Uchimbaji bauxite balaa tupu Kilimanjaro; Malori ya Tani 30 husafirisha kupeleka Kenya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Uchimbaji bauxite balaa tupu Kilimanjaro; Malori ya Tani 30 husafirisha kupeleka Kenya

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by nngu007, Jun 21, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Jun 21, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Mwandishi Wetu Same Toleo la 244 20 Jun 2012


  • Wateketeza msitu wa Shengena wa Same
  • Malori ya tani 30 husafirisha kupeleka Kenya

  MKATABA kati ya Carl Peters na Chifu Mangungo wa Msovero huko Usagara (Kilosa) ambaye, zama zile, alilaghaiwa na Mjerumani huyo na kummegea eneo kubwa la ardhi ya himaya yake unakumbukwa kuwa mmoja wa mikataba ya kilaghai kuwahi kutokea nchini.

  Hiyo iilikuwa mwaka 1884 wakati Carl Peters - wakala wa ukoloni wa taifa la Ujerumani alipokuwa akitafuta makoloni katika ardhi ya Afrika kwa ajili ya nchi yake.

  Chifu Mangungo anaweza kusamehewa kutokana na mazingira yaliyokuwepo wakati huo ya kutokuwa na elimu yoyote ya kumsadia kugundua ulaghai wa Carl Peters.


  Lakini miaka zaidi ya 120 baada ya ulaghai huo wa Carl Peters kwa Chifu Mangungo, bado mikataba mibovu isiyozingatia maslahi mapana ya wananchi imekithiri Tanzania; hususan sekta ya madini.


  Kuanzia katika dhahabu, almasi, tanzanite na madini mengine, malalamiko ni juu ya mikataba mibovu waliyoingia wawekezaji na serikali iwe ni ngazi ya kijiji, wilaya, mkoa au taifa. Na chanzo kikuu cha mikataba hiyo mibovu ni ufisadi.


  Moja ya mikataba ya aina hiyo ni ule wa uchimbaji wa madini ya bauxite katika kijiji cha Marien, kata ya Chome, wilayani Same ambako viongozi wa kijiji hicho wameingia na watu wanaoelezwa kuwa ni wawekezaji.


  Aidha, Halmashauri ya wilaya ya Same nayo pia imeingia mkataba na mwekezaji wa kutoza ushuru wa Shilingi 1,000 tu kwa kila tani moja ya udongo wa bauxite.
  Mikataba yote imegeuka shubiri kwa wananchi wa kijiji cha Marien wilayani humo.


  Madini hayo yanachimbwa katika kilele cha safu ya Milima ya Shengena wilayani humo, na tayari uchimbaji huo umeleta mtafaruku mkubwa baina ya wananchi kwa upande mmoja na mwekezaji huyo ambaye ni mfanyabiashara wa mjini Arusha.


  Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, baada ya kuchimbwa madini hayo husafirishwa kwa magari makubwa ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani kati ya 30 na 40 hadi nchini Kenya ambako hutumiwa kama malighafi katika uzalishaji wa saruji katika kiwanda cha Bamburi kilichopo Mombasa, na pia mengine husafirishwa katika nchi za China na Japan ambapo taarifa zinaeleza kuwa hutumiwa kutengenezea vigae vya sakafu (tiles).

  Mwandishi wa Raia Mwema aliyetembelea vijiji vinavyozunguka eneo hilo pamoja na machimbo ya madini hayo, wiki iliyopita, alipata fursa ya kuzungumza na wadau mbalimbali kuhusu mradi huo ambao umezua malalamiko makubwa mkonai Kilimanjaro hususan wilyani Same.


  Historia ya uchimbaji wa bauxite
  Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali na baadaye kuthibitishwa na viongozi wa kijiji hicho, kwa mara kwanza madini hayo yaligundulika wilayani Same mwaka 2004.


  Mwaka huo huo viongozi wa kijiji walitia saini na wawekezaji wawili kile kinachoitwa "Hati ya Makubaliano (memorandum of understanding) mnamo Septemba 20. Wawekezaji hao wawili wametajwa katika hati hiyo kuwa ni Abdullah Suleiman na Kimimino O.Mjenga wa sanduku la barua 77 Makanya (mji mdogo uliopo barabara kuu ya Arusha-Dar es Salaam).


  Hati hiyo ya makubaliano (nakala tunayo) yenye vipengele saba ilitambulika kama mkataba rasmi kati ya kijiji hicho na watu hao wawili, na miongoni mwa yanayoainishwa katika hati hiyo, yenye kurasa mbili, ni pamoja na ajira kwa wakazi wa Chome ipewe kipaumbele.


  Makubaliano mengine yaliyoaanishwa ni usalama na amani kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi kama wanawake na watoto wanaopita kutafuta mahitaji kama maji na kuni, kuwepo kwa huduma za afya eneo la mradi kama vyoo, mwekezaji kuchangia sehemu ya faida anayopta katika shughuli za maendeleo kama ujenzi wa barabara, shule na zahanati.


  Mengine ni sheria zinazofuata mazingira zifuatwe, mkataba wa malipo ufanywe kati ya mwekezaji na kijiji na kazi ya kuchimba madini hayo isifanywe kwa kutumia baruti.


  Makubaliano hayo yalihitimishwa kwa kusainiwa na viongozi wa kijiji mbele ya hakimu mmoja wa Mahakama ya Mwanzo wilayani Same.


  Hata hivyo, shaka kubwa katika makubaliano hayo imo katika tarehe.

  Hati ya makubaliano hayo inaonyesha kuwa yalitiwa saini Septemba 20, lakini kikao cha kamati ya kujadili makubaliano hayo kinaonyesha kilifanywa Septemba 23 ikiwa ni siku tatu baada ya makubaliano hayo kutiwa saini.

  Kwa mujibu wa makubaliano hayo, wawekezaji hao wawili walitakiwa kuwa wamemaliza mkataba wao ifikapo mwaka 2009, lakini uchunguzi wa Raia Mwema unaonyesha kuwa hata kabla ya muda huo waliuza eneo la mgodi wao kwa kampuni moja ya mfanyabiashara huyo wa Arusha kwa Sh. milioni 500.


  Na kati mauzo hayo wahusika hakuwashirikisha viongozi wa kijiji hicho wala Halmashauri ya Wilaya ya Same. Baada ya muda mfupi, kampuni hiyo ya Arusha ilianza uchimbaji mkubwa wa madini ya bauxite.


  Malalamiko ya wanakijiji wa Marien
  Alen Mtaita ni askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyekuwa na cheo cha staff sergeant anayeishi katika kijiji cha Marien, na ndiye anayeongoza harakati za wananchi wa kijiji hicho za kutaka serikali kuzuia haraka uchimbaji wa madini hayo.


  Katika mazungumzo na Raia Mwema akiwa na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji na viongozi wa madhehebu ya dini, Mtaita alisema kuwa, tangu awali kile kinachoitwa mkataba ulikuwa ni "feki".


  "Kama unavyoona, mkataba ulisainiwa tarehe 20 Septemba 2004 lakini kikao cha kijiji cha kuujadili kilifanyika tarehe 23 mwezi huo huo. Je inawezekanaje mkataba utiwe saini halafu kikao cha kuujadili kifanyike siku tatu baadaye? Hapo utaona kuwa suala zima lilijaa utapeli tu", alisema.


  Mwanajeshi huyo mstaafu anaongeza: "Mkataba huu ni dhaifu kuliko ule aliosaini Carl Peters na Chifu Mangungo wa Msovero nyakati zile za ukoloni. Kwa hakika, hauna manufaa yoyote kwa wananchi wa kijiji chetu. Kwa kifupi, ni mkataba haramu." Aliendelea kusema kwamba hata mkataba baina ya Halmashauri ya Wilaya ya Same na mwekezaji huyo wa kutoza Shilingi 1,000 tu kwa kila tani ya bauxite inayosafirishwa nje ya nchi ni mkataba usio na malsahi kwa wananchi wa wilaya hiyo kwani kiasi hicho ni kidogo kulinganisha na faida anayopta mwekezaji ambaye huuza tani moja kwa dola 2,500 za Kimarekani ambayo ni zaidi ya Shilingi milioni 3.


  Mwananchi mwingine, Turariva Philip Mndeme (60), anaeleza kuwa wakati huo yeye alikuwa mmoja wa wajumbe wa serikali ya kijiji na anaamini baadhi ya viongozi wenzake wa kijiji hicho walighushi nyaraka za kikao na kuonyesha kuwa kulikuwa na ridhaa ya wanakijiji wakati si kweli.


