Uepukaji utapeli katika mauziano ya Ardhi na Nyumba

Mahesabu

JF-Expert Member
Jan 27, 2008
5,963
3,805
Na Mwandishi wetu
10th June 2011
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka ambaye ana dhamana ya kusimamia masuala ya ardhi.
Utapeli katika mauziano ya viwanja vya ardhi na nyumba umekithiri Tanzania japo hakujawa na takwimu toshelezi katika jambo hili.
Sababu kubwa za kushamiri utapeli wa ardhi Tanzania ni kwanza kutozielewa sheria na taratibu za uuzaji na ununuaji ardhi (kama zilivyoainishwa katika Sheria za Ardhi ya 1999 (namba 4 na 5) na pia sheria ya Usajili wa Ardhi (Sura ya 334) pamoja na sheria za mikataba na ushahidi, na kanuni zake.
Pili, tamaa ya mnunuzi kutaka kujipatia kiwanja haraka anapoamini amepata ‘dili' ya bei rahisi. Tatu, kukosekana kwa mfumo madhubuti na rahisi (kwa makaratasi na ki-kompyuta) kufikiwa kwa haraka Orodha Kuu ya Ploti za Ardhi na wamiliki wake (Land Titles Registry) na kila raia wa nani anamiliki ploti fulani ya ardhi.
Nne, kutokuwepo kwa Vitambulisho vya Taifa (National Identity Cards) kulikosababisha kuwepo nyaraka tofauti tofauti na wakati mwingine zisizoeleweka kuhusu watanzania.
Tano, kuwepo kwa wanasheria wachache (na wachache zaidi waliobobea katika masuala ya ardhi nchini). Sita, kukua na kusambaa nchini kwa matumizi ya teknolojia za kisasa kama programu za kompyuta zinazotumiwa na matapeli kutengeneza nyaraka feki na pia matumizi ya internet kujifunza mbinu za kisasa za kitapeli kwingineko duniani.
Saba; kiwango kidogo cha upelelezaji, ukamataji, ushtakiwaji na utiwaji hatiani wa matapeli wa ardhi nchini. Nane, kutokuwepo na utoaji taarifa na pia ufuatiliaji makini wale wanaotapeliwa. Tisa, kukosekana kwa Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Utapeli katika Nyaraka. Kumi, kutelekezwa kwa muda mrefu kwa viwanja ambavyo haviendelezwi na wenyewe kuwa mbali na viwanja hivyo kunakotoa mwanya kujitokeza ‘wamiliki' feki.
Kumi na moja, kukithiri kwa rushwa na kukosekana kwa maadili ya watendaji wa ardhi na katika serikali zilipo ardhi husika.
Maswali ya kujiuliza kabla ya kununua ardhi
Mnunuaji ardhi au nyumba yeyote mwenye busara hupaswa kujiuliza maswali makubwa matatu kabla hajafikia uamuzi wa kununua ardhi au nyumba: Mosi, je, muuzaji huyu anamiliki kweli hicho anachokiuza? Iwapo jibu hili ‘NDIYO' haitoshi kuishia hapo. Swali la pili ambalo linafuata ni, je, huyu ‘anayemiliki' anamiliki kihalali?
Kutojiuliza swali hili au kulifuatilia ndicho kiini hasa cha mamia ya watu kutapeliwa mamilioni katika manunuzi feki ya ardhi kila kukicha. Hii ni kwa sababu hutokea mtu akawa anaishi, kudhibiti au kuingia na kutoka bila wasiwasi mahali ilipo ardhi husika na tena kwa kipindi kirefu kiasi cha kuweka mazingira rahisi ya kuwapumbaza wengine waamini ni ardhi yake, kumbe unakuta aliachwa tu aangalie mahali hapo mwenyewe akiwa mahali pengine. Katika hili, lipo kundi la matapeli ambalo pia hutumia mwanya linapoona ardhi fulani yenye thamani iliyoachwa au kutelekezwa bila kuendelezwa kwa muda mrefu, kuitengenezea nyaraka feki na hata wakati mwingine kushirikiana na watendaji wa serikali za mitaa au vijiji husika na baadhi ya maafisa ardhi kufanya mitambo yao ya kitapeli iaminike zaidi.
Hili limekuwa tatizo sugu hasa maeneo ya mijini na pembezoni mwa miji kama Mbezi Beach, Tegeta, Boko, Mtoni Kijichi, Kigamboni na kwingineko ( Dar es Salaam) .
Basi katika hili mnunuzi sharti ajifunze kutoamini haraka haraka kila nyaraka au ‘mashahidi wa kuaminika' katika eneo ilipo ardhi au nyumba husika. Ni budi kutafiti zaidi.
