Ufahamu mgogoro wa Syria A to Z mpaka sasa

kimsboy

JF-Expert Member
Oct 17, 2016
8,991
17,888
VITA YA SYRIA: MSHINDI NI RAIS BASHAR AL ASSAD.
Ijumaa, Juni 7, 2019

Na Masudi Rugombana...
Mwezi Machi mwaka 2011 kulizuka maandamano jijini Deraa nchini Syria dhidi ya Serikali ya Rais Bashar al Assad. Ni maandamano yaliyoitishwa na makundi ya watu waliojiita watetezi wa Demokrasia wakilalamikia kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira, rushwa na ukosefu wa uhuru wa kufanya siasa.
Maandamano hayo yaliyochochewa na harakati zilizopewa jina Arab springs katika mataifa ya kiarabu ya Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya kati yalisambaa nchini kote Syria hasa katika miji mikubwa kama Damascus na Allepo. Ni maandamano yaliyogeuka uasi pale serikali ilipojaribu kutumia nguvu kutawanya makundi ya waandamanaji waliokuwa wakitaka Rais Bashar al Assad ajiuzulu.
Vurugu zilisambaa nchini kote na kupelekea wafuasi wa upinzani kukamata silaha na kupambana na vikosi vya Serikali katika kile kilichoitwa kujilinda wenyewe kwa kuvitimua vikosi vya serikali kutoka kwenye maeneo yao. Ni hatua hii ya magenge ya waandamaji kuanzisha uasi ndiyo iliyopelekea Rais Bashar al Assad kutangaza vita dhidi ya mangenge hayo aliyoyaita ya kigaidi yenye kufadhiliwa na mataifa ya kigeni.
Machafuko yalisambaa kwa kasi na hatimaye kuitumbukiza Syria katika vita vya wenyewe kwa wenyewe iliyopelekea uingiliaji kati wa mataifa ya kigeni yakiunga mkono pande hasimu. Ni Vita mbaya kuliko zote kuwahi kutokea katika eneo la Mashariki ya kati katika karne ya Ishirini na Moja ambayo mpaka sasa imeshasababisha vifo vya watu 465,000 na idadi ya wakimbizi zaidi ya milioni tano waliokimbilia nje ya Syria huku raia Milion kumi na tatu wakihitaji msaada wa kibinadamu ndani ya Syria.
NI PANDE ZIPI ZINAZOPIGANA KATIKA VITA INAYOENDELEA NCHINI SYRIA?
1. Serikali ya Syria dhidi ya Waasi
Waungaji mkono wakuu wa Serikali ya Syria ni Urusi, Armenia na Iran wakati Uturuki, Mataifa ya Ulaya Magharibi na nchi za Ghuba zikiongozwa na Saudi Arabia wanaunga mkono makundi ya Waasi na Magaidi wanapambana dhidi ya Serikali ya Syria.
Urusi ambayo imekuwa na vituo vya kijeshi huko Syria vya Hmeymim (Latakia Air base) na kambi ya jeshi la Wanamaji ya Tartus mnamo mwaka 2015 ilizindua kampeni kubwa ya mashambulizi ya anga dhidi ya makundi ya Waasi, kampeni ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa vikosi vya Serikali ya Syria kurejesha eneo kubwa la ardhi lililokuwa likishikiliwa na makundi ya waasi.
Kwenye mahojiano yaliyotangazwa na televisheni huko Urusi tarehe 11 Octoba 2015 Rais Vladimir Putin alisema kuwa uingiliaji wa nchi yake kijeshi nchini Syria ni jambo lililoandaliwa kwa umakini wa hali ya juu hapo kabla na kueleza kuwa lengo la Urusi ni kuimarisha serikali halali ya Syria na kujenga hali nzuri ya maridhiano ya kisiasa.
Iran ambayo imepeleka mamia ya wakufunzi wa kivita na maelfu ya wapiganaji inatumia mabilioni ya dola kuhakikisha kuwa mshirika wake wa miaka mingi Bashar al Assad anaendelea kusalia madarakani. Iran inatoa mafunzo ya kivita na silaha za kisasa kwa wapiganaji wa kundi la Hizbullah kutoka nchini Lebanon na wale wa kujitolea kutoka nchini Iraq, Yemen na Afghanistan ambao wanapigana bega kwa bega na vikosi vya Serikali ya Syria. Inakadiriwa kuwa adadi ya askari wa Iran wanaopigana vita na kutoa mafunzo ya kijeshi nchi Syria inafikia elfu kumi.
2. Marekani,Uingereza na Ufaransa dhidi ya Assad
Nchi hizo zimekuwa zikitoa msaada mkubwa wa mafunzo, fedha na silaha kwa makundi ya waasi hasa yale yenye msimamo wa Wastani wa kidini Kama Free Syria Army (FSA), National Front for Liberation na Revolutionary Commando Army kwa lengo la kumuondoa madarakani Rais Bashar al Assad. Misaada hiyo ya kijeshi ya mataifa hayo ya magharibi inatolewa katika kutekeleza ile kauli mbiu yao maarufu ya Assad lazima aondoke (Assad must go)
