Ufafanuzi juu ya Marubani wa Tanzania kukosa Ajira katika soko la ndani

Informer

JF-Expert Member
Jul 29, 2006
1,577
6,582
PROFESSIONAL ASSOCIATION OF TANZANIAN PILOTS
P.O. BOX 18059 DAR ES SALAAM TANZANIA
TEL. 0773783007 EMAIL: tzpatp@gmail.com

Dar es Salaam

Desemba 02, 2013


MARUBANI WA TANZANIA KUKOSA AJIRA KATIKA SOKO LA NDANI


1.0 UTANGULIZI



  1. Chama cha marubani wa ndege, Tanzania, kinapenda kujibu taarifa iliyotolewa na mamlaka ya usafiri wa anga, Tanzania, TCAA katika toleo la Novemba 19, 2013- gazeti la mwananchi lenye habari za kukanganya wananchi na serikali.
Limekuwepo tatizo sugu lililoshamiri na kuathiri ajira ya marubani wazalendo hapa nchini.

2.0 CHIMBUKO LA TATIZO

2.1 Mwaka jana ilitolewa taarifa katika gazeti la "the guardian", kutoka (Tanzania Air Operator's Association, TAOA), ambayo ilidai katika kifungu namba (4) kwamba chama cha marubani hakina mamlaka juu ya mwajiri kwenye masuala ya ajira na kwamba hata TCAA haina mamlaka hayo. Na katika kifungu namba (5) kwamba ni kinyume cha sheria na hatari kwa usalama kwa watu wasiojulikana kuchukua majukumu ya nani apewe au asipewe kazi. Waliweka takwimu ya marubani wa kigeni na wazawa nchini na orodha ya leseni na maelezo kwa ushirikiano kutoka TCAA.

Tukawasilisha barua kwa ofisi ya mkurugenzi mkuu, TCAA kupewa ripoti ile ilioandaliwa na idara ya kusimamia usalama wa anga. Tulihangaishwa hadi tukakata tamaa, kwa mantiki hiyo tulishindwa kujibu tuhuma hizo. Kuna baadhi ya viongozi wa zamani walio staafu kutoka TCAA wamejipenyeza katika makampuni ya ndege na washirika wao waliopo TCAA kugeuza sekta ya usafiri wa anga sivyo na kuhatarisha usalama wa anga.

2.2 TAOA na TCAA waelewe kuwa, sisi hatuna mamlaka lakini tunapaswa kutambulika na kuhusishwa kama kati ya wadau wakuu; marubani na pia chama chetu cha marubani katika maamuzi yanayotolewa katika sekta ya usafiri wa anga hata International Civil Aviation Organisation, ICAO MANUAL ibara ya 1.5 inatamka hivyo.

2.3 TAOA wameandika kuwa TCAA hawana mamlaka juu ya mwajiri…sisi tumeonyeshwa na kupokea mawasiliano mbalimbali inayoonyesha TCAA wakiwasilisha na kuwaombea vibali vya ajira kwenye wizara ya kazi, marubani wa kigeni kwa madai hatuna marubani wazalendo au hatuna vigezo fulani. Kwa hiyo wawe makini wakati wa kutoa taarifa sio ya kweli.

2.4 TAOA itambue kwamba chama cha marubani kama vile chama chao na vyama vilivyosajiliwa nchini sio cha "watu wasiojulikana" labda ya kwao TAOA inawasimamia waendesha makampuni ya ndege "wasiojulikana" kwa maana wengi wao ni wa nje ya nchi.

Hatujawahi kuchukua majukumu kama vile TAOA ilivyodai, sisi tunachangia mada na kutoa mapendekezo kama katiba inavyoruhusu.


3.0 MABADILIKO KATIKA SEKTA

3.1 Ni kweli awali marubani na wahandisi wa ndege waligharimiwa na serikali / wafadhili. Mfumo huu ulisitishwa mwaka 1990 na sio 1980 kama inavyodaiwa na TCAA. Kozi namba 14 ilikuwa ya mwisho kugharamiwa na serikali iliyofanyika Soroti, Uganda. Masharti yaliyotolewa na benki ya dunia/ international Monetary Fund, (I.M.F), ambayo yalihusisha nchi nyingi ikiwemo Kenya, Uganda na Tanzania kuwepo kwa mfumo wa ‘cost charing'. Wenzetu Uganda walianza kutumia mfumo huu, yaani serikali ikachangia asilimia 90 na wazazi asilimia 10 ya gharama za mafunzo. Viongozi wa D.C.A, (TCAA ilivyojulikana wakati huo), walikuwa na mfumo mbadala.

