Udini na Ugaidi ni uhalifu dhidi ya ubinadamu

Oct 5, 2015
88
476
UDINI NA UGAIDI
÷÷÷÷÷÷÷÷÷÷÷÷÷÷
Wakati vyombo vikubwa vya habari vikisongwa na habari za vita, hususani maeneo ya mashariki ya kati ambako vitendo vya kigaidi vimetamalaki, watu wengi huzipokea habari hizo kwa hisia za Kiimani. Pengine hilo ndio lengo hasa la wasusi wa vita hivyo.
Kumekuwa na dhana potofu ya kuhusisha baadhi ya dini na vitendo vya kigaidi. Lakini kwa bahati mbaya, wanadini wametekwa na mipango hiyo mahsusi na wao hujiona kama sehemu ya vita hivyo hata kama vita zenyewe hufanyika mbali na mipaka ya nchi zao.

Wakati majasusi wakipika vita kwa faida za kiuchumi na kijamii kwa mataifa yao, huku wakitumia dini na ugaidi kama viungo vya kupika vita hizo, wanadini huingia mkenge na kujihusisha na vita hivyo, kunaswa na mtego na kuharibu kabisa mifumo ya maisha katika mataifa yao, na zaidi kuharibu mantiki hasa ya maana ya dini.
Mtu anaweza kutengenezewa ugaidi, kisha akajikuta akiwa gaidi, na hiyo haimtofautishi na gaidi mwingine. Ikiwa dini imetumika kama nyenzo ya kumtengeneza mtu kuwa gaidi, basi dhana ingine huzaliwa, dhana ya udini.

Na. Christopher Cyrilo
Kitabu: Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi.
Mwandishi: Yericko Nyerere

"....Udini na Ugaidi ni uhalifu dhidi ya ubinadamu".
Udini na ugaidi ni uhalifu unaoweza kubomoa mustakabali wa maelewano baina ya mtu na mtu, au watu na watu na hata kundi moja la jamii ya watu na kundi linigne! Udini na ugaidi ni silaha inayotumika kwa kificho na mtu na/au watu wenye taathira ya woga na hutumia mbinu ya kuogepesha katika kutekeleza malengo yao. Kwa vyovyote iwayo, udini na ugaidi ni dhanna zinazofanana, isipokuwa, tofauti ni jinsi ya utekelezaji wa malengo yake. Kwa upande mmoja, katika Kitabu hiki cha Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi kinaangazia dhanna ya udini na kisha faslafa ya ugaidi katika kutoa mifano inayoweza kusaidia kuelezea hali halisi ilivyo na jinsi ilivyoasisiwa na inavyotishia amani ya dunia na kuvuruga maisha ya binadamu katika nyanja za siasa, uchumi na jamii.
Udini si dini. Na dini ni imani na njia ya maisha ya kiroho na ucha Mungu, Udini ni hali ya mtu kupendelea dini yake na kuifanya dini yake ni bora na inayostahili kutiiwa na kuheshimiwa kuliko dini ya mtu au watu wengine. Ni hali ya upendeleo wa fikra na mawazo ya kwamba watu wa dini fulani ndio wenye uhuru na haki ya kutawala maisha yote ya jamii, siasa na hata uchumi inapobidi. Ni imani ya kuwa bora kwa kundi moja la dini juu ya jingine. Pengine, udini ni ugonjwa wa kisaikolojia unaotokana na ubinafsi uliokithiri (kayaya) ambao humfanya binadamu kujiona yeye ni bora zaidi, na anachokiamini yeye, kila mtu yampasa aamini hata pasipokuwa na hoja za kisayansi zilizofanyiwa utafiti, kujaribiwa na kukubalika kuwa ni haki na kweli. Mazingira haya ya kujipendelea ni asili ya binadamu tangu utanguni, unaotokana na hali ya ubinafsi uliopindukia. (Rejea kisa cha Kaini kumuua Habili ambaye ni nduguye wa damu, tumbo moja na ziwa moja).
