Udhaifu wa muungano haujaletwa na mabadiriko ya 10 ya katiba ya zanzibar | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Udhaifu wa muungano haujaletwa na mabadiriko ya 10 ya katiba ya zanzibar

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Gamba la Nyoka, Feb 25, 2011.

 1. Gamba la Nyoka

  Gamba la Nyoka JF-Expert Member

  #1
  Feb 25, 2011
  Joined: May 1, 2007
  Messages: 6,594
  Likes Received: 6,755
  Trophy Points: 280
  UDHAIFU WA MUUNGANO HAUJALETWA NA MABADILIKO YA 10 YA KATIBA YA ZANZIBAR

  Makala hii imeandikwa na Wakili Maarufu hapa Zanzibar Bwana Awadh Ali SaidMakala iliyoandikwa na Mhe. Tundu Lissu, yenye kichwa cha maneno "Muungano wa Tanzania sasa umekuwa dhaifu zaidi'' iliyochapishwa katika gazeti la Mwanahalisi la Jumatano tarehe 09 – 15 February 2011 imesheheni upotoshaji wa mambo ya msingi kisheria na hivyo haistahiki kuachwa bila kubainisha ukweli na usahihi wa hoja alizoibua.


  Mwandishi amejaribu kujenga hoja inayotoa taswira kuwa Muungano wa Tanzania umezidi kuwa dhaifu kutokana na Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 ambayo yeye anaamini kuwa mabadiliko hayo "yamemong'onyoa misingi karibu yote ya muungano … yamebadili sura ya muungano wenyewe, mipaka yake na muundo wake" na kwamba anakhofu kuwa mabadiliko hayo "yanaweza kuwa chanzo kikuu cha kubomoka kwa Muungano na hata tishio kwa usalama wa mipaka ya Taifa".
  Hoja alizojenga juu ya maoni yake hayo ni kama ifuatavyo (na nitajaribu kuijadili moja baada ya nyengine na kuonesha udhaifu wa kila hoja husika.)
  Hoja ya kwanza ni kuwa Mabadiliko Ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar yaliitangaza Zanzibar '‘kuwa nchi yenye mipaka kamili" Anaendela kueleza kuwa "Rais anajua kuwa kabla ya mabadiliko hayo kufanyika, Zanzibar haikuwa nchi na wala mipaka yake haikutajwa" Anaegemeza hayo akirudia kifungu cha kwanza cha Katiba ya Zanzibar 1984(kabla ya marekebisho) kinachosema '' Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania"

  Katika hoja hii ya kwanza kuna mambo mawili; la kwanza kuwa Mabadiliko hayo ya kumi ndio yaliyoitangaza Zanzibar kuwa nchi, na la pili ni kuwa mabadiliko hayo ndio yaliyobainisha mipaka ya Zanzibar ambayo mwanzo haikutajwa. Yote mawili katika hoja hii sio ya kweli na ni ubunifu wa mwandishi mwenyewe. Tuanze na la kwanza la Zanzibar kuwa nchi.
  Ieleweke kwa ufupi tu kuwa Zanzibar ilianza kuwa na Katiba yake ya kwanza tokea baada ya Mapinduzi ya 1964 hapo mnano mwaka 1979 ambayo baadae ilifutwa na kuandikwa upya mwaka 1984, na hadi leo hii Zanzibar inaongozwa na Katiba yake hiyo ya 1984- ambayo imeshafanyiwa marekebisho mara 10. Sasa tujiulize jee! Katiba ya Zanzibar ya 1984 haikutaja Zanzibar kama nchi ila baada ya hayo marekebisho ya kumi yanayolalamikiwa? Ni kweli Katiba ya Zanzibar ya 1984 kabla ya marekebisho ya kumi ilieleza katika kifungu cha 1 kuwa " Zanzibar ni sehemu ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania" Lakini ukiwacha kifungu hicho cha kwanza vifungu kadhaa wa kadhaa au tuseme katiba yote ya Zanzibar (kabla ya hayo marekebisho ya kumi) yakiitaja Zanzibar kuwa ni nchi. Angalia vifungu (baadhi tu) ili tuweke sawa hili:

  (9)(i) Zanzibar itakuwa ni NCHI ya kidemokrasia na haki za kijamii.

