Udhalilishaji Wa Wataalamu Hauvumiliki!

Idimi

JF-Expert Member
Mar 18, 2007
14,888
10,369
Makala hii ilitoka katika gazeti la Majira, mwanzoni mwa mwaka huu. Niliandika maoni yangu pia muda huo huo, ingawa nimechelewa kuweka hapa. Sina uhakika kama mada hii ilishajadiliwa huko nyuma, kama ilijadiliwa mtanisamehe kwa kujaza forum, ila ni haki yangu kuichambua.
Makala hii ni ndefu kiasi, kwa hiyo naomba uvumilivu wako katika hili, ingawa naamini utafaidika ukiisoma. Pia utasaida kutowadhalilisha wasomi wa Tanzania kwa maoni yako.
Karibu.

Na Maura Mwingira, Oslo

RAISI Jakaya Kikwete amesema matatizo yanayojitokeza katika mikataba mbalimbali ambayo Serikali imeingia na wawekezaji, yanachangiwa na uwezo mdogo wa baadhi ya wataalamu wa Kitanzania wanaoshiriki katika majadiliano ya mikataba hiyo.

Ili kuondokana na tatizo, hili Rais Kikwete ameiomba Serikali ya Norway kuwapatia mafunzo na mbinu za kisayansi wataalam hao zitakazowapa uwezo wa kujadiliana na wawekezaji huku wakiweka mbele maslahi ya Taifa.

Alitoa ombi hilo juzi wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano Norwei ,Bw. Erick Solhein katika siku yake ya mwisho ya ziara yake nchini hapa.

Alisema Tanzania inawahitaji wataalamu na wakufunzi kutoka Norwei ,kwa kuwa huko nyuma waliwahi kutoa msaada mkubwa wakati wa majadiliano ya mikataba, kiasi cha kuwafanya wakubwa katika taasisi fulani ya kimataifa ya fedha, kutofurahiwa na umakini uliooneshwa na Tanzania.

"Nakumbuka tulipata mtaalamu mmoja mzuri sana kutoka kwenu,alitusaidia sana kiasi cha kuwaudhi wakubwa wake wale waliokuwa upande wa wawekezaji na walipoona wanazidiwa kete walifanya njama na kumwondoa.Tunawahitaji tena wataalamu kama yule waje kuwafundisha watu wetu," alisisitiza Rais.

Alifafanua kuwa hivi sasa Tanzania inaendelea kufanya ugunduzi wa rasilimali nyingi zikiwemo za gesi asilia na madini,hali aliyosema utaalamu na umasikini wa hali ya juu unahitajika ili mikataba itakayohusu uendelezwaji wake ufanyike kwa umakini na uangalifu mkubwa.

Norwei kupitia Waziri wake huyo,imekubali kulifanyia kazi ombi hilo pamoja na lile la kusaidia kiuwezo na vifaa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU).

Katika mazungumzo yao, Waziri huyo alimweleza Rais kwamba,Tanzania ndiyo nchi inayoongoza kupewa umuhimu wa pekee katika masuala ya misaada ya kimaendeleo kuliko nchi yoyote barani Afrika ukiacha Msumbuji.

Alisema Tanzania ni nchi iliyo karibu sana na Norwei na kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili na watu wake, haujawahi kutetereka tangu Tanzania ilipopata uhuru wake Desemba 9, 1961 .

Rais Kikwete pia alikutana na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi na kusoma nchini Norwei

Wanafunzi hao walisema wanaunga mkono uamuzi wa Serikali kupitia upya majina ya wanafunzi waliopewa mikopo ili kubainisha walio na uhalali na wasio na uhalali wa kupata mikopo hiyo.

Akisoma salamu hizo kwa niaba ya wanafunzi wenzake,Bw.John Chalikulu,alisema kuwa pamoja na kuiunga mkono Serikali,wanaomba mikopo hiyo itolewe kwa asilimia mia moja ili kuwanufaisha wanafunzi wote.