Waendeshaji wa makampuni ya ndege humu nchini walitakiwa kuchangia mfuko wa mafunzo. Wenye makampuni ya ndege na watoa huduma katika viwanja wa ndege walibebeshwa mzigo kwa kupitishwa na utaratibu wa ukusanyaji wa fedha na TCAA ijulikanayo Training Fund. Lakini juhudi zao haziwezi kuziba pengo la uhaba wa marubani Tanzania. Hivyo wazazi wengi wamekua wakipeleka watoto wao kusomea hii fani kwa gharama kubwa. Mategemeo yao yakiwa ni vijana hao kupata ajira hapa nchini baada ya kuhitimu. Rubani anapomaliza mafunzo ya awali anakuwa na masaa kati ya 200 hadi 250. Baada ya hapo hurudi nchini kwake ili nchi husika iliyo na mfumo mzuri wa mambo ya usafiri wa anga, inamuendeleza katika kujenga masaa ambayo ndiyo uzoefu ya kuruka angani / utaalamu wa kuendesha ndege ya aina fulani mathalani Cessna Caravan, Dash 8, Twin Otter n.k.


4.0 MAHITAJI YA TAASISI ZINAZOTOA BIMA YA NDEGE NA MIKOPO

4.1 Ndege huwekwa bima kubwa ya ajali hivyo taasisi ya bima na benki zinaweka masharti magumu (masaa ya kuruka mengi ambayo marubani wanaoanza hawana) Ndugu waTanzania kwenye ndege, huwa kuna rubani mkuu (captain) na rubani msaidizi (first officer/co-pilot). Rubani anayekubalika na bima na kuwajibika chochote litokalo ni rubani mkuu, kwa vyovyote vile atakua na masaa mengi tu. Huyu rubani msaidizi ataruka chini ya uangalizi wa rubani mkuu, kwa hiyo rubani msaidizi hahusiki na jinsi bima itakavyoandikwa na kutumika na yale masharti magumu ya bima haimhusu huyo rubani msaidizi kama vile wanavyodai TCAA.

Kama tulivyotaja awali, ni nchi husika kuwa na mfumo mzuri wa usafiri wa anga na kwa mfumo huu vijana wanapata uzoefu na kuweza kukubalika na masharti ya bima. TCAA haitafakari wala kujadili na wadau mambo kama haya. Huu mfumo unatumika na mashirika ya ndege mengi duniani kote, huku kwetu Afrika kuna mifano mingi: Air Tanzania, Ethopian Airlines, Egyptair , n.k. Marubani wote wazoefu wa Tanzania walioruka na wanaoruka kwenye ndege zinazotumiwa na marais wetu kuanzia hayati Mwl. Nyerere hadi Mhe Jakaya KIkwete na viongozi mbalimbali na pia marubani waliomo kwenye makampuni mbalimbali walianza hivyo.

5.0 KUTEREREKA KWA SHIRIKA LA NDEGE LA TAIFA- AIR TANZANIA (ATCL)

5.1 Kama walivyoelezea TCAA ni kweli kuterereka kwa ATCL kimeathiri pamoja na mambo mengine aijra ya marubani. Hii ndiyo iwe sababu ya kuwaachia marubani wa nje kuja kugeuza Tanzania kuwa shamba la bibi na kufanya wanachotaka katika nchi yetu? Mwaka 2009 wakurugenzi wa idara zote ATCL wakiwemo director wa operations na chief pilot , walipunguza marubani waTanzania waliosomeshwa kwa gharama nyingi kwasababu ya uhaba wa kazi kwenye shirika, na kuwachukua marubani wa kigeni watano wasiokuwa na vigezo stahiki na kuwasomesha nje kwa pesa ya walipa kodi.

Kwa hivyo tulikuwa na baadhi ya viongozi waliochangia kwenye msiba wa marubani kunyimwa haki yao ya kupata ajira nchini.
Tunaimani kubwa katika shirika la ATCL chini ya uongozi mpya wa marubani na wahandisi kuliendeleza vyema ATCL.

