Ufaransa yaipiga Google faini ya Tsh bilioni 621 kwa kujipendelea katika mfumo wa matangazo ya Kidigitali

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Kampuni ya Google imepigwa faini ya Euro milioni 220, sawa na zaidi ya Tsh. bilioni 621 na kutakiwa kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wake wa matangazo ya mtandaoni nchini Ufaransa.

Mamlaka za Ushindani wa Kibiashara nchini Ufaransa zimesema faini ya Google inatokana na kutumia nafasi yake ya ukubwa katika biashara ya mtandaoni kuwaminya washindani wake, ikiwalaumu Google kwa kupendelea mfumo wake wa matangazo ya kidigitali ya Google Ad Manager unaoipa nafasi kubwa jukwaa lake la matangazo ya kidigitali la AdX, ambapo wachapishaji wa matangazo huuziwa nafasi ya kutangaza.

Google imesema itafanya mabadiliko kwa kurahisisha makampuni mengine ya matangazo kutumia mfumo wake wa data kufanya matangazo, wakiahidi kubadili na kufanyia majaribio mabadiliko hayo katika miezi ijayo kabla ya kuyatoa ili kutumiwa na umma nchini Ufaransa, na baadhi kutumika kote duniani.

Kampuni hiyo inakabiliwa na mashtaka kadhaa nchini Marekani yanayofanana na hayo, ikishtakiwa kwa kukiuka vigezo vya ushindani wa kibiashara, huku makampuni mengine yenye mizizi mikubwa ya biashara za matangazo ya kidigitali kama vile Facebook yakichunguzwa na mamlaka za Ulaya kwa kutumia taarifa za watumiaji kujipendelea kibiashara.

Miezi miwili iliyopita, Google ilipigwa faini ya zaidi ya Dola milioni 36 za Kimarekani (sawa na Tsh bilioni 83) nchini Uturuki kwa madai ya kujipendelea katika matokeo ya utafutaji wa ulinganifu wa bei za hoteli nchini Uturuki kuliko zile za washindani wake. Google ilijitetea kwa kusema kuwa kufanya hivyo kumeongeza ushindani kibiashara katika soko la hoteli za kitalii nchini Uturuki.

Chanzo: Reuters

1623131388063.png
 
Back
Top Bottom