Akijibu hoja hizo na zingine, Rais Kikwete aliwashukuru Watanzania kwa kutambua umuhimu wa kuwa na vitambulisho vya kitaifa na akasema kuwa serikali imekwishanza kulifanya kazi.

Alisema kuwa nia ya Serikali ni kuwa na vitambulisho kabla ya uchaguzi mkuu 2010 kama mambo yote yatakwenda vizuri.
Chanzo cha habari hii ni http://www.majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=2501

UCHAMBUZI WA HOJA

KIKWETE NA WATAALAMU WA KITANZANIA
Kama itakumbukwa vyema, hivi karibuni rais wa Tanzania ndugu Jakaya Kikwete alikuwa na ziara ya Kikazi katika nchi za Skandinavia. Akiwa nchini Norway alipata wasaa wa kuongea na waziri wa maendeleo na ushirikiano wa nchi hiyo, Bw Erick Solheim. Alinukuliwa akisema kuwa mikataba ya ajabu ajabu ya kimataifa ambayo taifa linaingia na kusababisha kuathiri uchumi inatokana na kukosekana kwa wataalamu makini wa Kitanzania ambao aliwaponda kuwa wana uelewa mdogo sana kuhusu nini kimebebwa ndani ya mikataba hiyo, hasa ile ya kimataifa. Na kama haitoshi akaomba pia Norway isaidie kuelimisha baadhi ya wataalamu wetu ili hapo baadaye tusirejee makosa kama hayo.
Inakera sana kauli hii, hasa inapotolewa na kiongozi mkuu wa nchi. Sijajua Kikwete aliwaza nini mpaka akaongea kauli hii. Wanorway watatuelewaje wakati kuna Watanzania kibao katika sekta nyeti hapo hapo Norway? Kuna Watanzania wengi sana wanaofanya kazi kama hizo ambazo Kikwete anaziponda, iwe Norway ama kwingineko, sasa anataka serikali ya Norway ianze kutilia shaka wasifu (CV) kwa Watanzania hawa?
Kwa kuanzia nimesema kuwa sikubaliani kabisa na wazo hili la raisi, kuwa nchi yetu haina wataalamu wa kuchambua na kuelewa yaliyomo ndani ya mikataba hii ya kimataifa. Wataalamu wa uchambuzi wa mikataba tunao wengi sana ila nahisi wanakosa uzalendo kwa kutanguliza maslahi yao binafsi. Nasema hivi kwa sababu, watu ambao hushughulika na hii mikataba mara nyingi ni wale wanaotoka wizara ya sheria na mambo ya katiba, pamoja na taasisi nyingine nyeti ambao nina uhakika viwango vyao vya elimu ni vya shahada, kama sio za uzamili (masters) basi ni za uzamivu (Ph.D). Kwa hiyo wanajua wanachofanya, kwamba kwa nini wanafanya hivyo hilo ni suala lingine. Na mara zote wataalamu hawa wanapoajiriwa huwa wanashindanishwa kwa sifa za elimu na uzoefu wao, kwa maana hio wanakuwa wengi. Hivyo basi, mwisho wa mchakato huo huwa nikupata mtaalamu bora ambaye hatimaye mwisho wa siku huajiriwa. Tukichukulia mfano huu, tunaamini kuwa mtaalamu huyu ameajiriwa kulingana na uwezo wake, kwa hiyo anajua majukumu yake ya kazi. Sasa kama atasaini mikataba ya ajabu ajabu inayoua uchumi wa nchi inatakiwa kwanza tutilie shaka kiwango cha uelewa wa majukumu yake pamoja na kuthibitisha kiwango cha elimu yake. Pili tuangalie namna alivyoajiriwa, kama aliajiriwa kihalali kwa kushindanishwa na waombaji wenzake ama alipitia mlango wa nyuma (memo) na hivyo hana sifa za ushindani wa kazi hii (competence) . Ninaamini kama mtaalamu huyu alisaini mkataba mbovu na anajua kuwa ni mbovu na ana sifa zote muhimu, basi alifanya makusudi na inatakiwa apatilizwe na sio kulindwa.
Siwezi kuafikiana na uamuzi wa raisi Kikwete kuongea suala hili na mtu ambaye hakuhusika na mikataba hii (Bw Solheim), kwa hiyo hajui nini kilichomo, ingawa anajua kuwa mikataba feki hii inaimaliza nchi. Ilitakiwa raisi awaulize wahusika waliotia saini mikataba hii ambao nina uhakika bila shaka anawafahamu, wangemwambia kwa nini na kwa namna gani walisaini mikataba hiyo. Pia wangesema kama walisaini bila kujua ama walijua ila walifanya makusudi, ama walisaini chini ya shinikizo la mtu fulani. Kwa nini Kikwete amekwenda kuliongelea suala hili nje ya nchi? Wataalamu wa Kitanzania wamekuwa wakipiga sana kelele kutaka kujua kilicho ndani ya hii miktaba, lakini serikali imekuwa kimya, na wabunge wetu ndio wamezibwa midomo kabisa na chama chao. Hawataki kuiongelea, kisa? Nidhamu ya chama, wanaogopa kushikishwa adabu na chama chao. Mvinyo ule ule katika chupa tofauti.