6.0 MADAI YA CHAMA CHA MARUBANI TANZANIA KUHUSU MFUKO WA MAFUNZO YA MARUBANI NA WAHANDISI NDEGE

6.1 Tunapongeza juhudi za serikali kukabiliana na uhaba wa marubani nchini na kuimarisha na kusaidia vyuo humu nchini. Serikali inabidi itazame upya jinsi ya kuwawezesha vijana kwa kuwapatia mikopo ya masomo ya juu ili waweze kukamilisha mapungufu madogo na kuanza kazi mara moja hivyo kupunguza uhaba wa marubani hivi sasa.

6.2 Uongozi wa TCAA imechukua mapungufu ya uhaba wa marubani kama chambo katika maslahi yao binafsi. Waliochaguliwa wengi wao hawajakidhi au hawana sifa zilizo tangazwa magazetini, baadhi yao hawajafanyiwa vipimo maalum vya kiafya.

Baadhi ya vijana waliotuma maombi yao, walijibiwa na barua kutoka TCAA ikitamka: serikali imesitisha kusomesha wanafunzi kwa hivyo wajitegemee kufanikisha malengo yao.

Wamiliki wa makampuni wamelalamika kwamba mchango wao haujalenga wanafunzi waliostahiki kwani kulipa $65,000 kwa mafunzo tu kwa kumsomesha rubani mmoja na bado kuna madai ya kupelekewa fedha ya malazi na mahitaji mengine kwa kila moja wao. Idadi ya waliopelekwa Afrika Kusini chuoni ni 5, na kwa vile baadhi ya wamiliki wa makampuni hawakuhusishwa kwenye mchakato wa kutathmini kwani walikuwa na ndege au hata ‘simulator' ya kufanya hivyo. Walipendekeza kwamba marubani wazawa ambao wamefikia 40 leo, waliohitimu mafunzo mda mrefu wako kijiweni hivyo basi wasaidiwe kumalizia ratings zilizosalia kwa fedha na mda kidogo ili wajiunge na makampuni hapa nchini na shughuli hiyo ingefanyika humu nchini.

Wenye makampuni pia wamedai kwamba hata hao waliopelekwa Afika Kusini, wakihitimu, shida iko palepale ya masaa 500 hadi 1,000 yanayotakiwa kabla ya kumuajiri rubani Hivyo hakuna lililo fanyika kwa makini. Labda TCAA iwalazimishe wenye kumiliki makampuni kubadilisha mfumo wa kuajiri vijana hao wapya tena itakuwa upendeleo mkubwa kuwatafutia hao wapya kazi mbele ya waliofuzu mwanzoni.

7.0 USHAWISHI

7.1 Tunapenda kutoa shukrani nyingi kwa kampuni kama NorthenrAir, Tanganyika Flying Company kwa kuanzisha mfumo wa kusaidia vijana wetu katika kujenga masaa ya kuruka na kuwalipa posho nzuri. Hii imetokana na maamuzi yao binafsi baada ya kuona umuhimu wa kuajiri wazalendo. Mashirika mengine yanatakiwa kuchangia vivyo hivyo. Badala yake yanaleta vijana toka nje ili waje kujenga masaa hapa kwetu halafu warudi kwao wakiwa na uzoefu.

8.0 VIKAO VYA WADAU

8.1 TCAA kama kawaida yao katika mikutano ya wadau, chama cha marubani ambacho kina marubani wazawa na wanao changia katika sekta hii muhimu ya uchukuzi hatualikwi.

Kama tungealikwa, tungeshauri kuwa kutoa CV's za hawa marubani vijana wazalendo kwa uongozi wa mamlaka ya usafiri wa anga, TCAA ili zitangazwe katika TOVUTI ya TCAA haita saidia kwa sababu kama zilizotolewa katika taarifa ya TCAA magazetini ya tarehe 19/11/2013. Vijana hawana uzoefu, je watamvutia mwajiri gani? Na kutoa taarifa kwamba TCAA haihusiki katika masuala ya ajira. Tusikwepe majukumu, tuwajengee vijana wetu njia ya kujenga masaa, ndiyo tuwatoe kwenye tovuti badaye wakiwa wamebobea.