  (9)(2)(a) Mamlaka ya kuendesha NCHI ni ya wananchi wenyewe …

  (10) Kwa madhumuni ya kuendeleza umoja na maendeleo ya watu na ustawi wa jamii katika NCHI itakuwa ni wajibu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar:(

  10)(3) Itadhibiti uchumi wa NCHI kufuatana na misingi na madhumuni yaliyoelezwa na katiba hii.

  (12)(3) Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu yatalindwa na kuamuliwa na mahkama pamoja na vyombo vya NCHI na vinginevyo vilivyowekwa na sheria.

  (21)(i) Kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa NCHI…

  (23)(2) Kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasili ya Zanzibar, mali ya NCHi pamoja na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi…

  Kwa ujumla vifungu vya Katiba ya Zanzibar (kabla ya hayo marekebisho ya 10) vinavyoitambua Zanzibar kuwa ni nchi ni vingi mno lakini inaonesha mwandishi hakuviona au havikumpendeza. Yeye amependezwa na kimoja tu, cha kwanza tu, na ameng'ang'ania hicho hicho tu kujenga hoja utadhani Katiba ya Zanzibar ilikuwa na kifungu kimoja tu. Katiba ya Zanzibar ilikuwa na vifungu 135 na baada ya marekebisho ya kumi ina vifungu hivyo hivyo 135.
  Na labda iwe ni kupitikiwa, kwa vile hakuna mkamilifu, lakini mwandishi ni mwelewa msomi mahiri wa fani ya sheria. Na msingi mkuu katika kanuni za kutafsiri sheria (Statutory Interpretation ) ni kuwa ili uweze kupata tafsiri sahihi kwa waraka wowote (iwe ni Katiba, Sheria, Mkataba n.k.) ni kuwa unatakiwa uusome waraka wote ndipo uweze kufahamu maana, tafsiri au dhamira inayopatikana kwa ujumla katika waraka huo kuhusiana na jambo husika. Sio kuchopoa kifungu kimoja tu ukaegemeza hoja yako hapo hapo tu.
  Lakini bila ya kuangalia vifungu vyengine vya katiba hiyo ya kabla ya marekebisho ya 10 kama tulivyofanya hapo juu tuseme tuangalie hicho hicho kifungu kimoja tu, cha kwanza tu,kama alivyofanya mwandishi kinachosema '‘Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano" Sasa tujiulize Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri Ya Muungano inasimama katika utambulisho upi? Sawa ni sehemu ya Jamhuri, lakini utambulisho wake ni upi? Ni sehemu kama Mkoa, Wilaya, Tarafa, Jimbo, Kata au kitongoji? Zanzibar ina katiba yake, ina Rais wake, ina Mahkama zake, ina mawaziri wake, ina Baraza lake la kutunga sheria, ina watu wake (tena wana ID zao), ina bendera yake ,ina wimbo wake wa Taifa, ina Mamlaka yake ya Serikali za mitaa, ina magereza yake (vyuo vya mafunzo), ina vikosi vyake vya ulinzi, ina mapato yake na bajeti yake n.k. jee kuna Mkoa au Wilaya yenye yote hayo? Na yote hayo yapo kabla ya hayo mabadiliko ya kumi ya katiba ya Zanzibar. Hivyo hakuna ukweli wowote kuwa Zanzibar imetangazwa kuwa ni nchi kwa mabadiliko ya 10 ya katiba ya Zanzibar 1984.

  Tumalizie hoja ya kwanza kwa kujibu suala la mipaka. Mwandishi anasema:
  "Rais anajua kuwa kabla ya mabadiliko hayo kufanyika, Zanzibar haikuwa nchi na wala mipaka yake haikutajwa". Jee! Ni kweli mipaka ya Zanzibar haikutajwa kabla ya marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ? Tuangalie katiba ya Zanzibar 1984 kabla ya mabadiliko ya 10 kifungu cha 2(i) kinasemaje:2(i) "Eneo la Zanzibar ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba na visiwa vidogo vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano ikiitwa Jamhuri ya watu wa Zanzibar."
  Na baada ya marekebisho ya kumi kifungu hicho kinaendelea kuwepo kama kilivyo kuhusiana na suala la mipaka.

  "1) Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vidogo vilivyoizunguka bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya watu wa Zanzibar".
  Jee! kuhusiana na suala la mipaka ya Zanzibar tujiulize kuna ongezeko au jambo jipya lililozaliwa na mabadiliko ya kumi? jee ni sahihi kusema kuwa kabla ya mabadiliko ya kumi Zanzibar mipaka yake haikutajwa?

  Hoja ya pili ya mwandishi ni kuwa marekebisho haya yanadhoofisha Muungano kwa vile yameondoa mamlaka ya kuigawa Zanzibar katika mikoa kutoka mikononi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na kuweka mamlaka hayo kwa Rais wa Zanzibar. Hili ni kweli limefanyika katika marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar. Lakini tujiulize ni kwa nini limefanyika? Inaeleweka wazi kuwa ni Rais wa Zanzibar ambae kipindi chote tokea huo Muungano wa Tanzania uasisiwe 1964, ndie anayeigawa Zanzibar katika mikoa na wilaya. Hakuna kumbukumbu inayoonesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano amewahi kuigawa Zanzibar katika Mikoa au Wilaya. Sasa kwa takriban miaka 47 mamlaka hayo yalikuwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kikatiba lakini kiutendaji na kiutekelezaji aliyekuwa anatekeleza mamlaka hayo ni Rais wa Zanzibar; hivyo hiyo ilikuwa ni kasoro na ilistahiki kurekebishwa, na ndicho kilichofanyika. Haiwezekani tukadumisha vifungu ndani ya katiba ambavyo vinaonekana ni pambo tu. Hili litoshe kuonesha mkanganyiko uliomo katika katiba zetu.

  Hoja ya tatu ya mwandishi ni kuwa mabadiliko ya kumi yamepunguza mamlaka ya Mahakama ya rufaa ya Tanzania. Anasema:
  "Mabadiliko ya katiba yaliyofanyiwa yamekiuka katiba kwa kuinyang'anya Mahakama ya rufani ya Tanzania mamlaka ya kusikiliza rufaa zote zinazotoka katika mahakama kuu ya Zanzibar"Kwa ufupi haijawahi kutokea kwa mahkama ya rufaa kuwa na mamlaka ya kusikiliza rufaa zote zinazotoka katika mahkama kuu ya zanzibar tokea ianzishwe na kuwa na mamlaka kwa zanzibar.Katiba ya Zanzibar iliipa mamlaka mahkama hiyo kwa baadhi ya kesi tu. Tuangalie Katiba : "99 Mahkama ya rufani ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania itakuwa na uwezo wa kusikiliza rufaani toka mahkama kuu ya Zanzibar isipokuwa kesi zozote zinazohusika na:
  Tafsiri ya katiba hii

  Mambo ya kiislamu ambayo yameanza katika Mahkama za Kadhi.Mambo mengine yoyote yaliyoainishwa katika katiba hii na sheria nyengine yoyote iliyotungwa na Baraza la wawakilishi.
  Hivyo mabadiliko ya 10 hayakuongeza jipya lolote, pamoja na kuwa ni kweli mahakama hiyo sasa haitokuwa na uwezo wa kusikiliza rufaa kutoka mahkama kuu ya Zanzibar iliyotokana na mambo kuhusiana na vifungu vya haki za binadamu, na hili lilibainishwa tokea katiba haijafanyiwa marekebisho ya 10. Mamlaka ya mahkama ya rufaa ya Tanzania kwa Zanzibar ni kwa baadhi ya kesi tu, sio zote. Ieleweke kuwa kifungu cha 99(b) cha katiba ya Zanzibar 1984 kimetaja kwa ufupi tu "mambo yaliyoanzia mahakama ya kadhi" lakini kwa mujibu wa sheria no. 3/1985 iliyounda mahakama ya kadhi mambo yote ya ndoa, talaka, mirathi na haki stahiki za mtoto yote yanasikilizwa katika mahakama za kadhi endapo wahusika wote ni waumini wa dini ya Kiislamu.

  Hivyo pamoja na ukweli wa kuwa mabadiliko ya 10 ya katiba ya Zanzibar kwa kutumia kifungu cha 99(c) cha katiba ya Zanzibar kimeondoa uwezo wa Mahakma ya rufaa kusikiliza masuala ya haki za binadamu hili sio jipya, lipo kabla ya hayo marekebisho. Lakini hata kama tukihoji busara iliyotumika katika kuliondoa suala la haki za Binadamu katika mamlaka ya Mahakama ya rufaa bado sio sahihi kujenga hoja kama kwamba hili la kuondoa baadhi ya mambo katika mamlaka ya Mahakama ya rufaa ndio kwanza yaanzwe na mabadikiko ya 10 ya katiba na kama kwamba kabla ya hapo mahkama ya rufaa ilikuwa na uwezo juu ya mambo yote yaliyotokea mahkama kuu ya zanzibar.

  Hoja ya nne ya mwandishi ni kuwa mabadikilo ya 10 ya katiba ya Zanzibar yamekiuka katiba ya Jamhuri ya Muungano na kudhoofisha Muungano kwa vile sasa Zanzibar "imehalalisha uwepo wa vikosi vya Jeshi vya SMZ vinavyoviita Idara maalum" Ama kuhusu hili la "Vikosi vya kijeshi" kama alivyoviita mwandishi au '‘idara maalum" kama vinavyoitwa na katiba ya Zanzibar hapa sasa ni mshangao wa ajabu! Katiba ya Zanzibar, hata kabla ya hayo mabadilko ya kumi inaeleza kuwepo kwa Idara maalum na ambazo ni Jeshi la kujenga uchumi (JKU) kikosi maalum cha kuzuia magendo (KMKM) , Chuo cha mafunzo (cha wahalifu) na kifungu hichi hakikubadilishwa hata nukta!! Haikubadilishwa hata namba za vifungu , hayo yamo katika katiba zote mbili chini ya sura ya kumi kifungu 121 hadi kifungu 123 na hayakuguswa wala kurekebishwa lolote. Hizi ni Idara kongwe zipo Zanzibar na wala hazijaundwa na mabadiliko ya kumi na hayo mabadiliko ya kumi hata hayakugusa chochote kuhusu Idara hizi. Sijui haya yametokea wapi?

  Lakini tujiulize hivi Zanzibar chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina uwezo wa kuunda majeshi? Tena tutumie hiyo hiyo katiba ya Jamhuri ya Muungano aliyozungumzia mwandishi.
  Ni kweli, kama alivyosema mwandishi kuwa ibara ya 147 (i) ya katiba Ya Jamhuri ya muungano inasema wazi kwamba '‘ni marufuku kwa mtu yoyote au shirika lolote au kikundi chochote cha watu, isipokuwa Serikali kuunda au kuweka Tanzania Jeshi la aina yoyote"

  Laitani mwandishi angeangalia kifungu cha 151 cha katiba hiyo hiyo ya Muungano akaona neno "Serikali" lilivyotafsiriwa angeondoa shaka yoyote juu ya uwezo wa serikali ya Mapinduzi Ya Zanzibar kuweza kuunda na kuweka jeshi. Neno serikali linatafsiriwa kama ifuatavyo:

  "Serikali maana yake ni pamoja na serikali ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au Halmashauri ya Wilaya au Mji, na pia mtu yoyote anaetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya Serikali au Halmashauri"

  Naamini msomaji na hata mwandishi mpaka hapo ataona ni vipi katiba ya Muungano 1977 yenyewe inatoa fursa kwa serikali (ikiwemo SMZ) kama zilivyo tafsiriwa na katiba hiyo hiyo zilivyo na uwezo wa kuunda na kuweka jeshi.

  Pia mwandishi amegusia vyeo vipya vya Zanzibar vya makamo wa Kwanza wa Rais na Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar vilivyoundwa kufuatia mabadiliko ya kumi ya katiba ya Zanzibar kuwa nayo yamekiuka katiba ya Muungano na hivyo ni '‘batili na hayana nguvu yoyote ya kisheria" Ananukuu kifungu cha 64(3) cha katiba ya Muungano 1977 kudhihirisha huo ubatili aliodai. Kifungu chenyewe amekinukuu nusu tu.
  "Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la wawakilishi inahusu jambo lolote katika Tanzania Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka…"

  Lakini kwa mshangao utagundua kuwa kifungu hicho kinaendelea kumalizia kama ifuatavyo (lakini mwandishi ameona hiyo sehemu ya mwisho ya kifungu hicho asiinukuu, kwa nini, haieleweki)
  "… na pia endapo sheira yoyote iliyotungwa na Bunge inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Baraza la wawakilishi, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka"

  Sasa tujiulize muundo mzima wa serikali ya mapinduzi ya zanzibar na vyeo vya viongozi wa Serikali hiyo na watendaji wake ni jambo lililo chini ya mamlaka ya Bunge? Hamna popote katika katiba au sheria yoyote inayotoa mamlaka kwa Bunge juu ya kuunda vyeo au muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vyeo hivi vya makamo wawili wa Rais wa SMZ vimetokana na kundwa kwa Serikali yenye Muundo wa umoja wa Kitaifa lakini kama vyeo hivi ni batili basi kwanza huo muundo wenyewe uliopelekea kuwepo kwa vyeo ungekuwa ni batili! Mbona mwandishi kagusia vyeo tu hakuona kuwa kuna muundo mpya wa SMZ uliozaa vyeo hivyo?

  Muundo wa SMZ, vyeo katika SMZ kamwe hayajawahi kuwa mambo ya Muungano, ni mambo ya Zanzibar na yanayongozwa na katiba ya Zanzibar na yako ndani ya mamlaka ya baraza la wawakilishi.
  Mwisho mwandishi anasema "Ilikuwa ni vema mabadiliko hayo ya katiba kufuata njia sahihi za kisheria. Yangefanyika kwanza mabadikiko katika katiba ya Muungano kabla ya mabadiliko hayo kufanyika katika katiba ya Zanzibar" Hoja hii inatokana na msingi potofu kuwa katiba ya muungano ndio katiba mama na kuwa katiba ya Zanzibar ni katiba toto. Katiba hizi mbili zote ni sawa na hakuna ambayo ndio superior au supreme juu ya nyengine. Katiba ya Zanzibar ina nguvu juu ya mambo yote ya Zanzibar ambayo yako chini ya Zanzibar na hayako chini ya mambo ya Muungano. Na katiba ya Muungano ina nguvu kwa mambo ya Tanzania bara ambayo sio ya Muungano na yale mambo ya Muungano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.
  Hata kama baadhi ya taasisi , vyombo na vyeo vya zanzibar vinatambuliwa katika katiba ya Muungano, hiyo haimaanishi kuwa katiba ya Muungano ndio inayosimamia mambo hayo.

  Kwa kumalizia ningependa nigusie mambo mawili ambayo naamini ingependeza kama mwandishi angeyazingatia, la kwanza linatokana na maelezo yake kuwa "mabadiliko haya ambayo Rais ameyanyamazia yameifanya Zanzibar kuwa ni nchi yenye uhuru kamili" Naamini Zanzibar, pamoja na kuungana na Tanganyika na pamoja na kuwa ilisalimisha baadhi ya mamlaka yake kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano bado haikupoteza uhuru wake na hivyo ni huru na haijawahi kuwa koloni tokea ilipojikomboa na ukoloni.

  La pili linatokana na tishio kuwa "marekebisho haya yakifahamika vyema kwa baadhi ya wabunge, yanaweza kugeuza maridhiano yaliyofikiwa kuwa balaa, badala ya neema." Nakubali ni vyema marekebisho ya katiba yaliyoleta maridhiano ya muundo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar yakafahamika vyema sio tu na wabunge, bali na jamii kwa ujumla angalu itasaidia watu kujadili mambo baada ya kuyafahamu kuliko kujadili mambo kabla ya kuyafahamu kama inavyofanyika sasa.
  Mwisho nikubaliane na mwandishi kuwa Muungano wa Tanzania umezidi na unazidi kuwa dhaifu kila uchao na sababu za hayo zipo na ziko wazi lakini kamwe sio mabadiliko ya 10 ya katiba ya Zanzibar. Sababu hizo tutazijadili inshalla.
   
 2. Kibanga Ampiga Mkoloni

  Kibanga Ampiga Mkoloni JF-Expert Member

  #2
  Feb 25, 2011
  Joined: Aug 9, 2007
  Messages: 14,565
  Likes Received: 1,653
  Trophy Points: 280

  haisomeki
   
Loading...