Tanzania ina wataalamu wengi sana wa sheria, na pia kama haitoshi kuna makampuni mengi sana yanayotoa ushauri wa kisheria ndani ya nchi, sasa kama mikataba inakuwa na lugha tata ambayo wataalamu wa serikali hawaelewi, kwa nini serikali haikuwaomba ushauri watalaamu hawa, badala ya kuwadhalilisha nje ya nchi kwamba hawana viwango shindani? Ina maana madaktari wote na maprofesa wa sheria kutoka vyuo vyetu vikuu na vingine vilivyo nje ya nchi hawafahamu lugha za mikataba? Hapa bado sijashawishika kuamini hili jambo. Raisi kapotoka bila shaka, kwa hiyo sio vibaya kama atawaomba radhi wataalamu wa Kitanzania.
Kuna maswali kadhaa muhimu ambayo pia ni vyema kama mheshimiwa raisi atayatolea ufafanuzi, ili kuondoa shaka miongoni mwetu wananchi. Moja, kwa nini mikataba ambayo waathirika wake ni wananchi (walipa kodi) inakuwa ya siri? Wanaosaini wanafanya hivyo kwa niaba ya wananchi sio kwa niaba yao, kwa hiyo inabidi wananchi wajue kilichomo. Pili, kwa nini raisi Kikwete anamtetea raisi mstaafu ndugu Mkapa kuhusu utata wa mkataba wa rada? Kuna nini katikati hapa? Tatu, inasemekana kuwa mkataba wa rada wakati unasainiwa, raisi Kikwete alikuwa waziri wa mambo ya nchi za nje, kwa maana hiyo anajua kilichomo, kwa nini hakusimama kupinga ubovu wa mkataba huo? Kunani hapa? Nne, wakati mkataba wa makubaliano ya ununuzi wa umeme ule wa pale Tegeta yeye alikuwa waziri wa nishati na madini, je hakujua kilicho ndani ya mkataba ulio chini ya ofisi yake? Tano, mkataba tata wa umeme wa Richmond umesainiwa yeye akiwa raisi, na najua anajua kinachoendelea, kachukua hatua gani mpaka sasa? Kuna mtu yoyote kapatilizwa kwa udanganyifu huu? Au hio ndio ari, nguvu na kasi mpya?
Wananchi tunataka kujua majibu ya maswali haya, kwa hiyo sio vibaya kama tutapata ufafanuzi kutoka kwa raisi.
Nikirudi katika suala la kutetea wataalamu wa Kitanzania, mimi binafsi kama mtaalamu pia sina shaka hata kidogo na uelewa wa wataalamu wetu. Najiamini kusema hivyo kwa sababu kuna Watanzania wengi sana ambao raisi kawaponda lakini wanafanya kazi nzuri sana na wanaaminika, iwe ndani ama nje ya nchi. Nje ya nchi kwa mfano, tulikuwa na Dk Salim Ahmed Salim enzi za OAU, alifanya kazi vizuri tu na mpaka sasa bado anatumiwa kimataifa katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa Darfur nchini Sudan.Tunao akina Dk Asha Rose Migiro ambaye ni Katibu msaidizi wa Umoja wa Mataifa (UN) na Profesa Anna Tibaijuka wa shirika la makazi duniani (UN HABITAT) katika ngazi ya kimataifa na tunajivunia sana watu hawa. Tanzania imeaminiwa na umoja wa mataifa na kupewa kiti cha muda katika baraza la usalama la umoja wa mataifa. Kuna ukweli kuhusu umbumbumbu wetu hapa? Dk Migiro ni msomi mwanasheria, sasa kama raisi wake anasema hana viwango, kaenda umoja wa mataifa kufanya nini? Kama alikuwa hawaamini wasomi wa Kitanzania angepinga uteuzi wake na kumuomba Migiro arudi Tanzania. Je Dr Migiro na wanasheria wenzake walipewa nafasi kama mwanasheria kupitia mikataba tata ya serikali? Nasema tena kuwa najisikia uchungu sana kwa kauli hii dhalilishi ya kukera mbele ya wasomi wa Kitanzania ambao jumuiya ya kimataifa inawaamini sana na kuwatumia lakini serikali inawanyima mikopo ya elimu na kuwapiga teke. Na kwamba raisi anawaomba wataalamu wa Kinorway waje kuwafundisha wataalamu wetu uzalendo silikubali. Uzalendo haufundishwi na wageni, lazima utoke ndani ya nchi, ndio maana hapo chini nimesema kuwa hawa Wanorway na wenzao majirani wamewezeshwa kutumia bendera yao popote pale ili kuonyesha uzalendo wao. Je bendera ya Tanzania ni wakilishi kiasi gani? Bendera ni kitambaa tu cha rangi, lakini kina maana kubwa sana na bendera inaongea kimya kimya, si ya kuidharau hasa linapokuja suala la uzalendo.

Ushauri Kwa Raisi Kikwete
Suala la wataalamu wa serikali kusaini mikataba mibovu lina mizizi yake ambayo inatakiwa kung’olewa mara moja, ingawa yataka moyo kwani tumefikia pabaya. Hata hivyo hajachelewa sana, kwani ndio kwanza ana mwaka mmoja na robo madarakani. Kwanza, ingependeza sana kama mikataba yote ambayo ina athari kwa taifa ipitie kwa wawakilishi wetu bungeni na nakala zake tupewe sisi tuliowaweka madarakani, ili tujue nini kinachoendelea. Naamini mawazo ya Watanzania yanapishana kwa hiyo tukipewa mikataba tukaipitia na sisi huenda tukachangia vitu muhimu. Kuna uwezekano mkubwa wa kufanikiwa katika hili. Najua ni gumu kutekelezeka ndio maana nikasema hapo juu kuwa yataka moyo.

Pili, asilimia kubwa ya wataalamu waliosaini mikataba ya ajabu ajabu bado wako madarakani, kwa hiyo ni wakati muafaka wa kuangalia viwango vyao vya ushindani (competence) pamoja na wasifu wao (CV). Hili litaturahisishia kujua undani wao na hivyo kuwachukulia hatua za kinidhamu. Hili linawezekana sana tu, kinachohitajika hapa katika kufanikisha hili ni utashi wa kisiasa.

Tatu, tutenganishe siasa, kujuana, uanamtandao, ukereketwa, na utaalamu. Kama utatafiti utagundua kuwa si wataalamu wengi wapo katika siasa. Binafsi sielewi ni kwa nini. Kwa hiyo basi, kama mtu ana utalaamu lakini si mkereketwa basi apewe kazi ambayo ana utaalamu nayo, na wala sio kupewa mkereketwa ama mwanamtandao ama mtoto wa kigogo fulani, ambaye hajui majukumu ya kitaalamu ya kazi husika. Suala hili huenda ndio ambalo limebomoa kabisa uzalendo wa wataalamu Watanzania popote pale walipo. Suala hili liko wazi sana, kwani kila siku tunasikia matukio ya watu wasio na utaalamu wa kazi kuajiriwa katika sekta nyeti, kisa tu wanafahamiana na wakubwa wa nchi.

Nne, katika hotuba yako ya kwanza kabisa bungeni mwishoni mwa mwaka 2005, uliongelea suala la wananchi kukosa uzalendo. Binafsi sijaona hatua ulizochukua katika kuurudisha uzalendo wa Watanzania uliopotea. Suala ni kutafiti, kwamba kwa nini uzalendo wa Watanzania umetokomea? Je hawana imani na serikali? Hawana imani na wataalamu wao? Je hawana imani na vyama vyao vya siasa pamoja na sera zao? Je hawajaelimika vya kutosha?
Nafikiri utaungana nami nikisema kwamba katika nchi za Skandinavia ulizotembelea ulishangaa kuona watu wanapeperusha bendera za nchi yao katika nyumba zao, katika magari yao, katika ofisi na katika nguo zao. Bendera za nchi zao zipo kila pahala, hata kwenye bidhaa za kibiashara kama pipi, biskuti, chupa za soda, chupa za maji na kila bidhaa ambayo wana uhakika inavuka mipaka yao. Unafikiri ni kwa nini? Kwa nini Watanzania hatupeperushi bendera ya taifa letu katika sehemu zetu za kazi? Kwa nini bendera ya nchi ni mali ya serikali pekee na si mali ya serikali na wananchi? Kwa nini wananchi wanapeperusha bendera za vyama vyao na si ya serikali?
Si kila Mtanzania ni mwanachama wa chama fulani cha kisiasa na ninaamini (ingawa naweza kukosolewa), kuwa Watanzania walio wengi hawana vyama, ukilinganisha na walisajiliwa katika vyama vya kisiasa, sasa basi kama anahitaji kupeperusha bendera, apeperushe ipi kama si ya Marekani wakati haruhusiwi kupeperusha ya taifa lake? Kwa nini bendera ya Marekani ni maarufu sana Tanzania kuliko bendera ya taifa letu? Kwa nini watu wanaamua kujilipua (kuchana pasipoti)? Na wengine wanaojilipua ni wasomi. Kwa nini?
Nimesema bendera inaongea sana kuliko mtu anavyoweza kufikiri. Hawa wenzetu wamewekeza katika bendera. Inaonekana kama kichekesho lakini ndio hali halisi, hakuna njia ya mkato katika kutafuta uzalendo. Ndugu raisi, tumia nafasi hii kuwaelimisha Watanzania rangi za bendera yao na umuhimu wake ili kuwajengea uzalendo.
Tusiishie kuwalaumu wataalamu kuwa hawana uwezo wakati uwezo wanao ila hawapewi nafasi ya kufanya kazi zao kwa mujibu wa taaluma zao, kutokana na shinikizo la wanasiasa. Wanakosa uzalendo, kwani serikali haijawawezesha kuwa wazalendo.
Mungu ibariki Tanzania.
 
Kweli kabisa tatizo kubwa la viongozi wetu wanatanguliza undugu na urafiki katika kuteua watendaji pasipo kujali utaalamu wao na uwezo wa kufanya kazi matokeo yake ndo haya mikataba inasainiwa utadhani mtu alipewa dawa ya usingizi.Ni lazima sasa kuangalia uwezo wa mtu wa kufanya kazi na elimu ili taifa liendelee.Tanzania tuna wataalamu wengi tu ila wengi wamenyimwa nafasi na nafasi zao wamepewa wababaishaji,ona kama bungeni wabunge wengi elimu zao hafifu sana huku wasomi wamezagaa mitaani na wengine wanatumikia nchi za watu unaona maamuzi ya bungeni kama vile watu hawajafika hata chekechea
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom