UDSM yaelemewa

jyfranca

JF-Expert Member
Oct 3, 2010
297
8
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam kimeelemewa kutokana na uhaba wa malazi na huduma za chakula kwa wanafunzi.
Hali hiyo inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na chuo hicho kwa mwaka wa masomo wa 2010/2011.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wa mwaka wa pili hadi wa nne wametishia kufanya maandamano ya amani wakiwa wamevaa mashuka na sahani mkononi, wakati wa kumpokea Waziri Mkuu Mizengo Pinda, atakapowasili chuoni hapo. Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Wanafunzi hao wamedhamiria kufanya hivyo, ikiwa ni namna ya kuwasilisha malalamiko yao juu ya matatizo yanayowakabili kwa upande wa malazi na chakula. Kwa mujibu wa madai ya wanafunzi hao, zaidi ya wanachuo 5,000 wamechaguliwa kujiunga na chuo kwa masomo ya shahada za fani mbalimbali, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na uwezo wa chuo.
Ongezeko hilo kwa mujibu wa wanafunzi, limesababisha ukosefu wa vyumba vya kulala na kuchukua muda mrefu kupata huduma ya chakula katika kantini zilizopo chuoni, wakidai inawachukua zaidi ya saa mbili kukaa kwenye foleni kwa ajili ya kupata chakula.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata, zinadai wanafunzi kupitia viongozi wao, walifikia hatua ya kuandamana baada ya kuona kero hizo hazijapatiwa ufumbuzi. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani, kilifunguliwa Novemba 15, mwaka huu, ambapo wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliripoti wiki moja kabla na baadhi kupatiwa vyumba, wengine walikosa na kulazimika kwenda kupanga uraiani.

“Chuo hiki wanasoma watoto wa wakulima, ambao hawana uwezo wa kulipa gharama kubwa za malazi maeneo ya uraiani, hivyo wamekuja na mashuka kutoka nyumbani kwao na hawana vyumba wala vitanda, wanalala chini na kujifunika mashuka yao,” kilieleza chanzo chetu cha habari.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mwaka jana chuo kilichukua wanafunzi 3,000, lakini kulikuwa na matatizo lukuki na hakuna kilichorekebishwa. Licha ya kutokuchukua hatua zozote, mwaka huu wanafunzi wa mwaka wa kwanza wameongezeka hadi 5,000.

Akizungumzia madai hayo, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema ni kweli kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo mwaka huu.

Profesa Mukandala alisema wanafunzi waliochaguliwa kwa mwaka huu ni 5,130 lakini mpaka sasa waliodahiliwa ni 3,450.

Alisema uzoefu unaonyesha wanafunzi huomba nafasi lakini baadae hushindwa kuanza masomo, hivyo idadi hiyo inaweza kupungua. Alisema uongozi wa chuo hauhusiki kwa lolote kwa kuwa kazi ya kuchagua wanafunzi ilifanywa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Profesa Mukandala alisema hata mwaka 2006, wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo kwa mwaka wa kwanza walikuwa 5,000 lakini waliodahiliwa walikuwa 3,000.

Kuhusu tatizo la malazi, alisema kila mwaka kuna baadhi ya wanafunzi wanapata nafasi katika hosteli za Mlimani, Kijitonyama na Mabibo, lakini wapo wengine wanatafuta vyumba maeneo mengine.

Alisema mwaka 1961 wakati chuo kinaanza kilikuwa na wanafunzi 14, lakini mwaka huu wamefikia 18,000, hivyo lazima kuwe na utatuzi wa changamoto za miundombinu, vifaa na hata walimu, mambo ambayo yamewekewa mkakati wa kuyaboresha.

Kuhusu maandamano ya wanafunzi, alisema: “Sina taarifa juu ya wanafunzi kupanga kuvaa mashuka, lakini inapotokea mpo kwenye mazingira na watu wengi wenye mitazamo tofauti, huku kukiwa na ushawishi mwingi, inawezekana wakafanya hivyo.”

Juu ya utaratibu wa chakula, Profesa Mukandala alisema wamejitahidi kuweka maeneo sita ya wanafunzi kupatiwa chakula, ambayo ni Kafteria 1 na 2, Hill Park, Kiswahili, Yombo na Uhandisi.

Alisema kupanga foleni ni utaratibu wa kawaida kwa kuwa muda wa chakula wanafunzi wanatoka kwa mkupuo, hivyo inabidi wasubiriane. Hata hivyo, alisema hana uhakika kama wanaweza kupanga foleni kwa zaidi ya saa mbili.

Wakati huo huo, mgogoro wa wanafunzi 440 walioshindwa kudahiliwa na Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa ngazi ya shahada kwa mwaka wa masomo 2010/2011, umechukua sura mpya.

Hatua hiyo inatokana na wafanyakazi kuwaunga mkono wanafunzi na kumtupia lawama Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Hosea Rwegoshora.

Wafanyakazi hao wamedai Profesa Rwegoshera anaendesha taasisi kimaslahi na ndiyo sababu ya kushindwa kutatua matatizo yanayoikabili.

Akizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa wafanyakazi wa taasisi hiyo, alisema matatizo yanayojitokeza yanazuilika iwapo mkuu huyo atakuwa imara.

“Serikali ya wanafunzi (ISWOSO) ilishaandika barua mara kadhaa kuhusu matatizo yanayojitokeza, ili kupatikana kwa muafaka lakini mkuu wetu hataki kubadilika,’’ alisema.

Alisema suala la kutokuwa na bodi ya uongozi wa taasisi si chanzo cha kushindwa kudahili wanafunzi, kwani uwezo wa kufanya hivyo upo.

“Wanafunzi ni wengi na wangeweza kudahiliwa wakati mambo mengine yakiendelea taratibu. Pesa ya wanafunzi kutoka bodi ya mikopo imekwishafika.
Kama wanafunzi wangedahiliwa hata mgomo unaotangazwa hauwezi kutokea,” alisema.

Mtumishi huyo aliiomba serikali kuwa makini na kumsadia Profesa Rwegoshora kudhibiti migogoro ya mara kwa mara, ili wanafunzi wasome kwa amani.

Majina ya wanafunzi yameshatolewa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Akizungumzia mgomo huo wa wiki ijayo, Spika wa ISWOSO, Chrisant Mutatina, alisema wamechoka kusubiri na sasa wataonyesha mambo kwa vitendo.

Mutatina alisema wametoa muda wa kutosha kwa uongozi kulifanyia kazi suala hilo, lakini jambo la kushangaza umeshindwa kulipatia ufumbuzi.

Profesa Rwegoshora alipotafutwa na gazeti hili kwa njia ya simu ya mkononi hakuweza kutoa ushirikiano wa kutosha, akidai yupo nje kikazi.
 
Dr. Chungu amekazana kukaribisha wawekezaji kwenye ardhi ya chuo badala ya kujenga madarasa na sehemu za malazi. Kuna mambo tunafanya hakuna mchawi ni sisi wenyewe. Sasa zile investment zimeongea nini kwenye infrastuctures za chuo au ndio zimetengeneza ajira kama tunavyosikia?
 
Kila mwaka matatizo yaleyale tu and this is supposed to be our venerable institution.....
 
Back
Top Bottom