9.0 KUSHAURI UDHIBITI WA AJIRA KWA WAGENI

9.1 Tutashukuru Kama TCAA imefanya hivyo. Ikumbukwe tatizo hili kimekuwa sugu na tumevutana sana tukiomba tuhusishwe katika kutoa vibali vya ajira kwa marubani wa kigeni. Hadi leo ombi letu limegonga mwamba. Tunasema chama cha marubani kina uwezo wa kutambua ni rubani yupi mgeni mwenye sifa atatufaa nchini. Badala yake, tunapokea marubani wa kigeni ambao wengine hawana hata sifa stahiki.

9.2 Tunasikitishwa sana kwa kauli ya kamishna wa idara ya kazi, kwenye majibu yake kwa mkurugenzi mkuu, TCAA kuhusu chama chetu kisihusishwe. Yeye anaelezea kwamba mamlaka (TCAA) ilikuwa ndio inawakilisha sekta ya uchukuzi wa anga, hivyo hawana haja ya kuhusisha chama cha marubani .

Kwa hivyo basi, mamlaka- TCAA bado inaingilia maswala ya ajira ya marubani na wahandisi wa ndege, Tanzania. Tumejaribu kufuatilia na wizara ya kazi na TCAA kuhusu suala hili; wote wanatupiga chenga na kupuuza maombi yetu ya kutafuta ufumbuzi wa suala hili Tuna ushahidi wa kutosha kuonyesha jinsi hata barua zetu hawataki kuzipokea na hawapendi kutuona ili kuongea nao ofisini mwao.

10. 0 HOJA TATHMINI YA KISAIKOLOJIA KWA WATAHINIWA ILIFANYIKA OFISINI NA SIO KWENYE NDEGE

10.1 Unapotaka kupata kijana anayefaa kwenda kwenye mafunzo ya urubani yapaswa kuzingatiwa vilevile:
(a). anatakiwa awe na elimu stahiki
(b). anafanyiwa tathmini kwa kuruka angani (familiarization - aptitude test)
(c). anaruka na mkufunzi (rated instructor on type)
(d). vipimo vya afya yake kikamilifu.

Wote hao watano waliochaguliwa hawajakidhi baadhi ya vifungu tulizotaja hapa juu, na wengine hawajakidhi zote hapo juu. Vilevile, mtaalam wa urubani mzoefu kutoka TCAA aliyehusika hakuwa na ujuzi (type rating) ya ndege iliyokusudiwa kutumika. Pia, rubani aliyetumika kutoka wakala wa ndege za serikali TGFA, hakuwa mkufunzi kwenye aina ya ndege- Piper Navajo; PA-31 yenye namba ya usajili 5H-ILS, ndege ambayo ina injini mbili.

Sababu labda kwa kuwa wakufunzi wote wako kwenye chama cha marubani, PATP, na hawakutakiwa kujumuishwa. Ndege iliyotumika siyo kwa ajili ya vijana wanaoanza mafunzo. Ile ndege PA-31 Navajo, inatumika kwa marubani waliobobea kuruka na wenye uzoefu wa si chini ya masaa 250 na kuendelea na ni kwa ajili ya kupata multi engine rating (leseni ziada ya ndege yenye injini mbili) au Instrument rating( leseni ziada ya kuruka kwa kuangalia na kufuata vifaa maalum vinavyoongoza ndege wakati wa hali mbaya ya hewa). Lakini kwa kuwa ndege hii ilikuwa na matatizo ya kiufundi haikuweza kutumika kutathmini wanafunzi hao na hivyo wakahamia ofisini huko waliruka na makaratasi. Tunajiuliza ni kwanini mambo haya yote yalifanyika kwa haraka na bila mipangilio?

