Udsm kuna ukata, Ndalichako unalijua hilo?

Foundation

JF-Expert Member
Nov 25, 2010
1,421
596
Wanabodi.

Wote tunajua Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni miongoni mwa vyuo vikongwe hapa Tanzania na hata Afrika. Chuo hiki kwa sasa kipo kwenye ujenzi wa miundombinu hasa Mabweni, Maktaba na Majengo mengine. Ujenzi huu ulianza kipindi cha uongozi wa Rais Mstaafu Mh. Jakaya Mrisho Kikwete kupitia mpango wa kuendeleza Elimu ya Juu. Ujenzi kama huu ulifanyika pia Vyuo vya DIT, MUCE, DUCE, Chuo Kikuu Huria Tanzania. Ujenzi wa Mabweni na Maktaba umeanza wakati huu wa Mheshimiwa Magufuli.


Tunajua wote ili Chuo kiwe bora ni lazima mazingira ya kufundishia yaboreshwe(miundombinu), motisha kwa watumishi na Ruzuku itolewe kwa Chuo ili kiweze kujiendesha.

Mheshimiwa Ndalichako unajua kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina Ukata? Chuo hicho Kikongwe ambacho wewe ushawahi kuwa Mhadhiri wake kinashindwa kulipa pesa ya kutuma Tasinifu(Dissertation) nje ya Tanzania? Unajua kwamba kuna Tasinifu(Dissertation) zinakaribia Mwaka, hazijarudi mpaka leo? Unajua kwamba kuna zingine hazijaenda kutahiniwa(External Examination) zaidi ya miezi nane sasa kisa chuo hakina pesa? Huwenda Mukandara hakuambii, sasa mimi nakuambia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina ukata, Wakuu wa Idara, Shule na Vyuo wanalalamika chini kwa chini. Wanaogopa kusema kwa Sauti. Mimi nimeamua kukuambia Mheshimiwa Ndalichako.

Tunajua Serikali inajenga Miundombinu, tunajua pia Chuo kina mpango wa kuongeza Udahili wa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Uzamifu. Sasa Mheshimiwa, nani atakuja kusoma Chuo hicho kama Pesa ya kutuma Tasinifu(Dissertation) mnashindwa. Lakini wanafunzi wanajiuliza Ada wanalipa lakini kitu kidogo hicho kinawashinda. Au mnataka Wagome kama wanavyofanya Shahada ya Kwanza. Hawawezi kugoma, wana mambo mengi ya kufanya.

Mheshimiwa Ndalichako, ili kuthibitisha pitia Chuo cha Uhandisi(CoET) ili uone rejista ya Tasinifu zilizotumwa na zilizopo chuo. Utashangaa kuona zilizotumwa zinakaribia mwaka, hazijarudi mpaka sasa. Utashangaa kuona, zingine zililetwa chuo na wanafunzi wa shahada ya Uzamili zaidi ya miezi nane, hazijatumwa mpaka leo, zinapigwa vumbi tu kwenye makabati ya ofisi za Wakuu wa Idara. Wakuu wa Idara wanasema UKATA, wanaogopa kusema kwa sauti, wananong'ona kwa wanafunzi. Nenda Idara zote zikiwemo Idara ya Barabara(Transportation and Highway Engineering), Idara ya Rasilimali Maji( Water Resources Engineering) Idara ya Mihimili na Ujenzi(Structural and Construction Engineering), Idara ya Mitambo(Mechanical Engineering) nk ili uone uhalisia wa maneno yangu.


Ukifanya hivyo Mheshimiwa Ndalichako, huwenda VC Mukandara ataamka kutoka usingizini.

Mimi ni Mjumbe tu, na Mjumbe hauawi.


Nawasilisha.
 
Back
Top Bottom