  "Nakumbuka vizuri tulifanya vikao mimi nikiwa katibu wa kamati iliyoundwa na wananchi kujadili suala hilo. Katika mkutano wa hadhara jumla ya watu 154 walipiga kura ya kuukataa mradi huo" alieleza Mndeme.


  "Baadaye ndiyo tukakubaliana kuunda kamati, na mimi nikiwa katibu tuliandika barua kwenda kwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na tulieleza katika barua hiyo kuwa wananchi wameukataa mradi wa uchimbaji wa madini ya bauxite", alisema.


  Aliongeza kusema kuwa, wananchi waliukataa kwa sababu ya viongozi kugushi muhitasari wa vikao. "Ujanja huo ulifanywa kwa manufaa ya kikundi kidogo cha viongozi hao, na kimsingi ushawishi wa rushwa ulitumika katika maamuzi waliyofikia ambayo yalikuwa kinyume na maamuzi ya wananchi wengi walioukataa mradi." Alisema kuwa; licha ya kuiandikia barua serikali kuitaarifu kuhusu uamuzi wa wanakijiji kuukata mradi huo, haikuchukua hatua yoyote wakati huo hadi baadaye wawekezaji hao waliposhindwa kuendesha mradi huo, na kuamua kuuza kwa kampuni hiyo ya Arusha ambayo ilianzisha shughuli za uchimbaji kwa kutumia mashine kubwa zaidi na za kisasa.


  Kwa nini wanapinga uchimbaji bauxite
  Uchunguzi wa Raia Mwema umeonyesha kuwa, sababu kubwa inayosukuma wananchi kuupinga uchimbaji wa madini hayo ni pamoja na athari za kimazingira zinatokana na uchimbaji huo usiozingatia sheria zinazosimamia masuala ya mazingira.


  "Tangu kuanza kwa uchimbaji mkubwa mwaka 2009, kiwango cha maji yanayotokana na chemchem za chini ya milima ya Shengena kimepungua sana na baadhi ya chemchem hizo zimekauka kabisa", anasema mkazi wa kijiji hicho, Emmanuel Zotta ambaye ni imam wa msikiti wa Chome (anasema uislam si jina bali ni imani).


  Mwananchi mwingine ambaye ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Indini, George Neslson, anadakia kwa kutaja chemchem zilizokauka katika miaka mitatu iliyopita kuwa ni za Kitahiro, Mkame, Kampanga na Chaivumba.


  "Kukauka kwa vyanzo hivyo vya maji kumesababisha watu kushindwa kuzalisha mazao ya chakula na biashara yaliyokuwa yanategemea mifereji ya umwagiliaji maji.

  Tumepeleka hoja hii kwa watu wa serikali lakini wanatujibu "kifedhuli" kuwa hali hiyo inatokana na mabadiliko ya tabia nchi, na sisi tunajiuliza mabadiliko ya tabianchi ndani ya miaka miwili yamalize maji tuliyotumia kwa miaka zaidi ya 100?".


  Bi Niuhiael Mndeme (78) naye anaeleza kuwa sababu nyingine ya wananchi kuupinga uchimbaji huo madini ni hofu ya kutokea kwa maporomoko ya ardhi kwenye vilele vya mlima huo; kwani uchimbaji huo unaondoa uoto wa asili unaofahamika kwa lugha ya wenyeji (Wapare) kama magande. Alisema kuwa uchimbaji huo wa bauxite unaweza kufanya milima hiyo ya Shengena kuathiriwa na maporomoko ya ardhi kwa urahisi kutokana na kijiji cha Marien kuwa chini kabisa ya kilele cha milima hiyo.


  Licha ya umri wake mkubwa, Bi Niuhiael ana kumbukumbu ya tukio la Desemba 5, 1954, wakati huo akiwa bado msichana tu, ambapo maporomoko katika kijiji hicho yaliua mtoto mmoja na mifugo kadhaa.


  "Nakumbuka vizuri nyumba ya mama mmoja aitwaye Nipael Ntekaniwa ambaye yupo hai hadi sasa - mkitaka mkazungumze naye, nyumba yake iliangukiwa na maporomoko kutoka mlimani na alipoteza mtoto mmoja na mifugo kadhaa; huku wengine wakijehuruhiwa vibaya", alisema.