11.0 MARUBANI WAZOEFU AMBAO HAWAJAPATA AJIRA

11.1 Tatizo kubwa inafahamika kama hivi:
(a). baadhi ya makampuni ya ndege yanaendesha biashara kwa njia za mkato na hawatumii fedha zao katika kumboresha rubani wao haswa kama wewe ni mTanzania.
(b) mara nyingi utakuta hata katika ndege mpya walizonunua baadhi ya wamiliki wa ndege humu nchini hawabadilishi vifaa vibovu au kuvitengeneza na kuwa katika hali ya ubora ikumbukwe hii ni chombo kinacho ruka angani sio toroli ya mchanga unaegesha pembeni ikizimika.
(c). ushahidi upo wa baadhi ya wamiliki wa makampuni hawajali ushauri ya marubani kwenye masuala ya usalama wa anga, n.k
Kwasababu za kiusalama marubani wazoefu wamekuwa wakitoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu uvunjwaji wa sheria za anga na kwa usalama wao. TCAA inakiuka sheria ya kimataifa ya anga (ICAO regulations) kwa kupeleka taarifa hizo kwenye makampuni kwa maslahi yao hivyo basi kutoifanyia kazi tatizo la kiusalama badala yake wanajenga mahusiano na tabia ya kuwapendelea matajari. Marubani wengi waliolalamika ukiukwaji na uvunjaji wa sheria za usalama za anga wamepoteza kazi zao, na kuajiriwa tena inakuwa vigumu sana.

Bado kuna upendeleo katika kutolewa leseni za urubani. Kuna wahandisi pia wamejikuta wamekaa zaidi ya miaka 4 bila leseni za Tanzania, lakini wamesomea uingereza na kukarabati helikopta ambayo inaruka nchini. na hakuna wahandisi wataalam katika kitengo cha airworthiness TCAA mwenye leseni ya uhandisi wa helikopta Basi kwa mfumo huu sisi wazawa tutapata lini kupata msaada kama wanavyopewa wa nje??

Kwavile marubani wengi nchini hawana mikataba ya kazi, serikali nayo inakosa mapato yake, marubani wazoefu hawamo katika mfuko wa kijamii hivyo wanakuwa makini na makampuni ipi inayo mfumo mzuri wa mikataba inayoendana na hali ya maisha ya leo. Kwa hivyo rubani mzoefu mTanzania hapewi ajira na badala watamchukua kijana mgeni (wa nchi za nje) mwenye masaa machache na kumweka kazini bila mikataba, na kwavile huyo kijana anataka ili mradi masaa ya kujenga na japo posho kidogo. TCAA inaubavu wakutuuliza eti tujiulize kwa nini marubani wazoefu hawana kazi??.

Labda tujiulize ni kwa nini hatupewi ajira ndani ya TCAA au Wizarani tuyarekebishe haya.

12.0 HITIMISHO

12.1 Mamlaka ya Usafiri wa Anga, TCAA ni kwa usalama wa nchi yetu. Mtanzania anapojinyima ili amsomeshe mtoto wake ni kwa faida ya nchi yetu na usalama wa anga letu. Kama mamlaka haihusiki na matatizo ya marubani waTanzania kwasababu eti haikuhusika katika mchakato wa wao (vijana wanaojisomesha wenyewe) kwenda mafunzoni, mamlaka (TCAA) itatambua nini siku ikifika Rais wetu anaruka katika ndege TANZANIA ONE inayoendeshwa na marubani wa kigeni, Polisi Anga ndege zinarushwa na marubani wa kigeni, Jeshi letu la anga ndege zinarushwa na marubani wa kigeni, na mwishowe mamlaka ya usafiri wa anga TCAA utakao ongozwa na wageni??!!
Tunathamini sana mchango wa mamlaka vivyo hivyo mamlaka TCAA isikilize na kufanyia kazi ushauri wetu.

TUSIGOMBANIE FITO WAKATI NYUMBA TUNAYOIJENGA NI YETU SOTE.

-KAMATI YA UTENDAJI
CHAMA CHA MARUBANI, TANZANIA, (PATP)
 
Hapana,

Hawa wanahitaji msaada,hatuwezi kujipuuza kwa kiwango hiki.

Wanasiasa mliojaa humu mje hapa mtoe mchango wenu maana hizi ndio issues.
 
Hapana,

Hawa wanahitaji msaada,hatuwezi kujipuuza kwa kiwango hiki.

Wanasiasa mliojaa humu mje hapa mtoe mchango wenu maana hizi ndio issues.

Hii ni Agenda mpya, ambayo wanasiasa wanapashwa kuikomalia. Huu ni mwendelezo wa nchi kuwadharau wasomi wazawa.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom