Ufisadi BoT: Wako wapi kina Ngozi Okonjo wetu?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,086
Ufisadi BoT: Wako wapi kina Ngozi Okonjo wetu?

Johnson Mbwambo Januari 30, 2008
Raia Mwema

WIKI iliyopita nilijaribu kueleza jinsi baadhi ya Wahindi wanavyotugeuza (Watanzania wazawa) mabwege kwa kushirikiana na viongozi wetu, wenye uroho wa pesa, kuiba mabilioni ya pesa zetu ambazo zingetusaidia kupunguza umasikini nchini.

Nilisisimshwa na wingi wa ujumbe wa sms na e-mail niliotumiwa na wasomaji wa safu hii; huku wengi wakiunga mkono yale niliyoyaeleza. Kwa hakika, sijawahi kutumiwa meseji nyingi kiasi hicho tangu safu hii ianze, jambo ambalo, naamini, linathibitisha jinsi suala la mahusiano yetu na Wahindi tulionao hapa nchini linavyogusa wengi.

Wizi hii wa pesa za umma unaofanywa na kina Jeetu Patel na kina V.G Chavda, kwa kushirikiana na baadhi ya wazawa wenzetu tuliowapa dhamana ya uongozi, unasikitisha. Inasikitisha, hasa unapouangalia umasikini unaozunguka jamii zetu hususan vijijini.

Wakati, kwa mfano, wenzetu hao wanapochota mapesa hayo kutoka BoT (zaidi ya Sh. bilioni 500 katika mwongo mmoja tu uliopita) na kwenda kuyaficha katika mabenki ya Ulaya na Uarabuni, wananchi wetu wanakufa huko vijijini kwa kukosa hata dawa tu za kujitibu malaria; achilia mbali mama zetu wa mikoa ya Kusini ambao hulazimika kila siku kutembea kilomita tano na ndoo ya maji kichwani!

Lakini nataka kusema kwamba tatizo hili la baadhi ya Wahindi waovu kushirikiana na viongozi wazawa waovu kuiba pesa za wanyonge, si la Tanzania tu. Tumesoma habari za Kamlesh Pattni wa Kenya katika ile kashfa ya Goldenberg. Tumesoma pia habari za skandali ya Afrika Kusini ya manunuzi ya silaha iliyompeleka jela Schabir Shaik, na ambayo bado inamwandama Rais wa ANC, Jacob Zuma.

Wote, Pattni na Schabir, ni Wahindi na katika skandali zote mbili walishirikiana na viongozi wazawa. Kwa maana hiyo, na kwa namna fulani, nakubaliana na wale wote ambao katika meseji zao kwangu walisema kwamba tunapaswa kuwatupia lawama viongozi wetu (wazawa wenzetu) na si kina Jeetu Patel. Kwamba kama si uroho wa pesa wa viongozi wetu wanaotaka kuwa mabilionea, hawa kina Chavda, kina Patel na kina Schabir, wasingefanikiwa kutuibia!

Lakini kwa sababu ya kosa letu wenyewe la kuwaingiza madarakani viongozi wa namna hiyo, ndiyo maana tunaibiwa na kugeuzwa wajinga na wenzetu hao Wahindi. Wanasema mvunja nchi ni mwananchi! Na kama nilivyoeleza mwanzo, hali ni hiyo hiyo kwingineko Afrika.

Takwimu zinaonyesha kwamba bara la Afrika hupoteza kiasi cha dola bilioni 148 kila mwaka kutokana na vitendo vya wizi na ufisadi vinavyofanywa na viongozi, na kwamba kiasi hicho ni asilimia 25 ya mapato ya bara hilo kwa mwaka.

Takwimu pia zinaonyesha kwamba kila dola milioni 100 zinazoibwa, zingeweza kuhudumia bure waathirika 600,000 wa ukimwi, kutoa bure dawa za malaria kwa watu milioni 100, kutoa bure chanjo kwa watoto milioni nne na kutoa bure huduma za maji kwa kaya 250,000!

Labda swali la kujiuliza ni iwapo kama kuna uwezekano wowote mapesa hayo yaliyoibwa kurejeshwa? Kwa mfano, Rais Kikwete ameagiza uchunguzi wa ufisadi wa BoT ufanyike ndani ya miezi sita na watakaopatikana na hatia wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kurejesha mapesa hayo au kunyang’anya mali zilizopatikana kutokana na pesa hizo, kama vile majumba ya kifahari na magari ya kifahariu. Je hilo linawezekana?

Jibu langu ni kwamba hilo linawezekana, lakini ni kazi ngumu na ya muda mrefu na ambayo mafanikio yake yatatokana tu na uzalendo wa kujituma wa wale wote wanaochukizwa kupindukia na wizi huo wa pesa za masikini hususan wale watakaotumwa kufanya uchunguzi wa wizi huo. Maana linapokuja suala la Wahindi matajiri, uwezekano wa rushwa kutembea na hivyo kusababisha mafaili “kupotea” na hati mbalimbali kuchanwa, ni mkubwa.

Lakini kuwezekana mapesa hayo kurejeshwa inawezekana. Labda nitoe mfano mmoja tu wa juhudi za mtu mmoja zilivyowezesha kurejeshwa nyumbani kwa mamilioi ya pesa yaliyoibwa na kuwekwa katika benki za Uswisi. Namzungumzia Waziri wa zamani wa Fedha wa Nigeria, Ngozi Okonjo-Iweala.



NGOZI Okonjo-Iweala

Ilimchukua Mama huyo wa Nigeria takriban miaka minne ya kazi ngumu ya kufuatilia huku na kule, lakini mwisho wake aliwezesha, mwaka 2006, kurejeshwa Nigeria kwa dola milioni 500 zilizokuwa zimeibwa na mtawala wa zamani wa nchi hiyo, Sani Abacha na kufichwa katika mabenki ya Uswisi.

Mama huyo alihangaika sana na kuna wakati alikatishwa tamaa hata na viongozi wenzake, lakini alilichukulia jambo hilo kama crusade yake binafsi, na matokeo yake alifanikisha mapesa hayo kurejeshwa Nigeria na kutumbukizwa katika miradi ya maendeleo ya jamii.

Kwa hiyo si kweli kwamba haiwezekani mapesa tuliyoibiwa yakarejeshwa. Ni kazi ya muda mrefu (si chini ya miaka mitano) na inayohitaji pesa, lakini ni kazi inayowezekana kabisa kufanyika. Kinachotakiwa ni kuwa na kina Ngozi Okonjo-Iweala wetu ambao watalichukulia jambo hili kama crusade yao binafsi.

Ingawa kwa nchi kama Phillipines iliwachukua miaka 18, lakini angalau, hatimaye, iliweza kurejesha nyumbani milioni 624 zilizokuwa zimeibwa na mtawala wa zamani wa nchi hiyo, Ferdinand Marcos na kuwekwa katika benki za Uswisi. Kwa hiyo, haijalishi na sisi itatuchukua miaka mingapi; alimradi tu pesa hizo hatimaye zinarudishwa nyumbani kusaidia watu wetu masikini.

Katika kashfa ya manunuzi ya rada, kwa mfano, utafiti uliofanywa Uingereza unaonyesha kwamba akaunti moja ya Uswisi ilitumika kuweka rushwa ya pauni za Uingereza milioni 12 ( takribani Sh. bilioni 15) na kwamba pesa hizo ziligawiwa na kina Tanil Somaiya na Sailesh Vithlani kwa viongozi mafisadi wa Tanzania waliopitisha ununuzi wa rada hiyo.

Kina Ngozi Okonjo-Iweala wetu wanaweza kuanza kwa kufanya upelelezi na kutafuta ushahidi na nyaraka muhimu, kuwajua ni viongozi gani wa Tanzania waliopokea rushwa hiyo ya manunuzi ya rada kutoka katika akaunti hiyo ya benki ya Uswisi.

Wakishaukusanya ushahidi na vielelezo hivyo, wanaweza kuviwasilisha kwa asasi mpya iliyoundwa na Umoja wa Mataifa (UN) na Benki ya Dunia (WB) inayoitwa STAR – The Stolen Asset Recovery Initiative, ambayo itachunguza ushahidi huo na kama ni mzito itaanza utaratibu wa kuendesha mazungumzo na benki hizo za Uswisi kuhakikisha mapesa hayo ya umma yanarejeshwa nchini.

Nisisitize tena kwamba ni kazi ya muda mrefu, lakini inayowezekana kufanyika; hasa kama tuna kina Ngozi Okonjo-Iweala wetu watakaolivalia njuga suala hilo.

Ni jambo linalotia moyo kwamba shinikizo la muda mrefu la kuzitaka benki za Uswisi kuacha kuwa pango la kufichia mapesa yanayoibwa kutoka katika nchi masikini za Afrika, limesaidia kuzifanya benki hizo kubadilika. Hivi sasa benki za Uswisi hazina tena usiri wa miaka ile ya sitini, sabini na themanini.

Hivi sasa zinabanwa na sheria za kimataifa kutoa ushirikiano kwa asasi zinazofwatilia kuibwa kwa pesa za nchi masikini na kuwekwa huko. Na ndiyo sababu Ngozi Okonjo- Iweala, katika kipindi cha miaka minne tu, aliweza kuzirejesha nyumbani dola milioni 500 zilizoibwa na Abacha na kuwekwa kwenye benki za Uswisi.

Zamani juhudi za kurejesha mapesa hayo yanayoibwa zilionekana kama ni jambo linalozihusu nchi zenyewe zilizoibiwa mapesa hayo, lakini sasa STAR inatuthibitishia kwamba ni jambo linaloungwa mkono na Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa.

Majuzi tu hapa, Balozi wa Marekani nchini, Mark Green aliwaambia waandishi wa habari kwamba nchi yake iko tayari kuisaidia Tanzania kurejesha nyumbani mapesa yaliyoibwa BoT kama yamewekwa katika mabenki ya Marekani.

“Marekani iko tayari kusaidia kutafuta fedha zote zilizoibwa na kuzirejesha nchini. Hiyo ni sera yetu kwamba haturuhusu fedha za aina hii kuwako katika nchi yetu,” alisema Balozi Green.

Kauli hiyo ya Balozi Green ni uthibitisho mwingine kwamba msaada upo kama kina Ngozi Okonjo-Iweala wetu watajitokeza na kuanzisha crusade ya kurejesha nyumbani mapesa ya umma yaliyoibwa.

Kwa hiyo, kuna siku, hata kama ni miaka 20 ijayo, mapesa haya yanayoibwa Afrika, yatarejeshwa nyumbani. Kwa Tanzania tunachohitaji ni kuwa na kina Okonjo-Iweala wetu wa kulichukulia suala hilo kama crusade yao binafsi!

Je tunao kina Okonjo-Iweala wetu? Kama wapo, basi, nawajitokeze sasa kupambana na juhudi kubwa zinazofanyika hivi sasa za kuhakikisha kina Jeetu Patel, wamiliki wa Kagoda Agriculture Limited na wahusika wengine wa skandali hii ya BoT, hawafikishwi mahakamani.

Lakini je, tunao kweli kina Okonjo-Iweala wetu? Tafakari.
Email: mbwambojohnson@yahoo.com
 
Back
Top Bottom