi na itakapofika wakati tutamwaga kila kitu hapa hadharani, ni kweli waziri anahangaika kwa sasa namna ya kuingiza maslahi yake binafisi katika mradi huu. Tunamfuatilia.wana jf tulieni mambo yatamwagwa hapa hadharani kwa wakati muafaka. Sikuu njema kama hatutaonana humu tena!!!!
 


Kwa mujibu wa habari hizo, awali Waziri huyo katika juhudi zake za ‘kujitafutia’ ulaji alikuwa akifanya mawasiliano na kampuni moja ya Falme za Kiarabu (UAE), ambayo nayo imeelezwa kuwa na uhusiano mkubwa na wanasiasa kadhaa nchini


Hapa naona kuna harufu ya akina Al-Adawi wa Richmondi (Dowans)

 
Back
Top Bottom