  Bibi huyo anaongeza: "Nakumbuka vizuri wananchi walifanya kazi kubwa ya uokoaji wa wanafamilia 22 walionaswa na maporomoko. Walifanya kazi kwa siku mbili wakitumia majembe. Sasa leo serikali inaruhusu vipi uchimbaji madini juu ya mlima wa Shengena? Hii ni kutaharisha maisha ya watu wanaoishi chini ya mlima".

  "Nashindwa kuielewa serikali yetu. Mimi nasema heri ya wananchi wenzetu waliokwisha kufa kuliko wanaoishi; maana wanateseka sana. Mimi nasema; mwekezaji abaki na pesa zake, na sisi tubaki na ardhi yetu. Kwanza mwekezaji mwenyewe ni mbabaishaji tu, na wala hatumhitaji", aliongeza bibi huyo.

  Sababu nyingine ya kuupinga mradi huo wa uchimbaji bauxite, kwa mujibu wa wananchi hao, ni kwamba mradi huo hauwanufaishi kwa lolote; kwani mwekezaji hakuwahi kuchangia shughuli yoyote ya maendeleo kijijini mwao.


  "Kila tulipojaribu kuwasiliana na mwenye kampuni ili tuzungumze kuhusu kero zetu amekuwa na tabia ya kupuuza wito wetu na kututolea lugha chafu. Huyu mtu si muungwana hata kidogo", anaongeza kusema Amani Philip Mndeme ambaye ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Champishi.


  Aidha, taarifa zaidi kutoka kwa wananchi hao zinaeleza kuwa kampuni hiyo ya Arusha imekuwa inatoa Shilingi 100,000 kila mwezi kwa kijiji cha Mteke ambacho ni nyumbani alikozaliwa mkurugenzi wa kampuni hiyo. Fedha hizo eti ni kwa ajili ya matumizi ya barabara inayotumiwa na magari yake kusafirisha shehena ya madini hayo hadi kijiji kingine kilichopo katika uwanda wa chini cha Mwembe.


  Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mbonea Elinazi alilithibitishia Raia Mwema kuwa ni kweli kijiji chake hakina mkataba na mwekezaji huyo, na hali hiyo inatokana na makosa waliyofanya viongozi waliomaliza muda wao ambao waliingia makubaliano yasiyo halali.


  "Ni kweli kuwa kuna mgogoro mkubwa baina yetu na mwekezaji, na hali hiyo inatokana na mwekezaji huyo kuja kufanya uchimbaji wa madini bila kushirikisha kijiji na wananchi kwa ujumla wake. Hakuna mapato tunayopata hata kidogo na tumelalamikia sana suala hilo katika ngazi mbalimbali za kiserikali, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa", anaeleza mwenyekiti huyo.


  "Kwa sasa tumekwama. Hatuna la kufanya na mwekezaji mwenyewe ana kiburi.

  Anatumia lugha chafu dhidi ya viongozi wa kijiji na wananchi kwa ujumla.Wiki iliyopita alikuja mkuu wa wilaya kutembelea eneo la machimbo na alituahidi kuwa atashughulikia suala hilo, lakini hadi sasa bado hatujapata mrejesho wa ahadi yake." Hali ilivyo eneo la machimbo Majira ya saa 5 za asubuhi mwandishi wa Raia Mwema aliwasili katika kilele cha Milima ya Shengena baada ya safari ngumu ya usafiri wa pikipiki iliyochukua saa moja na nusu kufikia migodi hiyo kutokea kijiji cha Marien.


  Hapa hali ya hewa ni ya baridi kali sana inayoambatana na ukungu unaofanya mtu asiweze kuona kitu chochote mbele yake kwa zaidi ya mita 10, lakini pamoja na hali hiyo shughuli za uchimbaji kwa kutumia caterpillar na mashine za kuchimba udongo zinaendelea .


  Kabla ya kufikia machimbo ya kampuni hiyo unakutana na machimbo madogo yanayoelezwa kuwa ni mali ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) kupitia mkoa wa Arusha, Halima Mamuya. Katika machimbo hayo, vibarua hutumia machepeo, majembe na sururu kuchimba madini hayo. Machimbo hayo yako eneo la kijiji cha Mhero.


  Katika kilele cha milima ya Shengena, kwa chini kidogo, pia kuna wachimbaji wadogo wadogo wanaotafuta dhahabu katika vyanzo vya Mto Saseni ambao unaanzia katika milima hiyo.


  Wachimbaji hawa hutumia zana nyepesi za kazi kama vile majembe, ndoo za maji, na mapanga.


  Baada ya wachimbaji hawa wadogo kuona pikipiki umbali wa mita kama 100 hivi, walitimua mbio na kuacha kazi waliyokuwa wakifanya wakihofu kuwa huenda sisi ni askari au maafisa wa maliasili wanaolinda msitu wa hifadhi ya Shengena!

  Mwandishi pia alishuhudia msururu wa magari makubwa ya mizigo aina ya Astra yakitimua vumbi yakipita katika barabara yenye kona kali; huku yakiwa yameshehena mzigo wa udongo wenye madini ya bauxite tayari kwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi.


  Juu ya kilele cha Mlima Shengena ni machimbo yenyewe na shughuli za uchimbaji zinaendelea; huku pembeni ya mgodi huo ukionekana ‘mlima' mkubwa wa udongo unaotokana na mabaki ya udongo wa bauxite baada ya kuchambuliwa kitaalamu na mashine.


  Sehemu ya mgodi miti yote iliyokuwepo imekatwa ili kupisha shughuli za uchimbaji, na hata katika eneo wanalochimba dhahabu, hali pia si shwari; kwani miti iliyokwepo imekatwa, na kibaya zaidi wachimbaji hao wanatumia kemikali aina ya mercury kuchuja dhahabu katika udongo na maji.


  "Hii ndiyo hali halisi unayoiona hapa. Hakuna anayejali masuala yahusuyo mazingira. Mwekezaji hajali na wachimbaji wadogo pia hawajali. Wanatumia mercury kusafisha dhahabu katika chanzo cha Mto Saseni ambayo maji yake yanatumiwa na wananchi walioko vijiji vilivyoko chini ya milima hii ambao wanaathirika kiafya", anaeleza Nicholaus Kamoleka Mndeme.


  Mwekezaji amjia juu mwandishi
  Akizungumzia malalamiko hayo ya wakazi wa wilaya ya Same dhidi yake, kwa njia ya simu, mwekezaji huyo kwanza alihoji ni nani aliyemtuma mwandishi wa gazeti la Raia Mwema kwenda katika migodi yake.


  Mwekezaji:
  Nani amekutuma kwenda huko? Ulikwenda kutafuta nini? Mwandishi:Kwani kwenda katika migodi hiyo kijijini nahitaji hati ya kusafiria mheshimiwa?

  Nimekwenda kikazi baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wa Marien kuhusu mradi wako wa uchimbaji wa bauxite. Mwekezaji: Mimi najua umetumwa na maadui zangu ili uniharibie biashara zangu. Kwa hiyo andika unavyoona.


  Mwandishi:
  Adui zako ni akina nani? Mimi natekeleza majukumu ya kazi yangu tu. Je, madai kuwa huna mkataba na kijiji yana ukweli wowote? Mwekezaji: Si kweli, nisingeweza kuchimba madini kama sina nyaraka. Suala hili hata Waziri Mkuu,

  Mizengo Pinda, analifahamu, na usinipotezee muda wangu!


  Baada ya kauli hiyo, mwekezaji huyo ambaye hatutalitaja jina lake kwa sasa, alikata simu.


  Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Joseph Mkude alikataa kuzungumzia mgogoro baina ya mwekezaji huyo na wananchi kwa maelezo kuwa, suala hilo lipo ngazi ya kamati ya ulinzi na usalama, chini ya mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Same.


  Hata hivyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Herman Kapufi, hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya mkononi; kwani kila alipopigiwa iliita bila kujibiwa.   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Jun 21, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Lini Serikali yetu tukufu itakuwa na Uchungu na kujali wananchi wake badala ya kuwajali hao Wawezekaji Waongo?

  Sasa hiyo Bauxite watasema wameipata nchini Kenya, kama zamani ilivyokuwa Dhahabu ya Tanzania.

  Tunaanza kujenga nyumba zetu nzuri tunahitaji sakafu nzuri, wengi tunaagiza toka Kenya, na kwa Mshangao Mali Ghafi ni hizo

  zetu toka Same (BAUXITE).
   
Loading...