Udini hujionesha dhahiri kinamna namna hasa jinsi ya uendeshaji wa maisha ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, kwenye mazingira ya watu wenye mitazamo na falsafa tofauti juu ya imani na itikadi za dini (kwenye nchi ya dini mseto kama Tanzania).Umbile la udini huumbwa juu ya misingi ya: dhana mbaya dhidi ya binadamu wengine; roho ya chuki dhidi ya binadamu wengine; tabia inayoongozwa na uadui dhidi ya binadamu wengine; na mafundisho yasiyozingatia maisha huru, adilifu na yanayozingatia usawa.
Mafundisho yanayoatamiza fikira za udini, huathiri wafuasi wa dini husika juu ya kuwatendea binadamu wengine kinyume na uhuru, haki, usawa, uadilifu, na insafu kwa mujibu wa ujenzi wa ‘jamii ya watu walio sawa na huru’.
Uhuru ni zao la nafsi. Na mara zote nafsi huru ni ile inayojali nafsi za watu wengine katika kutamani kuwaona watu wengine wenye mitazamo ya kifalsafa na kiitikadi wakiishi maisha yenye staha na raha kama vile wanavyoishi wale wenye mitazamo ya falsafa kiitikadi zinazotofautiana nao. Huu ndio mwanzo wa maisha yanayozingatia thamani ya ubinadamu na utu wa watu wote kwa uhuru na haki ya kuishi kwa kutegemeana.
Sintofahamu, songombingo na sokomoko la kijamii, kisiasa na hata kiuchumi limewafanya binadamu kuwa kama wanyama wa mwituni wanaoishi pasipokufuata kanuni za asili za kimaumbile kwa mujibu wa maisha ya asili ya binadamu. Binadamu si mnyama na hawezi kuwa mnyama; japokuwa kifalsafa binadamu anaweza kuwa na mihemuko ya kikatili zaidi ya mnyama. Binadamu anaweza kumuua nduguye (k.v. Kaini alivyomwua Habili) na ndio kusema kwamba ni muhali kumuona simba akimuua simba mwenzie na kumtafuna hata akiwa na njaa (ya kufa). Binadamu mwenye hisia kali za chuki, uadui na uuaji ni hatari kwa vile anapopata nafasi ya kuwa juu ya wengine ndivyo anavyoweza kutumia nafasi yake ya kuwa juu kutamiza fikira zake za kujipendelea na kuwafanya wengine wasipate nafasi kama aliyo nayo yeye kwa mtazamo wa falsafa ya itikadi yake. Kutokana na mfumo wa maisha mseto tunayoishi binadamu tangu azali (mwanzo wa uumbaji na asili ya binadamu), tumewekewa sheria, kanuni na taratibu za silika kutofautiana kwa mitazamo ya kifalsafa na ya kiitikadi.
Hata hivyo, tofauti zetu hazikuwekwa kwa minajili ya kuwafanya wengine waonekane duni, dhaifu au dhalili mbele ya wengine, abadan! Isipokuwa ni tofauti zilizowekwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe ili kuwatofautisha binadamu wa jamii moja na wengine kwa mitazamo inayotofautiana lakini yenye asili moja.Tofauti nyingi zinatokana na fikira za upembuzi juu ya muktadha wa kuyaendea mambo yanayohitaji akili ang’avu ya utambuzi na jinsi ya kujitambulisha kama binadamu huru katika jamii ya watu wenye mitazamo huru na inayohitilafiana! Tofauti lazima ziwepo. Na, kwa tofauti hizo, zinazoruhusiwa na akili ang’avu na ya kawaida ndizo zinazotufanya tuwe na ‘uhuru wa maoni’. Kila mtu ana uhuru wa maoni. Na, kueleza maoni yake kwa fikira huru zinazozingatia uhuru na haki ya watu wengine. Udini unachukua sura ya unyama, kuwafanya watu wengine walazimishwe kukubaliana na utashi wa mtu, watu au kundi la watu wenye mitazamo ya kifalsafa na kiitikadi inayotofautiana na watu wengine.
Udini umezalishwa na watu na unaenezwa na watu wenye nia ovu na hisia za chuki au mawazo anzali yanye dhamira ya kupandikiza chuki ambayo ndiyo inayozaa uadui unaosababisha mbinu chafu za mapambano yanayogharimu maisha ya watu wasiokuwa na hatia.
Sasa, baada ya kuelewa dhanna ya udini, walau turejelee kwenye dhanna ya ugaidi na jinsi unavyochukuliwa na hata kupewa maana. Hapa, itafafanuliwa ugaidi ni nini, asili ya ugaidi na chimbuko lake kihistoria, na hata kutazama mifano baadhi. Hatimaye, tutaona ugaidi unavyohusiana na udini.
Ugaidi ni zoezi ovu linalotekelezwa na kundi fulani mathalani kuua, kupora kibabe, kutisha na kuwahangaisha watu ili kudumisha maslahi yao ya kibinafsi (tazama Kamusi ya Karne ya 21, Longhorn, 2011, ukurasa wa 518). Ukitazama fasili hii utafahamikiwa kwamba ugaidi ni uovu timilifu na unafanywa na watu waovu waliopindukia. Kwa misingi ya dini, uovu ni roho chafu na ya kishetani ambapo hakuna dini hata moja si tu kuunga mkono bali hata kuthubutu kuunga mkono kwa sababu uovu wa aina yoyote . Ugaidi unapingana vikali na misingi na sheria za dini na kwamba hakuna dini inayofundisha ugaidi, iwe dhahiri ama kwa siri kali.
Maisha ya binadamu yamejengwa kwenye msingi wa utu (yaani, u-bin-adamu wake). Na ndiyo kusema kwamba binadamu aliyekamilika ni yule anayetambua ubinadamu wake na anayejitambulisha kwa ubinadamu wake huku akizingatia maisha yenye msaada kimaana na kimaada kwa mujibu wa mwongozo wa haki unaotoka kwa Mwenyezi Mungu―Mwenyezi Mungu ambaye ndiye chanzo cha uhai!
Kwa maneno mengine, ukamilifu wa binadamu ni kuchagua kutenda mema.
Thamani ya binadamu ni uhai (pumzi) aliyopewa na Mwenyezi Mungu, Muumbizi; na hakuna awezaye kuchukua nafasi ya uumbizi wa thamani hii adimu na adhimu miaka dahari, pasipo mwisho! Dini (kama njia) zimewekwa ili binadamu afuate utashi wa ucha Mungu na kuwatendea binadamu wengine vile apendavyo yeye (binadamu) kutendewa! Kanuni ya thamani juu ya maisha ya binadamu ni kuishi kama mgeni au mpita njia anayetaraji kurejea kwa Mwenyezi Mungu, kupokea malipo yake ya haki kwa mujibu wa maisha yake ya hapa duniani.
Hakuna shaka yoyote kwamba ugaidi kama njia ya waovu ni kitisho cha dunia na ndio msingi wa mauti ya utu na ubinadamu. Historia ya ugaidi inaanzia mbali sana. Pengine, matukio ya ugaidi yameendelea kurekodiwa kwa zama nyingi na kwa nyakati mbalimbali za binadamu. Lipo tukio kubwa la kigaidi na ovu machoni pa wanandamu hata kama lilifanywa miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita! Hili ni tukio ovu la kuzima haki ya kuenea kwa falsafa ya ukombozi wa mwanadamu kutokana na uovu ulioenea zama hizo na ndio maangamizi ya kuenea kwake zama hizi. Ukitazama historia ya ugaidi wa zama za karne ya 14 hadi 18, utagundua kwamba magaidi (watu waovu) walikuwa wakitumia mbinu za kufanya vitendo kigaidi katika kufikia malengo yao ya kijamii, kisiasa na kijamii kwa kujenga mazingira ya hofu na kuwatia woga wahanga wao (rejelea: www.research-terrorism.com). Inawezekana sana, na hususani kwa wageni wa historia, wakadhani kwamba matukio makubwa ya kigaidi ni yale tu yaliyojitokeza tar. 11 Septemba 2001 almaarufu kama Septemba Kumi na Moja huko nchini Marekani. Hapana! Ugaidi umekuwapo duniani kwa muda mrefu na unaendelezwa kwa mtindo maalumu wenye kupangiliwa na kuwekewa mikakati maalumu ya utekelezaji na taasisi zenye malengo ya kimkakati katika kufanikisha mradi wenye malengo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kadhalika.
Tafadhali, tuchukue fununu ya ugaidi inayopigiwa chapuo na kiranja Marekani na washirika wake, ambao ndiyo unotazamiwa na kuchukuliwa kama sehemu ya mafundisho ya mapambano na vita dhidi ya ugaidi wa dunia. Haiyumkiniki kama wapo waliofanya utafiti wa kina na kujiridhisha pasipokuwa na shaka lolote kwamba ni nani aliyeuasisi ugaidi huu tunaouona leo, unaodhaniwa kuwa ni matokeo ya kundi la al-Qaeda. Nani ameanzisha kundi hili la al-Qaeda na kwa nini? Ni utafiti mpana unaoweza kuweka bayana uanzishwaji wake na malengo yake japokuwa ni nadra sana kukuta waandishi wameandika hususani wale wanaoandikia vyombo vya habari vya kimataifa.
Hapana shaka lolotete kwamba, al-Qaeda ilikuwa inaongozwa na Osama bin Laden! Ni nani huyu Osama bin Laden? Ushahidi wa moja kwa moja unaopatikana kwenye vyanzo vinavyoaminika pamoja na uongozi wa Marekani kukiri (kama alivyofanya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekeni, Hilary Clinton) kwamba al-Qaeda iliundwa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na kupewa kiasi cha dola za Marekani bilioni tatu ($ 3bn/-) ili kundi hilo liendeshe vita dhidi ya Urusi (USSR) ya zamani iliyokuwa ikiikalia Afghanistan (rejelea: The Insider | Conspiracy Theory News: New World Order, Conspiracy Theories, News, Government, Secret Societies, Freemasons, Extraterrestrials, War..., news.bbc.co.uk, na Information for the World's Business Leaders - Forbes.com). Kiongozi wa al-Qaeda alipata mafunzo yake ya kigaidi (chini ya usiamizi wa CIA) Marekani, na Marekani ilifahamu na ilijua malengo ya kuanzishwa kwakwe. Hata hivyo, kwa Marekani urafiki wao ni wa kimasilahi zaidi kuliko wa kuendelea. Na ndivyo walivyoifanya Al-Qaeda na kiongozi wake Osama bin Laden. Waliitumia Al-Qaeda kwa malengo ya kimaslahi na kimkakati zaidi na baadaye walipohitilafiana kimasilahi waliibatiza al-Qaeda jina la ugaidi na kuanzisha vita dhidi yake! Kwa mujibu wa kipengele hiki, ugaidi unaopigiwa kelele za makeke na Marekani na washirika wake wakuu, unapewa usaidizi wa hali na mali na taasisi maalumu kwa malengo maalumu. Kwa misingi hiyo, ndivyo ugaidi unavyoendelea kuatamizwa kwa masilahi na kwa nyakati tofauti za historia. Tukiachilia mbali mfano wa gaidi namba moja Osama Bin Laden (kama alivyobatizwa na Marekani na washirika wake) na ndivyo kundi la al-Qaeda lilivyofanywa lijulikane dunia nzima.
Pamoja na Al-Qaeda kuna makundi mengi yaliyoorodheshwa kwenye orodha ndefu ya makundi ya kigaidi duniani (k.v. Taliban, Tamir Tiger la Sri Lanka, Hamas la Palestine, na sasa IS iliyojizatiti katika maeneo ya Iraq, Uturuki na Syria). Hii orodha ni kwa mujibu wa nchi zenye maslahi yake kwenye hii vita inayoitwa ya ugaidi duniani.
Pamoja na hayo, hata Afrika kulikuwapo na watu na makundi yaliyoitwa ya kigaidi enzi za harakati za kupigania uhuru miaka ya 1960 hadi mwishoni mwa miaka ya 1990. Makundi kama vile UNITA lililoongozwa na Dk. Jonas Savimbi wa Angola, na kundi la RENAMO lililoongozwa na Alfonso Dhlakama wa Msumbiji. Hata wakati mmoja mzee Nelson Mandela (Madiba) aliwahi kuwekwa kwenye orodha ya magaidi. Kwa vyovyote vile, ukimtazama aliyeitwa gaidi, Dk. Jonas Savimbi wa UNITA, alikuwa akipewa msaada na usaidizi wa kijeshi na Marekani kwa maslahi ya rasilimali za Angola.
Si kwamba sehemu hii imelenga kutoa shutuma kali dhidi ya mataifa tajwa kuwa ndio waasisi wa makundi ya kigaidi pengine labda kwa tofauti za kiitikadi ama dhana ya uzalendo na utaifa, hapana. Lengo la mjadala huu ni kuwaleta wasomaji pamoja waelewe kwamba ugaidi unaotangazwa ni ule unaotokana na harakati za watu na makundi yao katika kuendesha mfumo wa madai halali ya haki na yapo madai ya mfumo wa kigaidi unaoendeshwa kwa misingi ya maslahi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Katika mifumo yote, matumizi ya mbinu za kigaidi ni ya aina moja kwa vile falsafa ya ugaidi ni kuwatia hofu na kuwajengea woga wahanga wa vitendo vya kigaidi. Na hata wakati mmoja wa kupigania uhuru wa Afrika Kusini, mzee Mandela aliwahi kusema kwamba: “Pale njia ya amani inaposhindwa kuleta uhuru, haki na usawa basi njia iliyopo ni kuendesha harakati za kudai uhuru, haki na usawa kwa njia ya mapambano.”
Pamoja na hali zote nilizoeleza awali, napenda niweke wazi kwamba, kuna dhana mbili za ugaidi. Ugaidi unaoendeshwa na magaidi wanaotumiwa na watu au makundi ya watu (hata serikali) katika kufikia malengo ya kimkakati katika kutawala siasa, uchumi au jamii; na kuna ugaidi unaoendeshwa na mtu mmoja mmoja katika kufanikisha malengo ya kibinafsi au malengo ya kutumiwa na mtu au kundi la watu wenye mitazamo ya kifalsafa na kiitikadi kwa mujibu wa malengo yao ya kimkakati. Ugaidi umekuwa na utaendelea kuwa ni uhalifu, uwe unafanywa na mtu, watu au kikundi cha watu kwa malengo yoyote yale. Na hapa ni vema tukiweka wazi kwamba: ‘Kuna watu wanaotumia ugaidi kuficha malengo yao’. Hii ni njia ya udanganyifu uliofichama, ambao baadhi ya wataalamu huita uongo uliosukwa kwa utaalamu wa kiwango cha juu cha upeo.
Inawezekana wanaoficha uongo kwenye ugaidi wana dhamira ovu kama ilivyokuwa mwaka 2003, wakati Marekani ilipotengeneza uongo na kuivamia Iraq na kumuua Saddam Hussein kwa madai ya uongo (?). Au kama Marekani ilivyotengeneza uongo dhidi ya Kanali Muammar Gaddafi na kumuua (?). Na vivyo hivyo, Marekani na baadhi ya tawala na mamlaka za nchi kote duniani zenye nia ovu zinavyotumia alama ya ugaidi kuwapa watu makosa ya ugaidi wasiokuwa na hatia ya ugaidi. Ili kwa kutumia uongo huo wa kutengeneza, waweze kufanikiwa malengo yao kidola na kiuchumi huku wakiwahukumu na au kuwaua binadamu wasiokuwa na hatia. Huu ni ushenzi kufuru na batili katika ustaarabu wa jamii ya binadamu. Au ndiyo kusema, baadhi ya watu wanavyoitumia alama ya ugaidi kuwanasibisha watu wa dini isiyokuwa yao ili wapate kuwatenga na hata kuwapiga vita na kuwaua pasipo na hatia ya ithibati ya dhamira ya kutenda makosa.
Kuthibitisha hili, turejelee matini ifuatayo inayoelezea jinsi Papa Francis alivyoelezea uhusiano kati ya Ugaidi na Uislamu:
Siku ya Jumapili ya tar. 29 Januari, mwaka 2017, Papa Francis aligonga vichwa vya Vyombo vya Habari ulimwenguni baada ya kushutumu vikali ‘ungu fedha’ kuwa ndio injini ya mifarakano (vurugu/uchafukoge) inayotokea Ulaya na Mashariki ya Kati. Aliendelea kuhoji kuwa uchumi katili (uchumi kandamizi) wa kiulimwengu unawapelekea kuwagawa watu katika vurugu. Akijibu swali kutoka kwa mwandishi mmoja iwapo au hakuna upatano (uhusiano) kati ya Uislamu na Ugaidi hususan akilenga shambulizi baya alilofanyiwa Kasisi na Muislamu mwenye Msimamo Mkali (Muslim Extremist) juma lililopita huko Ufaransa, Papa Francis alisema:
“Ugaidi umekua kwa kuwa hakuna chaguo lingine (njia nyingine) na isitoshe ‘ungu fedha’ ndio umekuwa mhimili mkuu wa uchumi na si mtu.”
“Huu ndio msingi wa ugaidi, dhidi ya ubinadamu,” aliongezea. “najiuliza namna gani vijana wengi wa Ulaya wanaacha kazi halali na badala yake wanaingia katika shughuli za mihadarati (madawa) na mivinyo au kuingia katika Kundi la Dola la Kiislamu (Islamic State) (bila shaka itakuwa ni ungu fedha).”
Papa Francis anaamini kuwa hakuna dini inayoanzisha vurugu. Na, uzoevu wake katika majadiliano ya kidini anaonesha kuwa waislamu wanatafuta amani. “Si sawa na si haki kusema kuwa uislamu ni ugaidi,” Papa Francis alisisitiza.
“Iwapo nitasema ubaya wa Uislamu, itanilazimu niseme ubaya wa Ukatoliki. Si Waislamu wote ni wabaya, na si Wakatoliki wote ni wabaya,” Papa alisema tena, akiliondoa kundi la Dola ya Kiislamu kuwa linawakilisha Uislamu mzima.
“Karibia dini zote, kwa kawaida kuna vikundi vidogo vyevye msimamo mkali (Fundamentalist Groups),” hata kanisa Katoliki, Papa alisema. “mtu anaweza kuua kwa ulimi na pia kwa kisu.”
Aidha, siku ya Jumatano ya tar. 25 Januari, 2017, Papa Francis alitoa maoni sawa, akihoji kuwa mapigano yanayoendelea sasa huko Mashariki ya Kati, ni vita ya kiuchumi na malengo ya kisiasa na si dini au kile kinachojulikana kama ugaidi wa Kiislamu.
“Kuna vita ya fedha,” Papa alisema Jumatano. “kuna vita ya rasilimali asilia. Kuna vita ya kutawala watu. Baadhi wanaweza kufikiri nazungumzia vita ya kidini. La hasha. Dini zote zinataka amani; ni watu wengine wanaotaka vita.”
Kutokana na mawazo ya Papa Francis, ni busara kuacha njia ya udanganyifu juu ya kuwasingizia watu makosa wasiyokuwa nayo; hususan makosa ya ugaidi, kwa sababu zisizokuwa na mashiko ya kisayansi na kiuchunguzi. Sisi sote ni nasaba wa baba na mama mmoja, ni wajibu wetu kuishi kama ndugu hata kama tunatofautiana mitazamo na falsafa na au hata itikadi. Tukumbuke; tunapoishi pamoja lazima tukubali tofauti zetu.

Kitabu: Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi.
Kitabu kinapatikana Duka la Vitabu la House of Wisdom, Posta, kwa Tsh. 80,000/=

Mwandishi; Yericko Nyerere
0715865544
0755865544
 
Hii mada wakati naisoma nikaanza kuaandaa points kabisa. Lakini nilipoona kua imeandikwa na Y.Nyerere nikaghafilika kabisa na sijamaliza kuisoma coz YN hana alijualo kwenye nyanja za Dini na Ujasusi. But ni Muunga vipande vya simulizi mzuri..
 
Back
Top Bottom