Pia mataifa hayo ya Magharibi yanatoa msaada mkubwa ya fedha, silaha na mafunzo kwa wapiganaji wa kikurdi wa Syria Democratic Forces (SDF) wanaopigania kuundwa kwa taifa lao huko katika mkoa wa Rojava, Kaskazini ya Syria.
Ikumbukwe kuwa Wakurdi hawapigani na vikosi vya Syria bali wanapigana kukomboa maeneo yao yaliyotekwa na Waasi na Magaidi wa kundi la Islamic State wanaopigana dhidi ya majeshi ya serikali ya Syria. Hivyo basi Wakurdi wanapigana na makundi yote ya Waasi kama ilivyo kwa vikosi vya Serikali ya Syria.
3. Uturuki dhidi ya Wakurd
Uturuki ambayo inaunga mkono vikundi vyote vya waasi vinavyopigana dhidi Serikali ya Syria na wapiganaji wa Wakikurdi kwa kuvipatia Silaha, fedha na Wakufunzi wa kijeshi ili kufikia lengo la kumuondoa madarakani Rais Bashar al Assad imejikuta katika mkwamo mbaya. Mafanikio ya Wapiganaji wa Kikurdi huko kwenye mkoa wa Rojava yamekuwa ni kitisho kikubwa kwa Uturuki ikihofia kuwa ushindi wao utachochea harakati za kujitenga kwa jamii kubwa ya Wakurdi inayopatikana kusini mwa Uturuki kupitia kundi lao la Wapiganaji la Kurdistan Workers Party (PKK) linalopigania kuanzishwa kwa taifa la Kurdistan.
Hali hii imeifanya Uturuki kutumia nguvu kubwa kulisadia kundi la Free Syria Army (FSA) ili liweze kuwadhibiti Wakurdi wa Syria wasipate mafanikio zaidi huko Kaskazini ya Syria, jitihada ambazo zimeshindwa kuzaa matunda.
Pia Uturuki imekwenda mbali zaidi hadi kufikia uamuzi wa kupeleka majeshi yake huko Kaskazini ya Syria na kuiteka Wilaya ya Afrin mnamo Machi 18, 2018 katika kile kilichoitwa Operation Olive Branch lengo likiwa ni kuzuia kujitanua zaidi kwa Wapiganaji wa Kikurdi Kaskazini mwa Syria.
Hatua za Uturuki dhidi ya Wakurdi kwa kiasi kikubwa zimevuruga kabisa ushirikiano baina yake na Marekani katika vita vya Syria kwani imekuwa ikiishutumu waziwazi Marekani kuwa uamuzi wake wa kuwaunga mkono Wakurdi Kaskazini ya Syria ni kitisho kikubwa kwa usalama wa Uturuki. Ikumbukwe kuwa Marekani ina vituo vya Kijeshi kwenye maeneo yanayoshikiliwa na Wapiganaji wa Kikurdi Kaskazini ya Syria.
4. Saudi Arabia na Mataifa ya Kiarabu ya Ghuba dhidi ya Iran.
Mataifa ya kiarabu yameongeza ufadhili wao kwa Makundi ya Kigaidi ya Kisalafi na Kiwahabi yenye msimamo mkali ya Islamic state (IS) na Hay'at Tahrir al-Sham kwa lengo la kupambana na kile kinachoitwa "KITISHO CHA USHAWISHI WA IRAN".
Kundi la Hyat Tahrir al-Sham kwa sasa ndio kundi hatari zaidi la kigaidi nchini Syria, kundi hili ni muungano wa makundi manne ya kigaidi ya Jabhat Fateh al Sham (Al Qaeda tawi la Syria) , Ansar al Din front, Jaysh al Sunna na Nour al Din al Zenki Movement.
Makundi hayo kwa sasa yanakabiliana na Majeshi ya Serikali ya Syria kwenye mkoa wa Idlib yalipokimbilia baada ya kushindwa vibaya sana na majeshi ya Rais Assad katika maeneo mengine nchini Syria. Kundi la Islamic State kwa kiasi kikubwa limeshasambaratishwa vibaya na majeshi ya Urusi, Iran na Syria na kwa kiasi kikubwa kundi hilo sio tishio sana kwa Utawala wa Assad. Kwa sasa limekuwa likifanya mashambulizi machache ya kushtukiza.
5. Mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya harakati za Iran ndani ya Syria.
Wakati rais Bashar al Assad akiwa katika hatua za mwisho za kuyasambaratisha makundi ya Waasi na Magaidi nchini Syria, mshirika wake mkubwa Iran amekuwa akiendelea kujiimarisha kijeshi ndani ya Syria kwa baraka za Serikali ya Syria.
Iran pia imekuwa ikiimarisha harakati za kupenyeza silaha za kisasa na wakufunzi wa kijeshi huko Lebanon kwa ajili ya kuliimarisha kundi la Hizbullah sambamba na kujiimarisha kijeshi nchini Syria kwa kufungua makambi, maghala ya Silaha, na kujenga viwanda vidogo vya kuunda makombora.