Swali la tatu muhimu ambalo mnunuzi anayetaka kununua kiwanja au ploti ( iwe wazi au imejengwa ) ni kufanya utafiti zaidi. Ni vema ukasisitiza kuchukua hata nakala ya hati yoyote inayoonyesha majina ya muuzaji, picha yake (kama ndiye anayekuuzia basi angalia picha yake ifanane na picha iliyoko katika hati hiyo ), anuani yake, mwajiri wake na kadhalika na kisha wewe mwenyewe (na ni hekima zaidi nyote wawili pamoja) muongozane hadi ilipo ofisi ya ardhi ya serikali mkalithibitishe hilo. Kama unajali zaidi thamani ya fedha yako na kuepuka kufa kwa presha pale itokeapo ukabaini baadaye umetapeliwa, basi ni busara ufunge safari hadi katika ofisi ya Msajili wa Hati za Ardhi Tanzania ( Registrar of Titles ) ambayo iko ghorofa ya Kwanza katika jengo la Wizara ya Ardhi na Makazi, jijini Dar es Salaam (ghorofa ya kwanza). Ofisi ya Msajili wa Hati ina nyaraka zote zinaoonyesha nani ni mmliki halali wa kila ardhi iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Ardhi Tanzania.
Japo utapeli ni mgumu kuuzuia kwa asilimia 100 (hasa pale uhalifu unapojumuisha mtandao wa wahalifu wenye kushirikiana na maafisa husika na pia kuwa na uelewa au uzoefu mkubwa wa masuala ya sheria na uchakachuaji nyaraka) bado unaweza kuuzuia ukitumia uangalifu, tahadhari na ufuatiliaji makini zaidi (due diligence).
Na umuhimu mwingine wa kukagua Rejista ya Hati za Ardhi ( Land Titles Registry ) ni kwamba kupitia hapa , utaweza kubaini kama hiyo ardhi haina migogoro au maslahi ya wengine kisheria, kama vile rehani za kibenki, madai ya wengine kisheria katika ardhi hiyo na kadhalika.
Mambo haya yasiyoonekana kwenye hati yanajulikana kisheria kama (encumbrances) na yanaweza kukufanya ununue ploti na baadaye ukashangaa kukutana na watu wenye maslahi ya umiliki sehemu au yote katika ardhi hiyo yanayotambulika zaidi kisheria kuliko yako.
Kupitia ofisi ya Msajili wa Hati za Ardhi, unaweza kupambanua mchele na chuya kwa kulinganisha Hati ya Umiliki Ardhi (Land Title Deed) unayoonyeshwa na muuzaji pamoja na Hati (na Picha) iliyomo katika faili la Serikali.
Hadi hatua hii utaweza kujua kama hicho ulichoonyeshwa na muuzaji ni jua au mbalamwezi kwa maana ni hati halali au feki.
Mara nyingi unapofikia hatua hii, wauzaji matapeli wa kawaida wanakuwa hawataki kuendelea na biashara au wanaingia mitini na usiwaone tena kwa kuogopa kuumbuka.
Umuhimu wa kutumia Wanasheria
Lakini haya tu hayatoshi. Kuna jambo moja la msingi kuliko yote, ambalo wengi wa wanaotapeliwa ardhi hulidharau au kutolizingatia: Kukubali kutumia fedha kidogo kutumia wataalam waliobobea katika masuala haya ya ununuzi wa ardhi (Conveyances).
Unaweza kupata majina ya wanasheria wote wa Tanzania (na pengine maeneo waliyojikita zaidi) kupitia Kituo cha Haki na Demokrasia ( Kinondoni Studio, Dar es Salaam; Chama cha Wanasheria Tanzania ( TLS ), Kamati ya Msaada wa Kisheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (kila Ijumaa), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ( LHRC ), Kijitonyama au Kinondoni, Dar es Salaam; Ofisi ya Mawakili katika Mahakama Kuu ya Tanzania; Chama cha Msaaada wa Sheria Tanzania (NOLA), Sinza Africa Sana, Dar es Salaam), Chama cha wanasheria Wanawake (TAWLA); WLAC; Vyama vya kisheria visivyo vya kiserikali; Shule/Vitivo vya Sheria katika vyuo Vikuu; Maktaba za Serikali na zile za Sheria, Ofisi za Wanasheria Mbalimbali; Vyombo vya Habari; mtandao wa internet; Vitabu vya Orodha za Majina ya Posta/simu au kuuliza kwa watu wanaoaminika.
Ni muhimu sana kutumia wanasheria kwa sababu ya elimu na uzoefu wao katika masuala haya.
Elimu itakayokusaidia usitapeliwa kirahisi
Ni muhimu pia kujielimisha binafsi katika masuala ya ardhi, yakiwemo manunuzi yake. Yapo machapisho mengi ya kuanza nayo lakini machapisho muhimu zaidi katika kuzielewa sheria za ardhi uuzaji wake (Conveyanves) ni yale yaliyoandikwa na marehemu Profesa Zebron Gondwe, Profesa Gamaliel Mgongo Fimbo, Profesa Ringo Tenga (Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye kile cha Tumaini); Dk. Kennedy Gastorn, Profesa Rodney W. James na mhadhiri wa Sheria Ebenezer Mshana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kitabu cha Sheria za Mikataba cha Profesa Nicholasu Nditi nacho ni muhimu sana kuijua sheria hiyo ilivyo nchini kwa vile hutumika sana katika masuala ya ardhi pia.



CHANZO: NIPASHE
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom