Ufisadi Chuo Kikuu Mkwawa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ufisadi Chuo Kikuu Mkwawa

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Feb 12, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Feb 12, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  UONGOZI wa Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa(Muce), unakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali chuoni hapo.

  Ufisadi huo unaodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa chuo hicho ni pamoja na wizi wa fedha za chuo kupitia mikataba ya zabuni, upendeleo, kujilipa mishahara mara mbili pamoja na kuendesha akaunti za benki za muda maalum(Fixed Deposit), kwa kutumia fedha za Serikali, au za wafadhili na hivyo kuchelewesha malipo mbalimbali ya watoa huduma na kwa wanafunzi.

  Uongozi wa chuo hicho umethibitisha baadhi ya madai na kuyakanusha vikali mengine, huku ukidai kuwa hizo ni njama za baadhi ya watu, au wafanyakazi wanaotaka kuchafua taswira ya taasisi hiyo ya elimu ya juu.

  Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa kuna wafanyakazi watatu(majina yao tunayo), wa chuo hicho ambao wamekuwa wakijilipa mishahara mara mbili.

  Nyaraka kadhaa ambazo Mwananchi imeziona zinaonesha kuwa mfanyakazi wa kitengo cha computer chuoni hapo (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye ngazi ya mshahara wake ni kati ya Sh318,620 na 339,860 kwa mwezi kwa kupendelewa amekuwa akilipwa mshahara wa Sh750,000 kwa mwezi tangu Agosti 2006 alipoajiriwa.

  Kwa mujibu wa taarifa za kiuchunguzi, mtumishi huyo alipangiwa kiwango hicho cha mshahara na wakubwa wake wakimwambia kwamba mshahara huo "ni kwa ajili yake tu", kauli mbayo haikuwa na maelezo ya kuridhisha.

  Mwingine ambaye alikuwa akifanya kazi katika ofisi ya uhasibu (pia jina tunalo), ambaye mshahara wake unapaswa kuwa Sh622,578 kwa mwezi, amekuwa akijilipa au kulipwa mshahara huo pamoja na mshahara mwingine wa Sh700,000 kila mwezi.

  Mfanyakazi huyo hulipwa mishahara hiyo kwa ustadi mkubwa kwa kupitia akaunti za chuo hicho za benki mbili tofauti ambazo ni CRDB tawi la Iringa na NBC tawi la mjini humo, japokuwa hikufahamika mara moja ni benki gani kati ya hizo hutumika kumlipa mshahara wenye utata.

  Kadhalika uchunguzi unaonyesha kuwa mfanyakazi wa tatu ambaye tayari amekwishaacha kazi katika chuo hicho (jina lake pia tunalihifhadhi), licha ya kwamba mshahara wake ulikuwa wa Sh911,060 alikuwa akichota mshahara mwingine wa Sh507,590/- kupitia akaunti za chuo hicho za CRDB na NBC.

  Taarifa kutoka Muce zinadai kwamba hivi sasa wafanyakazi wote watatu wanaotuhumiwa kujipatia fedha kwa kujilipa au kulipwa mishahara miwili kila mwezi hawapo chuoni hapo kutokana na sababu mbalimbali.

  Mmoja wa watuhumiwa hao inadaiwa yuko mkoani Tanga ambako amekwenda likizo, wakati mwingine anadaiwa kuacha kazi ghafla, kitendo kinachotafsiriwa kuwa anakimbia mkono wa sheria baada ya kuvuja kwa taarifa zinazomuhusisha na ufisadi huo. Mtuhumiwa wa tatu inadaiwa kuwa yuko rumande ambako anashikiliwa na polisi wa jijini Dar es Salaam akikabiliwa na kesi nyingine.

  Akizungumzia madai ya watumishi hao kulipwa mishahara mara mbili, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Phillemon Mushi alikiri kufanyika kwa ufisadi huo lakini akasema tayari hatua zimechukuliwa dhidi ya wahusika.

  Hata hivyo, uchunguzi unaonesha kuwa watuhumiwa hao hawajachukuliwa hatua za kisheria zaidi ya kuondolewa katika idara walizokuwa wakifanya kazi na kuhamishiwa idara nyingine tofauti za chuo hicho.

  Madai mengine yanayoukabili uongozi wa chuo hicho ni wizi wa fedha za umma kupitia mikataba ya mzabuni aliyekuwa akitoa huduma ya mtandao (jina tunalo).

  Taarifa zinaonesha kuwa, kulingana na mkataba wake, malipo ya mzabuni huyo kwa mwezi ilikuwa dola za Marekani 13,040 lakini baadhi ya watumishi wa Idara ya Uhasibu na Ugavi walikuwa wakishirikiana kulipa mara mbili kiasi hicho cha fedha.

  Wizi huo ulikuwa unafanikishwa kwa ustadi mkubwa kwa kuandika hundi mbili zenye kiasi cha dola za Marekani 13,040 sawa na Sh19,951,200 kwa kila hundi huku zikionesha kuwa anayelipwa ni mzabuni huyo na kwamba wizi huo unadaiwa kufanyika kati ya mwaka 2006/2007 na 2008/2009.

  "Lakini baada ya hundi hizo kuwa zimepita kila mahali kwa ajili ya kuidhinishwa, hundi moja ilikuwa inawekwa kwenye akaunti tofauti na wafanyakazi hao kugawana fedha hizo,” anasema mtoa taarifa wetu.

  Mwananchi lilifanikiwa kupata namba za hundi na akaunti iliyokuwa inatumika kufanikisha wizi huo, ambapo vyanzo vyetu kutoka ndani ya benki za CRDB na NBC Iringa mjini vimethibitisha kuchukuliwa kwa fedha hizo kwa kutumia hundi hizo.

  Hata hivyo, Professa Mushi alipoulizwa juu ya suala hilo alisema ni jambo la zamani (anataja mwaka 2009) na kwamba kwa sasa hilo siyo jambo la kujadiliwa.

  "Jamani hebu mtuache nasi tufanye kazi basi hata kidogo hiyo 'issue' (hilo suala) ni la zamani mno, hata huyo (anataja jina la mzabuni) hayupo tena hapa chuoni,” alisema Professa Mushi na kuongeza:

  "Unajua inaonekana mmeiba taarifa ya ukaguzi ambayo hata haikuwa imekamilika na ilikuwa siri, huyo mtu anayekuletea mambo hayo anatapatapa tu”.

  Wakati Profesa Mushi akielezea kuhusu madai hayo, Muce pia inakabiliwa na tuhuma za kutumia fedha umma kuendesha akaunti za muda maalum (Fixed Deposit Account) bila kuweka wazi faida inayotokana na akaunti hizo.

  Uchunguzi unaonesha kuwa, mpaka Juni mwaka jana, chuo hicho kilikuwa kinaendesha akaunti zaidi ya nne za muda maalum (namba za akaunti hizo tunazo) ambazo zilikuwa na zaidi ya Sh500 milioni.

  Akaunti nne ambazo zipo kwenye benki moja yenye tawi mjini Iringa zinaonesha kuwa akaunti ya kwanza ilikuwa na kiasi cha Sh10,090,999.55, nyingine ilikuwa na kiasi cha Sh201,247,671.23, pia ilikuwepo akaunti yenye Sh252,853,107.40 na ya mwisho ilikuwa na kiasi cha 75,195,042.70 ambapo jumla yake ni Sh 539,386,820.88.

  Alipohojiwa kuhusu akaunti hizo, Professa Mushi alisema aulizwe Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho (Fedha na Utawala),Professa Machiwa kwa maelezo kuwa ndiye alikuwa anafahamu vyema suala hilo.

  Professa Machiwa alipoulizwa alidai kuwa akaunti hizo hazikuwa kwenye orodha ya akaunti za chuo hicho na kwamba hakuwa anazifahamu wala kuwa na taarifa nazo.

  "Hata nikikuonyesha taarifa yangu ya kila siku akaunti hizo hazimo labda kamwone mhasibu wa chuo anaweza kuwa ana taarifa zaidi,” alisema Professa Machiwa lakini kabla mwandishi hajaondoka akaamua vinginevyo:

  "Hebu ngoja nimpigie mhasibu aende benki naye akaangalie ili atuletee taarifa kama akaunti hizo ni za Mkwawa University, kwa hiyo njoo baadaye nitakupa taarifa,” alisema.

  Hata hivyo, mwandishi aliporejea mchana wa Januari 28 mwaka huu, Professa Machiwa alisema watu wa benki walikuwa wamegoma kutoa taarifa za akaunti hizo mpaka waandikiwe barua.

  "Nimeandika barua nimeshawapelekea hivyo naomba uje wiki ijayo na kwa kuwa sitakuwepo, utakuta taarifa kwa katibu muhtasi wangu,” alisema .

  Mwananchi lilifuatilia kwa siku tatu mfululizo bila kupata majibu kwa katibu muhtasi wake na kuamua kumtafuta tena Professa Mushi kwa simu ambaye baada ya kuulizwa suala hilo alisema: "Mbona Professa Machiwa ameshakujibu, usinisumbue,” alisema kwa kifupi na kukata simu.

  Hata hivyo, baadaye alipiga simu kwa mwandishi wa Mwananchi na kueleza kuzifahamu akaunti hizo na kudai kuwa pia zilikuwa za zamani na kwamba hivi sasa hazipo tena kwani zimeishafungwa.

  "Unaziona kama ni nyingi lakini akaunti ni moja tu yaani kila akaunti ya kwanza inapokuwa tayari faida inachukuliwa na kufunguliwa akaunti nyingine,” alisema.

  Professa Mushi alifafanua kuwa fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti ya muda maalum zilitoka kwa wafadhili ambao hata hivyo hakuwataja na kwamba zilikuwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo lakini baada ya mkandarasi kusuasua, waliamua kuziweka kwenye akaunti ya muda maalum ili kuepusha kuzitumia kwa shughuli zingine.
   
 2. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #2
  Feb 12, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  yaleyaleeeeeeeeeeee yaani wafanyakazi hawabadiliki jamani sasa sijui hata tufanye nini ili kuliokoa taifa hili mishahara mtu anachukulia kwenye benki mbili na bado uongozi unamfuga tu mbaya zaidi hii ni sehemu ambayo tunaamini imejaa vichwa vya wasomi kweli kazi ipo!
   
Loading...