Israel inazichukulia hatua hizo za Iran kama maandalizi rasmi ya kuanzisha vita dhidi yake mara tu baada ya kumalizika kwa vita vya Syria.
Je kwanini Urusi haimsaidii mshirika wake Iran kukabiliana na mashambulizi ya anga ya Israel?
Harakati hizi za Iran dhidi ya Israel haziungwi mkono na Urusi kwa sababu zinakwenda kinyume na lengo rasmi lililopelekea mataifa hayo washirika kujiingiza katika vita vya Syria, lengo ambalo ni kumsadia Rais Bashar al Asad kupambana na makundi ya waasi wanaotaka kuingusha serikali yake.
Pia inaelezwa kuwa Urusi haina makubaliano na Iran ya kuipa ulinzi dhidi ya Mashambulizi ya anga (air cover) yanayofanywa na Israel kwenye maghala yake ya Silaha nchini Syria na misafara ya shehena za silaha zinazopelekwa nchini Lebanon kwa ajili ya kundi la Hizbullah kwa kuwa kufanya hivyo kutavuruga uhusiano mzuri uliopo baina ya Israel na Urusi.
Kwa sababu hiyo Russia haiwezi kuruhusu mtambo wake wa kisasa wa S 400 utumike kwa lengo la kuzuia mashambulizi ya Israel dhidi ya vikosi vya Iran na Hizbullah kwa sababu kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kujiingiza katika vita visivyoihusu.
Pia kumekuwa na mchuano mkubwa wa kimaslahi baina ya Urusi na Iran nchini Syria huku kila upande ukitaka kunufaika na zabuni mbali mbali zinazotangazwa na Serikali katika harakati za ujenzi wa Syria mpya. Wakati Iran ikitarajia kuchukua tenda ya kuendesha bandari ya Latakia, Urusi tayari imechukua tenda ya kuzalisha mafuta na gesi pamoja na vituo vya kuzalisha umeme kwa muda wa miaka 25 ijayo.
Kwa hivyo basi Russia imekubaliana na ombi la Israel la kufanya mashambulizi nchini Syria dhidi ya maghala ya Silaha ya Iran na misafara ya magari yanayobeba shehena za silaha kwenda Lebanon kwa ajili ya kuliimarisha kundi la Hizbullah. Sharti kuu la makubaliano baina ya Urusi na Israel ni kwamba kabla ya kushambulia ni Lazima Israel itoe taarifa kwa Urusi na kueleza ni maeneo gani inayotaka kushambulia ili kama kuna Wakufunzi wa kijeshi wa Urusi waweze kuondoka katika maeneo hayo ili kuepuka maafa.
Ukiachilia mbali askari wa Urusi waliokufa kwenye tukio la ndege ya Urusi iliyotunguliwa kimakosa na mfumo wa kujihami mashambulizi ya anga wa S200 (SA-5 Gammon) wakati ulipokuwa ukishambulia ndege za Israel, hapajawahi kutokea maafa kwa askari wa Urusi yaliyosabishwa na hayo Mashambulizi ya Israel. Hata askari wa Syria wanaouliwa katika hayo mashambulizi ni wale tu wanaofanya kazi pamoja na askari wa Iran katika hayo maeneo.
Ikumbukwe kuwa Rais Vladmir Putin ni mshirika mkubwa wa Israel. Anaelezwa kuwa ndiye Raia wa kwanza wa Urusi kuwa na uhusiano mzuri sana na Israel kuliko marais wote waliowahi kuongoza Urusi. Uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo ni wa kiwango cha hali ya juu kwani Waziri mkuu wa Israel Binyamin Netanyahu na Rais Vladmir Putin wameshakutana na kufanya mazungumzo mara kumi na moja ndani ya miaka mitatu.
Mbali na ushirikiano wa kibiashara unaokuwa kwa kasi baina ya Urusi na Israel, taifa hilo la Kiyahudi lina idadi kubwa ya wananchi wanaoongea lugha ya Kirusi kuliko taifa lolote Duniani nje ya bara la Ulaya. Zaidi ya Waisrael milioni moja na laki tano wana asili ya Urusi hivyo sio rahisi Putin kushirikiana na Iran kuhatarisha usalama wa taifa la Israel lenye mahusiano ya kindugu na Urusi.
Inachofanya Urusi ni kuhakikisha ushirikiano baina yake na Iran unabaki kwenye agenda moja tu ambayo ni kupambana na kuwashinda waasi wanaotaka kumuondoa madarakani Rais Bashar al Assad. Urusi haitaki kutumika kama ngao ya Iran katika harakati za taifa hilo la Kiajemi dhidi ya Israel.
Kwa kuwa Israel inashirikiana na Marekani pamoja na Urusi katika kufanikisha mashambulizi yake dhidi ya harakati za Iran nchini Syria

Nini hatma ya vita ya Syria
Upepo wa vita kwa sasa unavuma vizuri sana kwa pande mbili zisizo na uhasama mkubwa. Upande wa Rais Bashar al Assad unaoungwa mkono na nchi za Iran na Urusi na ule wa Wakurdi unaoungwa mkono na Marekani.
Wakurdi kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kudhibiti sehemu kubwa ya Jimbo lao la Rojava huko kaskazini Mashariki ya Syria huku Bashar al Assad akifanikiwa kukomboa asilimia 80 ya ardhi ya Syria ambayo ni maeneo ya mashariki, Magharibi, kusini, kati na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Syria ukiwemo mkoa wa Allepo.
Ni mkoa mmoja tu wa Idlib ndio upo mikononi mwa makundi ya Waasi. Na kwa sasa vikosi vya Serikali ya Syria, hizbullah na Iran vikisaidiwa na ndege za kivita za Urusi vinasonga mbele zaidi kuwaondoa waasi ndani ya mkoa wa Idlib. Ushindi kwa majeshi ya Serikali huko Idlib ni jambo lisilokuwa na Shaka.
Ni dhahiri kuwa baada ya kuuteka mkoa wa Idlib na kuwafyekelea mbali Waasi Rais Bashar al Assad na Washirika wake Urusi na Iran hawatakuwa tayari kuingia moja kwa moja vitani na Uturuki katika wilaya ya Afrin mkoani Rojava wala kupambana na Vikosi vya Marekani vilivyopo kwenye mkoa wa Rojava. Pande tatu yaani Serikali ya Syria chini ya Assad, Iran na Urusi kwa upande mmoja na Wakurdi, Marekani na Uturuki kwa upande wa pili zitalazimika kukaa mezani ili kufikia makubaliano ya kuundwa kwa Serikali ya mseto baina ya kambi ya Assad na Wakurdi, makubaliano ambayo yatawawezesha Wakurd kuwa na utawala wao wa ndani katika mkoa wao wa Rojava.
Ikiwa hapatakuwa na makubaliano baina ya pande mbili basi kuna uwezekano Wakurd wakajitenga na kuunda taifa lao wakiungwa mkono na Marekani na nchi za Ulaya Magharibi.
Hivyo basi mwisho wa Vita vya Syria utashuhudia ushindi kwa kambi ya Assad na wananchi wa jamii ya Wakurd katika mkoa wa Rojava.

SHUKURANI ZIMWENDEE MASOUD RUGOMBANA KWA MAKALA HAYA
FB_IMG_15598992212457967.jpg
 
Hao waandishi wanafanana majina na asad Wapo very biased

Hiyo bado ni story kutoka kwenye mtazamo wa mtu and not history
 
Hawa ni waashuru
Wale ambao jenerali wao Naamani aliponywa na Elisha
Pia Yona ndio alijaribu kukimbia jukumu la kupeleka ujumbe wa Mungu kwao.
Hivi Syria ndio kwa Wafilisti wasio tahiriwa?
 
Back
Top Bottom